Friday, January 25, 2013

BIBI WA GESI YA MTWARA ANUSURIKA KUTEKWA NA MTU ALIYEDAIWA KUWA MWANAUSALAMA

Story ya Idrisa Bandali, MTWARA
BIBI SOMOE AKIWA NA MWANDISHI WA STORY HII, BWANA IDRISA
MKUU wa Kaya ya Msimbati ambako gesi asilia inachimbwa mkoani Mtwara, Bibi Somoe Mtiti (106) amenusurika ‘kutekwa’ na mtu anayedaiwa kuwa ni ofisa usalama wa Taifa baada ya wananchi kuvamia gari lake na kuliteketeza kwa moto jana usiku.
Hivi karibuni Bibi Mtiti aliionya serikali juu ya mpango wake wa kusafirisha gesi ghafi kwenda Dar es Salaam kwa madai iwapo serikali itapuuza onyo hilo bomba hilo litasafirisha maji badala ya gesi kusudiwa.

MTOTO WA BIBI SOMOE
Kwa mujibu wa wanakijiji hao, Mtu huyo ambaye ana asili ya kijiji hicho waliyemtambua kwa jina la Seleman Babu aliwasili kijijini hapo siku ya tukio saa 10 jioni akiwa na gari ndogo aina ya Mark II na kwenda nyumbani kwa shangazi yake.

Habari zinadai kuwa saa 2 usiku Babu, alikwenda nyumbani kwa Bibi Mtiti akiwa na gari pamoja na shangazi yake aliyetajwa kwa jina la Fatuma Saidi Tom.

“Unajua yule bibi tunamlinda, sasa ilipoonekana ile gari usiku pale, watu wakaanza kujiuliza linafanya nini…wakaanza kusogea , kadiri mda ulivyokuwa unakwenda ndivyo watu walivyozidi kuongezeka” alisema Juma Ayoub mkazi wa kijiji hicho.
Asha Hamisi ni mtoto wa pili wa Bibi Mtiti, akihadithia juu ya tukio hilo alisema yapata saa 2 usiku wakiwa wanakula chakula alipokea wageni wawili ambao baada ya kumaliza kula waliomba kuongea na mkuu huyo wa kaya.
MABAKI YA GARI ILIYOCHOMWA

“Alikuja kijana na mama wakaniomba kuongea na bibi…alimuliza bibi kama ana uwezo wa kwenda Mtwara, bibi akajibu hawezi…wakaniuliza mimi kama naweza kwenda badala yake nikawaambia siwezi…akasema ametumwa na Rais Jakaya Kikwete na Hawa Ghasia..wamjie bibi wakazungumze nae mambo ya gesi” alisema Hamis
Aliongeza kuwa “Alisema kama bibi yupo tayari Jumanne ijayo watamfuata kwa gari…mimi nikasema sitaki…nilipochungulia nje nikaona watu wengi wamezunguka”
“Kwa kuwa tunamfahamu tulimwambia aondoke mpango aliojia haufai, akawa anabisha, tukaendelea kumsihi..wakati huo watu wanazidi kuongezeka…alipotoka akakosea njia, alipotita hakukuwa na njia…watu walimfuata wakaanza kumrushia mawe…aliacha gari akakimbia…ndipo wananchi walipoliteketeza gari kwa moto” alisema Manzi Mohaedi Faki mtoto wa tano wa Bibi Mtiti
SHANGAZI WA MTUHUMIWA BI FATUMA
Fatuma Tom ambaye ni shangazi wa Babu amethibitisha kumpokea mwanae huyo na kumsindikiza kwa Bibi Mtiti na ambako alimuomba mkuu huyo wa kaya akubali kuondoka nae kwenda Dar es Salaam kwa maelezo kuwa ametumwa na viongozi wake wa juu.
“Ni mwanangu mtoto wa kaka yangu, alikuja akaniomba nimepeleke kwa bibi akamsalimie tuliondoka saa 2 usiku…watu walituzingira na hali ilipokuwa mbaya niliondoka na kumwacha mwanangu pale, nae alikimbia na ndipo walipochoma moto gari” alisema Tom
Alifafanua kuwa “Huyu mwanangu anaishi Dar es Salaam, anafanya kazi usalama wa Taifa…nadhani alirudi jana hiyohiyo Mtwara”
Mwnyekiti wa kijiji cha Msimbati, Salum Tostao alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa ofisi yake haikupokea mgeni yeyote kutoka serikalini kwa siku hiyo.
“Ni kweli gari imechomwa lenye namba za usajili T 609 BXG mali ya Mussa Babu…taarifa hii ni kwa mujibu wa nyaraka tulizookota kutoka ndani ya gari hilo” alisema Tostao
Selemani Babu alikanusha madai ya yeye kwenda kijijini hapo jana na alisema “Hapana, hapana labda umekosea…na..na..na..umekosea…sijakwenda maimbati jana…kwanini asiwe Mussa, umekosea sio mimi kwa heri”

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki alisema hana taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo kwa kuwa mhusika hajakwenda polisi kulalamika

No comments: