KWA KUWA, Sisi, Wananchi wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania tumeamuarasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii
inayoheshimu na kuzingatia misingi yautu, uhuru, haki, usawa, udugu, amani,
umoja na mshikamano katika nyanja zote za maisha yetu;
NA KWA KUWA, tunaamini kuwa misingi hiyo
inaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye mfumo wa demokrasia na utawala bora
ambayo Serikali yake inasimamiwana Bunge lenye Wabunge waliochaguliwa na
wanaowawakilisha wananchi na Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki
bila woga wala upendeleo wowote, nakuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa
na kudumishwa na kwamba wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu;
NA KWA KUWA, umuhimu wa kutunza mali ya Mamlaka
za Nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu, ubadhilifu, na
kuhimiza matumizi bora na endelevu ya rasilimali na maliasili zetu pamoja na
kulinda na kuhifadhi mazingira yetu kwa mustakabali wa maisha ya kizazi cha
sasa na vizazi vijavyo;
NA KWA KUWA, umuhimu na faida za kujenga, kukuza
na kuendeleza, amani, umoja, urafiki na ushirikiano miongoni mwa Watanzania,
Mataifa mbalimbali ya Afrika na Dunia kwa ujumla;
KWA KUWA, azma ya kujenga Umoja wa Bara la
Afrika katika misingi ya Umajimui wa Afrika ambao inadhihirishwa na Muungano wa
iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar;
NA KWA KUENDELEZA, dhamira yetu hiyo ni muhimu:
(a) kulinda, kuimarisha na kuudumisha Muungano
wa nchi za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar;
(b)
kujenga Taifa huru na linalojitegemea;
(c) kuimarisha na kuendeleza utawala wa sheria;
(d) kukuza na kuendeleza maadili, uwajibikaji
na uwazi;
(e) kujenga umoja na mshikamano utakaowezesha
kutimiza malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kimazingira na kulinda urithi
kwa ujumla;
(f) kujenga na kuendeleza ukuu wa mamlaka ya
watu;
(g) kujenga na kuendeleza utii wa mamlaka ya
Katiba; na
(h) kuimarisha na kudumisha uzalendo kwa Taifa
miongoni mwa Watanzania;
NA KWA KUZINGATIA, urithi tulioachiwa na
Waasisi wa Taifa letu wa kujenga
nchi yenye Umoja wa Watu wake ambao hawabaguani
kwa misingi ya ukabila, udini,
rangi,
jinsi au ubaguzi wa aina nyingine yoyote;
NA
KWA KUZINGATIA, uzoefu wa zaidi ya Miaka Hamsini ya Uhuru na Miaka Hamsini ya
Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na umuhimu wa
ushiriki mpana na bayana wa wananchi katika utungaji wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania; 2
HIVYO
BASI, KATIBA HII YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ILIYOPENDEKEZWA NA BUNGE
MAALUM LA KATIBA imetungwa na SISI WANANCHI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA upitia KURA YA MAONI kwa madhumuni ya kujenga
jamii kama hiyo, na kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaongozwa
na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na utawala wa sheria,
kujitegemea na isiyokuwa na dini. ‐ 3 ‐
SURA YA KWANZA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
SEHEMU YA KWANZA
MIPAKA, ALAMA, LUGHA, UTAMADUNI NA TUNU ZA
TAIFA
Jamhuri ya Muungano
1.-(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
Shirikisho lenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri
ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za
Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.
(2) Jamhuri ya Muungano ni Shirikisho la
kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea,
utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.
(3) Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa
katika Ibara ndogo ya (1), ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Katiba hii, kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano
hayo.
Eneo la Jamhuri ya Muungano
2. Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la
Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake
ya bahari.
Alama
na Siku Kuu za Taifa
3.-(1)
Alama za Taifa ni:
(a) Bendera ya Taifa;
(b) Wimbo wa Taifa; na
(c) Nembo ya Taifa,
kama zitakavyoainishwa katika sheria
itakayotungwa na Bunge.
(2) Siku
Kuu za Kitaifa zitakuwa ni:
(a) Siku ya Uhuru wa Tanganyika,
itakayoadhimishwa tarehe 9 Disemba;
(b) Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar,
itakayoadhimishwa tarehe 12 Januari;
(c) Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
itakayoadhimishwa tarehe 26 Aprili; na
(d) Siku Kuu nyingine zitakazoainishwa na
sheria za nchi.
(3) Kila
Siku Kuu ya Kitaifa itakuwa ni siku ya mapumziko.
Lugha
ya Taifa na lugha za alama
4.-(1)
Lugha ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano ni Kiswahili na itatumika katika
mawasiliano rasmi ya kitaifa na kiserikali.
(2)
Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), lugha ya Kiingereza inaweza
kutumika kuwa lugha rasmi ya mawasiliano ya kiserikali pale itakapohitajika.
(3)
Serikali itaweka mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa mawasiliano ya lugha
mbadala zikiwemo lugha za alama na nukta nundu kwenye sehemu muhimu za umma na
katika vyombo vya habari vinavyotangaza habari zake kitaifa kwa ajili ya watu
wenye mahitaji maalum.
‐ 4 ‐
Tunu za Taifa
5.
Jamhuri ya Muungano itaenzi na kuzingatia Tunu za Taifa
zifuatazo:
(a)
utu; (b) uzalendo; (c) uadilifu; (d) umoja; (e) uwazi; (f) uwajibikaji; na (g)
lugha ya Taifa.
SEHEMU
YA PILI
MAMLAKA
YA WANANCHI, UTII NA HIFADHI YA KATIBA
Mamlaka ya wananchi
6.
Jamhuri ya Muungano ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia inayozingatia haki
ya kijamii, na kwa hiyo:
(a)
wananchi ndio msingi wa mamlaka za nchi, na Serikali itapata madaraka na
mamlaka yake kutoka kwa wananchi ambao kwa umoja na ujumla wao wanaimiliki na
kuipatia Katiba hii uhalali;
(b)
lengo kuu la Serikali litakuwa ni maendeleo na ustawi wa wananchi;
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi; na
(d) wananchi watashiriki katika shughuli za
Serikali kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
Watu na Serikali
7.-(1) Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na vyombo vyake, katika uendeshaji na utekelezaji wa shughuli zake
utazingatia azma ya kukuza umoja wa kitaifa na kudumisha heshima ya Taifa.
(2) Kwa madhumuni ya masharti ya Ibara ndogo (1),
mamlaka ya nchi na vyombo vyake vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote
kwa lengo la kuhakikisha kwamba:
(a) utu na haki nyingine zote za binadamu
zinaheshimiwa na kuthaminiwa;
(b) sheria za nchi zinasimamiwa na kutekelezwa;
(c) Serikali itahakikisha kuwa shughuli
zinazofanywa zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa
Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa
jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine;
(d) ardhi ikiwa rasilimali kuu na msingi wa
Taifa, inalindwa, inatunzwa na kutumiwa na wananchi wa Tanzania kwa manufaa,
maslahi na ustawi wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo;
(e) maendeleo ya uchumi wa Taifa yanapangwa na
kukuzwa kwa ulinganifu na kwa pamoja na kwa namna ambayo inawanufaisha wananchi
wote;
(f) kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi
anafanya kazi, na kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu
kipato chake; ‐ 5 ‐
(g) utu, heshima na haki nyingine zote za
binadamu zinahifadhiwa na kudumishwa kwa kuzingatia mila na desturi za
kitanzania na kwa kufuata mikataba mbalimbali iliyoridhiwa na Jamhuri ya
Muungano;
(h) mamlaka za nchi zinatoa fursa na haki
zilizo sawa kwa wananchi wote, wanawake na waume, bila ya kujali rangi, kabila,
nasaba, dini au hali ya mtu;
(i) aina zote za dhulma, vitisho, ubaguzi,
unyanyasaji, rushwa, uonevu au upendeleozinaondolewa nchini;
(j) utajiri wa rasilimali na maliasili za Taifa
unaelekezwa katika kuleta maendeleo, kuondoa umaskini, ujinga na maradhi; na
(k) nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya
demokrasia na kujitegemea.
Mamlaka na utii wa Katiba
8.-(1) Bila ya kuathiri masharti ya Katiba za
Washirika wa Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, Katiba hii itakuwa sheria kuu
katika Jamhuri ya Muungano.
(2) Mtu yeyote, chombo, taasisi, jumuiya na
wakala wowote wa mamlaka ya nchi na mamlaka binafsi zinao wajibu wa kuzingatia masharti
ya Katiba hii na kuyatii.
(3) Sheria yoyote, mila, desturi au uamuzi
wowote wa chombo cha dola, ofisa wa Serikali au mtu binafsi ni sharti ufuate na
kuendana na masharti yaliyomo kwenye Katiba hii na kwamba, sheria, mila,
desturi
au uamuzi wowote ambao hautawiana au kwenda
sambamba na masharti ya Katiba hii utakuwa batili.
Hifadhi ya Katiba
9.-(1) Mtu au kikundi cha watu hakitachukua au
kushikilia mamlaka ya nchi isipokuwa kwa mujibu wa Katiba hii.
(2) Kitendo chochote kinachokiuka masharti ya
Ibara ndogo ya
(1) ni batili na ni kitendo cha uhaini kama
itakavyoelezwa katika sheria za nchi.
(3) Kwa madhumuni ya kuhifadhi masharti ya
Ibara ndogo ya (1) na (2), Serikali itaweka utaratibu wa kuisambaza Katiba hii
kwa wananchi na kuiweka katika mitaala ya elimu ili kuwezesha wananchi kuifahamu,
kuilinda na kuitii.
SURA
YA PILI
MALENGO MUHIMU, MISINGI YA MWELEKEO WA
SHUGHULI ZA SERIKALI NA SERA ZA KITAIFA
Utekelezaji wa malengo ya Taifa
10.-(1) Malengo ya Taifa yaliyoainishwa ndani
ya Katiba hii yatakuwa ni mwongozo kwa Serikali, Bunge, Mahakama, vyama vya siasa,
taasisi, asasi na mamlaka nyingine na kwa kila mwananchi katika matumizi au
kutafsiri masharti ya Katiba hii au sheria nyingine yoyote na katika
utekelezaji wa uamuzi wa kisera kwa madhumuni ya kujenga jamii huru, makini na
iliyo bora.
(2) Serikali itatoa taarifa Bungeni si chini ya
mara moja katika ‐ 6 ‐ kila mwaka, kuhusu hatua zilizochukuliwa na
mamlaka ya nchi ili kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Taifa yaliyoainishwa
katika Katiba hii.
Malengo Makuu
11.-(1) Lengo Kuu la Katiba hii ni kulinda,
kuimarisha na kudumisha udugu, amani, umoja na utengamanowa wananchi wa Jamhuri
ya Muungano kwa kuzingatia ustawi wa wananchi na kujenga Taifa huru lenye
demokrasia, utawala bora na kujitegemea.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya
(1), lengo hilo kuu litaendelezwa na kuimarishwa katika nyanja zote kuu, ikijumuisha
nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kimazingira.
(3) Katika kutekeleza malengo ya Taifa ya:
(a)
kisiasa, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili –
(i)
kuhakikisha kuwa inazuia, inapinga na kuondoa dhulma, vitisho, ubaguzi,
unyanyasaji, rushwa, uonevu na upendeleo miongoni mwa wananchi kwa misingi ya
asili ya mtu, sehemu anayotoka, nasaba,kabila, jinsi, dini au imani yake;
(ii)
kuhakikisha uwepo wa amani na kujenga utamaduni wa kuenzi, kuheshimu na
kudumisha amani, umoja na utengamano, ushirikiano na uvumilivu wa kisiasa kwa
madhumuni ya kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi;
(iii)
kuhakikisha uwepo wa ulinzi, usalama na ustawi wa watu na mali zao, na kuepuka
kufanya jambo lolote litakalohatarisha au kwenda kinyume na lengo hilo;
(b) kijamii, Serikali inachukua hatua zinazofaa
ili:
(i) kuhakikisha kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa
na kudumishwa kwa kufuata mila, desturi na Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki
za Binadamu na mikataba mingine ya kimataifa iliyoridhiwa na Tanzania;
(ii) kuhakikisha kwamba Serikali na vyombo vyake
vyote vya umma vinatoa nafasi na fursa zilizo sawa kwa raia wote, bila ya
kujali rangi, kabila, dini, nasaba, hali ya mtu au mahali alipo;
(iii) kujenga utamaduni wa kuwepo ushirikiano, maelewano
na maridhiano, uvumilivu na kuheshimu mila, desturi na imani ya dini ya kila mtu;
(iv) kuhakikisha kuwa msaada na hifadhi ya
jamii inatolewa kwa watu wasiojiweza, wazee, wagonjwa, watoto na watu wenye ulemavu;
(c)
kiuchumi, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili:
(i) kuwaletea wananchi maisha bora kwa kuondoa umaskini;
(ii) kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa
kwa njia ambazo zitahakikisha kuwa utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa
na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya
mtu mwingine;
(iii) kuweka mazingira bora kwa ajili ya
kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi;
(iv) kuweka mazingira bora ya kufanya biashara
na kukuza fursa za uwekezaji;
(v) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo,
ufugaji na uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi
na nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao;
(vi) kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa
mazao kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, utafutaji na uendelezaji wa masoko ya
mazao yao;
(vii) kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji
wa mizania ya bei za mazao na pembejeo;
(viii) kuimarisha na kuendeleza uwekezaji wa
ndani, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, maeneo ya ufugaji na vifaa vya uvuvi;
(ix) kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa
fursa na nafasi za wazi kwa watu wote na kuanzisha shughuli za kiuchumi na
kukuza mazingira yaliyo bora kwa ajili ya kuhamasisha sekta binafsi katika
uchumi;
(x) kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya
kazi anapata fursa ya kufanya kazi, kwa maana ya kufanya shughuli yoyote halali
inayompatia kipato;
(xi) kuweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha
utekelezaji wa haki ya mtu kujipatia elimu na kuwa huru kupata fursa sawa ya kutafuta
elimu katika fani anayoipenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo
wake;
(d) kiutamaduni, Serikali itachukua hatua
zinazofaa ili:
(i) kulinda na kuhifadhi urithi wa asili,
malikale na sehemu zenye umuhimu wa kihistoria au kidini ili
kuepuka uharibifu, udhalilishaji na wizi au utoroshwaji
nje ya nchi;
(ii) kulinda, kuhifadhi na kuendeleza tamaduni
za watu wa jamii mbalimbali ambazo zinaendeleza
na kukuza utu na hadhi yao kwa namna ambayo haikinzani
na Misingi ya Kitaifa, na Malengo Muhimu na Sera za Taifa;
(iii) kutambua, kulinda na kuendeleza lugha ya Kiswahili;
na
(e) kimazingira, Serikali itachukua hatua
zinazofaa ili kuhakikisha kuwa ni haki na jukumu la kila kizazi kulinda na
kudumisha mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Sera kuhusu Mambo ya Nje
12. Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano
inalenga nainazingatia maslahi ya Taifa na mamlaka kamili ya nchi na kwamba sera
hiyo inatekelezwa kwa uwazi ili:
(a) kukuza ushirikiano wa kikanda na
ushirikiano wa kimataifa;
(b) kukuza ushirikiano wa kiuchumi wenye tija
kwa Taifa;
(c) kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa mataifa ya
Afrika kwa kushiriki katika hatua mbalimbali za mtangamano wa kiuchumi wa
kikanda;
(d) kuheshimu sheria za kimataifa;
(e) kuzingatia mikataba ya kimataifa, mikataba
ya kikanda yenye maslahi kwa Jamhuri ya Muungano na kutatua migogoro ya
kimataifa kwa njia ya majadiliano, usuluhishi, maridhiano na mahakama;
(f) kukuza uzingatiaji wa haki za binadamu na
uhuru wa watu;
(g) kupambana na makosa ya kimataifa ya
kijinai; na
(h)
kuheshimu uhuru wa mataifa mengine.
SURA
YA TATU
MAADILI
NA MIIKO YA UONGOZI NA UTUMISHI WA UMMA
SEHEMU
YA KWANZA
MAADILI
YA VIONGOZI WA UMMA
Dhamana
ya Uongozi wa Umma
13.-(1)
Madaraka anayopewa kiongozi wa umma:
(a)
ni dhamana na atatumia madaraka hayo na kutekeleza wajibu wake kwa:
(i)
kuzingatia masharti ya Katiba hii; (ii) kuheshimu wananchi; (iii) namna
inayokuza hadhi ya taifa na kulinda heshima ya ofisi anayoitumikia; na (iv)
kukuza imani na heshima ya ofisi kwa wananchi;
(b) yanatoa wajibu kwa kiongozi kuwatumikia
wananchi.
(2) Dhamana ya uongozi na heshima kwa kiongozi
wa umma itazingatia mambo yafuatayo:
(a) uteuzi kwa misingi ya mwenendo wa mtu,
uwezo, sifa au uchaguzi uliyo huru na haki;
(b) uwezo pasipo upendeleo katika kufanya
uamuzi na kuhakikisha kwamba uamuzi haufuati udugu, ukabila, udini, upendeleo,
rushwa au vigezo vingine visivyo sahihi;
(c) utoaji wa huduma pasipo upendeleo na kwa
kufuata maslahi ya umma kwa kuonyesha-
(i) uaminifu katika utekelezaji wa kazi za
umma; (ii) wajibu wa kutangaza maslahi binafsi ili kuepuka
mgongano wa maslahi; (d) uwajibikaji kwa umma
katika kufanya uamuzi na vitendo; na
(e) nidhamu na kujituma katika kutoa huduma kwa
umma.
Kanuni za Uongozi wa Umma
14.-(1) Kiongozi wa umma, akiwa ama katika kazi
za ofisi au kazi binafsi au wakati amejumuika na watu wengine, atahakikisha kwamba
mwenendo wake:
(a) hauruhusu kutokea mgongano wa maslahi kati
ya maslahi binafsi na maslahi ya utumishi wa umma;
(b) hauhatarishi maslahi ya umma kwa ajili ya
maslahi binafsi; au
(c) haushushi hadhi ya ofisi anayofanyia kazi.
(2) Kwa madhumuni ya Ibara ndogo ya (1),
mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha Tume ya Maadili ya Uongozi
na Uwajibikaji kusimamia utekelezaji wa masharti yanayohusu kanuni za uongozi wa umma.
(3) Wadhifa “Kiongozi wa Umma” kama
ulivyotumika katika Sehemu hii utajumuisha viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa
kama watakavyoainishwa kwenye sheria itakayotungwa na Bunge.
Zawadi katika Utumishi wa Umma
15.-(1) Zawadi au kitu chochote kitakachotolewa
kwa mtumishi wa umma katika shughuli za kiserikali ni zawadi kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na itawasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitia kwa
Katibu Mkuu wa Wizara au taasisi ya Serikali inayohusika, akiainisha:
(a) aina ya zawadi; (b) thamani ya zawadi; (c)
sababu ya kupewa zawadi; na (d) mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo.
(2) Mtumishi wa Umma -
(a) hatafungua au kuendesha akaunti ya benki
nje ya Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi
zinaruhusu; na
(b) hataomba au kupokea mkopo au faida yoyote
kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya mtumishi wa umma.
‐ 10 ‐
(3) Bunge litatunga sheria itakayosimamia,
pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi
inayohusika na masharti ya Sehemu hii na masharti mengine yanayohusu utekelezaji
wa masharti ya Ibara hii.
Wajibu
wa kutangaza mali na madeni
16.-(1)
Kiongozi wa Umma atalazimika kutangaza, ndani ya siku thelathini baada ya
kupata uongozi na baada ya kuacha uongozi, mali na thamani zake na madeni yake
katika Tume ya Maadili na Uwajibikaji.
(2)
Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), Kiongozi wa Umma atalazimika
kutangaza mali zake na madeni:
(a)
yake binafsi; (b) ya mwenza wake wa ndoa; na (c) watoto wake walio chini ya
umri wa miaka kumi na nane, mara moja kila mwaka, au kadri itakavyoamuliwa na
sheria.
Mgongano
wa kimaslahi
17.-(1)
Kiongozi wa Umma hatashiriki katika jambo au shughuli yoyote ambayo ana maslahi
nayo yeye binafsi, mwenza wake, mtoto
wake, jamaa yake, rafiki au mtu yeyote wake wa karibu.
(2)
Kiongozi wa umma hatozungumzia kitu chochote katika Baraza la Mawaziri, Bunge,
kamati au chombo kingine chochote rasmi ambacho ana maslahi nacho ya moja kwa
moja au vinginevyo, isipokuwa tu kama atatoa taarifa ya mgongano huo wa maslahi
katika vyombo hivyo.
(3)
Itakuwa ni marufuku kwa Kiongozi yeyote wa Umma, kushiriki kuongeza au kwa
namna yoyote ile, kuboresha maslahi yanayohusu wadhifa alionao, na endapo
atashiriki, basi masharti hayo mapya yataanza kutumika kwa Kiongozi atakayekuja
baada ya yeye kuondoka au kumaliza muda wa kukaa madarakani.
(4) Bunge litatunga sheria itakayosimamia,
pamoja na mambo mengine, masuala ya:
(a) ngazi au orodha ya Viongozi wa Umma,
wanaopaswa kutangaza mali zao;
(b) utaratibu wa utwaaji wa mali za Viongozi wa
Umma zilizopatikana kwa njia za ukiukaji wa sheria;
(c) utaratibu wa kumwajibisha Kiongozi wa Umma
aliyeenda kinyume na maadili na Miiko ya Uongozi;
(d) uanzishaji wa mitaala inayohusu maadili na
uraia, mashuleni na vyuoni; na
(e) uanzishaji wa mitaala inayohusu Katiba mashuleni
na vyuoni.
(5) Kiongozi wa Umma hataruhusiwa kushika
nyadhifa mbili au zaidi au kutumikia Mihimili ya Dola zaidi ya mmoja kwa wakati
mmoja.
Matumizi ya mali ya umma
18. Haitaruhusiwa kwa Kiongozi yeyote wa Umma
kutumia au kuruhusu kutumika kwa mali yoyote ya umma, zikiwemo zilizokodishwa
kwa Serikali, kwa madhumuni ya kumpatia yeye binafsi au mtu mwingine yeyote
manufaa ya kiuchumi.
Matumizi ya masharti ya maadili kwa Watumishi
wa Umma
19. Masharti yaliyoainishwa katika Ibara za 13
mpaka 18 yatatumika pia kwa watumishi wa umma baada ya kufanyiwa marekebisho
stahiki.
SEHEMU YA PILI
MIIKO YA UONGOZI WA UMMA
Utii wa Miiko ya Uongozi wa Umma
20.-(1) Bila ya kuathiri masharti yoyote ya
Katiba hii, kiongozi yeyote wa Umma atapaswa kuheshimu na kutii maadili ya viongozi wa umma, ikiwemo
Miiko ya Uongozi.
(2) Miiko ya Uongozi inayorejewa katika Ibara
ndogo (1), itakuwa kama ifuatavyo:
(a) Kiongozi wa umma hatopaswa:
(i) kuvunja au kukiuka masharti ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano;
(ii) kutoa au kupokea rushwa;
(iii) kujilimbikizia mali kinyume cha sheria;
(iv) kusema uongo au kutoa taarifa zisizo za
ukweli;
(v) kutoa siri za Serikali kinyume na sheria;
(vi) kutumia wadhifa, nafasi au cheo chake kwa manufaa
yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa au marafiki zake au mtu yeyote aliye
na uhusiano naye wa karibu;
(vii) kufanya vitendo vya uzembe, uvivu,
ubaguzi, kiburi, dharau au unyanyasaji wa kijinsia.
(b) Kiongozi wa umma atapaswa:
(i) kuheshimu na kuendeleza dhana ya
uwajibikaji wa pamoja, kwa viongozi wanaohusika; na
(ii) kuheshimu na kuendeleza maadili ya
viongozi wa umma, ikijumuisha:
(aa) kuwa na tabia na mienendo inayokubalika katika
jamii;
(bb) kuheshimu, kutunza na kulinda mali za umma;
na
(cc) kutambua, kuheshimu na kuzingatia Kanuni
za Maadili na Mienendo ya Watumishi wa Umma, Kanuni za Kudumu za Watumishi wa
Umma, nyaraka za umma na miongozo mbalimbali ya Serikali kuhusu viongozi na
watumishi wa umma.
(iii) kutenganisha shughuli za biashara na
masuala yanayohusiana na uongozi.
(3) Kiongozi yeyote wa umma ambaye anatuhumiwa
na kuthibitika kwa makosa ya:
(a) kimaadili;
(b) udhalilishaji wa mtu au wa kijinsia; na
(c) wizi au ubadhirifu wa mali za umma, atasimamishwa kazi mpaka suala lake
litakapoamuliwa kwa mujibu wa sheria au taratibu nyingine zinazowahusu viongozi
wa umma.
Marufuku baadhi ya vitendo
21.-(1) Mtumishi wa umma aliye katika ajira ya
kudumu hataruhusiwa kuingia katika ajira nyingine yoyote yenye malipo ya mshahara.
(2) Mtumishi wa umma haruhusiwi kuchaguliwa au
kuteuliwa kushika madaraka katika chama cha siasa.
(3) Mtumishi wa umma aliyestaafu na anayepokea
malipo ya pensheni kutokana na fedha za umma haruhusiwi kuwa mwenyekiti, mkurugenzi
au mtumishi zaidi ya vipindi viwili katika:
(a) shirika au kampuni inayomilikiwa au
kuendeshwa kwa fedha za umma; au
(b)
chombo chochote cha umma.
SURA
YA NNE
HAKI
ZA BINADAMU, WAJIBU WA RAIA NA MAMLAKA ZA NCHI
SEHEMU YA KWANZA
HAKI ZA BINADAMU
Uhuru, utu na usawa wa binadamu
22.-(1) Binadamu wote huzaliwa huru na wote ni
sawa.
(2) Kila mtu anayo haki ya kuheshimiwa,
kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Haki ya kuishi
23. Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata
hifadhi ya maisha yake kutoka katika Serikali na jamii kwa mujibu wa sheria.
Marufuku kuhusu ubaguzi
24.-(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria na
wanayo haki ya kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
(2) Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na
mtu, mamlaka ya nchi au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya
sheria yoyote au katika kutekeleza kazi au shughuli yoyote ya mamlaka ya nchi.
(3) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa
na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi
ama wa dhahiri au kwa taathira yake.
(4) Haki ya raia, wajibu na maslahi ya kila mtu
na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya
mamlaka ya nchi vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.
(5) Kwa madhumuni ya masharti ya Ibara hii na
kwa kuzingatia masharti ya Ibara ndogo ya (4), neno “kubagua” maana yake ni
kutimiza utashi, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa
wao, kabila, mahala walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsi au
hali yao ya maisha kwa namna ambayo watu wa aina fulani wanafanywa au
kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya vipingamizi
ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida
iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima.
(6)
Neno “kubagua” lilivyotumiwa katika Ibara ndogo ya (2), halitafafanuliwa kwa
namna ambayo itaizuia mamlaka ya nchi kuchukua hatua za makusudi zenye lengo la
kurekebisha matatizo mahsusi katika jamii.
(7)
Kwa madhumuni ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria, mamlaka ya nchi itaweka
utaratibu unaofaa na unaozingatia misingi kwamba -
(a)
wakati haki na wajibu kwa mtu yeyote vinapohitajika kufanyiwa uamuzi na
mahakama au mamlaka nyingine inayohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya
kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia atakuwa na haki ya kukata
rufani au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na uamuzi wa mahakama au
mamlaka nyingine inayohusika;
(b)
ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu
aliyehukumiwa kwa kutenda kosa hilo hadi itakapothibitika mahakamani kuwa anayo
hatia ya kutenda kosa hilo;
(c)
ni marufuku kwa mtu kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chochote ambacho wakati
alipotenda kitendo hicho hakikuwa ni kosa chini ya sheria;
(d)
ni marufuku kwa mtu kupewa adhabu ambayo ni kubwa kuliko adhabu iliyokuwapo
wakati kosa linalohusika lilipotendeka;
(e)
kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu na faragha
itahifadhiwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi wa tuhuma na uendeshaji
wa masharti ya jinai na katika shughuli nyingine
ambazo mtu anakuwa katika kizuizi cha mamlaka ya nchi au katika kuhakikisha
utekelezaji wa adhabu; na
(f)
ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazotweza au
kudhalilisha.
Haki ya kutokuwa mtumwa
25.-(1)
Kila mtu ana haki ya kutotendewa au kutotumikishwa kama mtumwa, kutofanyishwa
kazi za kulazimishwa au kutweza, na kwa msingi huo, ni marufuku kwa mtu:
(a)
kufanywa au kutendewa kama mtumwa;
(b)
kulazimishwa kufanya kazi bila hiyari yake; au
(c)
kusafirishwa kwa nia ya kufanyiwa biashara au faida ya mtu mwingine.
(2)
Biashara ya kusafirisha binadamu ni marufuku katika Jamhuri ya Muungano.
Uhuru
wa mtu binafsi
26.-(1)
Kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi akiwa mtu huru.
(2)
Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa
ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini,
kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake vinginevyo, isipokuwa tu
katika-
(a) hali na kwa kufuata utaratibu uliowekwa na
sheria; au
(b) kutekeleza hukumu, amri au adhabu
iliyotolewa na mahakama kutokana na shauri au kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.
Haki ya faragha na usalama wa mtu
27.-(1) Kila mtu anastahili kuheshimiwa na
kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na nyumbani
kwake, kutoteswa au kudhalilishwa, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na
mawasiliano yake ya binafsi.
(2) Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu,
mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria kuhusu hali, namna na kiasi ambacho
haki ya mtu ya faragha na ya usalama wa nafsi yake, mali na maskani yake, yanaweza
kuingiliwa bila ya kuathiri masharti ya Ibara hii.
Uhuru wa mtu kwenda anakotaka
28.-(1) Kila raia anayo haki ya kwenda kokote
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka
nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa, kuhama au kufukuzwa kutoka
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(2) Kitendo chochote halali au sheria yoyote
yenye madhumuni ya -
(a) kupunguza uhuru wa mtu kwenda anakotaka na
kumweka chini ya ulinzi au kifungoni; au
(b) kuweka mipaka kwa matumizi ya uhuru wa mtu
kwenda anakotaka ili-
(i)
kutekeleza hukumu au amri ya mahakama;
(ii)
kumlazimisha kutimiza kwanza wajibu wowote anaotakiwa na sheria nyingine
kuutimiza; au
(iii)
kulinda manufaa ya umma kwa jumla au kuhifadhi maslahi fulani mahsusi au maslahi
ya sehemu fulani ya umma, hakitahesabiwa au sheria hiyo haitahesabiwa kuwa ni
kinyume cha masharti ya Ibara hii.
Uhuru wa maoni
29.-(1) Kila mtu:
(a) anao uhuru wa-
(i) kuwa na maoni na kueleza fikra zake; (ii)
kufanya mawasiliano na vile vile anayo haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano
yake; (iii) ubunifu na sanaa; (iv) kitaaluma na tafiti za kisayansi; na
(b) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote
kuhusu:
(i) matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli
za wananchi; na
(ii) utekelezaji wa mamlaka ya nchi kuhusu sera
za kitaifa na shughuli ya maendeleo ya jamii; na
(iii) masuala mengine muhimu kwa jamii.
(2) Utekelezaji wa haki zilizoainishwa katika
Ibara ndogo ya (1), utajumuisha wajibu muhimu kwa mwananchi na wajibu huo
unaweza kupunguza haki hizo kutokana na:
(a)
vita au machafuko ya kisiasa; au
(b)
propaganda kuhusu vita, ushawishi wa chuki kwa misingi ya rangi, ukabila,
ubaguzi wa kijinsia, dini au masuala yoyote yanayoweza kuleta madhara kwa
Taifa.
Uhuru wa habari na vyombo vya habari
30.-(1)
Kila mtu anao uhuru wa-
(a)
kutafuta, kupata na kutumia habari na taarifa na kusambaza taarifa hizo; na
(b)
kuanzisha vyombo vya habari na njia nyingine za upashanaji wa habari bila
kujali mipaka ya nchi.
(2)
Vyombo vya habari vitakuwa huru na vile vile vitakuwa na:
(a) haki ya kupata, kutumia na kusambaza habari
na taarifa wanazopata;
(b) wajibu wa:
(i) kusambaza habari na taarifa kwa wananchi;
na
(ii) kuheshimu na kulinda utu, heshima, uhuru
na staha ya wananchi dhidi ya habari na taarifa wanazozitumia,
wanazozitayarisha na kuzisambaza.
(3) Serikali na taasisi zake, asasi za kiraia
na watu binafsi watakuwa na wajibu wa kutoa habari kwa umma juu ya shughuli na utekelezaji
wa shughuli zao.
(4) Masharti ya Ibara hii yatalazimika
kuzingatia masharti ya sheria ya nchi itakayotungwa kwa ajili hiyo na kwa
madhumuni ya kulinda usalama wa Taifa, amani, maadili ya umma, haki, staha na
uhuru wa watu wengine.
Uhuru wa imani ya dini
31.-(1) Kila mtu anao uhuru wa mawazo, imani na
uchaguzi katika mambo ya imani ya dini na anao huru pia wa kubadilisha dini, imani
yake au kutokuwa na imani na dini.
(2) Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na
kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari kwa mtu binafsi ili mradi
asivunje sheria za nchi.
(3) Shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini
itakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya Serikali.
(4) Hifadhi ya haki zilizotajwa katika Ibara
hii itakuwa chini ya taratibu zilizowekwa na sheria ambazo ni muhimu katika
jamii ya kidemokrasia kwa ajili ya usalama, amani, maadili na umoja wa jamii na
wa kitaifa na vitasimamiwa kwa utaratibu ulioainishwa kwenye sheria za nchi.
(5) Ni marufuku kwa mtu, kikundi au taasisi ya
dini kutumia uhuru wa kutangaza dini kwa kukashifu imani na dini nyingine,
kujenga chuki au kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya kutetea imani au dini.
(6) Dini na imani ya dini haitatumika kwa namna
yoyote itakayowagawa wananchi, kuleta uhasama au kuharibu amani miongoni mwa
wananchi.
(7) Neno “dini” kama lilivyotumika katika Ibara
hii litatafsiriwa kwamba maana yake ni pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengine
yanayofanana au kuambatana na neno hilo nayo yatatafsiriwa kwa maana hiyo.
Uhuru wa mtu kujumuika na kushirikiana
na wengine
32.Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya
kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani,
kujumuika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa
zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni
ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.
Uhuru wa kushiriki shughuli za
umma
33.-(1) Kila raia wa Jamhuri ya Muungano ana
haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa
kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu
uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
(2) Kila raia ana haki na uhuru wa kushiriki
kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake
au yanayolihusu Taifa.
Haki ya kufanya kazi
34.-(1) Kila mtu ana haki ya kufanya kazi ya kuajiriwa
au kujiajiri mwenyewe.
(2) Kila mtu ana haki na fursa sawa kushika
nafasi yoyote ya kazi, uongozi au shughuli yoyote iliyo chini ya mamlaka ya
nchi.
Haki za wafanyakazi na waajiri
35.-(1) Kila mfanyakazi ana haki zifuatazo:
(a) kufanya kazi bila ubaguzi wa aina yoyote;
(b) kupata ujira na malipo halali kulingana na
kiasi na sifa za kazi anayofanya;
(c) kuunda au kujiunga na chama cha wafanyakazi
mahala pa kazi; na
(d) kushiriki katika shughuli za chama cha
wafanyakazi;
(2) Kila chama cha waajiri na wafanyakazikitakuwa
na haki ya:
(a) kuamua kuhusu uongozi, programu na shughuli
zake; na
(b) kuanzisha, kujiunga na kusimamia shirikisho
lao.
(3) Kila chama cha wafanyakazikitakuwa na haki
ya kufanya majadiliano ya pamoja na mwajiri na kuingia mikataba ya hali bora ya
kazi.
(4) Bunge litatunga sheria itakayoweka masharti
kuhusu haki za wafanyakazi na utaratibu utakaowezesha wafanyakazi kutumia haki
zao.
Haki ya kumiliki mali
36.-(1) Kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na
hifadhi ya mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya
(1), itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni
ya kuitaifisha au madhumuni mengine bila malipo yanayolingana na thamani halisi
ya mali hiyo na yatakayotolewa mapema.
(3) Kwa madhumuni ya masharti ya Ibara hii,
haki ya umiliki na hifadhi ya mali haitahusu mali iliyothibitishwa kwamba
haikupatikana kwa njia halali.
Haki ya uraia
37. Kila raia ana haki ya kutambuliwa uraia
wake na kwa madhumuni haya, mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha
wananchi kupata hati ya kuzaliwa, kitambulisho cha uraia wake bila ya upendeleo
na ubaguzi wa aina yoyote, na pale inapohitajika, nyaraka za kumwezesha
kusafiri.
Haki ya mtuhumiwa na mfungwa
38.-(1) Mtu aliyekamatwa au aliyewekwa kizuizini
anayo haki ya:
(a) kuelezwa kwa lugha anayoifahamu -
(i) sababu ya kukamatwa;
(ii) haki ya kutokutoa maelezo yoyote; na
(iii) matokeo ya kutoa maelezo;
(b)kutoa maelezo;
(c) kuwasiliana na wakili na mtu mwingine
ambaye msaada wake ni muhimu kwa mtuhumiwa;
(d) kutolazimishwa kutoa maelezo ya kukiri kosa
ambayo yatatumika kama ushahidi dhidi yake; na
(e) kupelekwa mahakamani mapema iwezekanavyo.
(2) Mamlaka za nchi zitaweka utaratibu wa
sheria utakaowezesha:
(a) mtuhumiwa kupata nakala ya mashtaka yanayomkabili
na kumbukumbu ya mwenendo wa mashtaka;
(b) mtuhumiwa au mfungwa kupata nakala ya
mwenendo wa mashtaka baada ya shauri kukamilika mahakamani;
(c) mtuhumiwa au mfungwa kufikishwa mahakamani
ili kuthibitisha uwepo wake.
Haki ya watu waliyo chini ya ulinzi
39.-(1) Mtu aliye katika kizuizi au ulinzi
ataendelea kuwa na haki zote za msingi zilizoainishwa katika Katiba hii kwa
kiwango anachostahiki katika mazingira ya kuwekwa kizuizini au katika ulinzi.
(2) Mtu aliye katika kizuizi au ulinzi ana haki
ya kuiomba mahakama ili mamlaka ya nchi inayomuhifadhi kueleza sababu za yeye kuwekwa
au kuendelea kuwa katika kizuizi au ulinzi.
(3) Raia wa Jamhuri ya Muungano hatapelekwa
katikanchi ya nje yoyote kujibu mashtaka au kufanyiwa mahojiano ya aina yoyote
kinyume cha ridhaa yake.
Uhuru na haki ya mazingira safi na salama
40.-(1)
Kila mtu anayeishi katika Jamhuri ya Muungano ana haki ya kuishi katika
mazingira safi, salama na ya kiafya.
(2)
Haki ya kuishi katika mazingira safi, salama na ya kiafya inahusisha haki kwa
kila raia kutumia maeneo ya umma au sehemu mbalimbali za mazingira yaliyotengwa
kwa madhumuni ya burudani, elimu, afya, ibada, utamaduni na shughuli za
kiuchumi.
(3)
Mtu yeyote anayeishi Tanzania anao wajibu wa kutunza na kuendeleza mazingira na
kutoa taarifa kwa mamlaka za nchi kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo ni
hatarishi au linauwezekano mkubwa wa kuharibu au kuathiri mazingira.
Haki ya elimu na kujifunza
41.-(1)
Kila mtu ana haki ya:
(a) kupata fursa ya kupata elimu bila ya
vikwazo;
(b) kupata elimu bora ya msingibila ya malipo
na inayomtayarisha kikamilifu mwanafunzi ama kuendelea na elimu ya ngazi inayofuatia
au kuweka msingi wa kuanza kujitegemea;
(c) kwa elimu inayotolewa nje ya utaratibu wa
umma, kupata elimu kwa gharama nafuu; na
(d) kupata fursa sawa ya kupata elimu ya juu
ili mradi ana sifa stahiki kupata elimu hiyo, bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
(2) Kwa madhumuni ya Ibara ndogo ya (1), kila
mtu ana haki ya kuchagua taaluma na ajira anayoitaka kwa mujibu wa elimu yake
na ujuzi aliyonao.
Haki ya mtoto
42.-(1) Kila mtoto ana haki ya-
(a) kupewa jina na uraia;
(b) kutoa mawazo, kusikilizwa na kulindwa dhidi
ya uonevu, ukatili na udhalilishaji;
(c) kucheza na kupata elimu;
(d) kuhifadhiwa katika mazingira mazuri, kwa
walio katika ukinzani na sheria;
(e) kupata lishe bora, makazi na huduma ya
afya; na
(f) kushiriki katika shughuli zinazolingana na
umri alionao; na
(g) kupata malezi na ulinzi wa wazazi, walezi
au mamlaka ya nchi, bila ya ubaguzi wa rangi, utaifa, lugha, mtazamo wa
kisiasa, jamii anayotokea, mali, uzazi, kabila, dini, jinsi au aina nyingine za
hadhi.
(2) Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria
utakaowezesha utekelezaji na usimamizi wa haki za mtoto kwa kufuata msingi wa
kutoa kipaumbele kwa maslahi na manufaa ya mtoto.
Haki na wajibu wa vijana
43. Kila kijana ana haki na wajibu wa kushiriki
kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Jamhuri ya Muungano pamoja na jamii
kwa ujumla, na kwa mantiki hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali za
Washirika wa Muungano na jamii zitahakikisha kuwa vijana wanawekewa mazingira
mazuri ya kuwa raia wema na kupatiwa fursa za kushiriki kikamilifu katika
nyanja za kisiasa, kiuchumi,kijamii na kiutamaduni.
Haki za watu wenye ulemavu
44.-(1) Mtu mwenye ulemavu anastahiki:
(a) kuheshimiwa, kutambuliwa na kutendewa kwa
namna ambayo haishushi utu wake;
(b) kupata elimu kwa kutumia vifaa maalum na
kushiriki katika shughuli za kijamii;
(c) kuwekewa miundombinu na mazingira
yatakayowezesha kwenda anapotaka, kutumia vyombo vya usafiri na kupata habari;
(d) kutumia lugha za alama, maandishi ya nukta
nundu au njia nyingine zinazofaa;
(e) haki ya kusoma na kuchanganyika na watu
wengine; na
(f) haki ya kupata ajira na kugombea nafasi za
uongozi katika nyadhifa mbalimbali kwa usawa.
(2) Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria
utakaowezesha watu wenye ulemavu kushiriki katika nafasi za uwakilishi.
Haki za makundi madogo katika
jamii
45.-(1) Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa
sheria utakaowezesha makundi madogo katika jamii:
(a) kushiriki katika uongozi wa mamlaka za
nchi;
(b) yanapewa fursa maalum za elimu na fursa za
kujiendeleza kiuchumi na fursa za ajira;na
(c) kutengewa maeneo ya ardhi ambayo kwa
desturi makundi hayo kuitumuia kama eneo la kuishi na kupata riziki ya chakula.
(2) Serikali na mamlaka za nchi zitachukua
hatua za makusudi za kukuza na kuendeleza shughuli za kiuchumi na kuweka
miundombinu ya makazi, elimu na afya kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo
vya jamii ya watu walio katika makundi madogo.
Haki za wanawake
46.-(1) Kila mwanamke ana haki ya:
(a) kuheshimiwa utu wake;
(b) kuwa salama dhidi ya unyonyaji na ukatili;
(c) kushiriki bila ya ubaguzi katika chaguzi na
ngazi zote za maamuzi;
(d) kupata ujira sawa na mwanaume katika kazi;
(e) kulindwa dhidi ya ubaguzi, uonevu na mila
zenye madhara;
(f) kulindwa kwa ajira yake wakati wa ujauzito
na pale anapojifungua; na
(g) kupata huduma ya juu ya afya inayopatikana.
(2) Mamlaka husika za nchi zitaweka utaratibu
wa kisheria utakaosimamia masuala yanayohusu utekelezaji wa masharti ya Ibara
hii ikiwa ni pamoja na kukuza utu, usalama na fursa za wanawake wakiwemo wajane.
Haki za wazee
47. Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu
utakaowezesha wazee kupata fursa ya:
(a) kushiriki katika shughuli za kijamii;
(b) kuendeleza maisha yao;
(c) kutambuliwa utu wao na kuheshimiwa pasipo kudharauliwa;
(d) kulelewa na kupata misaada kutoka katika
familia zao jamii na mamlaka ya nchi; na
(e) kupewa fursa ya kuendelea kutumia utaalamu
na ujuzi wao kwa faida na manufaa ya jamii.
No comments:
Post a Comment