Wednesday, April 9, 2014

HII NDIYO STORY KAMILI KUMHUSU HALIMA MDEE

HII NDIO HISTORIA YA MAISHA YANGU, NA MWENENDO MZIMA WA MAISHA YANGU KWA UJUMLA.
Mimi ni mbunge kijana ambaye baada ya kuwa mbunge wa viti maalumu kwa kipindi cha miaka mitano, niliamua kupambana kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010 na kufanikiwa kukinyakua kiti cha Jimbo la Kawe.
Mi ni miongoni mwa wanawake wachache katika taifa letu niliyepata ubunge wa kuchaguliwa. Wengine wanasema mimi ni jembe, wengine wananiita kamanda, wengine wamenibatiza jina mpambanaji, mwanasiasa mzalendo, kiongozi na mwakilishi wa kweli wa watu wangu.
Sifa zangu, zilivuma wakati nikiwa mbunge wa viti maalumu.
Ingawa mimi ni mwanachama wa CHADEMA, lakini muda wote nilisimamia hoja za kitaifa na kuzitetea.
Muda wote nilionyesha uzalendo. Mimi si miongoni mwa wale wanaopayuka na kutukuza ushabiki wa vyama vya siasa, bali naangalia maslahi ya taifa.
Wote mmenishuhudia nilivyosimama kidete kutetea suala la ardhi. Jimbo langu la Kawe, lina migogoro mingi ya ardhi na amekuwa mstari wa mbele kuwatetea watu wanaodhulumiwa ardhi yao.
Bila kuweka chumvi au ushabiki, ninaweza kusimama kugombea jimbo lolote nchini. Kazi ninayoifanya bungeni inaonekana, si miongoni mwa wale wanaokwenda kusinzia na wakizinduka usingizini wanashangilia na kupitisha kila hoja bila ya mchango wowote wa mawazo.
Mimi si miongoni mwa wabunge wanaotega vikao vya Bunge; mmeshuhudia wote ninavyofuatilia masuala yote yanayokuwa yakijadiliwa bungeni.
Ingawa wakati mwingine mimi nina vijembe vya hapa na pale, lakini si vijembe vya kijinga kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia wabunge wakiporomosha matusi makubwa kama wendawazimu vile na badala ya kuwapuuza wanapandishwa vyeo, na wengine sasa hivi ni mawaziri.
Mimi nina vijembe vya siasa na lugha za vijana. Katika hali ya kawaida vijembe kama hivi, ambavyo si matusi vinakubalika.
Lakini vingine vya kuwatukana, kuwadhalilisha watu ni mwiko kwenye jamii iliyostaarabika.

Bunge letu lina watu wanaoongea sana na wengine ni wataalamu wa kuongea na kuchekesha kama Jangala vile, lakini kuna wabunge wachache sana wanaoongea kwa umakini, kwa kuhesabu maneno na kuhakikisha mbali na mantiki kila neno lina maana nzito kulingana na hoja inayojadiliwa.
Mimi ni miongoni mwa wabunge hao wachache.
Kuna wabunge ambao unaona wanajiandaa kabla ya kuongea na wanakuwa wamepitia kwa undani hoja zinazokuwa mezani.
Unaona kwamba kazi hiyo ya kuwawakilisha wananchi wanaifanya kwa moyo wao wote; si kwa lengo la kufurahisha mashabiki wa vyama vyao vya siasa, bali kwa lengo la kuijenga nchi yetu.
Wabunge vijana kwa vyama vyote, wanajitahidi kuwa makini kwa kazi yao ya ubunge.
Chama tawala kuna vijana makini sana, bahati mbaya ni kwamba baadhi yao wanalewa ‘uchama’ na kusahau kwamba kitu muhimu ni Tanzania Kwanza, na wala si vyama vya siasa.
Na wengine wanalewa si kwa vile wana mapenzi makubwa na chama chao, bali wanatamani na kutaka kukitumia chama chao kupata madaraka au kama njia ya kujitajirisha.
Sina maana kwamba najisifia Bali ninachokinena Ndicho Nikifanyacho , maana hata bila Mimi kusema sifa zangu zinajitosheleza.
Mimi ni msomi mwanasheria ambaye hadi leo hii bado naendelea kusoma.
Mimi ni mbunge nisiyekuwa na makeke, sina uchu wa madaraka, ni msomi ambaye nimeamua kuwawakilisha watu wangu.
Ninafanya kazi ya uwakilishi na wala si kutumia ubunge kujitajirisha. Ninajisimamia, siyumbishwi na naishi maisha yangu ninavyoamini mimi bila kuiga au kufuata mkumbo bila kutafakari kwa kina mwelekeo wa maisha.
Na kwa vyovyote vile mimi ni mwanamama wa kuaminika. Mnanifahamu wengi kwamba kwangu ndiyo ni ndiyo na hapana ni hapana.
Na mara chache kutupata watu wa namna hii! Wote Mnanifahamu kwa jina la Halima, lakini nilibatizwa jina la Theodosia. Hata hivyo natumia zaidi jina nililorithi kutoka kwa bibi yangu mzaa baba, Halima.
Mimi nimezaliwa katika familia ya Wakristo na nilibatizwa na kuitwa Theodosia.
Ukoo wangu ni waumini wa dini ya Kiislamu isipokuwa baba yangu na kaka yangu ambao walibatizwa na familia yangu ikaridhia wawe Wakatoliki.
Mimi nimezaliwa Machi 18, 1978 katika Kijiji cha Makanya, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro nikiwa ni mtoto wa mwisho katika familia ya Profesa James Mdee aliyekuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Nilianza kusoma elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mlimani jijini Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 1991.
Nilichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana Zanaki mwaka 1992 na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1995.
Mwaka 1996 hadi 1998 nilisoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilakala mkoani Morogoro na 1999 nilijiunga na UDSM, ambako nilisomea sheria na kuhitimu mwaka 2003.
Nilipata ajira katika Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana mwaka 2004 nikiwa ofisa maendeleo kama mwanasheria hadi 2005, nilipoamua kuacha kazi na kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ambako nilishiriki kuwapigia kampeni wagombea mbalimbali wa CHADEMA kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa viti maalumu.
Uchaguzi Mkuu wa 2010, nilijitosa kugombea ubunge kiti cha Jimbo la Kawe na kushinda kwa kishindo.
Ingawa nimezaliwa Kilimanjaro, lakini nimeishi maisha yangu yote Dar es Salaam, ndiyo maana niliamua kugombea ubunge Dar es Salaam na si Kilimanjaro, maana mbunge makini ni lazima ajue kwa undani maisha ya watu anaowawakilisha.
Na kusema kweli hata watu wa Jimbo langu la Kawe wanafahamu pasipo na shaka kwamba mbunge wao, anayafahamu matatizo yao.
NAWASIHI KAKA ZANGU DADA ZANGU NA WADOGO ZANGU PIA, MAISHA SI KUKATA TAMAA BALI NI KUJITAHIDI SANA KATIKA MASOMO ILI KUWEZA KUTIMIZA NDOTO ZAKO ZA MAISHA YAKO YA BADAE,
AHSANTE!!

No comments: