Monday, September 24, 2012

ASASI ZATAKIWA KUACHA KUTEGEMEA WAFADHILI


STORY YA AHMAD NANDONDE , MARA

Asasi zisizo za Kiserikali Mkoani Mara zimetakiwa kuacha kutegemea wafadhiri wa nje na badala yake wafanye jitihada za kutafuta vyanzo vya mapato ili waweze kujitegemea katika shughuli zao za kila siku.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa kituo cha utoaji Elimu,Rasilimali na Utawala (ROMMA) Ruta Mutakyahwa kutoka Jijini Dar es salaam katika mafunzo yaliyoshirikisha asasi zipatazo 10 katika kujifunza mbinu mbalimbali za kupata rasilimali/fedha ili kuendeleza miradi ya maendeleo katika jamii.

Amesema kila asasi imeanzishwa ikiwa ina malengo yake na wafadhiri wanaojitolea kuzisaidia asasi hizo wamezikuta hivyo ni wajibu wa kila asasi kuhakikisha inajipanga ili kuweza kujiendesha ili wafadhiri pale wanapokosekana waweze kujiendesha bila kukwama katika shughuli zao.

Ruta ambaye ndiye anayeendesha mafunzo hayo kwa muda wa siku tano katika ukumbi wa kanisa la Anglicana dayosisi ya Mara ametoa ushauri kwa asasi ziweze kujitangaza kwa shughuli wanazozifanya ili kila mmoja aweze kuzifahamu kwani kutaongeza uwezo wa kufahamika katika jamii.

Kwa upande wake Mratibu wa Shirika la Maendeleo ya watu wa Bukwaya (UMABU) Burude Ndago ambao ndio waandaaji wa mafunzo hayo kwa ufadhili wa Shirika la Terre des Hommes-Netherlands la Nchini Huolanzi amesema baada ya kufadhiliwa na Mashirika mbalimbali kwa muda mrefu baada ya mafunzo hayo watajengeka uwezo zaidi katika kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato ili baadae waweze kujiendesha.

Amesema kwa kuanzia kabla ya kupewa mafunzo hayo tayari wanao mradi wa kusukuma maji kutoka katika Kijiji cha Etaro na kuyapeleka katika Kijiji cha Nyegina katika Wilaya ya Musoma Vijijini ambapo mradi huo utawasaidia kupata kipato ambacho kitawasaidia kupata fedha ambazo kwa kiasi fulani kitawasaidia katika kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

Ndago amesema wameandaa mkakati wa kuwafikia wale wote wanaotoka katika maeneneo ya Bukwaya walio katika sehemu mbalimbali ili waweze kuchangia Maendeleo katika eneo hilo ili jamii nzima iweze kufikiwa katika kutatuliwa masuala ya kijamii yanayowazunguka.

Mafunzo ya kujenga uwezo wa utafutaji rasilimali kwa mashirika hayo 10 ambayo ni washirika wa Terre des Hommes-Netherland yatafanyika kwa siku tano ambayo yatawasaidia washirika kuandika maandiko ya ndani na kuacha kuwategemea wahisani kutoka nje ya Nchi

No comments: