Wednesday, October 24, 2012

MFUMO WA SHERIA UNAHITAJIKA KURUHUSU MABADILIKO YA SERIKALI - MBOWEMwenyekiti wa CHADEMA 
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametaka kuwe na mfumo wa kikatiba na sheria kwa ajili ya kusimamia mabadiliko ya uongozi kufanyika kwa amani kutoka serikali moja kuja nyingine.
Alisema hali hiyo itaepusha nchi kuingia katika vurugu na mkanganyiko wa kisiasa pale chama kilichoko madarakani kikishindwa uchaguzi.
Mbowe alisema ingawa hiyo inaweza kuonekana kuwa ni dhana mpya, kutokana na umuhimu wake kwa ajili ya mustakabali mwema wa taifa, ni vyema Watanzania wakaanza kuitafakari kisha wadai kuwepo kwa mfumo huo wa kikatiba na sheria.
Katika hilo alitolea mifano namna ambavyo nchi ya Ghana ilipitia katika misukosuko kutoka utawala wa Jerry Rawlings kwenda NPP ya Rais Kuffour.
Akizungumza kwenye mikutano ya kampeni ya uchaguzi mdogo katika kata za Mpapa, wilayani Momba na Myovizi, Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya, akiwanadi wagombea wa CHADEMA katika maeneo hayo, Mbowe alisema ni hatari kwa nchi kama Tanzania ambayo sasa inapitia kwenye wimbi la mabadiliko makubwa, ikiwemo ya kisiasa, kukosa mfumo huo.
“Ni muhimu sana kuwa na sheria itakayohakikisha mabadiliko kutoka serikali ya chama fulani kwenda chama kingine au serikali moja kwenda serikali nyingine, kufanyika kwa amani na kwa kuhakikisha maslahi ya umma na nchi yanazingatiwa.
“Lazima tuepuke hali kama hiyo. Wenzetu Ghana walijifunza, walipoingia madarakani wakaamua kutunga sheria ya kusimamia kipindi cha mabadiliko kutoka uongozi wa serikali moja kwenda nyingine,” alisema.
Alisema Watanzania wanaweza kujiuliza kwa nini Marekani inachukua siku 72 kwa rais kuapishwa na kukabidhiwa rasmi mamlaka ya kuongoza nchi, tangu achaguliwe, ni kwa sababu kuna vitu vya muhimu sana vya kusimamiwa na kufanyiwa kazi kabla utawala mpya haujakabidhiwa Ikulu.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, alikumbushia namna ambavyo sehemu ya mabilioni ya ufisadi wa EPA yalihamishwa Desemba 31, 2010 wakati wa kuapishwa Rais Kikwete, alisema hilo lilichangiwa na kukosekana kwa mfumo huo wa kikatiba na kisheria, ni kama vile mali za nchi zinakuwa hazina uangalizi au mwangalizi.
Mwenyekiti huyo yuko kwenye ziara ya kuwanadi wagombea udiwani wa chama hicho katika kata mbalimbali mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe na Iringa, katika uchaguzi mdogo unaohusisha kata 29 katika mikoa mbalimbali nchi nzima, ambapo wananchi wa maeneo hayo watapiga kura Oktoba 28.
CHANZO. Tanzania Daima na Chadema blog

No comments: