Friday, December 28, 2012

ALICHOKISEMA MKUU WA MKOA WA MTWARA KUHUSU MAANDAMANO YA WANANCHI


SIKU moja baada ya maelfu ya wakazi wa Mtwara kuandamana kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa huo Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia amejitokeza na kusema aliwasamehe bure kuwaita wananchi hao wapuuzi bali alipaswa kuwaita Wahaini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwa njia ya simu ya mkononi, Simbakalia alionesha kutosumbuliwa na azimio la tisa la umoja wa vyama vya siasa walilolitoa wakati wa maandamano ambalo linamuomba Rais Jakaya Kikwete amuondoe katika wadhifa huo, kwa madai amewatukana wakazi wa Mtwara kwa kuwaita wapuuzi kutokana na kupinga gesi asilia inayochimbwa mkoani humo kupelekwa Dar es Salaam.

“Tunamuomba Rasi Jakaya Mrisho Kikwete amuondoe katika nafasi ya ukuu wa mkoa ndugu Joseph Simbakalia na kutuletea mwingine kwa sababu ametutukana hadharani, tumeshindwa kuvumilia, HATUMTAKI” ilisema sehemu ya tamko hilo lililosomwa na Suleiman Litope katibu wa umoja huo wa vyama vya siasa

Vyama vilivyounda umoja huo ni Chadema, NCCR-Mageuzi, SAU, TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, vikiwa na kaulimbiu ya gesi kwanza vyama baadeye, hapa hakitoki kitu.

Desemba 21, mwaka huu katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Mtwar (RCC) kilichoketi ukumbi wa Boma, Simbakalia alisema hawezi kuudhiriki katika maandamano aliyoyaita ya kiupuuzi.

“Nina kazi nyingi za maana , siwezi kuacha kazi hizo na kuja kuusikiliza upuuzi wenu, huo ni upuuzi” alisema Simbakalia wakati akifunga kikao hicho.



Katika ujumbe mfupi wa maandishi uliotumwa kwenye simu ya mwandishi wa habari hizi na mkuu huyo wa mkoa unaonesha kuwa Simbakalia anajutia kutoa kauli ya kuwaita wapuuzi kwa sababu haikuwa sahihi kwa watu hao kuitwa hivyo kutokana na ukubwa athari ya jambo wanalopinga.

“Congo ilianza kusambaratika ndani ya miezi kadhaa baada ya kupata uhuru 1961, na Waziri Mkuu Patrice Lumumba akauawa. Majimbo mawili yenye utajiri mkubwa wa madini (Katanga na Kasai) yaliamua kujitenga ili utajiri huo usitoke kwa faida ya Wakongomani wote” ilisomeka sehemu ya ujumbe huo ambao aliutuma baada ya mwandishi kumtumia ujumbe wa kumtaka ajibie tuhuma hizo.

Ujumbe huo uliendelea kusema “Hadi leo Congo ni Nchi lakini hakuna utaifa, uzalendo wala Taifa…hayoyalifanywa na vyama vya kisiasavilivyokumbatia sera za “Majimbo” na “Ukanda”….Mtwara tunashuhudia vyama vya kisiasa vyenye sera na malengo ya kuvunja umoja na kusambaratisha Taifa kwa sababu ya gesi asilia”

Akionesha msisitizo wa hoja yake Simbakalia alisema “Kuwaita watu kama hao Wapuuzi ni kuwasamehe bure kwa sababu utaishia kuwapuuza. Ukweli hao ni WAHAINI wanaolenga kuliangamiza Taifa kulisambaratisha kwa sababu ya choyo na uroho wa rasilimali”

1 comment:

Anonymous said...

Na ajue kusini haitakuwa kama jimbo la Katanga,DRC bali kama SUDANI KUSINI kinyume na hilo itakuw NILE DELTA,kwishanei!!!!