Saturday, December 8, 2012

MDAU DAUD CHARLES NA NASAHA ZAKE KUHUSU MAPENZI


YALIANZA kuumbwa maisha halafu mapenzi ndiyo yakafuata. Aliumbwa Adam, baadaye akaletewa Hawa kisha mapenzi ndiyo yakaanza. Hii ina maana kuwa maisha yalianza kwa upande wa Adam kabla ya mapenzi. Hili zingatia katika kutafsiri sura ya kule uendako Hata wewe jiulize, ulipozaliwa ulikuwa hujui mapenzi ni nini? Hapa sizungumzii mapenzi ya kawaida, yale ambayo mtu anaweza kuyapata kutoka kwa wazazi wake au ndugu zake wengine. Yanayotajwa hapa ni mapenzi katika maana yake halisi. Mapenzi ya ndani kabisa.
Yale ambayo huwafanya watu waziache familia zao za asili na kwenda kutengeneza nyingine. Nayazungumzia yale ambayo yanawafanya watu wanauana, wengine wanakunywa sumu. Yanayowatesa watu mpaka wanashindwa kula na kadhalika.
Swali ni moja; Kama iliwezekana kuishi bila mapenzi mpaka ulipofikisha umri wa utu uzima, iweje leo yakutawale mpaka ushindwe kujiendesha mwenyewe? Haipingiki kwamba mapenzi ni muhimu lakini hayapaswi kutawala ubongo wako. Utafeli haraka.
Mapenzi ni mazuri kwako endapo utaweza kuyamudu. Yakikushinda wewe ni mtumwa. Kaa, tuliza akili halafu tafakari. Baada ya hapo chukua hatua. Haijalishi umeshaathirika kiasi gani, muhimu kwako ni kuzingatia kwamba inawezekana kubadilika.
Japo unapenda mno, unajitahidi kuonesha unajali katika mazingira yoyote. Umemfanya mwenzako sawa na mboni yako kwa namna unavyomtunza. Kama yeye harudishi mapenzi unayompa, hajali na kukupa heshima kulingana na ile unayompa, angalia maisha yako kwanza.
Angalizo; Ukimng’ang’ania sana, atakugeuza punda. Atajipa kiburi kwamba anaweza kufanya lolote nawe utatii kwa sababu unampenda. Usidanganywe na imani zisizokuwepo, binadamu hawekwi kiganjani wala kwenye chupa. Una akili hai, tazama mbele pengine hapo si kwenye bahati yako.
Kama anashindwa kukuthamini kwa namna unavyompenda, hawezi kuyapenda maisha yako. Atakutumia atakavyo, akishatimiza malengo yake, atakuacha ukihangaika na dunia. Wakati huo yeye yupo na mtu wake anayempenda, atakuwa anakenua na kukucheka.
Akikaa na marafiki zake, atawaambia kwamba yeye ndiye alikuwa nyota yako, kwamba ulipokuwa naye maisha yako yalikuwa rahisi na hivi sasa umechoka baada ya kuachana naye. Hatazungumza jinsi alivyokutesa, akakuweka roho juu, akakusababishia maumivu ya moyo mpaka ukashindwa kutekeleza majukumu yako.
Usikubali muda wako upotee bure. Maisha yako ni ya thamani, yupo nawe leo lakini kesho inawezekana si wa kwako lakini maisha yatabaki kuwa yako kwa mazingira yoyote yale. Hoja yangu hapa ni kwamba mapenzi yasikutawale mpaka ukasahau maisha.
Wengi waliishia njiani, walijiaminisha wanapendana kutoka ndani ya kuta za nyoyo zao. Wakaahidiana kuwa hakuna kitakachowatenganisha. Siku yalipotimia, ahadi zote zikayeyuka. Hupaswi kung’ang’ania ulipo, bali yafaa ujiulize, je, hapo ndipo kwenye bahati yako?
Watu kwenye ndoa wameachana, si kwamba walipenda la hasha! Wachumba wanaishia njiani, vilevile marafiki walioamini wanachanua, wakapeana mkono wa kwa heri. Ni vizuri kukubali kwamba jitihada hazishindi kudura. Pamoja na mapenzi yako makubwa, unavyojali, unavyomheshimu kama si bahati yako hamuwezi kudumu.
Haijalishi utu wako ni wa thamani kiasi gani. Mzee Nelson Mandela ‘Madiba’, alitoa talaka kwa bibi yetu, Winnie. Waliishi miaka mingi, wakazaa watoto ambao wengine kwa sasa ni wakubwa kabisa. Baadaye akagundua Winnie si bahati yake, leo yupo kwenye ndoa na Graca Machel, maisha yanaendelea.
Kumbe Graca ndiye bahati ya Mzee Mandela. Ilivyo ni kwamba Winnie alitangulia kwa lengo la kukamilisha safari ya maisha ya babu yetu huyo anayeheshimiwa mno duniani. Chukua mfano huo, halafu jipe matumaini. Maisha ni matamu mno bila ya huyo wako ambaye si bahati yako.maishani

No comments: