Mheshimiwa
Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kunipa afya njema na kuniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge hili,
kuwasilisha maoni na mapendekezo ya Kambi
ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2012/2013 kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za
Bunge, kanuni ya 99(7).
Mheshimiwa
Spika, napenda kutoa shukrani za
kipekee kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Aikael
Mbowe (Mb) kwa imani yake kubwa kwangu na kuniteua kuwa Waziri Kivuli wa Wizara
hii. Nami natoa ahadi kwake kuwa nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu na kwa jinsi Mwenyezi
Mungu atakavyonijalia, natumaini kwa uwezo wake nitatimiza matarajio yake
kwangu.
Mheshimiwa
Spika, napenda kuishukuru familia
yangu kwa imani na uvumilivu waliouonesha wakati wote ambao ninakuwa mbali nao
nikiwa katika shughuli za ujenzi wa
Taifa. Maombi yenu ni muhimu.
Mheshimiwa
Spika, nitakuwa sijatenda haki
kwa wananchi wa Jimbo la Karatu kama sitawashukuru kwa imani kubwa waliyo nayo
kwangu na kwa chama changu cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), nami
nawaahidi kuwa nitaitunza na kuiheshimu imani yao kwangu, kuendelea
kushirikiana nao kuleta maendeleo katika Jimbo na Wilaya yetu na mwisho
kukifanya CHADEMA kuwa chama kiongozi kwa wilaya na kwa nchi nzima katika
uchaguzi wa mwaka 2015. Asanteni Sana.
Mheshimiwa
Spika, napenda kuwapongeza
wananchi wa vijiji vya Kiburumo, Kongwa na Nyarutanga waliofanya uchaguzi wao
jana na kauli moja kupitia sanduku la kura wameipatia CHADEMA ushindi mkubwa wa
kuongoza Serikali katika vijiji hivyo, chini ya Mwenyekiti Juma Hamza-Kiburumo,
Juma Iddi Kibali- Kongwa na Changanya Midenge-Nyarutanga. Hizo ni mvua za vuli
masika inakuja. Tunasema hivi (The sun
never set in CHADEMA) CHADEMA hakuna kulala mpaka kieleweke.
Mheshimiwa
Spika, mwisho lakini kwa umuhimu
mkubwa nawashukuru waheshimiwa wabunge wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja
na Kamati nzima ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa ushauri na ushirikiano
mkubwa walionipatia katika utendaji wangu kazi ndani na nje ya Bunge. Asanteni
sana!
2.
Umuhimu
wa Ulinzi na Usalama katika Nchi Yetu
Mheshimiwa Spika,
ni ukweli usiopingika kwamba nchi inapokuwa salama ndipo watu wake huweza
kuishi kwa amani na utulivu. Amani na utulivu vinapotawala katika nchi, watu
wake huwa na uhuru wa kufanya shughuli mbalimbali kwa ajili ya kujipatia
mahitaji yao ya kila siku na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi yao.
Mheshimiwa Spika,
Tanzania imekuwa ikisifika duniani kwa kudumisha amani hadi kuitwa “Kisiwa cha
Amani”. Mwezi Agost 2000, Rais Mstaafu wa Marekani Bill Clinton aliuita Mji wa
Arusha kuwa ni “Geneva of Afrika” kutokana na mji huo kuwa ni kitovu cha
usuluhishi na upatanishi wa migogoro ya kimataifa. Hii ni sifa kubwa kwa
Tanzania kwa kuaminiwa na mataifa mengine kuwa ni “Mlinzi wa Amani”.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inataka Serikali ielewe kwamba amani haipatikani kwa kutokuwa
na vita katika nchi tu, ila amani huongezeka kama wananchi wanapata mahitaji
yao ya msingi ambayo huwafanya waishi maisha ya staha. Amani huendelea kuimarika
na kukomaa iwapo nchi itakuwa inatawaliwa kwa misingi ya haki, sheria na usawa katika
mgawanyo wa rasilimali za nchi kwa faida ya wananchi wake wote.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inatambua na inaheshimu vyombo vya Ulinzi na Usalama katika
kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu. Kambi inatambua vilevile kuwa ni kazi
ngumu zaidi kuwalinda watu wasio na
amani mioyoni mwao kutokana na kukosa haki zao za msingi. Hivyo ni dhahiri kuwa
amani ya kweli ya nchi yetu itakuwepo na itaendelea kuwepo endapo Serikali
iliyopo madarakani na Serikali itakayokuwa madarakani itatafuta kwanza amani ya
nafsi za watu kwa kuwatimizia mahitaji yao ndipo kazi ya ulinzi wa amani katika
nchi itakuwa rahisi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa Jeshi ni chombo huru ambacho hakitakiwi
kuwa na itikadi ya chama chochote cha siasa au kuwa na mlengo wowote wa imani
ya kidini. Lakini kwa masikitiko makubwa ni kwamba sasa hivi wanasiasa wameanza
kuingilia mchakato mzima wa uajiri wa wanaojiunga na jeshi hilo. Hili limekuwa
linaharibu sifa kubwa ya jeshi letu, jambo linaloweza kugawa jeshi kwa misingi
ya uchama. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuachia Jeshi lenyewe mchakato
mzima wa uajiri kwa kulingana na matakwa ya jeshi lenyewe kuliko shinikizo la
wanasiasa kuingiza watoto wao, jamaa zao na watoto wa rafiki zao.
3.0 Mapitio ya Utekelezaji wa
Bajeti 2011/2012
Mheshimiwa Spika,
kwa ujumla fedha iliyoidhinishwa kwa Wizara hii ilitolewa kwa kiwango cha kuridhisha
isipokuwa fedha ya maendeleo ilikuwa ni asilimia 40% tu ya fedha
iliyoidhinishwa na bunge. Hii haileti taswira nzuri, kwani maendeleo katika
wizara hii yako chini ya wastani.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Kamati ya Bunge ya tarehe 7 Juni, 2012 ni kwamba
fungu 57 Ulinzi lilipokea shilingi bilioni 129.
Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 30
ni fedha maalum (ring fenced) kwa ajili ya kununua meli za kivita, ambao
mchakato wake umeanza na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2012. Kambi ya
Upinzani tunaitaka serikali ihakikishe kuwa ahadi hii inatimia kwa maslahi ya
ulinzi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Ulinzi kwa kamati ya bunge changamoto
inayoathiri bajeti ya Wizara ya Ulinzi ni kuchelewa kutolewa kwa fedha kutoka
hazina kwa wakati, jambo ambalo limesababisha kushindwa kutekeleza baadhi ya
majukumu yake kwa wakati.
Mheshimiwa Spika,
tuapenda kusisitiza kwamba Serikali iepuke urasimu kwa mambo yanayohusu ulinzi
na usalama wa nchi yetu. Kama bajeti imepitishwa na bunge, jambo la kufanya ni
kutoa fedha hizo kwa wakati ili kutekeleza majukumu yaliyopangwa.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa zilizopo gharama za kuondoa matrekta bandarini kwa mwaka
2011/2012 zilitumika jumla ya shilingi 4,048,325,331.
Hakika fedha hizi ni nyingi sana kwa kazi ya kuondoa tu matrekta bandarini.
Kambi ya Upinzani,
inataka kupata majibu ni Matrekta mangapi yaliondolewa na gharama ya kuondoa
trekta moja ilikuwa kiasi gani? Na gharama hizo zilikuwa ni kwa ajili ya
shughuli gani haswa?
4.0
Vyombo
vya Ulinzi na Usalama na Wajibu wake kwa Wananchi
Mheshimiwa Spika, madhumuni
ya vyombo vya ulinzi na usalama ni kuwalinda raia wote wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Ila kinyume na dhamira hiyo, uzoefu hapa kwetu Tanzania inaonekana
kama vile vyombo hivi ni kwa ajili ya kuilinda Serikali. Ni kweli kwamba vyombo
hivi vina jukumu pia la kuilinda Serikali, lakini kuna baadhi ya matukio ambayo
inaonekana dhahiri vyombo hivi vikiacha jukumu la kuwalinda raia na badala yake
kuwapiga na kuwanyanyasa raia.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya “Tanzania Land Alliance” (TALA) ya tarehe
30 Machi 2012 inasemekana kwamba mnamo
tarehe 17 Machi, 2012 askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliwaua
kwa kuwapiga risasi watu watano na kuwajeruhi wengine watatu katika eneo la Maguba, Kitongoji cha Lupemenda, Kijiji cha
Kiwale, Kata ya Igawa, Tarafa ya Malinyi
wilayani Ulanga.
Mheshimiwa Spika,
katika tukio hili watu waliopoteza maisha ni Sanyiwa Ndahya (28), Lutala Ndahya
(45), Kulwa Luhende (48), Ng’erebende Nchambi Lukuresha (26) na Kashinje
Msheshiwa (35).
Waliojeruhiwa ni Zina Msheshiwa (29),
Msheshiwa Ndahya (53), Khama Chisongelile Tiga (30).
Mheshimiwa
Spika, taarifa
ya uchunguzi wa TALA inaonesha kuwa wanajeshi waliohusika hawakuwa wakifanya
doria kama ilivyodaiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga isipokuwa walivamia na
kupora mifugo, fedha na mali ya wananchi
na wakawa wanadai shilingi 10,000/= kwa kila kichwa cha mfugo ili wawaachie.
Siku hiyohiyo walipora kiasi cha shilingi 205,000/= kutoka kwa watu wawili.
Mheshimiwa
Spika, si nia ya
Kambi ya Upinzani kuwasilisha Ripoti nzima ya tukio hili hapa, nia yetu ni
kutaka kupeleka ujumbe kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwamba vitendo kama hivi vinalivunjia
Jeshi letu heshima kwa kiwango kikubwa sana mbele ya wananchi wa Tanzania na
hata katika medani za kimataifa.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inasikitishwa sana na
majibu ya kejeli yaliyokuwa yakitolewa na Mkuu wa Wilaya na Katibu Tawala wa
Wilaya ya Ulanga kwa wachunguzi wa TALA
kwamba mauaji ya wananchi hao ni jambo la kawaida kama ajali nyingine. Mkuu wa
Wilaya alilinganisha mauaji hayo na ajali ya gari iliyowapata wanamuziki wa
FIVE STAR TAARAB iliyotokea Mikumi mwaka 2011.
Mheshimiwa Spika,
majibu kama hayo licha ya kuendelea kuwaumiza kisaikolojia ndugu wa marehemu na
majeruhi, ni ishara mbaya kwa wananchi kwamba Serikali haiwajali wananchi wake[1].
Mheshimiwa
Spika, taarifa hizi
za tukio la Jeshi la Wananchi kuwanyanyasa na kuwaua raia hazijengi
taswira nzuri kwa Jeshi letu na kwa Raisi wa nchi ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi na Uslama.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inataka Serikali ielewe kwamba wananchi wameipa dhamana ya
kumiliki nguvu za dola kwa madhumuni ya kuwalinda na kuwatetea. Kitendo cha
nguvu hizi kutumika kuwaua na kuwanyanyasa wananchi ni matumizi mabaya ya dola
na kwa maana hiyo Serikali sasa imekosa sifa ya kumiliki nguvu za dola.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili kama ina taarifa za
matukio ya Askari wa Jeshi la Wananchi kuwapiga, kuwanyanyasa na kuwaua raia
wanyonge wasio na silaha. Pili Serikali ieleze mbele ya Bunge hili hatua zilizochukuliwa
kwa askari waliohusika na mauaji ya Ulanga.
5.0 Ahadi za Serikali na
Utekelezaji wake katika Wizara ya Ulinzi na JKT Kuimarisha Kamandi ya Jeshi la Wanamaji
Mheshimiwa Spika,
Serikali iliahidi kuimarisha kamandi ya Jeshi la Wanamaji ili kukabiliana na vitendo
vya uharamia. Aidha, serikali iliahidi kununua meli za kivita kwa ajili ya
ulinzi wa Exclusive Economic Zone. Majibu ya Serikali kuhusu ahadi hii ni kwamba
wizara ipo katika hatua nzuri ya kuimarisha uwezo wa kulinda eneo la Exclusive
Economic Zone bila kutaja mambo mahsusi iliyofanya. Pia kwenye ununuzi wa meli
za kivita, Serikali inajibu kuwa upo mchakato ikiwa ni miaka miwili tangu ahadi
hiyo itolewe.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaamini kwamba katika mambo ambayo hayahitaji kabisa propaganda za kisiasa ni pamoja na ulinzi na
usalama wa nchi yetu. Ni aibu kwa Serikali kuahidi jambo muhimu hivi kwa ulinzi
wa nchi na kutolitekeleza kwa wakati. Ni
aibu vilvile kwa Serikali kukiri kuwa na uwezo mdogo wa kufanya operesheni
katika eneo la bahari kuu.
Mheshimiwa Spika, udhaifu
katika kuimarisha kamandi hii ni dhahiri kumelisababishia taifa hasara kubwa
kwani kumekuwa na wizi mkubwa wa rasilimali samaki. Meli iliyonaswa ikiiba
samaki katika ukanda wetu wa bahari kuu, ni sehemu tu ya matukio ya kihalifu, ila
matukio kama haya ya wizi wa rasilimali samaki yako mengi ila Serikali
inashindwa kuyakabili kwa kukosa meli ya kivita kwa ajili ya kufanya doria
katika eneo la bahari kuu.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na kamandi yetu ya Wanamaji kutokuwa na vifaa vya kutosha na vya
kisasa, makampuni yanayotafuta mafuta na gesi kwenye ukanda wa bahari kuu yameamua
kuajiri makampuni binafsi ya ulinzi yenye silaha nzito kutoka nje ya nchi,
jambo ambalo ni la hatari kwa usalama wetu kama taifa.
Kambi ya Upinzani
tunaitaka serikali kupiga marufuku mara moja makampuni ya nje kuingia na silaha
nzito kwenye bahari yetu na tuimarishe kamandi ya Jeshi la wanamaji mara moja
ili itumike kufanya shughuli hiyo ya kutoa ulinzi kwenye makampuni haya na hiyo
itasaidia kuifanya bahari yetu kuwa salama.
6.0 Kuimarisha na Kukarabati Maghala ya Silaha
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali iliahidi kuimarisha na kukarabati maghala
makubwa na madogo ya kuhifadhi risasi, milipuko, mabomu na vifaa vingine. Maelezo
ya Serikali katika ahadi hii ni kwamba JWTZ linaendelea na jitihada za
kukarabati maghala hayo ingawa tatizo ni kwamba fedha zinazopatikana
hazitoshelezi kukarabati na kuboresha maghala yote kwa wakati unaostahili.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inasikitishwa sana na majibu mepesi ya Serikali kwa mambo
mazito ya kiusalama kama haya. Wote tunakumbuka madhara makubwa yaliyotokana na
milipuko ya mabomu katika maghala ya silaha huko Mbagala na hatimaye Gongo la
Mboto, Dar es Salaam. Raia walipoteza maisha, wengine walipoteza mali na nyumba
zao kuharibiwa vibaya na wengine kubaki na ulemavu wa kudumu katika viungo
vyao. Madhara haya yaliwapata wanajeshi wetu vilevile.
Mheshimiwa Spika,
katika mazingira ya hatari namna hii, ni aibu kwa Serikali kusema kuwa haina
fedha za kukarabati maghala ya Silaha lakini fedha za kulipa posho zisizo na
tija hazikosekani. Hii ni ishara kuwa Serikali haijali usalama wa wanajeshi
katika maghala hayo na raia walio jirani na maghala hayo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inasisitiza tena kwamba masuala yanayohusu ulinzi na usalama
wa nchi yetu siyo ya mzaha hata kidogo. Serikali ihakikishe kwamba fedha za
kutekeleza mikakati ya kiulinzi na usalama zinatolewa kwa wakati na mikakati
hiyo itekelezwe kwa wakati uliopangwa.
7.0 Hali ya Usalama wa Mipaka ya
Tanzania
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa hotuba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliyowasilishwa
hapa Bungeni mwezi Julai, 2011 ni kwamba
mipaka ya nchi yetu ni shwari isipokuwa katika mpaka wa kusini ambapo tatizo la
mpaka katika Ziwa Nyasa halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Spika,
kuendelea kuwa na tatizo katika Mpaka wa Ziwa Nyasa si dalili nzuri kwa usalama
wa nchi yetu. Aidha, kuendelea kwa tatizo hili bila ufumbuzi wa mapema,
kutadumaza uhusiano wetu na nchi jirani ya Malawi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa ya kiini cha mgogoro wa mpaka
katika Ziwa Nyasa, na hatua ambazo zimechukuliwa hadi sasa kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa
Spika, kumekuwepo
na malalamiko mengi toka kwa wananchi waishio maeneo ya mipakani mwa mkoa wa
Kagera na nchi jirani kuwa wanavamiwa na makundi yanayosadikiwa kuwa ni askari
wa majeshi na kuwaibia mali zao na mahali pengine kuingiza makundi makubwa ya
mifugo katika mashamba yao.
Hivyo basi, Mheshimiwa
Spika, taarifa kuhusu usalama na ustawi wa mkoa wa Kagera unaonekana kuwa sio salama. Hili
ni eneo ambalo Serikali imeshindwa kulitawala kiasi kwamba Umoja wa Mataifa
unatambua kwamba hili ni eneo hatari kiusalama.
Mheshimiwa Spika, suala hili la kuvamiwa kwa wananchi na kutishiwa ni la muda mrefu
na Kamati mbalimbali za Kudumu za Bunge
zimekwenda na kujionea hali halisi lakini kwa masikitiko makubwa ni kwamba hali
ya usalama wa wananchi bado iko mashakani. Aidha, kwa sasa inakadiriwa kuna wahamiaji haramu wapatao 35,000 na mifugo yao zaidi ya
200,000 katika mistu ya hifadhi na maeneo mengine katika mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa mbali ya wahamiaji
hao haramu, kuna tatizo kubwa katika ziwa Tanganyika ambapo kila mara wavuvi
katika ziwa hilo wameporwa na wanajeshi wenye silaha nzito kutoka nchi jirani.
Hivi, kwa matukio haya yote, kama nchi
tunapata wapi uthubutu wa kusema kuwa
mipaka yetu na wananchi wetu ni salama?
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kupitia
Jeshi letu kuweka ulinzi katika mipaka ya mkoa
wa Kagera hasa kwenye Ziwa
Victoria pamoja na kutoa ulinzi wa uhakika kwenye ziwa Tanganyika.
Aidha,
tunaitaka serikali ilieleze Bunge hili ina mkakati gani wa makusudi wa
kuwalinda wananchi wa Mkoa wa Kagera dhidi ya matishio kutoka kwa wahamiaji
hawa haramu ambao wameishawaua au kuwajeruhi rai kadha licha ya kuwapora maeneo
yao.
8.0 Jeshi la Kujenga Taifa
Mheshimiwa Spika,
pamoja na umuhimu wa Jeshi la Kujenga Taifa katika kujenga ukakamavu, nidhamu
na uzalendo miongoni mwa vijana wetu, jeshi hili pia limekuwa ni kiungo muhimu
katika kukuza uchumi wa nchi kutokana na shughuli mbalimbali za uzalishaji
mali.
Hata
hivyo, kufuatia kusitishwa kwa programu ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa
mujibu wa Sheria mwaka 1994 nidhamu miongoni mwa vijana imeshuka sana, uzalendo
pia umeshuka na ndio maana vijana wengi wanashabikia vitu vya nje kuliko vya
nchi yao; ukakamavu umeshuka na uvivu miongoni mwa vijana umeongezeka.
Mheshimiwa Spika,
tayari hofu ya kuwa na Taifa la watu wazembe, wavivu, wasio wazalendo imeanza
kujitokeza. Hata hivyo, hofu hii imeanza kutulizwa kidogo baada ya hotuba ya
Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na
makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa
mwaka 2012/2013. Katika hotuba hiyo ukurasa wa 51, Waziri Mkuu alisema …. . “Jeshi la Kujenga Taifa limekamilisha
ukarabati wa makambi 10 ya Jeshi la Kujenga Taifa yenye uwezo wa kuchukua
vijana 20,000 kwa wakati mmoja. Kwa
mwaka 2012/2013, jumla ya Vijana 5,000 wataanza tena kujiunga na Jeshi la
Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria”.Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika,
ni jambo jema kuwa Serikali imetambua umuhimu wa vijana kujiunga na Jeshi la
Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria kwa vijana wetu waohitimu kidato cha sita.
Kambi ya Upinzani inataka kufahamu kama zile sababu za kusitisha mafunzo ya JKT
kwa vijana zimekwisha kabisa? Lengo la swali hili ni kuhakikisha kwamba
utaratibu huu wa kujiunga na JKT unaoanza tena unakuwa ni endelevu na sio wa
msimu. Pili, Kambi ya Upinzani inataka kujua vilevile kuwa Serikali ina mpango
gani kwa wale vijana waliokosa mafunzo hayo tangu yalipositishwa?
8.1
Viwanda, utafiti na uendelezaji wa Teknolojia Jeshini
Mheshimiwa Spika, teknolojia
ni jambo la msingi na muhimu sana katika kujenga jeshi la kisasa. Kabla ya kuwa
na teknolojia ya kisasa suala la kwanza ni kuwa na rasilimali watu ambayo inao uwezo
wa kubuni au kupokea na kuitumia teknolojia ya kisasa.
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya Mheshimiwa Waziri[2],
alisema kuwa “……… ni kuendeleza utafiti na maendeleo ya teknolojia ya kijeshi katika
viwanda vya kijeshi vya mashirika ya Mzinga na Nyumbu”, mwisho wa kunukuu.
Kwa nukuu hiyo inaonyesha kuwa utafiti ni kwa ajili ya vifaa vya jeshi tu. Hii
ni kutolitumia vyema Jeshi kwa manufaa ya wananchi na nchi kwa ujumla kama
wenzetu wa mataifa yaliyoendelea wanavyotumia majeshi yao.
Mheshimiwa Spika,
katika hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2008/2009 iliongelea
kuhusu umuhimu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia[3];
naomba kunukuu: “Ili taasisi zetu za
ulinzi zifanikiwe zinahitaji kuwa wazi, kuwa wavumbuzi na kukubali kubadilika
na kuendana na maendeleo ya kisayansi na teknolojia. Mtaalamu wa fizikia
Rutherford alinukuliwa akisema kwamba “we
are short of money so we must think”. Wanajeshi wetu wafahamu kuwa tuna tatizo
la rasilimali fedha, hivyo inawalazimu kuwa wavumbuzi na wabunifu zaidi
kukabiliana na changamoto zilizopo hivyo tunahitaji vipaji binafsi. Mwisho
wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, vipaji
binafsi vya watendaji vinatafutwa toka ngazi za chini na kulelewa. Utaratibu
huu ulikuwepo miaka ya nyuma, lakini kwa sasa nchi yetu imejikuta ikipoteza
vijana wengi wenye vipaji kukimbilia nchi za nje na sasa wanafanya kazi huko.
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge Jeshi letu lina mkakati gani
wa kuibua vipaji na kuviendeleza ili kwa miaka ijayo tuwe na wanasayansi vijana
wa kufanya tafiti sio tu kwenye nyanja za kijeshi bali pia kwenye nyanja za
kilimo, madawa, mitambo, mifugo n.k
Mheshimiwa Spika,
kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika Nyanja nzima za ulinzi
na usalama, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutenga ardhi ya kutosha kwa
ajili ya Jeshi kufungua Makambi yanayoweza kuhamishika kulingana na mahitaji ya
wakati huo kuliko kugawa ardhi kiholela kwa wageni ambao hadi sasa hatujui watu
hawa wana nia gani na Taifa huko mbele.
8.2
Jeshi na Utekelezaji wa Kaulimbiu
ya “Kilimo Kwanza”
Mheshimiwa Spika, ni
jambo linalotia faraja kuona kwamba Jeshi letu la Kujenga Taifa linatekeleza
kwa vitendo Kaulimbiu ya Kilimo Kwanza. Kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika Bunge la Bajeti, Julai 2011 ni kwamba
katika mwaka 2010/2011 Jeshi la Kujenga Taifa lilima ekari 1,625 za kilimo cha
mbegu bora kwa matarajio ya kuvuna tani 1,039 za mbegu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika,
pamoja mkakati huu mzuri, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuboresha mfumo
huu usiwe wa kuzalisha mbegu peke yake bali pia kuwe na mikakati ya kujikita
zaidi kwenye kilimo cha mazao ya chakula
ili kuinusuru nchi na majanga ya njaa na pia kudhibiti mifumuko ya bei
inayotokana na ukosefu wa chakula nchini. Kambi ya Upinzani inataka Serikali vilevile
kutanua wigo wa shughuli za Jeshi la Kujenga Taifa kwa wananchi. Jeshi la
Kujenga Taifa lishirikiane na Wananchi kwa maana ya kuwaelimisha namna ya
kuendesha shughuli za kiuchumi na kijamii, mfano kilimo na utunzaji wa
mazingira kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika,
ili kutekeleza mkakati huu wa kuanzisha mahusiano ya Jeshi la Kujenga Taifa na
Wananchi katika shughuli za uzalishaji mali, Kambi ya Upinzani inapendekeza
kwamba wale watakaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, wawe wanafanya mafunzo ya
vitendo (internship) kwa wanachi, katika maeneo yatakayokuwa yamechaguliwa
ikiwa ni sehemu ya ukamilisho wa mafunzo yao.
8.3
Utunzaji wa Mazingira
Mheshimiwa Spika,
Jeshi la Kujenga Taifa linashughulika pia na utunzaji wa mazingira ikiwa ni
utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira. Hata hivyo, kwa mujibu wa Hotuba ya
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa aliyoitoa mwezi Julai, 2011, utunzaji
wa mazingira umefanyika tu katika makambi na maeneo ya Jeshi kwa kupanda miti
na kuhifadhi misitu katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inatoa pendekezo kwa Jeshi la Kujenga Taifa kuendesha
OPERESHENI MAALUMU YA KUPANDA MITI NCHI NZIMA kwa awamu kwa kushirikiana na
wananchi. Operesheni hii iendeshwe kwa utaratibu ule ule kwa watakaojiunga na
JKT kufanya mafunzo ya vitendo wakishirikiana na wananchi katika kutunza
mazingira.
Mheshimiwa Spika,
kwa kufanya hivyo, Taifa hili litaepushwa na unyemelezi wa jangwa na athari za
tabia nchi zinazotokana na uharibifu wa mazingira. Kambi ya Upinzani inataka
mabadiliko katika Jeshi la Kujenga Taifa ili kazi zake ziwe ni za Kujenga Taifa
kweli na sio kujenga na kuendeleza makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kama
ilivyo sasa.
8.4 Kashfa ya Ufisadi kwa Maafisa wa JKT
Mheshimiwa Spika,
katika hotuba ya Kambi ya Upinzani mwaka 2011/2012 tulizungumzia suala la SUMA
JKT kuingia mkataba wa ununuzi wa
matrekta na mfanyabiashara ambaye alihusishwa na matukio ya ufisadi. Hata hivyo
kwa mujibu wa taarifa rasmi za bunge za tarehe 13 Julai 2011 wakati waziri wa
ulinzi anafanya majumuisho ya bajeti ya wizara yake alikanusha habari hizi.
Alisema, na nanukuu:
“…..hakuna ukweli hata kidogo kwamba SUMA JKT
imeingia mkataba na mfanyabiashara, aliyemtaja Mheshimiwa Selasini”. Mwisho wa
kunukuu.
Mheshimiwa Spika,
magazeti ya Uhuru, Nipashe, Jambo Leo ya tarehe 3 Julai 2012 yana taarifa
kuhusu Maafisa wa Jeshi la Kujenga Taifa ambao pia ni wajumbe wa bodi ya
SUMA-JKT kushtakiwa mahakamani kwa ufisadi wa matumizi mabaya ya madaraka na
kuhamisha shilingi bilioni 3.8 kutoka katika akaunti ya Tanzania Korea
Partnership (TAKOPA) kwenda kwenye akaunti ya SUMA-JKT.
Mheshimiwa Spika,
taarifa hizi zinaashiria kuwa uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa una matatizo ya
uadilifu. Sasa kama Jeshi lenye jukumu la kujenga Taifa hili linaongozwa na
viongozi wa namna hii, Watanzania wategemee nini kwa vijana wanaojiunga na JKT?
Kambi ya Upinzani inashauri kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
afanye ukaguzi maalum katika Jeshi la kujenga Taifa na hususan SUMA- JKT. Pili,
Serikali itoe maelezo katika bunge hili kuwa ina mpango gani wa dharura wa
kusafisha taswira ya Jeshi la Kujenga Taifa ambayo imechafuka mbele ya jamii.
9.0
Maslahi ya Watumishi katika Jeshi la Wananchi na Jeshi la Kujenga Taifa
Mheshimiwa Spika,
ni welewa wa kawaida kwamba ili mtu aweze kufanya kazi kwa ufanisi ni lazima
apate mahitaji yake ya msingi yatakayomwezesha kuishi maisha ya staha. Kwa
kuzingatia jambo hili, na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa kazi za majeshi
yetu katika kulinda usalama na kujenga taifa letu, Kambi ya Upinzani
inapendekeza maboresho ya maslahi ya watumishi katika jeshi yafanyike ili
kuwapa motisha ili wafanye kazi kwa bidii zaidi.
Mheshimiwa Spika, Kambi
ya Upinzani inaitaka Serikali, kuandaa mazingira mazuri ambayo yatawasaidia
wastaafu wa Jeshi kupata nafasi ya kufanya shughuli zitakazowapatia kipato cha
ziada tofauti na mafao yao ya uzeeni. Kwa mfano Serikali iwakopeshe wanajeshi
wastaafu fedha ili waanzishe vyuo vya mafunzo kwa vijana watakaotumika katika
ulinzi shirikishi na ambao wataajiriwa katika makampuni binafsi ya ulinzi na
kutoa huduma ya ushauri wa kitaalamu (consultancy
services)kwa makampuni binafsi ya ulinzi.
10.0. Jeshi na Migogoro ya Ardhi na Fidia kwa Wananchi
Mheshimiwa Spika,
kwa muda mrefu sasa kumekuwa na migogoro mingi ya Ardhi baina ya wanajeshi na
wananchi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Migogoro hii imepelekea kuwepo kwa
mvutano baina ya wananchi na jeshi letu kwa upande mmoja na viongozi wa
wananchi kwa upande wa pili.
Mheshimiwa Spika,
mifano ya migogoro hiyo ni kama ile ya
Ilemela , Tarime, Kunduchi na maeneo mengine mbalimbali ambayo yamekuwa
yakilalamikiwa na wabunge kwa muda mrefu. Mara zote Serikali imekuwa ikitoa
majibu kuwa itawalipa fidia wananchi ili waweze kuondoka na kuyapisha maeneo
hayo kwa ajili ya Jeshi.
Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka huu wa fedha 2012/2013 zimeombwa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kulipa fidia
ya ardhi maeneo ya Mapinga, Shinyanga na Arusha.
Kambi ya upinzani
inaona kuwa hakuna nia ya dhati ya kumaliza migogoro hii baina ya jeshi letu na
wananchi kwani kiasi kilichotengwa ni kidogo mno kutosha kulipa fidia na hata
maeneo yaliyotengewa fedha ni mawili tu. Tunaitaka serikali iwe na nia ya dhati
ya kuwalipa wananchi fidia ili kumaliza migogoro hii ambayo inawafanya wananchi
walichukie jeshi lao.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
…………………………………….
Mch.
Israel Yohana Natse (Mb)
Msemaji
Mkuu Kambi ya Upinzani-Wizara ya Ulinzi ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
16.07.2012
[1] Chanzo: REPORT ON TALA-MEDIA JOINT MISSION ON
LAND RIGHTS FOR AGRO-PASTORALISTS AND FARMERS IN ULANGA DISTRICT (Gathering facts in response to
the killings of 5 people done by Tanzania Peoples Defense Forces in Maguba
area, Malinyi Ulanga 17th March, 2012)
[2]
Hotuba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha
2008/2009 uk. 20
[3]
Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya
Upinzani kwa mwaka wa fedha 2008/2009. Aya ya 14
No comments:
Post a Comment