Friday, March 2, 2012

PINDA UKUAJI WA PATO LA TAIFA KWA MIAKA KUMI... 2000-2010

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA NNE WA BUNGE TAREHE 26 AGOSTI 2011
Mheshimiwa Spika,
1. Leo tumefikisha Kikao cha 56 tangu tuanze Mkutano wa Nne wa Bunge lako Tukufu tarehe 7 Juni 2011. Mkutano huu ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kujadili Mpango na Bajeti ya Serikali pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara, Mikoa na Taasisi mbalimbali kwa mwaka 2011/2012. Tumejadili masuala mbalimbali na hasa ya kuiletea Nchi yetu maendeleo kwa takriban siku84. Huu ni muda mrefu ambao kwa vyovyote vile inatubidi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote zilizopangwa siku hizo kwa amani na utulivu.
Mheshimiwa Spika,
2. Katika muda wa takribani miezi mitatu tumemkosa mwenzetu Mheshimiwa Profesa Mark Mwandosya (Mb.), Waziri wa Maji, ambaye amekuwa katika matibabu Nchini India. Napenda niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwanza kumpa pole kwa maradhi na pili kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ili apone haraka na hatimaye kurejea nyumbani kujiunga na Waheshimiwa Wabunge wenzake na Wananchi wa Jimbo la Rungwe Mashariki katika ujenzi wa Taifa.
3. Lakini kwa masikitiko makubwa, napenda niwape pole Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge hili pamoja na Wawakilishi wa Baraza la Mapinduzi kwa Msiba Mkubwa wa kumpoteza mwenzetu Mheshimiwa Musa Khamis Silima kutoka Baraza la Wawakilishi pamoja na Mke wake, Bibi Mwanaheri Twalib waliopoteza maisha katika ajali mbaya iliyotokea Nzuguni-Dodoma. Tunamwomba Mwenyezi Mungu Azilaze Roho za Marehemu Mahala Pema Peponi. Amina.
Shughuli za Bunge
(a) Maswali
Mheshimiwa Spika,
4. Katika Mkutano huu, jumla ya Maswali 499 ya Msingi na mengine 1,183 ya Nyongeza yaliulizwa na kupata majibu kutoka Serikalini. Vilevile, jumla ya Maswali 62 ya Msingi na 34 ya Nyongeza ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu kila siku ya Alhamisi yaliulizwa na kupata majibu. Ninawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kwa kujibu Hoja za Waheshimiwa Wabunge vizuri. Maswali yalikuwa mengi, lakini mmeyajibu yote pamoja na yale ya Nyongeza kwa umahiri mkubwa. Nawapongeza sana.
(b) Miswada ya Sheria ya Serikali
Mheshimiwa Spika,
5. Tunahitimisha Mkutano huu tukiwa tumepata fursa ya kujadili Miswada, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Miswada iliyowasilishwa na Serikali ni ifuatayo:
  1. Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2011 [The Finance Bill, 2011];
  2. Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Biashara wa Mwaka 2011 [The Business Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2011]; na
  3. Muswada wa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2011 [(Appropriation Bill, 2011]
(c) Maazimio
Mheshimiwa Spika,
6. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge pia walikubali Azimio la Bunge la Kuridhia Kuongeza Muda wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma, yaani “The Consolidated Holding Corporation”.
(d) Kauli za Mawaziri
Mheshimiwa Spika,
7. Katika Mkutano huu, Mawaziri walitoa Kauli za Serikali zifuatazo:
i. Kauli ya Waziri wa Viwanda na Biashara kuhusu kuendelea kutumika kwa Mizani ya Rula (Steel Yard);
ii. Kauli ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kuhusu Hali ya Chakula Nchini;
iii. Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu Kampuni ya Uingereza ya BAE System; na
iv. Kauli ya Waziri wa Nishati na Madini kuhusu Hali ya Umeme Nchini kati ya tarehe 14 – 18 Agosti 2011.
MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO NA MIAKA15
Mheshimiwa Spika,
8. Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kwamba kabla ya kuanza kwa Mjadala wa Bajeti, mlipata fursa ya kupokea, kujadili na kupitisha MPANGO wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, kuanzia mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016. MPANGO huu unakusudia kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo kwa kipindi kilichobaki cha uhai wake wa Miaka 15 hadi 2025. Kwa kutumia MPANGO huu, katika kila kipindi cha Miaka Mitano, Nchi yetu inatakiwa kujipima kwa vitendo kujua tumefikia wapi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ambayo inaelekeza Tanzania kuwa Nchi ya Uchumi wa kati ifikapo 2025.
9. Katika Mpango huo, tumeamua kutekeleza Vipaumbele vichache kulingana na rasilimali kidogo tulizonazo. Kwa mfano, MPANGO wa Miaka Mitano unatoa Kipaumbele cha juu kwa Sekta za Kilimo na Miundombinu ya msingi. Maeneo mengine ni ukuzaji wa Rasilimali Watu na Matumizi ya Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki kikamilifu katika mjadala wa MPANGO huo. Michango yenu ilikuwa mizuri na itaisadia sana Serikali katika utekelezaji wa MPANGO huo.
Mheshimiwa Spika,
10. Napenda kusisitiza kuwa katika utekelezaji wa MPANGO huu na MIPANGO mingine itakayofuata hadi 2025, Serikali itaelekeza matumizi ya Rasilimali zake katika vipaumbele vichache ili kupata manufaa makubwa yaliyokusudiwa. Hivyo, Awamu Tatu za utekelezaji wa MPANGO wa MAENDELEO wa Miaka 15 utajikita katika Agenda Kuu Tatu zifuatazo:
Awamu ya Kwanza:Kufungua fursa mbalimbali zitakazochochea Ukuaji wa Uchumi kwa kasi kubwa hasa Sekta ya Kilimo, Nishati na Miundombinu (2011-2015);
Awamu ya Pili:Ujenzi wa Misingi ya Maendeleo ya Viwanda (2016-2020); na
Awamu ya Tatu:Kuimarisha Ubunifu na Ushindani wa Biashara Kimataifa (2021-2025).
Mheshimiwa Spika,
11. Napenda kutumia fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kuwaelimisha Wananchi katika Majimbo yao kuhusu MPANGO wetu wa Miaka Mitano tunaoanza kuutekeleza mwaka huu. Aidha, nawaomba Wananchi na Wadau wote wa Maendeleo washiriki kikamilifu katika utekelezaji wa MPANGO huu.
UMUHIMU WA UWEKEZAJI NCHINI
Mheshimiwa Spika,
12. Ukuaji wa Uchumi wa Nchi yoyote Duniani kwa sasa unasukumwa na mambo makubwa mawili ambayo ni ushiriki na Uwekezaji wa Sekta Binafsi na Ukuaji na Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Tupende tusipende na ili kuongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi wetu, lazima na sisi kama Taifa tujikite kwenye utekelezaji wa masuala hayo. Lazima tutumie kila mbinu ya kuvutia Wawekezaji kwenye Sekta zote na hasa kwenye Sekta ya Kilimo ambayo tuna fursa kubwa kwa maana ya Ardhi kubwa yenye rutuba na Vyanzo vingi vya Maji. Nchi zote Duniani zilizofungua Milango ya Biashara na kuvutia Uwekezaji wenye tija zimepata mafanikio na maendeleo makubwa.
Mheshimiwa Spika,
13. Serikali inatambua nafasi ya Sekta Binafsi kuwa Injini ya Kukuza Uchumi (Engine of Economic Growth) na kuzalisha ajira na ndiyo maana Serikali imetayarisha Sera na Kutunga Sheria mbalimbali za kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na kuendeleza Sekta Binafsi. Tangu mwaka 1986 Serikali imetekeleza mageuzi makubwa ya Sera za Uchumi Jumla (Macro-economic Policies) na Kitaasisi (Structural Reforms) ambazo zimetambua nafasi ya Sekta Binafsi katika Kukuza Uchumi. Mwaka 1997 ilitungwa Sheria ya Uwekezaji (Act No.7, The Tanzania Investment Act, 1997) na Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Act No. 19, The Public Private Partnership Act, 2010).
Mheshimiwa Spika,
14. Upo uhusiano mkubwa kati ya Uwekezaji na Ukuaji Halisi wa Pato la Taifa. Kwa mfano, katika kipindi cha Miaka Kumi (10) kuanzia mwaka 2000 hadi sasa tumeshuhudia Ukuaji wa Uchumi wetu ukiendelea kuimarika na kukua kwa Wastani wa Asilimia 6.8 kwa mwaka. Naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha kwa kifupi Watanzania wote Takwimu za Ukuaji halisi wa Pato la Taifa kuanzia mwaka 2000, ambapo Ukuaji wa Uchumi ulikuwa Asilimia 4.9; mwaka 2001 Asilimia 6.0; mwaka 2002 Asilimia 7.2; mwaka 2003 Asilimia 6.9; mwaka 2004, Asilimia 7.8; mwaka 2005 Asilimia 7.4; mwaka 2006 Asilimia 6.7; mwaka 2007 Asilimia 7.1; mwaka 2008, Asilimia 7.4; mwaka 2009 Asilimia 6.0; na mwaka 2010 Asilimia 7.0.
Mheshimiwa Spika,
15. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa ukuaji huo mzuri wa Pato la Taifa umechangiwa na Ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano ambayo ilikua kwa Wastani wa Asilimia 16.4, katika kipindi hicho cha miaka 10, Sekta nyingine zilizochangia ukuaji huo ni Sekta ya Madini ambayo ilikua kwa Wastani wa Asilimia 11.5, Sekta ya Ujenzi Asilimia 9.5, Sekta ya Fedha Asilimia 9.4, Sekta ya Viwanda Asilimia 8.0, Sekta ya Afya Asilimia 7.6, Sekta ya Majengo Asilimia 6.6, Sekta ya Utalii na Biashara Asilimia6.3 na Sekta ya Kilimo Asilimia 4.3.Ni dhahiri kuwa ukuaji huo wa Wastani katika kila Sekta umetokana kwa kiwango kikubwa na Uwekezaji wa Ndani na Nje wa Sekta Binafsi na kwa kiasi fulani Sekta ya Umma. Kwa leo ninaomba nizungumzie kidogo juu ya mchango na umuhimu wa Sekta Binafsi.
Mheshimiwa Spika,
16. Takwimu za thamani ya Mitaji ya Uwekezaji wa moja kwa moja kutoka Nje (Foreign Direct Investments - FDIs) zinaonesha kuwa jumla ya Mitaji iliyoingizwa Nchini katika kipindi cha miaka kumi ni sawa na Dola za Kimarekani Bilioni 5.6 ambayo ni sawa na Shilingi Trilioni 8.8 kwa kutumia kiwango cha sasa cha ubadilishaji Shilingi kwa Dola za Kimarekani. Aidha, thamani ya Mitaji hiyo iliongezeka kutoka Dola za Kimarekani Milioni 463.4 sawa na Shilingi Bilioni 385 mwaka 2000 hadi Dola za Kimarekani Milioni 744 mwaka 2008 sawa na Shilingi Bilioni 881 na ilishuka kidogo hadi Dola za Kimarekani Milioni 573 sawa na Shilingi Bilioni 821 mwaka 2010 kutokana na Mdororo wa Kiuchumi katika kipindi hicho. Hata hivyo, pamoja na Mdororo huo, Tanzania iliendelea kuongoza kwa kuvutia Wawekezaji katika kipindi hicho katika Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Sekta zilizoongoza katika kuvutia Mitaji mikubwa ya Uwekezaji wa moja kwa moja (FDIs) ni uzalishaji Viwandani; Mawasiliano; Madini; Utalii; Majengo ya Biashara; na Ujenzi na Usafirishaji. Uwekezaji katika Sekta hizi sio tu kwamba umevutia Mitaji, bali umeongeza Ajira, Mauzo Nje, umeingiza Teknolojia Mpya, na kubaini Masoko mapya.
17. Kwa kuzingatia Takwimu hizo, sio sahihi hata kidogo kupuuza mchango wa Uwekezaji katika Uchumi wetu.Ndiyo sababu tumekuwa tukisifiwa na wenzetu wanaotuona huko nje kwamba, kwa ukuaji huu wa Uchumi unaiwezesha Nchi yetu kufikia Uchumi wa Kati haraka. Tuko miongoni mwa Nchi Kumi za Duniani ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa, na miongoni mwa Nchi 17 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zinaongoza katika Kukua kwa Uchumi, kupunguza Umaskini na kuzingatia Utawala Bora. Vilevile, tuko miongoni mwa Nchi Nne Duniani mbili kati ya hizo kutoka Afrika kushiriki Mpango wa Ubia wa Kukuza Uchumi (Partnership for Growth). Mifano yote hii ni ushahidi tosha kwamba Tanzania inafanya vizuri katika kujenga misingi imara ya Uchumi. Lakini ninyi wote ni mashahidi; Serikali za Awamu ya Tatu na Nne chini ya Uongozi madhubuti wa Chama Cha Mapinduzi imebidi zichukue hatua thabiti za kufanya mageuzi makubwa ya Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii ili kufikia hatua hii. Mageuzi haya ili yakamilike na kufanikiwa ni lazima yawepo mageuzi makubwa ya Kifikra, Kimatendo na mahusiano na Jamii na Dunia kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
18. Pamoja na mafanikio haya, sina budi kuwatahadharisha Watanzania kwamba, safari ya kukamilisha kazi ya kuwaletea Watanzania maendeleo kamili bado ni ndefu na lazima tuongeze zaidi juhudi hizi na kamwe tusibweteke. “Ni dhahiri kwamba hadi hapa tulipofikia Tumethubutu, Tumeweza, sasa Tusonge Mbele”. Tunachohitaji ni utashi wa Kisiasa na dhamira ya kweli. Tukiamua kuundoa Umaskini tutaweza, kwani kama alivyosema Mtaalamu Bwana Justin Yifu Lins, Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia “Poverty is not a genetic Condition”. Umaskini siyo hali inayotokana na tatizo la Kurithishwa. “It is a set of Factors Producing an outcome; alter the Factors and the outcome Changes.” Ni hali inayotokana na mambo kadhaa wa kadha ambayo husababisha matokeo fulani Hasi ambayo ukiyabadilisha tu, matokeo hayo hubadilika na kuwa Chanya.
Mheshimiwa Spika,
19. Mageuzi yoyote huja na hofu na hivyo kusababisha wasiwasi miongoni mwa Jamii. Lakini tukitaka maendeleo ni lazima yawepo mageuzi ya dhati. Hivyo, mageuzi sharti yaendane na kujitoa Mhanga na ni lazima mageuzi yoyote katika Nchi yalenge kuboresha Maisha ya Watu Maskini walio wengi na siyo vinginevyo.
Mheshimiwa Spika,
20. Mpango wa Maendeleo wa Taifa umelenga kuifikisha Tanzania kuwa Nchi yenye Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025. Hili ni lengo zuri, lakini Wachumi wanatuambia kuwa ili Tanzania ifikie lengo hilo ni lazima Uchumi wake Ukue kwa Wastani wa Asilimia 8-10 kwa miaka 30 hadi 40. Uzoefu wa Nchi nyingine kama China unaonesha kuwa baada ya kutimiza kiashiria hicho, ndipo misingi ya kuelekea kwenye Taifa lenye Uchumi Mkubwa inapoweza kuanza kujidhihirisha. Hadi sasa Tanzania imeweza kusimamia vizuri Uchumi wake ambao umeendelea Kukua kwa Wastani wa Asilimia 7 kwa miaka kumi iliyopita. Rai yangu kwa Watanzania wote ni kwamba, hapa tulipofika tusirudi nyuma, ‘tusonge mbele’ ili ndani ya miaka Kumi na Mitano chini ya Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa tufike tunapolenga yaani Kuwa Nchi ya Uchumi wa Kati. Kutokana na uzoefu tulioupata na hatua mbalimbali tulizopitia, sioni kwa nini Tanzania isiweze kufika hapo.
Mheshimiwa Spika,
21. Historia ya Nchi zote Duniani inatuonyesha kuwa Mataifa yote yalianza kama Nchi Maskini zilizotegemea zaidi Nguvu Kazi ya Wananchi wake katika Kilimo na sehemu nyingine kama Uvuvi kwa ajili ya mahitaji ya Wananchi wake. Kutegemeana na aina ya Rasilimali zilizomo katika Nchi, kila Nchi iliamua ni Rasilimali gani waliyonayo ambayo inawapa fursa zaidi katika kuwaletea maendeleo ya haraka Wananchi wake. Rasilimali hiyo ndiyo waliyoitumia kubadili hali ya maisha ya Wananchi wake na Nchi kwa ujumla. Kwa upande wa Tanzania, fursa tulizonazo ni pamoja na Ardhi, Madini, Misitu, Vivutio vingi vya Utalii, Maji ya Bahari, Maziwa na Mito, Bandari inayotumiwa na Nchi nyingi zinazozunguka Nchi yetu, n.k. Vyote hivi vikisimamiwa vizuri na kwa maslahi ya Wananchi Maskini, Umaskini utaondoka ndani ya kipindi kilichopangwa.
22. Katika Mkutano huu tunaohitimisha leo, moja ya hoja zilizojadiliwa kwa hisia kali na tofauti ni suala zima la Uwekezaji, hususan umiliki wa Ardhi. Miongoni mwetu, kuna wanaotafsiri uwekezaji mkubwa kwenye ardhi kuwa ni unyang’anyi, uporaji na wizi wa ardhi ya Watanzania. Hali hii imezua dhana potofu ambayo inajijenga miongoni mwa baadhi ya Watanzania kwamba, unapotaja neno Mwekezaji kwa tafsiri ya haraka haraka ni Mtu Mporaji, Mwizi na Laghai. Nawaomba sana Watanzania tuwe waangalifu na Kauli za namna hii kwa kuwa tutawatisha Wawekezaji wanaotaka kuja na kuwafukuza Wawekezaji ambao tayari wapo hapa Nchini. Jambo ambalo ni hatari sana kwa Uchumi na Maendeleo ya Nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
23. Bunge ni Taasisi ambayo ina Heshima ya kipekee Duniani kote. Bunge ndiyo Taasisi inayotunga Sheria. Kwa maana hiyo, kile kinachosemwa ndani ya Bunge na Mbunge yeyote yule kinaheshimika. Wawekezaji na Wananchi wote wanafuatilia kwa karibu na kwa umakini mkubwa majadiliano yote ya Waheshimiwa Wabunge ndani ya Bunge. Aidha, kutokana na ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, majadiliano yote yanayotokea hapa Bungeni yanaonekana au kusikika Duniani kote. Watanzania wengi kote Mijini na Vijijini wanatuona na kutusikia. Wawekezaji kokote walipo wanatusikia na kutuona. Hivyo, maneno tunayosema kuhusu Wawekezaji siyo tu kwamba yanaweza kuwaogopesha na kuwafukuza, bali yanachochea Chuki miongoni mwa Wananchi dhidi yao. Uwekezaji ni Ushindani. Uwekezaji ni Biashara. Hakuna Mwekezaji anayependa kuwekeza mahali ambapo atapata hasara, hususan wakati huu ambapo kumekuwepo na Mdororo wa Uchumi. Lakini wakati tunayaongea hayo ni dhahiri pia kwamba tunapingana na juhudi za Serikali na hasa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye amekuwa Mstari wa Mbele katika kuwavutia Wawekezaji wa Ndani na Nje ya Nchi kuwekeza Nchini mwetu.
Mheshimiwa Spika,
24. Naomba nitumie tu mfano mdogo wa maneno ya Mheshimiwa Rais aliyoyatumia wakati akihutubia Mkutano wa Wawekezaji uliofanyika Milan, Italy tarehe 18 Julai 2007. Katika Mkutano huo alisema na naomba ninukuu kwa Kiingereza, Lugha aliyoitumia kwenye Mkutano huo:
“Tanzania, is no doubt, a great place to invest in Africa today. By saying this I am not trying to brag for nothing. I am simply saying the obvious. For over the past decade we have put in place the most conducive investment environment you can think of. We have flung our doors wide open for anyone interested to bring his money and do business with us in Tanzania. There are no restrictions or preconditions attached. You just bring your money, you do business. Period. Bureaucratic red-tape has almost been severed.”Mwisho wa kunukuu.
25. Anachosema Mheshimiwa Rais ni kwamba, Tanzania haina shaka ni Nchi inayofaa kuwekeza katika Bara la Afrika. Hali ya Uwekezaji ni nzuri na Milango iko wazi bila ukiritimba. Maneno haya mazito ya Mheshimiwa Rais ambayo amekuwa akiyatumia mara kwa mara kila anapopata nafasi ya kukutana na Wawekezaji Ndani na Nje ya Nchi yana dhamira ya dhati ya kuruhusu Wawekezaji wa Ndani na Nje kuwekeza Nchini mwetu bila bughudha yoyote. Ninawaomba sana Watanzania tuelewe hilo na TUSIBEZE UWEKEZAJI Nchini mwetu.
26. Mheshimiwa Freeman A. Mbowe – Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, na Waziri Kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Tamisemiwakati akichangia majadiliano ya Hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii naye alisema:
Namnukuu:“Mheshimiwa Naibu Spika, niingie katika Biashara ya Utalii, na hapa wa Uwindaji. Nilim-quote Baba wa Taifa kwa sababu mwaka 1961 alijua suala la Biashara ya Utalii hatuwezi kulifanya wenyewe bila kuwa na Wageni, huo ndiyo ukweli. Kuwafukuza Wageni nimeshasema sio kipimo cha Uzalendo hasa linapokuja hili suala la Biashara ya Uwekezaji wa Utalii. Kwa bahati mbaya sana na ni kweli Mheshimiwa Waziri katika siku za usoni ni vema Wizara yako ikaandaa Semina kutufahamisha na kufundisha Waheshimiwa ni nini maana ya Biashara ya Utalii wa Uwindaji? Watu wengi wana tabia ya kufikiri unapewa Kitalu kama hiki kina Wanyama unakwenda kuwinda Swala na Tembo, biashara imeishia hapo. Uwekezaji wa Utalii ni highly professional. Ni Utalii unaohitaji Utalaam wa hali ya juu. Skills za hali ya juu na ni capital intensive”. Mwisho wa kunukuu.
27. Anachosema Mheshimiwa Mbowe ni kwamba tunawahitaji Wawekezaji na hivyo tusiwafukuze kwa maneno na matendo yetu.Kutokana na maneno hayo ya Mheshimiwa Mbowe, napenda kusisitiza kuwa tunahitaji Wawekezaji katika Sekta zote. Ninaelewa ziko Nchi ambazo kutokana na ushindani katika kuvutia Wawekezaji wanatoa hadhi ya VIP kwa baadhi ya Wawekezaji. Ninaomba tuwalinde Wawekezaji wa Sekta zote na tusichague baadhi ya Sekta tu.
Jambo la msingi ambalo Bunge hili na Watanzania wote kwa jumla tunapaswa kulihimiza ni Serikali kuwa makini wanapoingia Mikataba na Wawekezaji ili Uwekezaji huo uweze kuwa wa manufaa kwa pande zote mbili; Mwekezaji na Taifa. Watumishi wa Umma wanaoingia Mikataba mibovu nao sharti wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa Sheria.
KILIMO
Mheshimiwa Spika,
28. Taarifa mbalimbali za Mashirika ya Kimataifa zinaonesha kuwa hali ya Chakula Duniani, na Nchi jirani siyo ya kuridhisha. Kwa mujibu wa Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (World Food Programme) za mwezi Agosti 2011, idadi ya Watu wanaokabiliwa na upungufu wa Chakula katika Nchi zilizo kwenye Pembe ya Afrika (Horn of Africa) hususan Somalia, Kenya, Uganda, Ethiopia na Sudan Kusini imefikia takriban Watu Milioni 13. Hawa wote wanahitaji Chakula cha Msaada. Uhaba huo wa Chakula unatokana na Ukame pamoja na Vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya Nchi hizo. Hali hii ni hatari kwa Nchi jirani kama ya kwetu. Madhara ya Uhaba wa Chakula yatakayotokea katika Nchi hizo na hasa Kenya na Uganda yataathiri sana Ukuaji wa Uchumi wetu, tupende tusipende.
Mheshimiwa Spika,
29. Uhaba huo wa chakula kwa Majirani zetu ni changamoto kubwa kwa Nchi yetu ambayo nayo inakabiliwa na upungufu wa chakula katika Mikoa 15 kwenye maeneo ya jumla ya Wilaya 58. Upungufu wa chakula katika Nchi jirani umesababisha ongezeko la bei ya chakula hasa Mazao ya Nafaka na hivyo, kuchochea kushamiri kwa biashara ya mazao ya chakula kutoka Tanzania kwenda katika Nchi hizo. Kutokana na hali hiyo, natoa rai kwa Wananchi kuchukua tahadhari ya kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha kabla ya kuuza mavuno yao yote ya msimu uliopita.
30. Serikali imechukua hatua za kukabiliana na tatizo la upungufu wa chakula Nchini kwa kufanya yafuatayo:
i) Serikali imeimarisha Akiba ya Chakula kwenye Maghala ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) ambapo hadi tarehe 22 Agosti 2011 kulikuwa na Tani 143,609.8 za mahindi;
ii) Mwezi Julai, 2011 Serikali imetoa Tani 29,777 za Chakula kwenye Halmashauri 26 zenye upungufu mkubwa wa Chakula;
iii) Serikali itaiwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kifedha ili iweze kununua Chakula cha kutosha kutoka kwa Wakulima wa Mikoa yenye ziada ya Rukwa, Iringa, Mbeya na Ruvuma;
iv) Tunaendelea na mchakato wa kuhamisha Akiba ya Chakula kutoka katika Maghala ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula ya Sumbawanga, Makambako na Songea na kuyasafirisha kwenda Mikoa yenye Uhaba mkubwa wa Chakula ya Shinyanga, Singida, Arusha na Dodoma;
v) Ununuzi wa mahindi kwenye Mikoa yenye ziada ya Nyanda za Juu Kusini unaendelea, na kuanzia tarehe 8 Mei 2011 hadi tarehe 22 Agosti 2011 ni Tani 12,610.4 ambazo zimenunuliwa;na
vi) Serikali itaendelea kusitisha uuzaji wa Mazao ya Nafaka nje ya Nchi hadi mwezi Desemba 2011 ili kukabiliana na upungufu wa Chakula Nchini.
Mheshimiwa Spika,
31. Hadi tarehe 31 Julai 2011, Wafanyabiashara wakubwa wa Nafaka Nchini walikuwa na jumla ya Tani 124,524 za Nafaka zikiwemo Tani 113,000 za Ngano, Tani 11,000 za Mahindi na Tani 520 za Mchele. Katika kipindi kama hicho mwaka 2010 akiba ya Ngano ilikuwa Tani 137,909, Mahindi Tani 11,520 na Mchele Tani 3,072 katika Maghala ya Wafanyabiashara hao ambayo ni kubwa ikilinganishwa na ya sasa.
Mheshimiwa Spika,
32. Natoa wito kwa Wananchi kutumia aina mbalimbali za vyakula tulivyo navyo na waepuke kuchagua vyakula. Kwa wale wenye Mifugo wanashauriwa wauze Mifugo yao ili wanunue chakula. Vilevile, nawahimiza Wafanyabiashara wenye uwezo wa kununua chakula kutoka maeneo yenye chakula kingi kufanya hivyo, na wawauzie Wananchi bila kuwalangua.
KIPAUMBELE KWENYE KILIMO
Mheshimiwa Spika,
33. Kutokana na mabadiliko ya Hali ya Hewa ambayo yanatishia uzalishaji na upatikanaji wa chakula cha kutosha Nchini, ni muhimu kutoa Kipaumbele katika Sekta ya Kilimo. Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano umetoa Kipaumbele cha kwanza katika Sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ufugaji Nyuki.
34. Napenda kutumia fursa hii kuwaomba Watanzania wenzangu kupenda Kilimo kwani ndicho kitakachotusaidia kukuza Uchumi na Kuondokana na Umaskini kwa haraka. Vijana watapata ajira endelevu kwenye Kilimo na Viwanda vyetu vitapata Malighafi ya kutosha. Natoa wito kwa Wakulima kuongeza tija ya uzalishaji katika maeneo waliyo nayo ya Kilimo. Kipaumbele kitolewe katika Kilimo cha Umwagiliaji, kutumia Mbegu Bora, Pembejeo na Zana Bora za Kilimo. Nitumie nafasi hii kuziagiza Halmashauri zote Nchini kuweka msukumo wa kipekee kwenye Kilimo na kutumia kikamilifu Skimu za Umwagiliaji katika maeneo wanayoyasimamia ili kuongeza uzalishaji wa Mazao ya Chakula.
Mheshimiwa Spika,
35. Wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika hapa Bungeni, Serikali ilipata michango mingi mizuri ambayo tunaahidi kuwa tutaifanyia kazi. Kwa kifupi naomba kuelezea maeneo machache:
a) Upatikanaji wa Mbolea
Mheshimiwa Spika,
36. Mahitaji ya Mbolea Nchini ni takribani Tani 400,000. Kati ya hizo, Ruzuku ya Serikali ni Tani 180,000 sawa na Asilimia 45. Hadi tarehe 31 Julai 2011, upatikanaji wa Mbolea ulikuwa Tani 153,479.9 sawa na Asilimia 38.4 ya mahitaji ya Mbolea. Hata hivyo, kiwango hiki cha Mbolea kilichopo kitaongezeka hadi Tani 357,000 sawa na Asilimia 89 ya mahitaji baada ya kuingizwa Nchini kiasi cha Tani 206,000 kati ya sasa na mwisho wa mwezi Septemba 2011. Mbolea hiyo imeagizwa na Makampuni ya Export Trading, YARA na Premium Agrochem. Vilevile, Kiwanda cha Minjingu baada ya kupata Mashine mpya kinaweza kuzalisha kiasi cha Tani 250,000 kwa mwaka, na hivi sasa kuna Mbolea zaidi ya Tani 20,000 ambazo zinasubiri kusambazwa. Kwa maana hiyo, hatutarajii kuwa na upungufu wa Mbolea katika msimu wa 2011/2012 kama ambavyo imekuwa katika miaka iliyopita. Serikali inaendelea kuyahimiza Makampuni kuchukua Asilimia 80 ya Mbolea hiyo ambayo kwa sasa ipo Dar es Salaam, na kuipeleka Mikoani.
b) Bei ya Zao la Pamba
Mheshimiwa Spika,
37. Michango yaWaheshimiwa Wabunge hasa wale wanaotoka Mikoa inayozalisha Pamba walielezea kwa uchungu tatizo la kushuka kwa bei ya Zao la Pamba katika Soko la Dunia, jambo ambalo limesababisha bei za hapa Nchini kushuka na kuwa chini ya Shilingi 1,100/= kwa Kilo. Kwa sasa bei ya Pamba katika Soko la Dunia inapanda na hata bei katika Soko la Ndani imeanza kupanda pia. Hivi sasa bei ya ushindani kwa kilo moja ya Pamba ni kati ya Shilingi 900/= na 1,100/=. Aidha, wanunuzi wote walioomba Leseni ya Kununua Pamba wamepewa. Kila mnunuzi anaruhusiwa kununua Pamba eneo lolote aliloomba. Tunawasihi Wakulima wa Pamba wauze Pamba yao sasa wakati bei imepanda.
c) Maendeleo ya Sekta ya Mifugo, Uvuvi na Nyuki
Mheshimiwa Spika,
38. Kwa muda mrefu, Serikali imekuwa ikitoa msukumo kwa Sekta za Mifugo, Uvuvi na Nyuki, lakini kasi ya ongezeko la tija katika Sekta hizo bado hairidhishi. Napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kuwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano Serikali imedhamiria kutoa msukumo wa kipekee katika Sekta hizo. Kama tulivyofanya katika Sekta ya Kilimo, ambapo tunatekeleza Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP). Sasa wakati umefika wa kubuni Mipango Maalum ya Kuendeleza Sekta za Mifugo, Uvuvi na Ufugaji Nyuki kama ulivyo wa ASDP. Lengo ni kuwezesha Sekta hizi kukua kwa kasi na kuchangia Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini kwa haraka. Hii ni kwa sababu Wananchi wetu wengi wanategemea Sekta hizi katika maisha yao ya kila siku. Wizara husika zitafanya kazi na Tume ya Mipango kuandaa Mipango chini ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa.
d) Utekelezaji wa Azma ya KILIMO KWANZA
Mheshimiwa Spika,
39. Serikali imejizatiti kutekeleza Azma ya KILIMO KWANZA ya kuleta Mapinduzi ya Kijani kupitia utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (Agricultural Sector Development Programme-ASDP) na Programu Kabambe ya Uendelezaji na Modenaizesheni ya Ushirika. Lengo la Taifa katika Mipango hii ni:
i. Kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada kwa kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula;
ii. Kupanua Kilimo cha Umwagiliaji na kuweka msukumo maalumu katika matumizi ya Teknolojia mpya za Umwagiliaji pamoja na kutumia Nishati za Jua na Upepo katika kusukuma maji shambani, kutumia Maji ya Ardhini, Mabwawa, Mito na Maziwa kwa kumwagilia kwa Matone ili kufikia lengo la Hekta Milioni Moja chini ya Mpango wa Taifa wa Umwagiliaji ifikapo mwaka 2015;
iii. Kupanua uzalishaji na ubora wa mazao ya bustani (mbogamboga, matunda na maua) na kujenga uwezo wa Wakulima na Vyama vyao vya Ushirika kutayarisha, kufungasha na kuuza bidhaa na mazao yao Nje ya Nchi;
iv. Kuongeza uzalishaji wa Mbegu Bora na kuhimiza matumizi ya Kanuni za Kilimo Bora ili kuongeza tija katika Kilimo;
v. Kupanua uzalishaji wa mazao makuu ya biashara ambayo ni pamoja na Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Tumbaku, Pareto na Zabibu. Kuongeza pia uzalishaji wa mbegu za mafuta na kuhimiza usindikaji; na
vi. Kuhimiza ushiriki wa Sekta Binafsi kwa utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Kilimo katika Kanda ya Kusini ya Tanzania (SAGCOT) na kuhimiza ushirikishwaji na Uwekezaji wa Sekta Binafsi.
Mheshimiwa Spika,
40. Serikali imedhamiria kuleta Mapinduzi ya Kilimo Nchini. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote tushirikiane na Serikali kutoa msukumo na Kipaumbele kwenye Kilimo. Mimi naamini Kilimo ndicho kitakachotukomboa.
UMUHIMU WA KULIPA KODI
Mheshimiwa Spika,
41. Katika majadiliano yaliyofanyika katika kipindi chote cha Bunge hili la Bajeti, moja ya mambo ambayo yamechukua uzito mkubwa ni mahitaji makubwa ya fedha za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na shughuli za Serikali ikilinganishwa na kiasi kidogo cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya Wizara zote. Wote tulishuhudia mjadala wenye hisia kali ya kuitaka Serikali kuongeza fedha katika maeneo muhimu kiuchumi. Ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa Mapato ambao umesababisha Wizara nyingi kupewa kiwango kidogo cha Fedha za Bajeti, lazima Serikali iangalie upya Vyanzo vyake vya Mapato. Moja ya Vyanzo vikubwa vya Mapato kwenye Nchi mbalimbali ni utozaji na ukusanyaji wa Kodi. Yapo maeneo yenye fursa kubwa ambayo yakitumika vizuri yanaweza kuongeza wigo wa Mapato. Ili ukusanyaji wa Mapato uongezeke ni lazima:
i. Kuangalia upya Mfumo wa Ukusanyaji Kodi kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwemo Sekta za Maliasili zetu kama vile Madini, Mazao ya Misitu, Uvuvi na Kudhibiti Misamaha ya Kodi;
ii. Kuendelea kutekeleza Mkakati wa kurasimisha Rasilimali na biashara zisizo rasmi;
iii. Kuboresha mazingira ya Uwekezaji na ukuaji wa Sekta Binafsi;
iv. Kuboresha Mfumo wa Kodi unaotumika katika kutoza Sekta Isiyo Rasmi. Hii ni pamoja na kusimamia Usajili wao;
v. Kuimarisha usimamizi wa ridhaa ya kulipa Kodi kwa kuboresha huduma ili kuzuia kuwepo kwa dalili za Uvujaji Mapato; na
vi. Kuchukua hatua kali za Kisheria kwa wale wote watakaobainika kukwepa Kodi na wale Wafanyakazi wa Umma wanaowasaidia kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika,
42. Upo msemo wa wenzetu wa Ulaya na Marekani usemao “Nothing is Certain But Death and Taxes”. Ni kweliMsemo huu hauna ladha kuutumia, lakini unaonesha umuhimu wa Kulipa Kodi. Kwa tafsiri nyepesi unaonesha ugumu wa kukwepa kulipa Kodi kama ilivyo vigumu kukwepa kifo. Wako Waandishi wa zamani ambao walijaribu kutafsiri msemo huu uwe mwepesi kidogo, lakini ukweli ukabaki na umuhimu wake.
43. Sheria ya Kodi inatamka bayana Majukumu ya Mamlaka ya kukusanya Kodi Nchini. Kwa maana hiyo, ni lazima kila Mlipa Kodi atimize wajibu wake. Kwa upande wake, Mlipa Kodi ana haki ya kutendewa haki sawa bila upendeleo kwa kuzingatia Sheria za Kodi na kupata huduma bora kutoka kwa Chombo chetu cha Ukusanyaji Kodi ambacho hapa kwetu ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mheshimiwa Spika,
44. Nitumie nafasi hii kuwapongeza baadhi ya Walipakodi Wakubwa kwa Serikali na ambao wamefanya vizuri kati ya kipindi cha mwaka 2005 na 2011. Kwa kipindi hicho, Makampuni yaliyoongoza kwa kulipa kodi ni pamoja na:
i. Tanzania Breweries Ltd. (Shilingi Bilioni 165.4);
ii. National Microfinance Bank (Shilingi Bilioni 108.6);
iii. Tanzania Cigarette Company (Shilingi Bilioni 92.1);
iv. National Bank of Commerce (Shilingi Bilioni 89.9);
v. CRDB Bank Ltd. (Shilingi Bilioni 79.2);
vi. Tanzania Ports Authority (Shilingi Bilioni 76.8);
vii. Tanzania Portland Cement (Shilingi Bilioni 73.4);
viii. Airtel (T) Ltd. (Shilingi Bilioni 63.6);
ix. Tanga Cement Company Ltd. (Shilingi Bilioni 43.6);
x. Standard Chartered Bank Ltd. (Shilingi Bilioni 40.0);
xi. Citibank (T) Ltd. (Shilingi Bilioni 35.7);
xii. Resolute (T) Ltd. (Shilingi Bilioni 32.1);
xiii. Tanzania International Container Terminal Services (Shilingi Bilioni 25.9);
xiv. Tanzania Distillers Ltd. (Shilingi Bilioni 13.4); na
xv. Group Five International (PTY) Ltd. (Shilingi Bilioni 9.5).
45. Napenda kutoa rai kwa Makampuni yote Nchini kuiga mfano huu mzuri. Wito wangu kwa Makampuni, Wafanyabiashara Wakubwa kwa Wadogo na Wananchi wote ni kuongeza juhudi katika kufanya biashara zao ili zizalishe kwa wingi na kupata faida kubwa zaidi. Faida kubwa itachangia katika kuongeza Mapato ya Serikali kwa njia ya Kodi na hivyo kusaidia kukuza uchumi, kuongeza Pato la Taifa na la Mwananchi mmoja mmoja na kuondoa Umaskini. Niwadhihirishieni kwamba, Serikali inatambua umuhimu wao kwa maendeleo ya Nchi yetu na itahakikisha inaongeza juhudi zake za kuweka Mazingira Wezeshi kwa Makampuni hayo kufanya shughuli zao vizuri ili kuwezesha kulipa Kodi kwa mujibu wa Sheria.
UONGEZAJI WA PATO LA MTANZANIA
Mheshimiwa Spika,
46. Lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ni kuiwezesha Tanzania kuwa na Uchumi wa Kipato cha Kati (Middle Income Country) ifikapo mwaka 2025. Kwa mujibu wa Takwimu za Taasisi ya Taifa ya Takwimu (National Bureau of Statistics) za mwaka 2010; wastani wa Kipato cha Mtanzania kimefikia Dola za Kimarekani 545, sawa na Shilingi 770,464. Hivyo, katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka 15 tunayo changamoto kubwa ya kuongeza kwa kasi kubwa Kipato cha Mtanzania ili kufikia lengo lililokusudiwa la kufikia Dola za Kimarekani 3,000 ambazo ni sawa na Shilingi Milioni 4.8 kwa mwaka au Shilingi 400,000/= kwa mwezi ifikapo mwaka 2025 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya Uchumi wa Kati.
Mheshimiwa Spika,
47. Napenda kutumia fursa hii kueleza kidogo kuhusu mwenendo wa takwimu za Mikoa kuhusu kiashiria hiki cha Wastani wa Kipato cha Mwananchi (Regional Per-Capita Income). Mtiririko wa nafasi za Mikoa kwa mwaka 2010 za Wastani wa Kipato cha Mwananchi kwa mwaka ni kama ifuatavyo:
i. Dar es Salaam - Shilingi 1,740,947
ii. Iringa - Shilingi 979,882
iii. Arusha - Shilingi 945,437
iv. Mbeya - Shilingi 892,877
v. Kilimanjaro - Shilingi 879,432
vi. Ruvuma - Shilingi 866,191
vii. Mwanza - Shilingi 829,647
viii. Manyara - Shilingi 772,364
ix. Tanga - Shilingi 763,203
x. Morogoro - Shilingi 744,234
xi. Rukwa - Shilingi 726,658
xii. Mtwara - Shilingi 700,436
xiii. Lindi - Shilingi 673,096
xiv. Mara - Shilingi 642,528
xv. Pwani - Shilingi 572,466
xvi. Tabora - Shilingi 528,832
xvii. Shinyanga - Shilingi 510,023
xviii. Kigoma - Shilingi 499,428
xix. Kagera - Shilingi 491,713
xx. Dodoma - Shilingi 485,211
xxi. Singida - Shilingi 483,922
Mheshimiwa Spika,
48. Takwimu hizo zinaonesha kuwa Theluthi Moja tu ya Mikoa yote ya Tanzania ndiyo yenye Wastani wa Pato la Mtu ambalo ni juu ya Wastani wa Pato la Mwananchi Kitaifa la mwaka 2010 la Shilingi 770,464. Vilevile, Takwimu hizo zinaonesha kuwa Mikoa Mitano ya mwisho kwa mlinganisho wa Wastani wa Kipato cha Mwananchi ni Shinyanga, Kigoma, Kagera, Dodoma na Singida. Hata hivyo, hali halisi inaonesha kuwa Mikoa hii ina fursa nyingi za kuongeza Mapato kutokana na shughuli mbalimbali za uchumi, na fursa za kibiashara zilizoko lakini Takwimu za Mapato ya Mikoa hii haziwiani na hali halisi za maisha ya Wananchi wa Mikoa husika kwa fursa walizonazo. Mikoa niliyoitaja ndiyo inaongoza kwa eneo kubwa la Ardhi nzuri na idadi kubwa ya Mifugo Nchini ambayo pia ina fursa kubwa ya kuwaongezea Mapato. Pia Mikoa hii ina idadi kubwa ya Wananchi wanaojishughulisha na Kilimo cha Mazao yenye tija kubwa kama vile Pamba, Karanga, Alizeti na Ufuta. Aidha, biashara imeshamiri sana kwenye Mikoa hii, hivyo hakuna sababu ya Mikoa hii kuwa nyuma katika kipato cha Mwananchi. Vilevile, Mikoa mingine yote inayo fursa tele za kuwaongezea Wananchi wake Kipato na kupunguza Umaskini.
Mheshimiwa Spika,
49. Ninapenda kuzungumzia suala hilo kwa sababu Kiwango kidogo cha Pato la Mwananchi ni changamoto kubwa kwa Viongozi wote kuanzia ngazi ya Wizara, Mikoa, Wilaya na kila Mkurugenzi wa Halmashauri na Watendaji katika ngazi zote. Viongozi na Watendaji wote tunatakiwa kujibu Hoja ya namna ya kuongeza Kipato cha Mwananchi kwa kuelekeza nguvu kwenye Sekta za Uzalishaji na huduma za kiuchumi pamoja na biashara zenye tija. Faraja ninayoipata hapa ni kwamba tunazo fursa tele kwenye Sekta ya Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Urinaji Asali, Utalii, Maliasili, Madini na biashara. Fursa hizi zikitumika vizuri zinaweza kuongeza Kipato cha Mtanzania na kuwezesha kupunguza Umaskini kwa haraka.
Mheshimiwa Spika,
50. Tatizo ninaloliona mimi ni kuwa bado hatujawa Wabunifu zaidi na tunahitaji kuwashirikisha Wananchi katika kuibua na kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Natoa wito kwa Viongozi wote kujipanga vizuri ili kuwawezesha Wananchi wetu kuondokana na kipato kidogo kwa kuongeza tija na uzalishaji katika Sekta zote. Kwa maoni yangu ningependa kila Kiongozi, katika ngazi zote na hasa Wakurugenzi wa Halmashauri wajielekeze katika kutafakari mbinu watakazotumia kuongeza Pato la Mwananchi katika maeneo waliyopangiwa kuyasimamia.
MCHANGO WA VIWANDA VIDOGO VIDOGO KATIKA MAENDELEO YA NCHI
Mheshimiwa Spika,
51. Wakati Serikali ikielekeza nguvu zake katika Sekta ya Kilimo na Sekta nyingine zenye uwezo wa haraka wa Kukuza Uchumi, kuinua Pato la Taifa na hatimaye kuondoa Umasikini, lazima tuangalie pia uendelezaji wa Sekta ya Viwanda na hasa Viwanda Vidogo Vidogo (Small and Medium Enterprises – SMEs) kwa ajili ya kusindika mazao. Nchi nyingi zimeweka mkazo mkubwa katika kuiendeleza Sekta hii. Aidha, uchumi wa Nchi hizo hutegemea sana Sekta hii na hivyo zimeweka mikakati maalum kwa ajili ya kuiendeleza. Serikali ya Tanzania ilitambua mapema umuhimu wa Sekta hii na hivyo ikaanzisha Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mwaka 1973 ili kuratibu Sekta hii tu. Vilevile, mwaka 2003, Serikali ilitunga Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (SME Development Policy) iliyotoa Mwongozo wa namna ya kuiendeleza Sekta hii ikiwemo kutatua changamoto zinazoikabili. Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano 2011/2012 - 2015/2016 unasisitiza kuwepo kwa Viwanda vya Msingi ambavyo vitatumia Malighafi inayopatikana humu Nchini. Aidha, msisitizo uko katika kuweka mazingira mazuri ya Biashara ya kuwezesha pia kuanzishwa kwa Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (SMEs) vyenye Kukuza Ajira.
Mheshimiwa Spika,
52. Mchango wa Sekta hii katika Uchumi wa Nchi ni mkubwa na uko katika nyanja nyingi. Kwanza Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo imekuwa ikitoa mchango mkubwa wa kuongeza thamani mazao ya Kilimo na Maliasili. Vilevile, Sekta hii imekuwa ya msaada mkubwa katika kupunguza Upotevu wa Mazao baada ya Mavuno (Post Harvest Losses). Wajasiriamali Wadogo wengi wamekuwa wakijihusisha na Usindikaji wa Vyakula.
53. Mbali na Taasisi nyingi zinazotoa mafunzo ya Usindikaji wa Vyakula, SIDO imeweza kutoa mafunzo ya Usindikaji kwa Wajasiriamali zaidi ya 7,000 katika Mikoa yote ya Tanzania. Wengi wa Wajasiriamali hao sasa wanajishughulisha na Usindikaji wa Vyakula. Sekta hii pia ina fursa nzuri ya kutumia Malighafi zinazopatikana Nchini.
54. Pili, Sekta hii imeendelea kutoa mchango mkubwa katika Ajira kwa Watanzania. Hii ni kwa sababu Sekta hii huwezesha makundi ya Kijamii, hasa Wanawake na Vijana ambao wengi wao wamekosa Ajira katika Sekta nyingine kutokana na viwango vyao vidogo vya elimu na uzoefu mdogo wa kuweza kupata nafasi ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi. Serikali itaendelea kuweka mkazo mkubwa wa kuendeleza Sekta hii ili iweze kutoa ajira zaidi na kuboresha Vipato vya Wananchi na hatimaye kupunguza Umaskini.
55. Tatu, Sekta hii ni chimbuko la maendeleo ya Ujasiriamali na Sekta Binafsi ya Nchi yetu. Historia inaonesha kuwa Wajasiriamali wengi waliofanikiwa walianza na Sekta hii na hatimaye wakakua. Kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuwezesha maendeleo ya Viwanda Vidogo Nchini. Programu ya Kuboresha Mazingira ya Biashara (BEST) kwa kiasi kikubwa ililenga kurahisisha mazingira ya utendaji wa Sekta hii. Pia, Serikali imeanzisha Mifuko mbalimbali ya Mitaji ikiwemo ule wa Kuendeleza Ujasiriamali (National Entrepreneurship Development Fund-NEDF) ili kuwasaidia Wajasiriamali Wadogo kuanzisha na kuendeleza biashara zao.
56. Serikali itaendelea kuboresha Sekta hii kwa kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu. Ninatoa rai kwa Wadau wengine ikiwa ni pamoja na Waheshimiwa Wabunge, Wabia wa Maendeleo, Taasisi zisizo za Kiserikali na Sekta Binafsi tushirikiane kuendeleza Sekta hii, kwani ina fursa nzuri katika Kuongeza Ajira, Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini.
MAENDELEO YA UTALII NCHINI
Mheshimiwa Spika,
57. Utalii ni Sekta ambayo ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa Sekta nyingine za Kiuchumi na Kijamii kama vile Usafirishaji, Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo, Sanaa za Mikono na Michezo. Utalii ni Tasnia pekee ambayo huweza kuongeza Ajira kwa haraka sana. Inakadiriwa kwamba kila Mtalii mmoja anapokuwa Nchini huchangia takriban fursa 12 za ajira za aina mbalimbali. Vilevile, Tasnia ya Utalii inachangia robo ya Mapato ya Fedha za Kigeni tunazopata kwa mwaka. Kwa kiasi kikubwa Utalii wetu umetegemea sana Mbuga na Hifadhi za Wanyamapori kwa upande wa Tanzania Bara na Utalii wa Ufukweni kwa upande wa Zanzibar. Masoko yetu Makuu ya Watalii ni Marekani, Uingereza, Ujerumani, Italia, Afrika Kusini, Canada, Uholanzi, Hispania, Australia na Ufaransa.
Hali ya Biashara ya Utalii
Mheshimiwa Spika,
58. Katika mwaka 2010, idadi ya Watalii kutoka Nje ya Nchi iliongezeka kwa Asilimia 10 kutoka Watalii 714,367 mwaka 2009 hadi Watalii 782,699 mwaka 2010. Watalii hao walitembelea Vivutio mbalimbali hapa Nchini na waliliingizia Taifa Dola za Kimarekani Bilioni 1.25 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani Bilioni 1.15 zilizopatikana mwaka 2009. Ongezeko hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za kutangaza na kuhamasisha Utalii nje ya Nchi pamoja na uboreshaji wa Sekta ya huduma za Kitalii, hususan Hoteli na Miundombinu ndani ya Nchi.
59. Mwaka 2011, Watalii wa Kimataifa waliotembelea Hifadhi za Taifa kuanzia Januari hadi Juni wameongezeka kwa zaidi ya Asilimia 21.73 hadi kufikia Watalii 197,736; ikilinganishwa na Watalii 162,437 waliotembelea Hifadhi hizo katika kipindi hicho, mwaka 2010. Vilevile, katika kipindi hicho hicho Watalii wa Ndani wameongezeka kwa zaidi ya Asilimia 152 kutoka Watalii 121,976 mwaka 2010 hadi 308,038 mwaka 2011. Hizi ni dalili kwamba juhudi za Serikali na Wadau wote wa Utalii katika kukuza Utalii Nchini zimeanza kuzaa matunda tarajiwa. Hata hivyo hatuna budi kuendeleza juhudi hizi maradufu ili kuongeza Pato la Taifa.
60. Pamoja na mafanikio hayo na mengine ambayo yalitajwa vizuri kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati wa kuwasilisha Makadirio ya Bajeti ya mwaka 2011/2012, zipo changamoto zinazoikabili Sekta ya Utalii na Wizara kwa ujumla. Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia majadiliano ya Wizara hii wameainisha changamoto nyingi kuanzia Watumishi wasiokuwa waaminifu, utoroshaji wa Nyara za Serikali, Ujangili kwenye Mbuga za Wanyama na nyingine nyingi. Napenda kuwaahidi Watanzania kuwa Serikali haitakaa kimya kuona Maliasili zake zinaibiwa na kunufaisha Watu wengine na siyo Watanzania. Uchunguzi wa kina utafanyika kwa hoja zote zilizotolewa hapa Bungeni na hatua stahiki zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhujumu Rasilimali zetu. Nichukue nafasi hii kuwaagiza Wafanyakazi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake kufanyakazi kwa uadilifu na uamifu mkubwa kwa manufaa ya Taifa letu. Kumbukeni Vyeo mlivyopewa ni dhamana na Taifa haliwatarajii kutumia dhamana hiyo kwa manufaa yenu Binafsi, bali kwa manufaa ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika,
61. Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikichukuwa hatua mbalimbali ili kuhakikisha Sekta ya Utalii Nchini inakua na kuendelea. Pamoja na mambo mengine, Serikali itaendelea kufanya yafuatayo ili kuongea tija ya Sekta ya Utalii hapa Nchini:
i. Kushirikiana na Wadau wa Maendeleo kuelekeza Rasilimali zaidi katika kujenga na kuboresha miundombinu itakayochochea maendeleo ya Utalii hapa Nchini, hususan maeneo ya Kusini na Magharibi mwa Nchi;
ii. Kuhamasisha uwekezaji kwenye maeneo ya utalii na kuandaa mazingira bora ikiwemo kuimarisha mafunzo kwa Watoaji huduma za Utalii Nchini;
iii. Kuendelea na zoezi la kupanga Hoteli katika Kadaraja ili kudumisha ubora wa huduma za Malazi;
iv. Kuongeza kasi katika kutangaza Vivutio vya Utalii katika Masoko mapya na kudumisha Utangazaji kwenye Masoko ya asili;
v. Kuhamasisha uwekezaji katika huduma zinazokidhi matakwa ya Watalii wa Ndani; na
vi. Halmashauri kuhamasisha uwekezaji katika huduma za Utalii.
Mheshimiwa Spika,
62. Hivi sasa Tanzania inafikika kwa urahisi na kwa muda mfupi kutoka Nchi za Ulaya Mashariki, Asia ya Kati na Mashariki ya Mbali. Hali hii imeboreka zaidi baada ya baadhi ya Mashirika ya Ndege ya Nje kama ya Nchi za Qatar, Uturuki na Oman kuongeza safari za kuja Nchini.
63. Hivyo, napenda kuwakumbusha Wadau wote wa Utalii Nchini kuwa, ili kukuza biashara na uchangiaji wa Sekta ya Utalii katika uchumi wa Taifa, hatuna budi kujipanga na kufanya Kampeni maalum kutangaza Utalii katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za SADC ili kukuza Utalii na kuongeza Pato la Taifa na Ajira.
ELIMU
Mheshimiwa Spika,
64. Niruhusu niongelee kidogo Sekta ya Elimu na hasa Matokeo ya Kidato cha Sita na nafasi ya Chuo Kikuu Huria.
Matokeo ya Kidato cha Sita
Mheshimiwa Spika,
65. Matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Kidato cha Sita mwaka 2011, yanaonesha kuwa Watahiniwa 44,720 walifanya Mtihani wa kumaliza Kidato cha Sita. Kati yao Watahiniwa 41,142 walifaulu sawa na Asilimia 92.1 ya watahiniwa wote.
66. Jambo la kutia moyo ni kuwa Wanafunzi walifanya vizuri katika Masomo ya Sayansi ikilinganishwa na miaka ya nyuma hasa mwaka 2010. Kwa mfano, ufaulu wa Hisabati uliongezeka kutoka Asilimia 79.1 ya Wanafunzi 5,882 mwaka 2010 hadi Asilimia 81.5 ya Wanafunzi 6,723 mwaka 2011, Kemia uliongezeka kutoka 77.4 ya Wanafunzi 8,480 mwaka 2010 hadi Asilimia 80.0 ya Wanafunzi 9,071 na Fizikia uliongezeka kutoka Asilimia 63.2 ya Wanafunzi 5,125 mwaka 2010 hadi Asilimia 67.0 ya Wanafunzi 5,724 mwaka 2011.
67. Hii ni hatua nzuri katika maendeleo ya Sayansi hapa Nchini ikizingatiwa kuwa Masomo ya Sayansi yamekuwa na ufaulu usioridhisha kwa muda mrefu. Napenda kutoa Pongezi kwa Wanafunzi na Wadau wote waliohusika katika kuleta mafanikio haya.
Mheshimiwa Spika,
68. Serikali kwa kushirikiana na Bunge tumeshaonesha kuridhishwa kwetu na juhudi za Wanafunzi hawa kwa kuwaalika Wanafunzi Wavulana 10 na Wasichana 10 waliofanya vizuri kwenye Mtihani huo Kitaifa ndani ya Bunge lako Tukufu na kuwapongeza na kuwapa zawadi.
Aidha, kupitia Bunge lako Tukufu tulitoa zawadi ya Meza za Maabara zinazohamishika kwa Shule za Sekondari 7 za Kata zilizosaidia kuandaa baadhi ya Wanafunzi waliokaribishwa hapa Bungeni. Kwa kushirikiana nawe Mheshimiwa Spika, tulizindua Meza hiyo hapa kwenye Viwanja vya Bunge. Hizi zote ni jitihada za kutoa msukumo kwa Wanafunzi, Walimu, Wazazi na Wadau wengine kuinua ufaulu wa Masomo ya Sayansi.
69. Napenda kuwahamasisha Wanafunzi wapende Masomo ya Hisabati na Sayansi. Bila Hisabati na Sayansi katika Karne hii ya Utandawazi ni dhahiri kuwa hatutakuwa na Watu Wabunifu na Wagunduzi katika Kizazi chetu. Tuandae mazingira bora ya kuwasaidia Watoto wetu kupenda kusoma Masomo ya Sayansi na Hisabati ambayo yana fursa kubwa katika Soko la Ajira na pia yana umuhimu wa kipekee katika Mazingira ya Dunia tunayoishi leo.
Elimu ya Juu na Nafasi ya Chuo Kikuu Huria
Mheshimiwa Spika,
70. Tanzania ina Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki 42. Kumekuwa na mafanikio makubwa katika Elimu ya Juu katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mfano, Udahili katika Vyuo vya Elimu ya Juu uliongezeka kutoka Wanafunzi 45,501 mwaka 2006/2007 hadi 140,000 mwaka 2010/2011 katika Vyuo Vikuu vya Umma na Binafsi. Ongezeko hili ni sawa na Asilimia 206 kwa kipindi cha Miaka5. Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Chuo hiki ndicho kimekuwa kinadahili idadi kubwa ya Wanafunzi kuliko Vyuo Vikuu vingine vyote Nchini katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mfano, katika mwaka 2007/2008, Chuo kilidahili Wanafunzi 25,829 sawa na Asilimia 34 ya Wanafunzi 76,172 waliodahiliwa katika Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki katika mwaka huo. Katika mwaka 2010/2011, Chuo Kikuu Huria kilidahili Wanafunzi 44,272 sawa na Asilimia 32 ya Wanafunzi 139,638 waliodahiliwa katika Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki mwaka huo. Idadi hiyo ya Wanafunzi waliodahiliwa katika Chuo Kikuu Huria inadhihirisha umuhimu wa Chuo hicho kwa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Spika,
71. Chuo hiki kilichoanzishwa mwaka 1993, kinatoa mafunzo kwa Watanzania kwa gharama nafuu kuliko Vyuo Vikuu vingine Nchini. Aidha, Chuo kinatoa fursa ya kusoma bila Mwanafunzi kulazimika kuacha ajira yake, kinatoa elimu kulingana na ratiba ya Mwanafunzi katika shughuli zake za siku hadi siku. Hii ni fursa muhimu kwa Watanzania wote wanaotambua kuwa “Elimu haina Mwisho”. Chuo Kikuu Huria huendesha Elimu na Mafunzo kwa kutumia mbinu mbalimbali za kufundisha kwa Masafa. Elimu Masafa inaweza kufafanuliwa kama “Elimu inayotolewa na Chuo, Taasisi au Kikundi cha Wanataaluma kwa kutumia mbinu za TEHAMA ambapo Wanafunzi hufanya mawasiliano na Wahadhiri kwa Mtandao, Redio au Televisheni bila kuwapo Darasani kama ilivyo kwenye Vyuo vingine vya Masomo kwa njia ya Darasani”.
72. Elimu ya Masafa inaweza kutolewa mahali popote hata katika ngazi ya Vijijini iwapo umeme wa uhakika na Mawasiliano ya Simu, Redio, Video, na Intaneti yatakuwapo. Vituo vinaweza kuanzishwa na watu wengi wakapata Elimu hiyo kwa kuunganishwa na Chuo chenye Wahadhiri wenye sifa walio mbali na sehemu hizo.
Mheshimiwa Spika,
73. Kutokana na umuhimu wa Mawasiliano ya Simu, Redio, Video na Intaneti katika Elimu ya Masafa, ninaelewa tunazo changamoto za kuhakikisha Miundombinu ya Mawasiliano ipo hadi Vijijini. Wakati Serikali inajitahidi kupanua Mtandao wa Mawasiliano hadi Vijijini, napenda kuwasihi Watanzania hususan Watu walio Kazini (In- Service) kuchangamkia Elimu hii ya Masafa kwa kujiunga na Chuo Kikuu Huria Tanzania na Vyuo vingine vinavyotoa Elimu kama hiyo.
74. Hata hivyo, Takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa Wanaume ndio wanaochangamkia fursa hii kwa wingi kuliko Wanawake. Kwa mfano mwaka 2007/2008 Wanawake waliodahiliwa na Chuo Kikuu Huria walikuwa Asilimia 23 tu ya Wanafunzi 19,909 waliodahiliwa. Mwaka 2010/2011 Wanawake walikuwa Asilimia 30 ya Wanafunzi 44,272 waliodahiliwa. Hivyo, nawahimiza Wanafunzi wa Kike bila kujali tofauti za umri kutumia fursa hii ya Elimu ambayo inamwezesha Mwanamke kupata Elimu wakati akiendelea na majukumu yake kwa Familia na Taifa. Nawaomba Wananchi wote kujiunga na utaratibu huu wa Elimu kwa Masafa ili kujiletea maendeleo ya haraka.
Ajali za Barabarani
Mheshimiwa Spika,
75. Nimeongea kwa kirefu masuala mbalimbali yanayohusu Uchumi na Maendeleo ya Nchi yetu. Lakini kabla sijahitimisha hotuba yangu, niruhusu kwa masikitiko makubwa kuongelea tena kuhusu Ajali za Barabarani. Takwimu zinaonesha kwamba Ajali za Barabarani zimekuwa zikiongezeka kwa kasi ya Wastani wa Asilimia Nane (8) kwa mwaka kati ya mwaka 2005 na 2010 na idadi ya Vifo vilivyotokea iliongezeka kwa Wastani wa Asilimia 8.3 kwa mwaka katika kipindi hicho. Utafiti uliofanywa na Wizara za Ujenzi, Uchukuzi na Mambo ya Ndani ya Nchi naonesha kuwa, ajali hizo husababishwa na uzembe wa watumiaji wa barabara, ubovu wa magari na ubovu wa barabara.
Mheshimiwa Spika,
76. Pamoja na hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa kukabiliana na tatizo la Ajali za Barabarani, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kutekeleza mabadiliko makubwa katika suala la Usalama Barabarani kama ifuatavyo:
i. Kutunga Sera ya Usalama Barabarani mwezi Septemba 2009;
ii. Kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2011/2012, Serikali itaanzisha Wakala wa Taifa wa Usalama Barabarani (National Road Safety Agency) kwa kutumia Sheria ya Wakala wa Serikali ya mwaka 1997. Wakala atasimamia kwa karibu Sheria ya Usalama Barabarani;
iii. Katika mwaka huu wa fedha wa 2011/2012, Serikali italeta hapa Bungeni Muswada wa Sheria mpya ya Usalama Barabarani badala ya Sheria iliyopo ya mwaka 1973; Sheria hii itawezesha kutekelezwa kwa Mikakati ya kukabiliana na Ajali ikiwa ni pamoja na kuainisha Muundo wa Kitaasisi wa kusimamia Usalama Barabarani;
iv. Kuanzisha utaratibu kufunga vifaa vya kuwezesha ufuatiliaji wa mahali gari lilipo wakati wowote na mwendo kasi wake kwa kuanzia na Mabasi na Malori ya kwenda Mikoani;
v. Kuanzisha utaratibu wa Mafunzo, Majaribio na Mitihani ya Nadharia na Vitendo kwa Madereva walio kazini;
vi. Kuendeleza elimu ya darasani kuhusu Usalama Barabarani katika Shule za Msingi na Vyuo vya Ualimu na Umma kupitia Redio, Runinga, Magazeti, na Matangazo mbalimbali;
vii. Jeshi la Polisi wa Usalama Barabarani kuendelea kuwachukulia hatua kali za Kisheria kwa wale wanaovunja Sheria za Usalama Barabarani.
Mheshimiwa Spika,
77. Ajali hizo za barabarani zinajumuisha pia Ajali za Pikipiki na Bajaji. Ajali zilizohusu Pikipiki na Bajaji nazo zimeongezeka kutoka jumla ya Ajali 1,683 mwaka 2007 hadi 4,363 mwaka 2010. Ongezeko hili ni Wastani wa Asilimia 38 kwa mwaka. Jumla ya Vifo vilivyotokana na Ajali hizo ni Watu 193 mwaka 2007 ikilinganishwa na Vifo 683 mwaka 2010, sawa na ongezeko la Wastani wa Asilimia 53 ya Vifo kwa mwaka.
78. Ili kukabiliana na ongezeko hili ya Ajali na Vifo Serikali imefanya yafuatayo:
i. Mwaka 2010, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imetunga Kanuni za Sheria ya Leseni za Usafirishaji ya mwaka 1973, kuhusu usafiri wa Pikipiki na Bajaji iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009;
ii. Kanuni hizo zinawataka waendesha Pikipiki na Bajaji kuzingatia masharti yafuatayo:
  • Pikipiki na Bajaji zitaruhusiwa kupita na kuegeshwa katika barabara mahsusi na maeneo yaliyoainishwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
  • Mwendesha Pikipiki haruhusiwi kubeba zaidi ya Abiria mmoja;
  • Mwendesha Bajaji haruhusiwi kubeba zaidi ya Abiria watatu;
  • Mwendesha Pikipiki na Bajaji anapaswa kuzingatia kikomo cha mwendo kasi kinachooneshwa katika Alama za Barabarani na kwa wakati wowote haruhusiwi kuendesha kwa mwendo unaozidi Kilometa 50 kwa saa;
  • Mwendesha Bajaji haruhusiwi kupakia idadi ya Abiria inayozidi idadi iliyoainishwa katika leseni yake ya usafirishaji Abiria;
  • Mwendesha Pikipiki anapaswa kuvaa Kofia ya Chuma yenye alama inayoonesha eneo lake la usafirishaji wa Abiria;
  • Mwendesha Pikipiki anapaswa kuhakikisha kuwa Abiria wake amevalia Kofia ya Chuma;
  • Mtoto wa umri wa miaka tisa (9) au umri wa chini yake haruhusiwi kuwa Abiria kwenye Pikipiki;
  • Mwendesha Pikipiki haruhusiwi kutumia Simu ya Mkononi au Chombo kingine cha Mawasiliano wakati anaendesha Pikipiki;
  • Mwendesha Bajaji atapaswa kuzingatia kuwa na Mikanda ya Usalama ya kuwafungia kwenye viti kila Abiria na ni sharti Bajaji ziwe na milango pande zote mbili ili kuwakinga Abiria;
  • Mtoto wa umri wa miaka tisa (9) au umri wa chini yake haruhusiwi kuwa abiria kwenye Bajaji isipokuwa kama ameambatana na Abiria mwenye umri mkubwa;
  • Mwendesha Pikipiki au Bajaji anapaswa kuzingatia Sheria ya Usalama Barabarani.
Mheshimiwa Spika,
79. Tayari SUMATRA kwa kushirikiana na Halmashauri zote Nchini zimetiliana saini Makubaliano ya kusimamia utekelezaji wa Kanuni hizo katika maeneo ya Halmashauri.
Aidha SUMATRA, Jeshi la Polisi wa Usalama Barabarani na Halmashauri kwa pamoja wanatekeleza Mikakati ya kuhakikisha kuwa Waendeshaji wa Pikipiki na Bajaji wanazingatia Kanuni hizi ili kupunguza ajali.
Mheshimiwa Spika,
80. Sina maelezo ya kuonesha masikitiko yangu kuhusu kiwango cha kutisha cha Ajali za Barabarani zinazotokea mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya hapa nchini. Ninachoweza kusema ni kuwataka wahusika wakuu katika Serikali kuchukua hatua za dhati na kwa haraka kutekeleza Sera, Sheria, Kanuni, Mipango na Mikakati mbalimbali iliyokwishaanzishwa ya kukabiliana na Ajali za Barabarani.
81. Naiagiza Wizara ya Ujenzi kuhakikisha inawasilisha hapa Bungeni mwezi Novemba 2011, Muswada wa Sheria mpya ya Usalama Barabarani ili kuwezesha utekelezaji wa haraka wa masuala mbalimbali yatakayoainishwa na Sheria hiyo kwa lengo la kudhibiti Ajali za Barabarani mapema zaidi. Aidha, Askari wa Usalama Barabarani kwa kushirikiana na SUMATRA na Halmashauri mbalimbali Nchini kwa pamoja wasimamie utekelezaji wa Kanuni za Sura ya 317 ya Sheria ya Leseni za Usafirishaji ya mwaka 1973 iliyofanyiwa Marekebisho mwaka 2009, kuhusu usafiri wa Pikipiki na Bajaji.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
82. Kabla ya kuhitimisha hoja yangu, napenda nisisitize maeneo machache yafuatayo:
Moja: Uko uhusiano mkubwa kati ya Ukuaji wa Uchumi na Uwekezaji. Tumeweza kusimamia Uchumi wa Nchi yetu na kuwezesha kukua kwa viwango vinavyoridhisha ambavyo hata Mataifa mengine na Mashirika ya Nje yanatusifia. Hata hivyo, bado safari ni ndefu ya kuwaletea maendeleo Watanzania. Tunahitaji mageuzi makubwa Kifikra na Kiuchumi ili kutuwezesha kufikia lengo letu la Kuondoa Umaskini. Tunazo fursa ambazo tukizisimamia vizuri Umaskini utaondoka katika muda mfupi zaidi. Niwaombe Watanzania wenzangu tutumie fursa hizo ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu Wawekezaji wa Ndani na Nje kuwekeza Nchini bila kuwaogopesha.
Pili: Tunalo tatizo la Uhaba wa Chakula katika Nchi zote za Mashariki ya Afrika Tanzania ikiwa ni mojawapo. Tatizo hilo linakua kutokana na Ukame unaoendelea. Nawaomba Wananchi wote kuchukua tahadhari ya kutumia chakula kidogo tulichonacho. Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa Chakula Nchini;
Tatu: Tunayo nafasi ya kutumia Kilimo katika kubadili maisha ya Mtanzania. “KILIMO KWANZA” ndiyo Kaulimbiu na Azma yetu ambayo ni kichocheo katika kusukuma yale yaliyomo katika Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo ASDP kwa Vitendo. Nasisitiza kwamba Kaulimbiu ya “KILIMO KWANZA” siyo mbadala wa ASDP. Tuitumie Kaulimbiu hii kusukuma shughuli zilizoainishwa katika Mpango huu kuendeleza Kilimo kwa kasi zaidi;
Nne: Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Nyuki zinategemeana kwa kiasi kikubwa. Watanzania wengi wanategemea matumizi ya mazao ya Sekta hizi kama Chakula lakini vilevile kama silaha ya kupambana na umaskini. Tushirikiane na Serikali kuziendeleza Sekta hizi ili kuondoa umaskini kwa Wananchi wetu. Tunayo fursa kubwa katika Sekta ya Nyuki, tuanze kuitumia vizuri Sekta hiyo kujenga Uchumi wa Nchi yetu;
Tano: Tumepitisha Bajeti ya Serikali ambayo inategemea sana ukusanyaji wa Mapato ya Ndani ili kupunguza utegemezi wa Vyombo vya Nje. Tuongeze juhudi kufanya kazi ili Mapato yaongezeke na hivyo kuongeza makusanyo ya Kodi. Aidha, tutumie fedha za Bajeti tuliyoipitisha iwe mfano wa kuigwa kwa kupanga na kutumia vizuri Rasilimali tulizonazo;
Sita: Tunahitaji kwa dhati kabisa kuweka Akili zetu zote katika kuongeza uzalishaji katika Sekta zote za Kilimo, Viwanda, na kuboresha huduma za Utalii. Tuongeze kasi katika kuhamasisha uzalishaji na tija katika maeneo yote.
Shukrani
Mheshimiwa Spika,
83. Napenda nimalizie kwa kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Nikushukuru kwa namna ya pekee wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri kulingana na Kanuni za Bunge. Aidha, niwashukuru Wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe na Mheshimiwa Sylvester Massele Mabumba, Mbunge wa Dole kwa kuongoza vizuri baadhi ya Vikao vya Bunge wakati wa Mkutano huu. Ninawashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu ya dhati na yenye mantiki kwa ajili ya Maendeleo ya Nchi yetu. Niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Watumishi na Wataalam wote wa Serikali waliosaidia kujibu Maswali na Hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge zilizojitokeza hapa wakati wa Mkutano huu. Vilevile, nawashukuru Waandishi wa Vyombo vya Habari kwa kuwapatia Wananchi habari kuhusu Majadiliano yaliyokuwa yanaendelea hapa Bungeni.
84. Napenda kuwashukuru Madereva wote ambao wamekuwa makini katika kazi ya kuwaendesha viongozi wote wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na Wataalam kutoka sehemu mbalimbali Nchini na kuwawezesha kufika hapa Dodoma kuhudhuria Mkutano huu wa Nne. Vilevile, nawashukuru Wananchi wa Mkoa wa Dodoma, Wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Mhandisi Dkt. James Alex Msekela kwa ukarimu wao kwa muda wote tuliokaa hapa. Navishukuru pia Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambavyo vimehakikisha muda wote tumekaa kwa Amani na kwa Utulivu mkubwa. Mwisho namshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah na Watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa huduma nzuri zilizowezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa katika Mkutano huu bila matatizo. Nitumie fursa hii pia kumpa Pole Dkt. Kashilillah kwa maradhi yanayomsumbua wakati wa kipindi tulichokuwa hapa na kumtakia apone haraka na kurejea katika Afya Njema.
Mheshimiwa Spika,
85. Wakati tunahitimisha Mkutano huu leo na kuelekea katika Majimbo yetu, nitumie muda huu kumwomba Mwenyezi Mungu awatangulie, awalinde na awaongoze katika safari ya kurejea nyumbani. Tunapokaribia kumaliza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, napenda niwatakie Waislamu wote na Wananchi wote kwa ujumla Idd-El-Fitr njema!!
Mheshimiwa Spika,
86. Baada ya maelezo hayo napenda kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 8 Novemba 2011, Siku ya Jumanne, Saa 3:00 Asubuhilitakapokutana katika Ukumbi huu, hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
87. Naomba kutoa hoja.

No comments: