Wednesday, November 21, 2012

WIZARA KUKABILIANA NA SARATANI YA MLANGO WA UZAZI


Story ya Ahmad Nandonde , MUSOMA

WIZARA ya afya na Ustawi wa Jamii,imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa wa Saratani ya mlango wa uzazi unawakabili wanawake wengi nchini.

Kwa mujibu wa wizara hiyo wakina mama wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi wako katika hatari kubwa ya kupatwa na ugonjwa wa Saratani ya mlango wa uzazi.

Mwakilishi wa wizara ya Afya Dk Safina Yuma,ameyasema hayo mjini Musoma katika mkutano wa wataalam wa afya mkoani Mara ambao unalenga pia kutoa mafunzo kwa watalaam hao watakaoanza kutoa huduma hiyo kwa wanawake wa mkoa wa Mara.

Amesema kuwa wizara ya afya na ustawi wa jamii imeanza kuchukua hatua hiyo kwaajili ya kutoa tiba bure kwa wakinamama watakaogundulika kuwa na ugonjwa huo na wakiwa katika hatua za awali kabla ya tatizo hilo kuwa kubwa zaidi.

Mwakilishi huyo wa wizara ya afya alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali wamechukua hatua hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya wa ndani na nje ya nchi ili kunusuru maisha ya wanawake watakaogundulika kuwa na ugonjwa huo.

Kwa upande wake afisa mradi wa afya idara ya kinga Mtawa wa kanisa katoliki Sr Margaret Ishengoma,alisema kuwa ugonjwa huo wa saratani ya mlango wa uzazi ndio saratani inayoongoza kuua kwa akina mama walio wengi zaidi.

Amesema kuwa kati ya wanawake 100 wa wilaya ya Rorya katika kijiji cha Shirati waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi saba kati yao walibainika kuwa na vijidudu vya saratani ya mlango wa Uzazi huku watatu kati yao wakiwa tayari na ugonjwa wa saratani.

Kwa mujibu wa Sr Ishengoma,alisema kuwa kuanzia leo Novemba 21 watalaam hao kutoka hospitali ya mkoa wa Mara na vituo vya afya wataanza kufanya uchunguzi wa kina kwa wanawake katika hospitali ya mkoa wa Mara.


Uchunguzi huo unafanyika baada ya mkurugenzi wa mpango wa IMA world health Jim Cox kukabidhi vifaa vya uchunguzi kwa kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Mara Dk Omari Gamuya ambavyo vitatumika kwa kazi hiyo.

No comments: