Thursday, July 12, 2012

BAHAKITA KUWASHITAKI MADAKTARI WALIO KWENYE MGOMO

Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania (BAHAKITA) limesema linakusudia kuwafungulia mashitaka Madaktari Mabingwa wote pamoja na Madaktari waliokuwepo kwenye Mafunzo kwa Vitendo (Interns) ambao walishiriki katika mgomo kwenye hospitali mbalimbali nchini na kusababisha wagonjwa kukosa huduma za matibabu huku wengine wakipoteza maisha yao.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya baraza hilo kukaa na Madaktari waliokua katika mgomo na kukubaliana kuwa waiombe radhi Serikali pamoja na wananchi kisha warudi kazini, lakini Madaktari hao wamekiuka makubaliano hayo na kuendelea na mgomo jambo lililoonyesha kwamba hawakuwa tayari kupata suluhu.

Katibu wa BAHAKITA, Said Mwaipopo amesema wameshauriana na Wanasheria wao na kuamua kuwafungulia kesi ya mauaji Madaktari hao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam tarehe 16 Julai 2012.


Amesema, “kwa tukio zima jinsi lilivyokwenda, limeonyesha kwamba Madaktari hawataki wala hawana shida tena ya kurudi kazini kwa sababu ni wazi kwamba kuna mtu yuko nyuma yao wanaemtumikia. Sisi kama Watanzania, sehemu ya jamii tumekaa na Wataalamu wetu wa Sheria tumekubaliana kwamba Jumatatu tunakwenda kufungua kesi Mahakamani kwa Madaktari wote waliogoma wakati wamesomeshwa na kodi zetu na Serikali yetu imewasomesha, tutawafungulia kesi ya kusababisha mauaji pale Muhimbili, kwa hiyo tunachofanya hivi sasa ni kwenda pale Muhimbili kwa mganga mkuu kuchukua orodha ya watu waliopoteza maisha.”

Source : millardayo.com
GAZETI LA MTANZANIA WAMEANDIKA HIVI...
Akijibu hoja hizo, Katibu wa MAT, Dkt. Edwin Chitage amesema hawaogopi kufikishwa mahakamani na kwamba wao waliwapokea viongozi hao kwa nia njema wakiamini ni viongozi wa dini.

“Kama wamesema watatufikishwa mahakamani wao waende halafu tutakutana nao…sisi tuliwapokea kwa nia njema kabisa kwa sababu walituomba wenyewe..lakini baada ya kikao cha Jumamosi siku ya Jumapili wakatupigia simu kuomba tukutane nao,sisi tulikutana nao lakini cha kushangaza walitueleza kwamba wamepigiwa simu na mtu wa Ikulu akiwataka kutuambia kwamba inabidi tuandike barua ya kuomba msamaha halafu tuwape wao ili waipeleke…sisi tulishangaa jambo hili… sisi hatutafanyi kazi hiyo,” alisema Dkt.Chitage.

No comments: