HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI- OFISI YA RAIS MIPANGO MHE.
CHRISTINA LISSU MUGHWAI (MB), KUHUSU TAARIFA YA HALI YA UCHUMI KWA MWAKA 2011
NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2012– 2013
Utangulizi
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mujibu wa Kanuni ya 96(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007, naomba
kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu taarifa ya hali ya
uchumi kwa mwaka 2011/2012 na mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13
kama ulivyowasilishwa na Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na
Uratibu.
Mheshimiwa
Spika,
Kwanza
kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na
kutuwezesha kuwa hapa siku hii ya leo. Kwa masikitiko makubwa napenda kutoa
salaam za rambi rambi kwa familia, ndugu, jamaa, wapenzi na viongozi wote wa CHADEMA kwa msiba mkubwa wa
kuondokewa na mmoja wa waasisi wa chama chetu Mzee Mohamed Ally Nyanga “Bob”
Makani. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, na aipe familia yake
moyo wa Subira na Ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Spika,
Pongezi
za pekee ziwaendee viongozi wote, wanachama na wafuasi wote wa CHADEMA kwa kazi
kubwa na yenye mafanikio makubwa wanayoendelea kuifanya katika kukiimarisha na
kukijenga chama nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, Ili Mpango wowote ufanikiwe katika
malengo yaliyokusudiwa, ni lazima kuwe na dhamira ya dhati ya kuutekeleza.
Kambi ya Upinzani imebaini kwamba Serikali haina dhamira ya dhati ya
kuutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano kwa kushindwa kutenga
fedha za kutosha kugharamia miradi ya maendeleo kama ilivyoainishwa katika
Mpango. (Rejea Mpango wa Maendeleo 2012/13:
na Bajeti ya Serikali kama ilivyowasilishwa)
MAPITIO YA MWENENDO WA UCHUMI WA TAIFA
1. Ukuaji wa Pato la
Taifa
Mheshimiwa Spika,
Takwimu
za Serikali zinaonyesha kuwa mwaka 2011 Pato halisi la Taifa lilishuka kwa
kiwango cha asilimia 0.6 ikilinganishwa na mwaka 2010. Kwa maana kwamba 2011 ukuaji
wa Pato la Taifa ulikuwa asilimia 6.4 na mwaka 2010 ulikuwa ni asilimia 7.0.
Sekta ndogo ya mawasiliano ndiyo iliyoongoza kwa ukuaji wa asilimia 19.0, sekta
ya uzalishaji viwandani asilimia 7.8, sekta ya kilimo ilipungua kutoka asilimia
4.2 mwaka 2010 hadi asilimia 3.9 mwaka 2011.
Mheshimiwa
Spika,
Sura ya kwanza ya kitabu cha
Hali ya Uchumi wa Taifa Katika mwaka 2011 inakiri kwamba kulikuwa na ukuaji
mdogo wa pato la taifa. Hata hivyo, Serikali inamlaumu Mwenyezi Mungu kwa
kusababisha ukuaji huo usioridhisha wa pato la taifa: ”Kiwango kidogo cha ukuaji kilitokana na hali mbaya ya ukame iliyojitokeza
katika sehemu mbalimbali nchini ambapo imeathiri sekta ya kilimo.” Hata hivyo,
Mheshimiwa Spika, katika hali inayohitaji maelezo zaidi kutoka Serikalini,
Serikali inadai - katika aya ya 234 ya kitabu hicho hicho – kwamba: “Mwaka 2011,uzalishaji wa mazao ya chakula hususani ngano, mihogo,
maharage, ndizi na viazi uliongezeka ikilinganishwa na mwaka 2010 kutokana na
hali nzuri ya hewa na mtawanyiko mzuri wa mvua kwa ustawi wa mazao.” Mkanganyiko
huu ni dalili ya ukosefu wa umakini katika kuandaa taarifa muhimu za Serikali
na unaitia Serikali hii aibu!
Mheshimiwa Spika,
Kama
ilivyokuwa kwa mwaka 2010, serikali imeendelea kukiri kuwa ukuaji huu wa pato
la taifa haukupunguza umaskini kama ilivyotarajiwa kwasababu sekta zilizokuwa
haraka hazitoi ajira kwa wananchi wengi hasa waliopo vijijini ambao wanategemea
kilimo. Ni lini sasa serikali itaweka bayana mikakati inayotekelezeka
itakayowafanya wananchi waliowengi wanufaike na ukuaji huo wa uchumi? Waziri
Kivuli wa Fedha atakaposoma bajeti mbadala ataweka bayana mikakati
itakayoelekeza ukuaji wa uchumi kwa wananchi walio wengi na hasa wa kipato cha
chini na waishio vijijini.
2. Mfumuko wa Bei
Mheshimiwa Spika,
Kuongezeka kwa kasi kwa bei za
bidhaa na huduma kuliathiri sana Bajeti ya Serikali ya mwaka unaokwisha. Wakati Mfumuko wa Bei mwezi Julai mwaka wa
Fedha 2011/2012 ulikuwa asilimia 13, ulifikia asilimia 19.2 mwezi Novemba mwaka
huo wa Fedha. Hii maana yake ni kwamba, Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na
Bunge mwezi Juni 2011, ilipunguza uwezo wake wa kununua bidhaa na huduma kwa
takribani asilimia 6. Hii ni sawa na shilingi 780 bilioni kuyeyuka katika Bajeti katika
kipindi cha miezi Minne tu ya utekelezaji wa wake. Aidha
kufikia mwezi Desemba 2011, mfumuko wa bei ulifikia
asilimia 19.8 na mfumuko wa bei za chakula ulipanda hadi asilimia 25.6 kutoka
asilimia 6.3 Desemba 2010. Kutokana na kasi hiyo ya ukuaji wa Mfumuko wa Bei ni
dhahiri kwamba, sehemu kubwa ya Bajeti na hasa Bajeti ya Maendeleo ilishindwa
kutekelezeka.
Mheshimiwa Spika,
Hali ni mbaya zaidi kwa
wananchi kwani Mfumuko wa Bei za vyakula umekua kwa kasi kubwa mno. Ofisi ya
Takwimu imeonyesha kuwa wakati mfumuko wa Bei za vyakula ulikuwa asilimia 14.8
mwezi Julai, umefikia asilimia 24.7 mwezi Novemba 2011. Ukilinganisha na bei za
vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya
robo kati ya Novemba 2010 na Novemba 2011. Jumla ya vyakula
ambavyo mwananchi alinunua kwa shilingi 10,000 mwaka 2010, sasa atanunua
kiwango kile kile kwa shilingi 12,500. Bei za vyakula zimeongezeka
kwa kiwango hiki wakati kipato cha mwananchi kipo palepale. Mwathirika mkubwa wa
mfumuko wa bei ni mwananchi wa kawaida mwenye kipato cha chini.
Mheshimiwa Spika,
Ukiangalia kwa undani utakuta
mfumuko wa bei wa bidhaa kama mchele, sukari, nyama na samaki umekua maradufu.
Bei ya mchele imekua kwa asilimia 50, sukari asilimia 50, nyama asilimia 30 na
Samaki kwa takribani asilimia 40. Bidhaa hizi zote ni muhimu sana kwa mahitaji
ya chakula kwa wananchi walio wengi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa Serikali hadi muda huu imeshindwa kutoa
suluhisho la mfumuko wa bei ambao kwa kiasi kikubwa unachangiwa na bei za
vyakula. Serikali imeendelea kutoa sababu za bei kupanda bila kutoa majawabu.
Wananchi wamechoka kusikia sababu za mfumuko wa bei, wanataka kuona hatua
mwafaka zinachukuliwa kudhibiti mfumuko huu wa bei na hivyo kupunguza ukali wa
maisha kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
kwa mwaka wa fedha 2008/2009 kwa mujibu wa Hansard za Bunge tulipendekeza
yafuatayo:
“Mheshimiwa Spika, bei
za mafuta ya dizeli kwa makao makuu ya mikoa kwa tarehe 16-31 mei 2008 ilikuwa
kama ifuatavyo kwenye baadhi ya mikoa, Dar es
salaam 1,654.09 petrol na 1,884.89 kwa dizeli kwa lita huku mafuta ya taa
yakiwa 1,488.24 kwa lita, Kagera 1,748.93 petrol na 1,979.73 kwa dizeli kwa
lita huku mafuta ya taa yakiwa 1,583.08 kwa lita, Kigoma 1,930 petrol na 2,080
dizeli kwa lita huku mafuta ya taa 1,550 kwa lita na hali katika mkoa wa Mbeya
1,850 petrol na 2,000 dizeli kwa lita huku mafuta ya taa 1,500 kwa lita na
Zanzibar diseli ni wastani wa shs.1850 . Kati
ya wastani wa bei ya 1800/- kwa lita. Hizi ni bei za mijini, vijijini ambako
kuna umasikini uliokithiri na mahitaji ya nishati kwa ajili ya usafiri,kilimo
n.k. wastani wa bei ni Tshs.2,200/- kwa lita.
Hivyo
hivyo kwa bei za bidhaa nyingine kama cement,mabati n.k. Je, umasikini
utapungua wakati sehemu kubwa ya jamii inaishi vijijini. Mhe.Spika,Nchi kama
India bei za vijijini na mijini ni tofauti na ndio maana wamemudu kuzalisha
chakula cha kutosha”.
Mheshimiwa Spika,
Asilimia kubwa ya
watanzania wanaishi maeneo ya vijijini na vipato vyao ni vidogo. Haiingii
akilini kuwa bei za bidhaa na huduma za vijijini ni kubwa kuliko za mijini kama
kweli kuna nia ya kuwakwamua wananchi walio wengi wa vijijini.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani tunazidi
kusisitiza ushauri tulioutoa kipindi hicho kuwa ufanyiwe kazi, kwani asilimia kubwa ya watanzania wanaishi maeneo
ya vijijini na vipato vyao ni vidogo. Ni lazima sasa Serikali ipange bei maalum
za nishati kwa maeneo ya vijijini ili kuongeza uzalishaji na kuwapunguzia
gharama za maisha. Tuige mfumo huu kutoka nchi ya India ambao ulifanikiwa kwa
kiasi kikubwa.
3. Thamani ya Shilingi ya Tanzania
Mheshimiwa Spika,
Thamani
ya shilingi ya Tanzania imeendelea
kushuka ukilinganisha na fedha za kigeni, na hii inatokana na kukosekana kwa
mikakati thabiti ya kuhakikisha kuwa shilingi inaimarika kwenye soko na hasa
kutokana na sera mbovu za kiuchumi na usimamizi usio makini. Kushuka kwa
thamani ya Shilingi licha ya kupanda kwa mauzo yetu nje kwa sekta zote mbili
tunazotegemea sana (Madini na Utalii) kunaacha maswali mengi kuhusiana na
chaguo letu kuhusu Hifadhi ya Fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
ya Upinzani inaunga mkono ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Mashirika ya Umma kwamba sasa Benki Kuu ya Tanzania ianze kutunza sehemu ya
Hifadhi ya nchi katika Dhahabu. Benki Kuu inunue dhahabu kutoka kwa wachimbaji
wadogo na pia tuangalie uwezekano wa kutoza sehemu ya mrahaba katika sekta ya
madini kama ‘dhahabu safi’ (‘pure gold’).
4. Misaada na mikopo
ya Kibajeti
Mheshimiwa Spika,
Serikali
katika hotuba yake inasema kuwa kwa kipindi cha Julai 2011 hadi Machi 2012
ilipokea misaada na mikopo toka nje ya
asilimia 85 ya makadirio ya Tshs.bilioni 869.4 kwa kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
ya Upinzani inaelewa kabisa umuhimu wa fedha hizo toka nje, lakini ni kweli
fedha hizo zinatumika kuleta maendeleo kwa wananchi? Fedha hizo zilikopwa kwa
miradi gani hasa ya maendeleo?
Mheshimiwa Spika,
Mambo
hayo yote ambayo Kambi ya Upinzani itayapa msukumo katika Hotuba ya bajeti yake
mbadala ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa utatuzi wake ni lazima uhusishe
mtazamo mpana wa kiuchumi.
5. Deni la Taifa
Mheshimiwa Spika,
deni
la taifa linaonekana kuongezeka kwa kasi ya ajabu sana na hivyo kupelekea Taifa
kuwa na mzigo mkubwa sana wa madeni. Kwa mujibu wa Hotuba ya Bajeti ya Mipango
iliyowaslishwa Bungeni Tarehe 14.06.2012, Uk. 12, aya ya 25 inaonyesha kuwa deni
la Taifa limeongezeka kwa asilimia 15.4 kati ya March 2011 hadi March 2012
kutoka Tsh trilioni 17.6 hadi Tshs
Trilioni 20.3. Cha kushangaza ni kwamba serikali inatuambia kuwa deni hilo
linahimilika ilihali wananchi ambao ndio walipaji wa deni hilo wako hohehahe
kimaisha. Aidha, hoja kwamba deni hili linahimilika inatia shaka kwa vile deni
letu la nje halijawahi kupungua katika kipindi cha miaka kumi iliyota.
Mheshimiwa Spika,
Katika
hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mwaka wa fedha 2011/2012
tulipendekeza ufanyike uchunguzi Maalumu kwenye Deni la Taifa ili Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali atuambie madeni haya tunayokopa kwa kasi ya
namna hii tunayapeleka kweye miradi gani (Matumizi ya Madeni) na namna gani
tunaweza kudhibiti Deni la Taifa. Mwaka
huu pia tunarejea ushauri huo huo kwani mwenendo wa kukopa unatakiwa ujulikane
na uwekewe uangalizi maalumu.
MAENDELEO
KATIKA SEKTA ZA KIUCHUMI NA KIJAMII
Mheshimiwa
Spika,
Sekta za kiuchumi na kijamii
ndiyo kioo cha kutolea tathmini ni jinsi gani utendaji wa Serikali kwa kipindi
kilichopita ulivyofanikiwa au ulivyoshindwa. Maoni ya Kambi ya Upinzani katika
hili ni kwamba Serikali imeshindwa vibaya kuwaonyesha wananchi kuwa ipo na
inafanya kazi.
Mheshimiwa
Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inahoji Serikali kushindwa kutoa fedha kwa wizara za Kisekta kama ambavyo
zilikuwa zimetengwa na Bunge hili ili kufanya kazi. Lakini kwa masikitiko
makubwa fedha hizo zilishindwa kupelekwa zote na hivyo kusababisha miradi na
huduma za jamii kutokutekelezwa. Hili limejidhihirsha kwa Kamati sita za Bunge
za Kudumu kukataa kupitisha bajeti za kisekta kwa kutaka maelezo ya utekelezaji
wa bajeti iliyopita. Madai ya Kamati
yalikuwa ni kwanini miradi haikutelezwa na pia ni kwanini fedha zinazoombwa ni
kidogo kuweza kutekeleza miradi na huduma katika sekta hizo; kabla ya kupitisha
bajeti hii mpya.
Mheshimiwa
Spika,
Katika bajeti ya mwaka
2011/2012 sekta ya miundombinu ilitengewa jumla ya asilimia 20.6 ya jumla ya
bajeti ya Tshs trilioni 13.5, na watanzania wote watakuwa ni mashahidi, je Reli
ya kati imekarabatiwa pamoja na Injini zake na mabehewa kama tulivyoambiwa
katika mwaka wa fedha unaoisha? Huku ni kulidanganya bunge pamoja na wananchi.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa maelezo zaidi kuonyesha jinsi
gani Serikali imeshindwa kutekeleza bajeti iliyopita yatatolewa na wasemaji
wakuu katika sekta mbali mbali za Uchumi
na Kijamii.
1. Uwezeshaji wananchi Kiuchumi
Mheshimiwa
Spika,
Kwa mwaka 2011 Serikali
inasema iliendelea utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
kupitia mifuko ya Uwezeshaji na ilitoa mikopo yenye thamani ya Tshs. Bilioni 7.1
Kambi ya Upinzani inauliza uwezeshwaji huu unafanywa kwa kutumia kigezo gani?
Kutokana na utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini
(REPOA), kuhusu upeo wa elimu kwa wananchi wanaoishi vijijini ambao
wanajihusisha na ujasiria mali. Asilimia 16.2 hawana elimu ya shuleni bali
elimu isiyo rasmi, asilimia 69.5 wana elimu ya msingi na asilimia 14.3 wana
elimu ya Sekondari au elimu ya juu.
Mheshimiwa
Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inauliza kwa viwango hivyo vya elimu, je uwezeshaji wa kutoa fedha bila ya
kutoa mafunzo ya biashara unaweza kuleta tija? Hii ni kutokana na ukweli kwamba
idadi kubwa ya watanzania wanaishi vijijini, hivyo uwezeshaji kiuchumi wa namna
yoyote ile ni lazima uangalie hali halisi kwa wananchi waishio vijijini. Bila mkakati wa kutoa elimu Kambi ya Upinzani
inahesabu kuwa haya ni matumizi ambayo hayakufanyiwa tafiti na hivyo ni upotevu
wa fedha za walipa kodi.
2. Miradi ya Kitaifa ya Kimkakati
Mheshimiwa Spika,
Kabla
ya kuangalia miradi ya kitaifa ya kimkakati,
naomba kunukuu ukurasa wa 92
kifungu cha 4.3.1 katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano toleo la kiswahili
kama kama ambavyo ulipitishwa na kuwekewa Azimio na Bunge lako tukufu kama
ifuatavyo: “kwa kuelewa kuwa wakati wote
kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa
inatenga asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya
kugharamia bajeti ya maendeleo kila mwaka.”
Mheshimiwa
Spika,
Kwa maana rahisi kulingana na
nukuu hiyo ni dhahiri kuwa Serikali haina fedha, kwani makusanyo yote ya mapato
ya ndani ni Tshs. Trilioni 9.08 wakati Matumizi ya Kawaida ni Tshs. Trilioni
10.6.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali imeainisha miradi ya
Kitaifa ya Kimkakati ambayo italeta maendeleo ya haraka hususani katika
kuchochea maendeleo ya maeneo mengine na hivyo kuongeza ajira, kukabiliana na
matatizo ya kiuchumi yaliyopo sasa na pia kuongeza pato la Taifa. Uk. wa 25 aya
ya 57 katika Hotuba ya Serikali ya taarifa ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo wa
Mwaka 2012/2013 inaeleza miradi husika.
Aidha ukiangalia Hotuba ya Waziri wa Fedha kuhusu makadirio ya mapato na
matumizi kwa mwaka 2012/2013 Uk.46 aya 78 (a) (i) inasema benki ya Exim China
itatoa mkopo wa Dola za Marekani 1,225.3 utakaosimamiwa na TPDC. Cha kushangaza
ni kuwa kwenye kitabu cha Miradi ya Maendeleo fedha hizo hazionekani, japokuwa
TPDC ni taasisi ya Serikali.
Mheshimiwa
Spika,
Huu ni udhaifu mkubwa katika
mfumo wetu wa bajeti, kwani unawafanya wabunge wasijiridhishe ni nini
wanapitisha. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inapendekeza kwamba Taasisi zote za
umma yakiwemo mashirika taarifa zao za mapato na matumizi kwa mwaka wa bajeti
ziwekwe kama viambatanisho kwenye Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka husika.
Mheshimiwa
Spika,
Aya ya 78(a) (ii) katika
kifungu kinachohusu Usafirishaji na Uchukuzi, Serikali imetenga kiasi cha Tshs.
Trilioni 1.382.9 lakini kati ya fedha hizo Fedha zinazohusiana na Reli ya Kati
ni Tshs. Bilioni 134.16 tu, na Wizara ya Uchukuzi imetengewa Fedha za Maendeleo
Tshs.Tshs. Bilioni 252.8. Fedha zote zinazobaki ni kwa ajili ya Wizara ya
Ujenzi.
Mheshimiwa
Spika,
Mgawo wa fedha kwa ajili ya
kuwekeza katika Reli ya Kati ambayo ni mojawapo ya Injini za uchumi zilikuwa
hazitoshi na ndiyo sababu kuu kwa Waheshimiwa wajumbe kushindwa kuipitisha
bajeti ya Wizara hiyo.
Mheshimiwa
Spika,
Kumekuwa na hadaa kubwa sana
kwa watanzania inayofanywa makusudi kwa wale waliopewa dhamana ya kuhakikisha kuwa
wananchi wanapata huduma stahiki kulingana na kodi wanazolipa. Kitendo
kilichofanywa na Waziri wa Uchukuzi, kuwaeleza wananchi akiwa katika Mkutano
Jangwani kuwa Reli imepewa fedha za kutosha kununua Injini za kisasa na
kutandaza mataruma ya kisasa na kupanda treni kutoka Dar kuja Dodoma ni hadaa
kubwa inayotuumiza sisi wote kama nchi.
Mheshimiwa
Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
kwa miaka yote ya nyuma tumekuwa tukisisitiza umuhimu wa Reli ya Kati na
tumetenga fedha za kutosha kwa Reli ya Kati katika bajeti mbadala kama
itakavyosomwa na Msemaji Mkuu wa Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa
Spika,
Katika miradi ya Kilimo kama
ilivyoainishwa katika aya ya 60 ya Bajeti ya Hali ya Uchumi na Mpango, kwa
kuoanisha na lengo la uwekezaji huo wa kuongeza ajira. Kambi ya Upinzani inaona
kuwa uwekezaji huu utasaidia kujenga matabaka badala ya kuhamasisha vijana
kuingia katika kilimo watakuwa ni manamba katika mashamba hayo na mwisho
umasikini utazidi.
Mheshimiwa
Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inasisitiza kuwa uwekezaji ufanywe kwa Serikali kuwawezesha wananchi kumiliki
mashamba madogo madogo kwenye maeneo ya mabonde husika kwa kutengeneza
miundombinu na kuikodisha kwa wamiliki wa mashamba hayo. Nchi nyingi
zinazozalisha mpunga kwa wingi kama Vietnam hawatumii mashamba makubwa bali ni
mashamba madogo ili watu wengi wajihusishe na kilimo badala ya mtu mmoja tu na
wengine kuwa vibarua.
MPANGO WA MAENDELEO
WA TAIFA 2011/12 – 2015/16
MAPITIO YA
UTEKELEZAJI WA MPANGO KWA MWAKA 2011/12 NA 2012/13
Mheshimiwa Spika,
Katika
mjadala kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliowasilishwa Bungeni mwezi
Juni mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji, pamoja na mambo
mengine, uwezo wa utekelezaji wa Mpango huo kama ulivyopitishwa na Bunge hili
tukufu. Kwa mfano, wakati Mpango unadai kwamba gharama zinazotarajiwa kwa
utekelezaji wake ni takriban shilingi trilioni 8.6 kwa mwaka au shilingi
trilioni 42.98 kwa kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango, katika
mwaka wa kwanza wa utekelezaji wake, Serikali ilitenga shilingi trilioni 4.9 tu.
Katika kujaribu kuhalalisha mgawo huo pungufu, Serikali ilijitetea kwamba mwaka
2011/2012 ulikuwa ni mwaka wa mpito wa utekelezaji wa Mpango.
Mheshimiwa Spika,
Fedha
zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
kwa mwaka huu wa fedha zinathibitisha kwamba kauli ya Serikali kwamba mwaka
2011/2012 ulikuwa mwaka wa mpito kwa utekelezaji wa Mpango ilikuwa na lengo la
kuwahadaa Watanzania. Hii ni kwa sababu, shilingi trilioni 4.5 zilizotengwa kwa
ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2012/2013 sio tu ni
pungufu ya gharama tarajiwa ya shilingi trilioni 8.6 za kutekeleza Mpango kwa
mwaka, bali pia ni pungufu ya fedha zilizotengwa kwa ajili hiyo kwa mwaka ulioitwa
wa mpito! Ni wazi kwa hiyo – kama Serikali yenyewe ilivyosema kuwa “Mpango huu
(ni) kipimo cha ufanisi wa Serikali na uchumi kwa ujumla” – kwamba Serikali hii
ya CCM haijawa na ufanisi wowote katika utekelezaji wake wa Mpango na katika uendeshaji
wake wa uchumi kwa ujumla!
Mheshimiwa Spika,
Serikali
imeshindwa sio tu katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa ujumla, bali
pia imeshindwa kutekeleza ahadi yake yenyewe kwa Bunge hili tukufu. Kwa mujibu
wa Mpango, “… Serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga angalau asilimia 35 ya
makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo
kila mwaka.” Kauli hii ya Serikali ilitiliwa nguvu na Azimio la Bunge hili
tukufu la tarehe 8 Juni 2011. Hata hivyo, Serikali ilianza mwaka wa kwanza wa
utekelezaji wa Mpango kwa kushindwa kutekeleza ahadi kwani ilitenga shilingi
trilioni 1.87 au asilimia 26.2 ya mapato yote ya ndani yaliyokadiriwa kuwa
shilingi trilioni 7.13.
Mheshimiwa Spika,
Hadithi
ya mwaka huu ni mbaya zaidi kuliko ya mwaka jana. Hii ni kwa sababu, kati ya takriban
shilingi trilioni 9 ambazo ni makadirio ya mapato ya ndani kwa mwaka huu wa
fedha 2012/2013, Serikali imetenga shilingi trilioni 2.2 au asilimia 24.4 ya
mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo. Hii ina maana
kwamba badala ya Serikali kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Mpango
ikilinganishwa na ulioitwa ‘mwaka wa mpito’, Serikali hii ya CCM imepunguza
ufanisi ikilinganishwa na makadirio ya mwaka huo wa mpito licha ya kwamba
makadirio hayo yalikuwa pungufu ya lengo la Mpango na kinyume cha Azimio la
Bunge. Kwa ushahidi huu, ni wazi kwamba Serikali hii hii, ya chama hiki hiki,
haina uwezo au nia ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
licha ya kuwa na nyuso tofauti katika safu za Serikali hiyo hapa Bungeni!
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwamba Bunge hili tukufu lisimamie Azimio
lake la tarehe 8 Juni mwaka jana kwa kukataa kuipitisha bajeti hii na kuitaka
Serikali iongeze kiasi cha fedha za ndani zilizotengwa kwa bajeti ya maendeleo
kufikia shilingi trilioni 3.15 ambayo ni asilimia 35 ya mapato yote ya ndani
kwa mwaka huu wa fedha 2012/2013. Kama bajeti yetu mbadala itakavyoonyesha, inawezekana
sio tu kufikisha kiwango hiki bali pia kukizidisha endapo Serikali itakuwa
makini katika ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato ya ndani.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba kama serikali iliyopo madarakani
inashindwa kusimamia Mpango wa Maendeleo ambao umezinduliwa kwa mbwembwe nyingi
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupitishwa na Bunge hili tukufu,
ni wazi kuwa Serikali hiyo haipaswi kuendelea kuaminiwa na wananchi kwamba ina
uwezo au nia ya kusimamia maendeleo yetu na uchumi wa taifa letu. Serikali hii
inapaswa kupumzishwa kwa manufaa ya nchi yetu ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Spika,
Bajeti
mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya mwaka jana ilipendekeza kupunguza
misamaha ya Kodi kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa; kupunguza kodi na tozo
kwenye Mafuta ya Petroli na Dizeli ili kupunguza mfumuko wa bei; kupunguza
matumizi ya Serikali kwa kuondoa posho za vikao kwa watumishi na viongozi wote
wa umma; na kuelekeza fedha zaidi kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu
ya Juu. Kati ya mapendekezo hayo, Serikali ilitekeleza pendekezo la kuongeza
fedha kwa Bodi ya Mikopo. Serikali ilipuuza au kushindwa kutekeleza mapendekezo
mengine yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani ndio maana matatizo
yanayowakabili wananchi yameendelea kuongezeka na hali yetu ya kiuchumi kwa
ujumla imezidi kuwa mbaya kuliko kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mwaka huu wa fedha, Kambi Rasmi ya Upinzani Upinzani, sambamba na kurejea
mapendekezo yake ya mwaka jana, inapendekeza mambo yafuatayo:
1. Kuanzia sasa, misamaha yote ya kodi lazima iidhinishwe na Bunge hili
tukufu kupitia Kamati yake ya Fedha na Uchumi ili kuhakikisha kwamba haizidi
asilimia moja ya Pato la Taifa;
2. Kuongeza bajeti ya maendeleo hadi kufikia asilimia 35 ya mapato ya ndani
na kuelekeza nyongeza hiyo kwenye maendeleo vijijini hasa kujenga miundombinu
kama vile barabara, nishati, maji safi, afya na elimu;
3. Kuelekeza fedha za kutosha
kukarabati Reli ya Kati na kufufua njia za Reli za Tanga, Moshi na
Arusha kwani usafiri wa reli ni nguzo muhimu kuinua uchumi wan nchi;
4. Kuongeza wigo wa kutoza tozo ya ujuzi (Skills Development Levy) ili
waajiri wote ikiwemo Serikali na mashirika ya umma walipe tozo hiyo tofauti na
sasa ambapo sekta binafsi tu ndiyo inayochangia. Aidha, tunapendekeza tozo hii ipunguzwe
kutoka asilimia 6 ya sasa mpaka kufikia asilimia 4 ambapo theluthi moja itaenda
VETA na vyuo vya ufundi na baki itaenda kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu ili kukabili changamoto ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu;
5. Kuongeza mapato ya ndani na kupunguza mikopo ya kibiashara kwa
kuhakikisha mapato ya ndani yanafikia 20% ya pato la taifa kwa kufanya
marekebisho ya kisheria na udhibiti ili kuiwezesha TRA kukusanya mapato zaidi kutoka
kwenye kampuni za simu na kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, mafuta na gesi
asilia.
6. Kuliandaa Taifa kuwa na uchumi wa gesi asilia kwa kuanzisha ama kuharakisha
mchakato wa utungaji wa Muswada wa Sheria ya Gesi;
7. Kupunguza au kufuta kodi kwenye bidhaa za vyakula vinavyotumiwa na
wananchi walio wengi kwa muda maalum ili kushusha mfumuko wa bei;
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo haya ni mawazo ya Wabunge walio wachache katika Bunge hili
tukufu. Katika utaratibu wa ‘wengi wape’ unaotumiwa na Bunge letu na katika
mazingira ya ushindani wa kisiasa katika nchi yetu, ni rahisi kudharau au
kupuuza ushauri wa walio wachache kwa kutumia nguvu ya uwingi ya chama tawala.
Endapo hilo litafanyika kuhusiana na mapendekezo haya, taifa letu litakuwa limekoseshwa
fursa ya kuvuna utajiri na uzoefu wa kitaaluma wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
na matokeo yake hayatakuwa mema kwa ustawi wan chi yetu. Kama alivyosema Mahatma Gandhi: “Mabadiliko ya kidemokrasia
hayawezekani iwapo hatupo tayari kusikiliza upande mwingine. Tunafunga milango
ya kufikiri wakati tunapokataa kuwasikiliza wapinzani wetu, au baada ya
kuwasikiliza tunawafanyia mzaha. Kutokuvumiliana kunapokuwa ndio mazoea,
tunajiweka katika hatari ya kutokujua ukweli.”
Mheshimiwa Spika,
Baada ya
kusema haya, naomba kuwasilisha.
------------------------------------------------
CHRISTINE
LISSU MUGHWAI (MB)
MSEMAJI MKUU
KAMBI RASMI
YA UPINZANI BUNGENI (MIPANGO)
18.06.2012
No comments:
Post a Comment