Sunday, June 10, 2012

MADAKTARI WAIPA SERIKALI SIKU 14

MadakaaADAKTARI wameikataa ripoti ya mazungumzo baina ya kamati yao na serikali kwa madai kuwa haijakidhi makubaliano yaliyofikiwa na sasa, wametoa wiki mbili kwa makubaliano hayo kufikiwa.

Aidha madaktari hao wamesema ikiwa muda huo utapita bila marekebisho wanayotaka kipengele kwa kipengele kufanyika, kamati irejee kwao nao wataamua nini cha kufanya.

Akizungumza na gazeti la HabariLeo baada ya mkutano huo wa ndani wa marejesho ya ripoti ya majadiliano kwa madaktari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt. Namala Mkopi alithibitisha kukataliwa kwa taarifa hiyo na kuzuiwa kuisaini.


“Kilikuwa ni kikao cha ndani, hivyo tuliyozungumza huko siwezi kukueleza ila kwa ujumla ni kwamba, taarifa wameikataa na wamekataa tusiisaini na kwa kuwa hatua hii ya mgogoro ilikuwa kwenye mazungumzo na serikali, wametuagiza kazi ya kufanya ndani ya wiki mbili tukamilishe,” alisema Dk Mkopi.

Taarifa hiyo ilikuwa katika hatua ya mwisho ya kusainiwa na upande huo wa madaktari ambao ndiyo walalamikaji ikiwa wamekubaliana na serikali baada ya vikao visivyopungua sita kufanyika katika kutafuta muafaka wa suala hilo.

Akifafanua zaidi alisema, madaktari wamewataka kutafuta majibu ya mwisho kabisa kuhusu mgogoro wao huo ulio katika meza ya mazungumzo yaliyotarajiwa ripoti hiyo kumaliza mazungumzo hayo baada ya juhudi za serikali kumaliza mgomo wa takribani mwezi mmoja uliofanyika nchi nzima.

“Wametutaka tufanye uendelevu wa yale mambo tuliyokubaliana, kujaribu kumaliza mgogoro, lengo letu awali ilikuwa ni kuhakikisha mgomo hautokei tena, ila ndio wenyewe wamekataa ripoti ya serikali ya mazungumzo yetu na kukataa tusisaini mpaka ifanyiwe marekebisho. Baada ya wiki mbili, wametaka mrejesho,” alisema Dkt. Mkopi. 

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya mkutano huo, majadiliano yalifanyika mara baada ya Mwenyekiti (Dkt. Mkopi) kuweka taarifa mezani mapema asubuhi na vipengele vya posho na mishahara viliongoza mjadala mzima.

Katika mazungumzo hayo, Serikali iliongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, ofisi inayoshughulikia masuala ya umma ikiwemo mishahara na timu ya madaktari iliongozwa na Dkt. Mkopi kama mwenyekiti.

Miongoni mwa madai yao ni pamoja na kulipwa posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi, posho za kazi katika mazingira magumu, kuongezwa kwa posho za kuitwa kazini kwa dharura, kupewa nyumba au posho ya nyumba, mikopo ya magari, kadi za kijani za Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) na kupandishwa mishahara kwa zaidi ya asilimia 100.


Source: http://www.wavuti.com

No comments: