Wednesday, January 2, 2013

MAASKOFU WAJITOSA SUALA LA GESI YA MTWARA


Story ya Idrisa Bandali , MTWARA
MAASKOFU wa Kanisa la Anglikan Dayosisi ya Newala na KKKT Dayosisi mpya ya Kusini Mashariki kwa nyakati tofauti wametoa kauli za kupingana na Rais Jakaya Kikwete kuhusu mradi wa usafirishaji wa gesi asilia inayovunwa mkoani Mtwara kupelekwa Dar es Salaam.
Wakingumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi bwana idrisa bandali leo, Askofu wa Kanisa la Angalikan Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung’a alisema anapingana na uwamzi wa serikali wa kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kupelekwa Dar es Salaam na badala yake anaishauri kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara.
“Lazima wananchi wa Mtwara waamuke, tumejifunza kule Songosongo, gesi imekwenda Dar es Salaam, si Kilwa wala Lindi iliyofaidika na gesi ile…gesi ibaki Mtwara, mikoa ya kusini iimarishwe” alisema Askofu Mnung’a
Aliongeza kuwa “Hii yote ni Tanzania hakuna ubaya wowote ule mitambo ya kufua umeme ikawekwa Mtwara…wafikirie leo hatuombei ila watu wakilipua Kidatu, nchi itakuwa gizani, lazima tutawanye rasilimali zetu sio kila kitu Dar es Salaam”
Askofu huyo alimpongeza mbunge wa Mtwara mjini Asnain Murji kwa kuweka wazi msiammo wake kuwa anapinga gesi kupelekwa Dar es Salaam na kumshangaa mbunge wa Masasi Mariam Kasembe akidai mbunge huyo hawakilishi maoni ya wananchi.
“Nimewaambia waumini wangu kuwa tuwe tayari kutetea rasilimali yetu….nampongeza Murji kwa kutetea maslahi ya wananchi, huyu mbunge wa Masasi namshangaa sana, eti anaunga mkono, mbunge wa aina hii anateteta maslahi yake” alisema Askofu Mnung’a
Akikumbushia historia ya mikoa ya kusini alisema kugeuzwa kwa uwanja wa mapambano wa vita ya ukombozi kusini mwa Afrika kumechelewesha maendeleo ya mikoa hiyo na hakuna fidia yeyote iliyolipwa kwa maeneo hayo.
“Baada ya Uhuru tulikuwa eneo la mapambano ya Uhuru kusini mwa Afrika hakuna fidia…usafiri wa meli umeondolewa, reli imeng’olewa, bandali ipo hoi, tutapinga kwelikweli, tumedharauliwa vya kutosha” alisistiza askofu huyo
Naye Askofu Mteule wa Kanisa la KKKT Dayosisi Mpya ya Kusini Mshariki, Mchungaji Lucas Mbedule alisema yeye hapingi gesi kwenda Dar es Salaam ila anazuia hadi pale ahadi za serikali zitakapotimizwa kwa wananchi wa Mtwara.
“Kwenye salamu zangu za Krismas niliwaambia waumini kuwa ni wakati wa kuidai serikali kutimiza ahadi zake kwa wananchi…wananchi wa Mtwara waliahidiwa viwanda, hakuna kiwanda hata kimoja gesi inaondoka, hapana sikubaliani nalo” alisema Mchungaji Mbedule
Aliongeza kuwa “Serikali itueleze bomba la gesi kwenda Dar es Salaam litatoa ajira ngapi kwa wananchi wa Mtwara hilo moja, pili bomba hilo litachochea vipi uwekezaji kwa mikoa ya kusini…kama hakuna majibu ya hayo basi mimi nazuia gesi isiende Dar es Salaam”
Alifafanua kuwa Rais Jakaya Kikwete aliwaahidi neema wananchi wa Mtwara kutokana na uchimbaji wa gesi na kwamba kabla ya kufikiria kuisafirisha gesi kwenda Dar es Salaam ni muhimu ahadi hiyo ikatekelezwa.
“Zaidi ya miaka 21 barabara ya Mtwara Dar es Salaam haijaisha, mikoa mingine inajengwa barabara zenye kilomita nyingi na zinakamilika na kuiacha hii ya kusini…hata juzi nimepita hapo bado barabara ni ya vumbi” alibainisha Mchungaji Mbedule
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislam (Bakwata) mkoani Mtwara, Marijani Dadi alionekana kukwepa kutoa msimamo wake na badala yake alishauri pande mbili zinazopinga kukutana ili kufikia uwamzi “Siwezi kusema itoke wala isitoke kwa sababu huku anayesema itoke hanieleza kwanini isitoke na huyu anasema itoke hajaniambia kwa nini itoke, siwezi kufanyia maamuzi suala kama hili” alisema Dadi
Sanmbamba na hilo Mbunge wa Mtwara Mjini Hasnein Murji leo ameanza kufanya mikutano na mbalozi pamoja na wenyeviti wa serikali za mitaa katika kuopata maoni yao juu ya suala zima la gesi asilia
Katika mikutano hiyo ambayo imefanyika katika kijiji cha naliendele kata ya naliendele na kata ya ufukoni ,viongozi hao kwa pamoja wamepinga kuondolewa kwa gesi hiyo wakihitaji kuona manufaa kwanza kwa wananchi wa mtwara
Suala la gesi kwenda Dar es Salaam limezua mjadala nchini hasa baada ya wananchi wa mkoa wa Mtwara kuandamana Desemba, 27 mwaka jana wakinga uwamzi huo wa serikali.

No comments: