Tuesday, October 2, 2012

MTWARA : WAANDISHI ZINGATIENI MAADILI


Story kutoka Blog ya msalichuma

WAANDISHI wa habari Mkoani hapa wamekumbushwa kuzingatia maadili ya kazi yao ili kuweza kuaminika katika kazi zao na jamii ambayo ndiyo mwajiri wao wa kwanza kiuwajibikaji.

Hayo yamebainishwa juzi katika warsha ya maadili ya uandishi wa habari pamoja na azimio la Dar es salaam juu ya uhuru na uwajibikaji wa vyombo vya habari ambayo yanaendelea kwa siku tatu katika ukumbi wa klabu ya waandishi wa habari ya Mtwara, ambayo yameandaliwa na baraza la habari la Taifa (MCT).

Bw. Deodatus Mfugale ni mmoja wa wawezeshaji ambaye alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuzingatia maadili ambapo huleta uandishi wa uwajibikaji, kukuza na kujenga taaluma, na ni mwongozo wa utendaji wa kila siku wa shughuli za kiuandishi.

Alisema kuwa ukizingatia misingi ya maadili utafanya kazi za kiuandishi kwa kujitawala mwenyewe bila kusukumwa na mtu mwingine lakini pia huleta ulinzi katika ufanisi wa maslahi yako na jamii kwa ujumla.

“Ukifanya kazi zako kwa kuzingatia maadili na misingi yake kunasaidia sana kwanza kukujenga wewe mwenyewe lakini pia jamii nzima inakuamini na isitoshe chombo unachokifanyia pia kinajenga uaminifu kwako na kwa jamii kinakuwa kioo chao” alisema Bw. Mfugale.

Aidha awali wakati wa kufungua warsha hiyo mwandishi nguli wa siku nyingi Bw.Chrysostom Rweyemamu aliwakumbusha waandishi wa habari wa Mtwara nguzo muhimu katika uandishi wa kuzingatia maadili ambazo alizitaja baadhi yake ikiwa ni ukweli, urari wa habari, usahihi na kutenda haki siku zote za kazi zako.

Aliwakumbusha pia kuwa kuna hatari ya uhuru wa habari kuweza kutoweka iwapo baadhi ya mambo  hayatafuatwa kwa uangalifu mkubwa ambapo miongoni mwayo maslahi duni kwa waandishi wa habari, kuwa na msimamo usioshaurika kwa viongozi na wamiliki wa vyombo vya habari, Rushwa, uelewa na ujuzi Mdogo, kufanya urafiki na Vyanzo vya habari lakini pia kuvunja maadili yenyewe.

Hata hivyo alibainisha kuwa kuna mtanziko na changamoto wakati wa kupata habari ambapo wakati mwingine mwanahabari unatakiwa kuwa makini wakati wa kutimiza majukumu yako na kubadilika kutokana na mazingira unayoyakuta katika eneo la tukio ili uweze kupata habari yako bila mgongano.

No comments: