THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kuomboleza vifo vya Wasanii watatu vilivyotokea hivi karibuni katika mazingira tofauti.
Wasanii hao ni Muigizaji wa Kundi la Kaole yaani Kaole Sanaa Group,Marehemu Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ aliyefariki dunia hivi karibuni kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu.
Aidha Msanii wa Filamu John Stephano Maganga alifariki dunia tarehe 24 Novemba, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Vilevile usiku wa tarehe 27 Novemba, 2012, Msanii mwingine maarufu wa Maigizo ya Vichekesho na Muimbaji wa Muziki wa Kizazi Kipya, Hussein Ramadhan Mkieti maarufu kwa jina la ‘Sharo Milionea’ alifariki dunia kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha, baada ya gari hilo kupinduka katika maeneo ya maguzoni Songa, Wilayani Muheza katika Mkoa wa Tanga. Marehemu Mkieti alikuwa njiani akielekea nyumbani kwao katika Kijiji cha Lusanga Wilayani Muheza - Tanga.
“Nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno kutokana na taarifa za vifo vya Wasanii hawa ambao kwa hakika mchango wao mkubwa katika Tasnia ya Muziki na Maigizo hapa nchini ulikuwa unatambuliwa na kuthaminiwa na wananchi wengi. Pengo waliloliacha Marehemu hawa ni kubwa na ambalo si rahisi kuzibika katika kipindi kifupi”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kwa kuwapoteza Wasanii hawa maarufu ambao wameliletea heshima Taifa letu katika nyanja za muziki na sanaa kwa ujumla”, ameendelea kusema Rais Kikwete na kuongeza,
“Kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi kwa Familia za Marehemu Wasanii wote hao ambao najua machungu waliyo nayo kwa sasa ni makubwa, nami naungana nao katika kuomboleza vifo vya wapendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza mahali pema peponi Roho za Marehemu, Amina”.
Rais Kikwete amewaomba Wanafamilia wote wa Marehemu wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi chote cha maombolezo ya wapendwa wao kwani yote ni mapenzi yake Mola. Aidha ameomba Rambirambi zake ziwafikie Wasanii wote nchini ambao, katika kipindi kifupi kilichopita, wamewapoteza Wasanii watatu maarufu ambao enzi za uhai wao wamesaidia sana kuinua kiwango cha sanaa hapa nchini.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
27 Novemba, 2012
No comments:
Post a Comment