Serikali imeyafungia kutochapishwa Magazeti ya
MWANANCHI na MTANZANIA kuanzia 27 Septemba,2013 kutokana na mwenendo wa
magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia
ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola hivyo kuhatarisha
amani na mshikamano ulipo nchini.
Gazeti la MWANANCHI limefungiwa kutochapishwa kwa siku
kumi na nne(14) kuanzia 27 Septemba,2013.Adhabu hii imetangazwa kwa Tangazo la
Serikali(Government Notice )Namba 333 la tarehe 27 septemba,2013.
Gazeti la MWANANCHI limepewa adhabu hiyo kutokana na
hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa
amani,mfano tarehe 17 Julai,2013 katika toleo Namba 4774 ilichapisha habari
isemayo “MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013” kwa kuchapisha waraka
uliozuiliwa kwa matumizi ya vyombo vya habari waraka huo ulikuwa wa Siri
haukupaswa kuchapishwa Magazetini.
Aidha, katika toleo la Jumamosi,tarehe 17 Agosti,2013
lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho “WAISLAM WASALI CHINI YA ULINZI MKALI”
habari hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa mkali mwenye hasira.Habari
na picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka Mbwa katika
maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya kiislam.Jambo ambalo halikuwa la
ukweli.
Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo halikupeleka
mbwa katika maeneo ya Misikiti.Serikali na jeshi la Polisi linaheshimu na
kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo Jeshi lake haliwezi
kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.
Hivyo basi,kwa gazeti hili kuchapisha habari
iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi
na waumini wa dini ya kiislam mbwa ni najisi hapaswi kuingia katika
maeneo ya ibada.
Gazeti la MTANZANIA limefungiwa kutochapishwa kwa siku
tisini(90) kuanzia tarehe 27 Septemba,2013 kwa kuchapisha habari zenye
uchochezi.Gazeti hili limeonywa mara nyingi lirekebishe mtindo wake wa
uandishi wa kichochezi na lizingatie maadili na Sheria na Kanuni za
fani ya Habari.
Pamoja na kuonywa gazeti hili halikuonyesha kuzingatia
maelekezo ya Msajili wa Magazeti, mfano ;katika toleo na 7262 la 20 Machi,2013
liliandika habari yenye kichwa kisemacho “URAIS WA DAMU”,tarehe 12
Juni,2013,toleo Namba 7344 lilichapisha makala isemayo “MAPINDUZI HAYAEPUKIKI”.
Aidha, siku ya Jumatano,tarehe 18 Septemba,2013 katika
toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha Kichwa cha habari kisemacho
“SERIKALI YANUKA DAMU” taarifa hiyo ilikolezwa na picha zilizo unganishwa kwa
ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta kutapakaza rangi nyekundu mithili ya
damu nyingi kumwagika .Katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila uthibitisho
kuwa Jeshi la Polisi linahusika na wahanga waliomizwa na watu wasiojulikana
kwa kumwagiwa tindikali na waliyovamiwa na kujeruhiwa vibaya.
Vile vile gazeti hilo limeishtumu serikali kuwa goigoi
katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi.
Kwa ujumla wake habari hiyo ni ya kichochezi ina lengo
la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama wavione
kuwa haviwasaidii.
Kutokana na makosa yalitajwa hapo juu serikali
imelifungia gazeti la Mtanzania kutochapishwa kwa muda wa siku tisini(90)
kwa Tangazo la Serikali Namba 332(Government Notice No.332) la tarehe 27
septemba,2013,.
Serikali inawataka wamiliki,wahariri na wanahabari kwa
ujumla kuwa makini,kuzingatia weledi,miiko na madili yataaluma uandishi wa
habari.
Serikali inawataka wamiliki na hasa wahariri kuhakisha
kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa vinazingatia
taaluma,kuweka mbele maslahi ya taifa letu kwa kuwa na uzalendo wa hali ya juu.
Serikali inavionya vyombo vya habari vinavyoutumia
uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia hatua kali ikiwemo ya
kuvifungia .Serikali haitakubali kuona vyombo vya habari kuwa chanzo cha
uvunjifu wa amani nchini.
Imetolewa na
MKURUGENZI IDARA YA HABARI
WIZARA YA HABARI,VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
No comments:
Post a Comment