Thursday, August 9, 2012

JAJI WARIOBA: MSIWALAZIMISHE WANANCHI KUOTA MAONI YAO


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba amevitaka vyama vya siasa, asasi za kidini na wanaharakati kuacha kuwaelekeza wananchi aina ya maoni wanayopaswa kutoa kuhusu Katiba Mpya.

Jaji Warioba ameyasema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia tathmini ya mikutano ya awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika mikoa minane ya Pwani, Dodoma, Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba.

Kwa mujibu wa Jaji  Warioba, vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali ziatapata muda wa kuwasilisha maoni yao Tume na hivyo si wakati muafaka asasi hizo zisizo za kiserikali kuwalazimisha wananchi watoe maoni wanayotaka wao.

Kuhusu idadi ya mikutano iliyofanyika katika awamu ya kwanza, Mwenyekiti huyo amesema Tume yake imefanya mikutano 386 katika mikoa minane ya awamu ya kwanza kwa muda wa mwezi mmoja na kwamba Wastani wa wananchi 188,679 walihudhuria mikutano hiyo ya Tume.
Awamu ya pili ya mikutano ya kukusanya maoni,inatarajiwa kuanza rasmi tarehe 27 Agosti, mwaka huu na ratiba ya mikutano hiyo itatolewa na Tume hivi karibuni.

No comments: