STORY YA http://francisgodwin.blogspot.com
ZIKIWA zimepita siku takribani tatu toka ajali mbaya itokee katika kata ya Mseke katika wilaya ya Iringa vijijini mkoani Iringa na kupelekea vifo vya wato watano wa familia moja na mmoja kujeruhiwa vibaya , ajali nyingine mbaya imetokea katika kata hiyo ya Mseke katika barabara ya Iringa -Mbeya na kupelekea vifo vya abiria zaidi ya 10 huku wengine zaidi ya 42 wakijeruhiwa vibaya.
Huku baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni vibaka wakivamia eneo hilo na kujaribu kupora mali za majeruhi wa ajali hiyo wakati wakisogea eneo hilo kwa ajili ya kusaidia majeruhi na kunusurika kichapo kutoka kwa baadhi ya abiria ambao mbali ya kupata ajali hiyo walikuwa na nguvu ya kupambana na vibaka hao.i hilo.
Pamoja na vibaka kujitokeza eneo hilo bado wananchi waliofika eneo hilo zaidi ya 200 walilazimika kufanya maandamano kuwafuata askari polisi wa usalama barabarani waliokuwepo eneo hilo wakishiriki zoezi la uokoaji ,wakitaka askari hao kumbana mkandarasi wa kampuni inayoendelea na ujenzi wa barabara ya Iringa -Mafinga ili kutoa mitambo yake kwa ajili ya kusaidia kunyanyua basi hilo ambalo lilikuwa limeangukia shimoni ili kuokoa majeruhi waliofunikwa na basi hilo .
Mashuhuda wa ajali hiyo ambao walipata kuzungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu leo walisema kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa 8 za mchana na chanzo cha ajali hiyo ni kugoma kuingia gia na kufeli kwa breki wakati likijaribu kupanda mlima mdogo uliopo eneo hilo pamoja na ubovu wa basi hilo lenye namba za usajili T 803 APV Nissani mali ya Msanya Trans ambalo lilikuwa likitoka mjini Iringa kwenda Usokami wilaya ya Mufindi .
John Kalinga ni mmoja kati ya mashuhuda wa tukio hilo alisema kuwa basi lilikuwa likielekea Usokami na baada ya kufika katika eneo la Kichakani lilikosa mwelekeo kutokana na mwendo kasi ambao dereva wa basi hiyo alikuwa akiendanao na hivyo kuyumba na kupinduka .
Hata hivyo alisema kuwa mara baada ya ajali hiyo kutokea abiria wote zaidi ya 50 waliokuwemo walifunikwa na basi hilo na kufanyika jitihada mbali mbali kutoka kwa wasamaria wema na kuweza kuokoa majeruhi hao ambao walikuwa wamefunikwa na basi hilo.
Kwa upande wake mmoja kati ya majeruhi wa ajali hiyo alisema kuwa basi hilo ni bovu ila kila wakati askari wa usalama barabarani wamekuwa wakiliacha kuendelea na safari jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa wananchi wanaotegemea usafiri huo katika eneo hilo la Usokami wilaya ya Mufindi.
No comments:
Post a Comment