Friday, September 7, 2012

TATHMINI YA MDAU IMAN KONDO , KWENYE FACEBOOK KUHUSU MAANDAMANO YA WAISLAMU DAR ES SALAAMLEO

Leo nimekuwa nikifuatilia habari za maandamano ya ndugu zetu waislam mkoa wa Dar es Salaam.

Sababu ya maandamano hayo imeelezwa kuwa ni kuitaka Wizara ya Mambo ya Ndani kuwaachia huru wananchi/waislamu waliowekwa chini ya ulinzi kwa kukwamisha shughuli ya sensa.

Baadae, vyombo vya habari ITV na Clouds FM vimetoa taarifa kuwa Wizara husika ametoa amri ya walioshikiliwa kuachiwa huru.

Kumekuwa na maoni mbalimbali juu ya tukio la maandamano na agizo la Wizara. Katika kufuatia maoni hayo, nimegundua kuna sehemu jamii inaelekea kukosea. Hivyo basi nimeona kuna haja ya kuandika haya ninayoandika.

Ili kuelewa vizuri yaliyotokea, ni vyema tukatambua kuwa katika tukio au matukio ya leo kuna mambo makubwa manne (4) yanayotakiwa kuangaliwa kila moja peke yake. Mambo haya yasichanganywe na kutolewa "hukumu moja". Mambo hayo ni haya yafuatayo:
1. Watanzania/waislamu kuandamana
2.Sababu inayowafanya waislamu kuandamana
3. Polisi kuheshimu haki ya watanzania/waislamu kuandamana
4. Wizara kutoa agizo la madai ya waislamu kutekelezwa.

Kama nilivyoandika awali, kila moja kati ya haya mambo linahitaji kuangaliwa kivyake na linaweza kuwa na mjadala mrefu tu. Mimi nitagusia kifungu namba tatu (3) kinachohusu polisi kuheshimu haki ya raia kuandamana.

Siku zote, kilio chetu kimekuwa kwa polisi kutokuheshimu haki za raia hasahasa linapokuja swala la maandamano ya kuishinikiza serikali.

Leo polisi wameonyesha ari tofauti. Hawajatumia nguvu wala kuzuia maandamano kwa namna yoyote ile. Ikumbukwa kuwa kuna magazeti leo yalishatoa fununu kuwa waislamu wataandamana na polisi walikuwa na nafasi ya kujiandaa kuwadhibiti waandamanaji iwapo wangekuwa na nia hiyo.

Kwa mtazamo wangu, kama watanzania tunaitakia mema nchi yetu. Kitendo cha polisi kuheshimu haki za raia kilichofanywa na polisi leo ni kitendo cha kupongezwa na kuhamasishwa kiendelee kuwepo siku zote. Ni dhahiri kuwa wapo waliochukizwa na kitendo cha watu fulani kukwamisha sensa au swala la waislamu kuandamana au wamechukizwa na kitendo cha wizara kutoa agizo la kuachia huru "watuhumiwa", lakini tukumbuke kuwa hizo ni mada nyingine zinazohitaji mjadala wake na si busara hata kidogo kuruhusu mada hizo zitupe upofu wa kuona jinsi polisi walivyoheshimu haki za raia na tukaachia mwanya wa kuwapongeza na kuwahimiza kuendelea hivyo.

Wanasaikolojia wanatufundisha kuwa jambo jema likifanyika likapongezwa, inaongeza uwezekano wa jambo hilo kujirudi. Likitokea jambo jema likapuuzwa, inapunguza uwezekano wa jambo hilo kujirudia. Tunataka kujenga Tanzania ambayo mambo mema yanajirudia kila siku na kwa leo, tuwapongeze polisi ili heshima yao kwa haki za raia liwe ni jambo linalojirudia na kuzoeleka kwenye jamii.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

No comments: