Saturday, November 9, 2013

LIPENI KODI KWA WAKATI, TOENI RISITI

Na Ahmad Nandonde, MUSOMA.
Wafanyabiashara mkoani mara wametakiwa kulipa kodi kwa wakati kwa mamlaka ya mapato tanzania TRA kwa kuzingatia taratibu mbalimbali za kibiashara ikiwa ni pamoja kuwapatia risiti wateja wao pindi wanapowauzia bidhaa.
Wito huo umetolewa jana na meneja wa mamlaka ya mapato tanzania mkoani mara Bw. Joseph Kalinga katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mlipa kodi zilizofanyika katika viwanja vya shule ya msingi mukendo mjini musoma ambapo amewataka wafanyabiashara kujijengea mazoea ya kulipa kodi zao kwa wakati bila udanganyifu ikiwa ni pamoja na kuwasihi kutoa risiti kwa wateja wao kwa bidhaa wanazokuwa wameuza ili kufanikisha zoezi la ulipaji kodi
Awali akisoma taarifa ya makusanyo ya mkoa Bw. Kalinga amesema mamlaka ya mapato mkoani hapa imeweza kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 79 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kiasi ambacho ni zaidi ya lengo lililokusudiwa la zaidi ya shilingi bilioni 68 sawa na asilimia 116.1.
Aidha Bw. Kalinga ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha ulioanzia mwezi julai 2013/2014 TRA imeweza kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 24 sawa na asilimia 91.24 huku wakitaraji kukusanya zaidi ya bilioni 110.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara, viwanda na kilimo (TCCIA) mkoani mara, Bw. Bartazal Bibogo amezitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya uchumi mkoani hapa ni pamoja na kufa kwa viwanda, uzalishaji wa chini ya kiwango pamoja na miondombinu mibovu na kusema kuwa kama viwanda na miundo mbinu ikiweza kuimarishwa basi mamlaka hiyo itaweza kuchangia ukuzaji uchumi kwa makusanyo makubwa ya kodi.
Bw. Gibogo amevitaja baadhi ya viwanda vilivyokufa na vingine kufanya chini ya viwango kuwa ni pamoja na mutex, vilian, musoma fish procesors na prime ketchi na kuongeza kuwa serikali na uongozi wa viwanda wanapaswa kukaa pamoja ili kuangalia chanzo cha kufa au kufanya chini ya viwango kwa viwanda hivyo na kisha kutafuta ufumbuzi ili kuimarisha uchumi wa mkoa wa mara.
Sherehe hizo za wiki ya mlipa kodi zilizanza tarehe 2 Nov mwaka huu yenye kauli mbiu isemayo "tulipe kodi kwa matokeo makubwa sasa" zimefikia tamati hii leo katika uwanja wa shule ya msingi mukendo na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa mara huku mgeni rasmi akiwa ni mkuu wa wilaya ya musoma mjini kwa niaba ya mkuu wa mkoa, ndugu jacksone msome.

No comments: