Tuesday, December 18, 2012

STORY ZA BUTIAMA , BUNDA NA RORYA HIZI HAPA


Story za AHMAD NANDONDE
>>>>>>>BUTIAMA
WAKAZI wa wilaya ya Butiama mkaoni Mara wametoa mapendekezo katika katiba mpya ya kutaka irejeshwe kwa azimio la Arusha ya kuzuia kiongozi yeyote wa umma asiwe mfanyabiashara.
Wananchi hao wametoa maoni hayo katika mdahalo ambao umefanyika katika eneo la Mwitongo ukihusu mabadiliko ya tabia nchi ambao umeandaliwa na Jukwaa la Manedeleo mkoani Mara kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society.
Wamesema kuwa kitendo cha viongozi wa umma kuwa wafanyabishara mara nyingi husababisha kukosekana kwa dhana ya uwajibikaji katika utendaji wa kazi.
Wananchi hao wamesema baadhi ya viongozi wamekuwa waharibifu wakubwa wa mazingira kwa kuwekeza katika maeneo yaliyokatazwa katika hifadhi za taifa, kujenga viwanda na hoteli katika ufukwe wa bahari, ziwani na mabondeni kwa kutumia nyadhifa zao.
Wameongeza kuwa viongozi hao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wawekezaji wa nje na kuzalisha taka za sumu zinazozagaa ovyo na kuwa mzigo kwa wananchi na kwamba viongozi hawawezi kusimamia sheria ya mazingira kwa kuwa wao ndio waharibifu wa kwanza.
Kwa sababu hiyo wamependekeza kurejeshwa kwa azimio la Arusha hasa kipengele cha kumzuia kiongozi kujihusisha na biashara na hivyo kufanya hatua kali kuchukuliwe kwa watu wanaoharibu mazingira.
>>>>>>>>>>>>>>BUNDA
CHAMA cha akiba na mikopo ya Muungano wa walimu wilayani Bunda MUWABU kimeongeza akiba ya lazima kwa shilingi milioni 6,697,300 sawa na asilimia 14 kwa mwaka 2012.
Katika taarifa ya MUWABU ambayo imesomwa na katibu wa chama hicho Bw. Mustapha Maagi katika mkutano mkuu wa mwaka imesema chama hicho kimeongeza akiba hiyo kutoka shilingi milioni 41,600,000 mwaka 2011 hadi kufikia shilingi milioni 48,297,300 mwaka 2012.
Amesema Hisa imeongezeka kwa shilingi milioni 10,114,000 kutoka shilingi milioni 17,600,000 mwaka 2011 hadi shilingi milioni 27,714,000 mwaka 2012 na idadi ya wanachama kuongezeka kutoka wanachama 333 hadi kufikia 380.
Awali katika taarifa yake Makamu Mwenyekiti wa MUWABU Bw. Sabato Munubi,amesema hadi kufikia Oktoba mwaka huu chama hicho kina dhima ya jumla ya shilingi bilioni 1,112,321,391 ambazo zinatokana na akiba za wanachama, amana na mkopo wa muda mrefu toka Benki ya CRDB.
Wakati huo huo Ofisa ushirika wa wilaya ya Bunda Bw. Saulo Runyeka ameitaka MUWABU kuwaajiri Meneja na karani mhasibu kwa taaluma ili kuepuka kupotea kwa kumbukumbu za kifedha na kuisababishia hasara chama hicho.
>>>>>>>RORYA
SERIKALI kupitia wakala wa kuhudumia barabara nchini TANROADS mkoani Mara,imeanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ambayo itaunganisha makao makuu ya wilaya ya Rorya na barabara kuku ya musoma,sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Barabara hiyo ambayo imeanza kujengwa kwa awamu kutoka eneo la Mika ambayo imetajwa kuwa itachangia ukuaji wa uchumi lakini pia itarahisisha mawasiliano katika eneo hilo.
Wakizungumza na waandishio wa habari baadhi ya wananchi na viongozi wa kijiji cha Bukwe wilayani Rorya pamoja na kuishukuru serikali kwa uamuzi wa ujenzi wa barabara hiyo,wamelalamikia kitendo cha baadhi ya madereva kutumia nguvu kupitisha magari yao katika barabara hiyo kabla ya ujenzi wake kukamilika.
Wamedai kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza gharama kubwa kwa mkandarasi huyo kampuni ya Gemen Engneering inayojenga barabara hiyo lakini pia inaweza kuchelewesha kukamilika kwa ujenzi huo.
Kwa upande wake mhandisi wa mradi huo kutoka kampuni ya Gemen Engneering ya jijini Mwanza mhandisi Mike Steven,amesema mradi huo umekuwa ukikumbwa na vikwazo ikiwa ni pamoja na wanasiasa kuchochea baadhi ya wananchi kupinga utekelezaji wa mradi huku wakiondoa vizuizi ambayo vimewekwa ili kuhakikisha kazi ya ujenziinaendelea bila vikwazo.
Meneja wa Tanroads mkoa wa Mara mhandisi Emanuel Korosso,akizungumza na waandishi wa habari amesema pamoja na changamoto zinazoukabili mradi huo amewataka wanasiasa kuacha tabia ya kuwatumia wananchi kupinga kutekezwa kwa mradi huo kwa kuingiza ukabila lengo likiwa kutaka mkandarasi kutoka katika eneo hilo.

No comments: