Monday, May 28, 2012

30 KIZIMBANI ZANZIBAR

Watu 30 wakiwemo wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe wakikabiliwa na makosa mbalimbali ikiwemo kuwashambulia Polisi,kuchoma moto matairi ya Magali barabarani na ukorofi.

Mbali na tuhuma hizo,pia wameshtakiwa kwa kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali kinyume na sheria pamoja na uzembe na ukorofi wa kuwashambuliya polisi kwa mawe.

Watuhumiwa hao walifikishwa katika mahakama nne tofauti, ikiwemo mahakama ya hakimu Mohammed Ali Mohammed walikofikishwa watuhumiwa wawili, wanne kwa hakimu Janet Nora Sekihola, 11 kwa hakimu Omar Mcha Hamza na 11 waliobakia, wamepandishwa mbele ya hakimu Valentine Andrew Katema.

Kwa nyakati tofauti watuhumiwa hao walishitakiwa kwa makosa ya kufanya mikusanyiko isivyo halali, uzembe na ukorofi pamoja kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani.

Watuhumiwa hao ni Mbarouk Said Khalfani (45), na Mussa Juma Issa (57) wanaodaiwa kuwa ni viongozi wa Jumuiya hiyo, ambapo walifikishwa mbele ya hakimu Mohammed Ali Mohammed, na kusomewa shitaka la kufanya mkusanyiko isivyo halali kinyume na kifungu cha 55 (1) (2) (3) na kifungu cha 56 cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Wengine ni Mbwana Hamadi Juma (50), Massoud Hamadi Mohammed (17), Mohammed Juma Salum (35), Abdulrahman Simai Khatib (19), Hashim Juma Issa (54) Matar Fadhil Issa (54).

Watuhumiwa hao kwa upande wao wamefikishwa katika kizimba cha mahakama ya hakimu Mdhamini Janet Nora Sekihola kujibu shitaka uzembe na ukorofi kinyume na kifungu cha 181 (d) cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Wengine walifikishwa katika mahakama ya hakimu Omar Mcha Hamza na Valentine Andrew Katema, wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani.

KATIKA HATUA NYINGINE

Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk amesema licha ya fujo ambazo zilitokea May 26 na 27 Usalama umeimarishwa vya kutosha na kuwataka Watalii waendelee kuja kufanya shuguli zao bila ya woga wowote.

Amesema Serikali inabeba jukumu la usalama wa Wageni ambao wanakuja Zanzibar na kufahamisha kuwa fujo lililotokea halikuathiri Sekta ya Utalii na maeneo yake muhimu.

Waziri Mbarouk ameyaeleza hayo alipokuwa akizungumza na Wawakilishi wa Mabalozi waliopo Nchini kuhusiana na fujo lililotokea jana na juzi kufuatia kukamatwa kwa kiongozi mmoja wa Jumuiya ya Kidini ya UAMSHO.

Amefahamisha kuwa maeneo muhimu ya Utalii yakiwemo Mji Mkongwe,Fukwe za bahari na Hoteli ni sehemu salama ambazo watu wanajishughulisha na kazi zao za kawaida na kuwaomba Mabalozi hao kuwafahamisha vyema wenzao kile ambacho kimetokea.

No comments: