Friday, December 7, 2012

POLISIMARA YATOA TAHADHARI KUFUATIA MAUAJI KUSHAMIRI


Story ya Ahmad Nandonde , MUSOMA
Kufuatia mauji ya kinyama na kutisha kuibuka mkoani Mara,hatimaye jeshi la Polisi mkoani mara limetoa tahadhari kubwa kwa wananchi wa Mkoani hapa hususan wanawake wanaoishi katika maeneo ya vijini kuwa makini pindi watakapokuwa katika shughuli za kilimo na utafutaji wa kuni.
Pamoja na tahadhari hiyo pia wananchi hasa wanawake wameombwa kutoa taarifa polisi pindi tu wanaposhuku kuwepo kwa jambo lolote ambalo inahatarisha maisha yao ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mara SSP Japhet Lusingu,ametoa taadhari hiyo ofisini kwake mjini Musoma wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na matukio ya mauji ambayo yameibuka katika siku za hivi karibuni mkoani Mara hasa katika wilaya ya Butiama na Manispaa ya Musoma .
Amesema tayari jeshi la polisi linawashikiria watu sita kuhusiana na mauji ya Bi. Sabina Mkireri mkazi wa kijiji cha Kiemba ambaye aliuawa kwa kuchinjwa kisha wauaji kuondoka na kichwa chake Desemba tatu mwaka huu.
Aidha amesema Desemba mbili mwaka huu majira ya saa moja usiku Bi Brandina Peru alikutwa porini akiwa amekufa baada ya kuchinjwa.
Kaimu kamanda huyo wa polisi mkoa wa Mara,amesema marehemu kabla ya kuuawa kikatili aliondoka nyumbani kwake desemba mosi mwaka huu akiwa peke yake kwenda porini kukata kuni na hakuweza kurudi nyumbani hadi alipokutwa amekufa kwa kuchinjwa.

Hata hivyo amesema kabla ya kuchinjwa wauaji hao walimvua nguo zote na kuweka kando kisha kumbaka na kwamba hakuna mtu yoyote aliyekamatwa hadi sasa na chanzo cha tukio bado kinachunguzwa.
Kwa sababu hiyo amesema jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kwaajili ya kuwasaka watu wanahusika na vitendo hivyo huku akiwaamba waandishi wa habari na viongozi wa kisiasa kutowatia hofu wananchi kwa kutoa taarifa bila kuthibitishwa na vyombo vya dola.
Kuhusu taarifa za viungo hivyo vya binadamu kutumika kwa imani potofu kwa shughuli za uchimbaji wa madini na uvuvi wa samaki alisema jeshi hilo linachunguza ukweli wa taarifa hizo.
Wakati huo huo,kamanda Lusingu,amesema mwanafunzi mmoja Hamis Lazaro wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Etaro ameuawa kwa kushambuliwa,mawe na kukatwakatwa na mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Amesema tukio hilo lilitokea saa 11.30 katika kijiji cha Kwikerege kata ya Etaro wilaya Butiama baada ya kukutwa chini ya uvungu wa kitanda kilichokuwa kikitumiwa na Nyakongo Nyangata ambaye alikuwa na mahusiano ya kimapenzi.
Hata hivyo kamanda huyo amesema mbali na madai ya marehemu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi huyo mwenzake lakini wananchi walijichukulia sheria mkononi baada ya kuisi kuwa ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakishiriki katika vitendo vya mauaji ya kinyama katika eneo hilo.

No comments: