Monday, January 14, 2013

MBATIA AKATIZA ZIARA YAKE MTWARA ,AREJEA DAR

Story ya Idrisa Bandali

MWENYEKITI wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amekatisha ziara yake mkoani Mtwara baada ya jana kunusurika kuuawa na baadhi ya wananchi waliudhuria mkutano wake wa adhara uliofanyika uwanja wa Mashujaa mjini hapa kwa madai hawakuridhishwa na hotuba yake.
Mbatia na wabunge wake Moses Machali (Kasulu mjini) na Agripina Buyogela (Kasulu vijijini) waliokolewa na polisi baada ya kujifungia katika ofisi za chama hicho wilaya ya Mtwara Mjini kwa zaidi ya saa moja na nusu kuanzia saa 12 kasoro ya jioni hadi saa 1: 17 polisi walipowasili eneo hilo.
Wananchi walizingira ofisi hiyo huku wakiimba nyimbo za kumshtumu Mbatia kuwa ni Mamluki aliyetumwa na serikali kulainisha msimamo wa wananchi wa mkoa huo kuhusu gesi inayovunwa kijiji cha Msimbati kutopelekwa Dar es Salaam.
Kadri jua lilivyokuwa linazama na giza kutanda ndivyo hali ya usalama wa viongozi hao ilivyozidi kuwa tete, wananchi walianza kutupia mawe ofisi hiyo na wengine kujaribu kuvunja mlango kwa kurushia vitu vinavyosadikiwa ni mabomu ya kuulia samaki baharini.
Mara mbili milipuko mithili ya bomu ilisikia mlangoni hapo na moto kujitokeza kitendo ambacho kiliashiria usalama wa Mbatia na viongozi wengine kuwapo mashakani iwapo polisi wasingejitokeza mapema kuwaokoa.
Mabomu ya machozi yaliyorushwa na polisi yalitosha kuwatawanya wananchi hao na Mbatia na wenzake kupata afueni ya kutoka katika ofisi hiyo ambapo hadi saa 7 usiku walikuwa kituo cha polisi.
Kutokana na dhahama hiyo, Mbatia amekatisha ziara yake na kurejea jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mtwara mjini Uledi Abdallah amesema viongozi hao leo walipaswa kufanya mkutano mkubwa kijiji Msimbati ambako gesi asilia inachimbwa lakini kutokana na hali iliyojitokeza juzi uongozi huyo amekatisha ziara yake.
“Nimesikitishwa sana, nimefadhaishwa sana na tukio la jana…alikuwa leo aendelee na ziara yake kule Msimbati lakini kutokana na sababu za kiusalama amekatisha…sisi umoja wa vyama tunasema tukio hile ni la kupandikiza, ili tuonekane tunahatarisha usalama wa wananchi….wanataka kuishawishi polisi watunyime vibali vya kufanya mikutano ili gesi waichukue kirahisi” alisema Uledi ambaye ni makamu mwenyekiti wa umoja huo

Aliongeza kuwa “Mbatia hakuongea jambo lolote baya…walikuja hapa akina Ghasia na mawaziri wengine wakasimama jukwaani wakasema gesi itakwenda Dar es Salaam lakini hawakufanyiwa vurugu kama hizi…hivi ni njama za vyama vya siasa ambavyo havipo katika umoja huu”
Hoja ambazo zinadaiwa kuwa sababisho la Mbatia kupishana na baadhi ya wananchi nia pamoja na kauli aliyoitoa kuwa “iwapo gesi itatoka” ili hali msimamo wa wananchi gesi haitatoka. Sababu nyingine ni kushindwa kuendana na kauli mbiu ya ‘gesi kwanza vyama baadae’ ambapo Mbatia mara kadhaa aliposema gesi kwanza, aliitikia ‘Mtwara badae’.
Hoja nyingine inayozungumzwa kuwa ni kichocheo ya vurugu hizo ni kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kumteua ubunge Mbatia, na kwamba wananchi wanaamini hawezi kupingana na ‘bosi’ wake huyo.

No comments: