HOJA
BINAFSI YA KABWE ZUBERI ZITTO(MB) KUHUSU KULITAKA BUNGE KUCHUNGUZA NA KUILEKEZA SERIKALI KUCHUKUA
HATUA DHIDI YA RAIA WA WATANZANIA WALIOFICHA FEDHA NA MALI HARAMU NJE YA NCHI
[Inatolewa chini
ya Kanuni ya 54(3)]
KWA
KUWAkumekuwa na uthibitisho kutoka Mamlaka za nchi ya Switzerland kwamba kuna
raia wa Tanzania wanamiliki fedha za kigeni katika Benki nchini na kwamba kuna
kanuni na taratibu za nchi zinazoendesha na kuongoza ufunguaji wa akaunti za
fedha za kigeni nje ya Tanzania kwa Watanzania wakazi (residents). Na kwamba kitendo
kilichofanywa na wahusika kuweka mabilioni ya fedha kwenye nchi za nje kinaweza
kuwa ni kinyume na sheria ya “FOREIGN EXCHANGE ACT, 1992”
NA KWA KUWA sheria hiyo kifungu cha
(10) cha Sheria ya Fedha za kigeni kinazuia utoroshaji wa fedha za kitanzania
na isipokuwa kwa kibali cha Gavana wa Benki Kuu tu, hakuna mtu yeyote atakaye
ruhusiwa kusafirisha fedha nje ya
Tanzania.
Na kinaeleza kuwa kwa msafiri anayekwenda nje ya nchi hatoruhusiwa
kuondoa na kiasi cha shilingi ambazo zinazidi dola za kimarekani hamsini. Vile
vile kwa mujibu wa Sheria hiyo kifungu cha 6 na 7 na waraka uliotolewa na
Gavana wa Benki Kuu kwamba Mtanzania yeyote mwenye kutaka kufungua akaunti
kwenye mabenki nje ya Tanzania lazima apate kibali cha Gavana.
NA
KWA KUWA masharti hayo ya sheria yanaweza kuwa yamekiukwa na wahusika kwa
kuhifadhi fedha za kigeni katika mabenki ya nje,
NA
KWA KUWA ukiukwaji huo ni dhahiri kuwa fedha zilizowekwa kwenye mabenki ya nje
kwa kiasi kikubwa ni fedha ambazo hazikupatika kwa njia za halali na kwamba
kuna uwezekano wa ukwepaji mkubwa wa kodi,
NA
KWA KUWA, nchi yetu imekuwa katika matatizo makubwa ya fedha za kigeni, jambo
ambalo limepelekea nchi kushusha thamani ya shilingi ili kukabiliana na gharama
za manunuzi ya bidhaa nje ya nchi,
NA
KWA HIYO BASI, ninaliomba Bunge hili liazimie:
1.
Kwamba Bunge lako
tukufu liunde Kamati Teule kuchunguza Raia wa Tanzania wenye kumiliki fedha za
kigeni na mali nje ya Tanzania. Kamati Teule hiyo ifanye kazi zifuatazo:
-
Kuchunguza mfumo
mzima wa utoroshaji wa fedha na kufichwa nje ya nchi,
-
kuchunguza na
kupembenua mali na fedha haramu dhidi ya halali zinazomilikiwa na raia wa
Tanzania katika taasisi za kifedha nje ya Tanzania,
-
kuchunguza utaratibu
mzima wa kugawa vitalu vya utafutaji mafuta na gesi kati ya mwaka 2003 mpaka
2008,
-
kuchunguza mtiririko
mzima wa utoroshaji wa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania kupitia Kampuni ya
Meremeta (pia Triannex pty ya Afrika Kusini na Deep Green Finance ltd) na
kupendekeza hatua za kuchukua dhidi ya wahusika wote wa utoroshaji wa fedha
kwenda nje,
-
kuchunguza umiliki wa
wa watanzania kwenye kampuni zote zenye mikataba ya utafutaji wa Mafuta na Gesi
hapa nchini na namna umiliki huo umekuwa ukibadilika, mapato (proceeds)
zilizotokana na mabadiliko hayo ya umiliki na kama kodi stahili zimekuwa
zikilipwa kutokana na kubadilika kwa umiliki huo,
-
kuchunguza kwa kina
mali za Watanzania wote waliowahi kushika nafasi za Uwaziri Mkuu kati ya mwaka
2003 mpaka 2010, waliowahi kushika nafasi za Uwaziri wa Nishati na Madini,
Uwaziri wa Ulinzi, Ukuu wa Majeshi, Ukatibu Mkuu wa wizara ya Nishati na
Madini, Ukatibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi, Uanesheria Mkuu wa Serikali,
Ukamishna wa Nishati, Ukurugenzi Mkuu wa TPDC, Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa
TPDC katika ya mwaka 2003 mpaka 2010.
2.
Kwamba Serikali ilete
muswada wa Sheria Bungeni ifikapo Mkutano wa 11 wa Bunge kwamba itakuwa ni
marufuku kwa Kiongozi yeyote wa Umma au mume au mke wake au watoto wake kuwa na
akaunti katika mabenki nje ya nchi isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali
rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
3.
Kwamba Serikali
iwasiliane na Benki ya Dunia ili kupitia Kitengo cha Assets Recovery Unit
mabilioni ya Fedha na mali zisizoondosheka zinazomilikiwa na Watanzania katika
mabenki ya nchini Switzerland, Dubai, Mauritius na visiwa na maeneo mengine
yote ambapo hufichwa fedha na Mali ili kukwepa kodi na kwamba mali hizo na mabilioni hayo
yaliyopatikana kiharamu yarudishwe nchini mara moja
4.
Kwamba katika muswada
tajwa hapo juu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aimarishiwe mamlaka ya kutoa
kibali kwa Mtanzania yeyote anayetaka kufungua akaunti ya Benki nje ya nchi na
kwamba kila mwaka Gavana atatangaza kwenye Gazeti la Serikali na magazeti
yanayosomwa na wananchi wengi orodha ya Watanzania walioomba na walioruhusiwa
kuwa na akaunti ya Benki nje ya Tanzania.
5.
Kwamba Watanzania
wote wenye akaunti za fedha nje waeleze wamezipataje na TAKUKURU wachukue hatua
za kisheria dhidi ya watu wote wenye kumiliki fedha na mali kinyume na mapato
yao halali.
6.
Kwamba Serikali,
katika mkutano wa Bunge wa 11 na baada ya Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge
kuhusu Raia wa Tanzania wenye kumiliki fedha za kigeni kwneye mabenki na mali
nje ya Tanzania ilete taarifa ya hatua ilizochukua ili kuziba mianya ya
utoroshaji wa fedha nje ya Tanzania.
7.
Kwamba Serikali
katika Bajeti ya mwaka 2013/14 itaanzisha kodi maalumu ‘financial transaction
tax’ ya angalau asilimia 0.5 ya thamani ya ‘transaction’ ili kuweza kuwa na
rekodi za uhakika za fedha ndani na zinazotoka nje ya nchi.
Mheshimiwa
Spika,
Naomba
kutoa hoja,
…………………….
KABWE
ZUBERI ZITTO(MB)
JIMBO
LA UCHAGUZI-KIGOMA KASKAZINI
08.11.2012
No comments:
Post a Comment