Thursday, July 12, 2012

NDUNGULILE ATAKIWA KUTHIBITISHA SHUTUMA DHIDI YA MADIWANI WA KIGAMBONI

Naibu Spika, Job Ndugai ameisoma barua ya madiwani wa kigamboni bungeni mjini dodoma muda mfupi  kabla ya kuhairishwa kikao cha asubuhi Bungeni leo, barua hiyo imehusu tuhuma walizorushiwa na Dkt. Ndugulile jana (alipokuwa akichangia bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), kwamba madiwani hao walipelekwa Bungeni baada ya kuhongwa na Wizara hizo.

Madiwani wenyewe ni hawa hapa Juma Nkumbi (Kibada), Dotto Msawa (Kigamboni), Albert Luambano (Tungi), na Suleman Mathew (Vijibweni).

Madiwani hao wanasema wanataka tuhuma hizo zithibitishwe Bungeni au waombwe radhi Bungeni.

Tayari Naibu Spika  Ndugai amesema atatoa kwa mbunge huyo Dkt. Ndugulile katika kikao cha leo jioni ili athibitishe au kukanusha maneno yake. MCHANGO WAKE UKO HAPA CHINI
MCHANGO WA MBUNGE WA KIGAMBONI MHE. DKT. FAUSTINE .E. NDUGULILE KATIKA BAJETI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI TAREHE 15 AGOSTI 2011

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ni rasilimali ya mnyonge, ni kitu pekee ambacho anacho. Ni lazima sasa tuwe na utaratibu mzuri na madhubuti kwa kuhakikisha kwamba matumizi ya ardhi yetu yanaratibiwa, yanasimamiwa na uwekezaji unaofanyika katika nchi yetu uwe wa makini.


Naomba nianze kutoa sababu kwa nini siungi mkono hoja hii.



Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kwanza ya kutounga mkono hoja, kule katika Kata ya Pembamnazi kuna mwekezaji anaitwa Amadori. Mwekezaji huyu kachukua eneo kubwa sana la Kata ya Pembamnazi. Hakuna maendelezo makubwa ambayo yanafanyika pale, wananchi wale wanalalamika, hawana sehemu za kulima wala kujenga makazi yao, nataka kujua mkataba ambao anao mwekezaji huyu ni wa aina gani, uhalali wa mkataba huo na kwa nini ardhi ile isitwaliwe na kugawiwa wale wananchi ambao wana shida kubwa sana ya ardhi? (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili, kwa nini siungi mkono hoja hii katika mradi wa viwanja 20,000 kule Kibada, wananchi wale waliuziwa viwanja na Serikali hii hii kupitia Wizara ambayo inawasilisha bajeti yake leo hii. Kuna maeneo pale Kibada wamepimiwa viwanja lakini barabara na miundombinu mingine haikutengenezwa. Wananchi wale wamejenga nyumba lakini hawana njia za kufikia katika makazi yao. Hii ni dhuluma kubwa sana ambayo inafanywa na upande wa Serikali. Nataka kujua mkakati ambao Wizara inao kuhakikisha kwamba wale wananchi wa kule wanajengewa zile barabara kwa sababu walipokuwa wanalipa zile gharama za viwanja walilipia pamoja na gharama za miundombinu. (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya tatu kwa nini siungi mkono hoja, kuna wananchi takriban 105 ambao walikuwa na maeneo yao, makazi yao na kujishughulisha katika masuala ya kilimo maeneo ya Dungu Farm nikiwemo mimi mwenyewe pamoja na wazazi wangu. Naomba ni-declare interest kwamba mimi na wazazi wangu tulikuwa na maeneo pale. Tathmini iliyofanyika watu walilipwa mazao lakini watu ambao walikuwa na nyumba na waliofanya maendeleo pale hawakulipwa hata senti tano. Sasa nataka kujua kupitia Waziri husika ni taratibu gani ambazo zitatumika ili wale watu waweze kupata haki zao za msingi ambazo wamekuwa wanazungushwa kwa muda mrefu. (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya nne kwa nini siiungi mkono hoja, katika eneo la Vijibweni, Wizara ya Ardhi bila kufuata utaratibu, imevamia eneo lile na kutaka kutwaa takriban heka 240 bila kushirikisha Viongozi, bila kufuata taratibu na sheria za nchi kwa pretext kwamba wanataka kujenga Bandari. Sasa kama kule Kurasini kunawashinda, kwa nini mnataka kuja Vijibweni na kuwahangaisha wananchi? Huu mpango ambao mnataka kuja nao, una fit namna gani katika Mji Kabambe wa Kigamboni? Cha kusikitisha zaidi katika suala kubwa na la msingi namna hii, Wizara inadiriki kutuma Maafisa wa ngazi za chini kwenda kukaa na kuongea na wananchi pasipo kufuata taratibu. Naomba zoezi hili lisitishwe na taratibu za msingi ziweze kufuatwa. Hata kwa suala la msingi kama upanuzi wa Bandari, lazima taratibu za msingi zifuatwe. Mheshimiwa Waziri naomba sana zoezi hilo lisitishwe ili utaratibu wa msingi uweze kufanyika.



Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya tano kwa nini siungi mkono hoja, katika eneo la Kisota, kuna viwanja 20,000 vilivyopimwa na Serikali, lakini watendaji wa Wizara ya Ardhi, wamepima na kutoa kwa wananchi viwanja vichache kuliko maeneo ambayo yamepimwa. Sasa hivi pale Kisota kuna mapori mengi kweli kweli, hali ambayo imepelekea kuwa na hali kubwa sana ya uhalifu.



Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri wa Wizara husika, wafanye audit ya maeneo yaliyopimwa na idadi ya viwanja vilivyotolewa kwa sababu wajanja wachache ndani ya Wizara ya Ardhi wanachokifanya sasa hivi, wanapita tena katika yale maeneo na kuanza kutoa kiwanja kimoja kimoja. Kwa hiyo, naomba hili suala lifuatiliwe, audit iweze kufanyika na yale maeneo ambayo tayari yamepimwa lakini viwanja havikutolewa basi hayo maeneo yaweze kutolewa kwa wananchi ambao wanahitaji.



Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya sita kwa nini siungi mkono hoja, ni suala la Mji mpya wa Kigamboni na nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wameniunga mkono katika suala hili. Suala hili ni kubwa na suala hili ni zito, lakini suala hili Serikali mnalichukulia kimzaha mzaha.



Wanakigamboni wanataabika tangu wameingia kifungoni Oktoba mwaka 2008 na hawana matumaini ya kutoka kifungoni. Hawajui tarehe ambayo mtawatoa kifungoni, Serikali imekuwa kimya mno na majibu ambayo yamekuwa yakitolewa ikiwa pamoja na yale ambayo yametolewa katika hotuba hii, kwa kweli hayaashirii kwamba Serikali inawatakia neema Wanakigamboni. (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kigamboni, hawawezi kuuza ardhi yao, hawawezi kuuza nyumba zao, hawawezi kuziendeleza na hawakopesheki. Kwa takriban miaka mitatu sasa hivi, hakuna kitu chochote cha maana ambacho kinaendelea pale Kigamboni na maswali ambayo Wanakigamboni wanayo na wangependa kupata majibu ni maswali manne tu. Mradi huu utaanza lini? Mradi huu utaanzia wapi? Haki zao za msingi ni zipi na hatima yao ni ipi? (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa miaka mitatu Serikali hii imekuwa inapiga chenga kutoa majibu ya maswali haya ya msingi. Nasikitika kusema kwamba sitaunga mkono hoja mpaka majibu ya haya maswali manne ya msingi yaweze kupatikana. (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, nitakubali mradi huu ikiwa tu mambo mawili yatafanyika; moja wananchi wa Kigamboni wanufaike na pili wananchi wa Kigamboni wasisumbuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kigamboni wamenituma, Serikali ilipotoa tamko ilisema kwamba ndani ya miaka miwili wangekuwa wameanza mpango wao, sasa wameshapita hiyo miaka miwili. Wananchi wa Kigamboni wamenituma, itakapofika tarehe 30 Juni, 2012 hawataki kusikia tena kuhusiana na masuala ya mradi huu. Naomba nirudie, wananchi wa Kigamboni wamenituma, kama Serikali haitakuja na mpango thabiti, itakapofika tarehe 30 Juni,2012, hawataki tena kuusikia mradi huu, chukueni mradi huo pelekeni sehemu nyingine yoyote, baada ya hapo wananchi wa Kigamboni hawautaki mradi na hawatatoa ushirikiano kwa Serikali katika suala hili. 
Ni vyema Serikali inapokuja na miradi kama hii, muwe mmeshajipanga, sio mnatoa zuio wakati wenyewe hamjajiandaa. Kuna matatizo ya msingi na nilipokuwa naangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 26 na 27, wanasema bado wako kwenye mchakato; wakati wananchi wa Kigamboni wanaumia, Serikali iko kwenye mchakato, wakati wananchi wa Kigamboni wanaendelea kuwa maskini, Serikali iko kwenye mchakato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe rai kwa Wabunge wenzangu, naomba mniunge mkono, naomba tusipitishe hii bajeti ya Wizara mpaka pale Serikali itakapokuja na majibu ya msingi, najua ndani ya Bunge hili Tukufu kuna Wabunge zaidi ya 50 ambao ni wakazi au wamewekeza katika Jimbo la Kigamboni, naomba waniunge mkono katika hili, tuwatetee wananchi wa Kigamboni, naomba bajeti hii isipite mpaka pale majibu ya msingi yatakapoweza kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema tena, kauli ambayo nimeitoa kwamba baada ya tarehe 30 Juni, 2012, kama Serikali hamtakuja na mpango thabiti ambao unaainisha na kujibu masuala ya msingi, naomba msije tena Kigamboni. Mimi nitakuwa wa kwanza kuwasimamia na kuwatetea wale wote ambao watakuwa wamevunja agizo la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu muwe makini, mkajipange, mje na mpango thabiti ambao utaonesha lini na wapi mnaanza na mnaanza na nini, haki za Wanakigamboni zitakuaje? Naomba niseme wananchi wa Kigamboni katika masuala ya fidia wanataka mambo matatu; kwa wale ambao hawatoweza, wapewe fidia yao na wahame na fidia iwe katika bei ya soko. Wale ambao watakuwa na uwezo wanataka kuingia ubia na wawekezaji na wengine ambao wana uwezo mkubwa zaidi wanataka kuyaendeleza yale maeneo yao wao wenyewe, watachukua fedha benki, watafanya hiyo kazi. Kwa hiyo, naomba utaratibu huo utumike, najua kabisa Mheshimiwa Waziri ana uzoefu mkubwa, wananchi wa Kigamboni wana imani ingawa majibu yake ya tarehe 31 Machi, 2011 hayakukidhi haja. Kwa hiyo, naomba arudi tena akiwa na majibu ya msingi katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, siungi mkono hoja.

No comments: