Story ya Idrisa Bandali, MTWARA
BAADA ya kutoonekana kwenye maandamano ya wakazi wa mkoa wa Mtwara ya kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam, yaliyofanyika Desemba, 27 mwaka huu, Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji ameibuka na kusema anaunga mkono wananchi hao kupaza sauti kutetea maslahi yao na kuongeza kuwa tamko lililotolewa wakati wa maandamano hayo lilikuwa dhaifu.
“Hoja ya msingi ni kwa namna gani bomba la gesi litanufaisha Wana-Mtwara…mimi kwa kiwango fulani sikubaliani na hoja ya gesi isiende Dare s Salaam lakini naungana na wananchi kudai tutafaidikaje na bomba hilo” alisema Murji aliongea katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi jana.
Alisisitiza kuwa “Ninakubali gesi iende Dar es Salaam kwa sharti la kuzalisha umeme tu, si kwa matumizi mengine, wakianza kuitumia kwenye viwanda watakuwa wametuua kabisa”
Alibainisha kuwa kitendo cha wananchi kuandamana ni haki yao ya msingi na hakipaswi kubezwa na mtu yeyote kwa sababu wanateteta haki yao ya msingi ya kufaidika na rasilimali yao.
“Leo hii waziri ananipigia simu kuniuliza mahitaji yetu ni yepi, hilo ni jambo la msingi ndiyo maana nasema tamko lililotolewa wakati wa maandamano ni dhaifu kwa sababu halielezi mahitaji yetu ni yapi…lazima kuwape conditions (masharti) kwamba gesi ikienda Dar es Salaam sisi tunahitaji hiki na kile” alifafanua Murji
Aliongeza kuwa “ Nimeandaa kikao na viongozi wa umoja wa vyama vya siasa vilivyoratibu maandamano hayo ili tukae tuainishe mahitaji yetu ni yapi iwapo gesi itakwenda Dar es Salaaam…lazima tuwe na mkataba , tusikatae tu, tueleze tunahitaji nini gesi ikienda Dar es Salaam.
Akizungumzia kauli ya mkuu wa mkoa huo, Joseph Simbakalia ya kuwaita wanaopinga gesi kupelekwa Dar es Salaam wapuuzi na baadae wahaini, Murji alisema “Hakupaswa kufanya hiyo si busara kuwaita watu wanaodai haki yao wapuuzi au wahaini”
Alieleza kuwa “Angekwenda kupokea maandamano na badaye angewaelimisha wananchi waliokuwapo hapo kuwa serikali imeamua hivyo kwa sababu kadhaa, wapo ambao wangemwelea, lakini kuwaita wapuuzi au wahaini sidhani kama itasaidia”
Kauli hiyo ya mbunge imekuwa wakati ambapo tayari mkuu wa mkoa huo Simbakalia amesisistiza kuwa alikuwa sahihi kuwaita wapuuzi nap engine wahaini, huku Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akikazia uzi kuwa walioandaa maandamano hayo ni watu hatari kwa usalma wa Taifa.
No comments:
Post a Comment