Friday, August 24, 2012

RAIA WA KOMORO WAOKOTWA BAHARINI ZANZIBAR


Wavuvi wawili Raia wa Komoro, wamekutwa katika Kisiwa Kidogo cha Pungume nje kidogo ya Zanzibar, huku hali zao zikiwa zimedhoofika kwa uchovu na njaa baada ya kupotea na kuishi baharini kwa muda wa siku 11 bila ya chakula.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar Kamishna Msaidizi ACP Yusufu Ilembo, amewataja wavuvi hao kuwa ni Othman Inzudin(24) na Nurdin Ahmed(18) ambao wote ni Raia wa Komboro.

Amesema kuwa wavuvi hao wakiwa na boti ndogo katika shughuli zao za uvuvi huko nchini Komoro, walipatwa na misukosuko ya mawimbi na upepo mkali na kupotea baharini, huku boti yao ikiwa imeishiwa mafuta.

Vijana hao wamejikuta wakiishi majini kwa muda mrefu bila ya chakula wakinywa maji chumvi ya bahari huku wakienda kwa kufuata mwelekeo wa upepo na mawimbi ya bahari hadi walipofika katika kisiwa hicho cha Pungume kilichopo kusini mwa Zanzibar.

Katika harakati za kujiokoa walilazimika kufungua injini ya boti yao na kuitosa majini kama njia ya kuifanya boti yao kuwa nyepesi ili isukumwe na mawimbi kwa urahisi na kuweza kutokea nchi kavu kunusuru maisha yao.

No comments: