Tuesday, June 26, 2012

MSIMAMO MPYA WA BAKWATA JUU YA SUALA LA SENSA HUU HAPA

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba ametoa msimamo wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania  (BAKWATA), akiwataka Waislamu wote nchini kushiriki Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 26, mwaka huu.

Kauli hiyo ya Mufti Simba  inakuja siku chache baada ya tamko la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania likiwataka Waislamu wote kutoshiriki kwa shughuli hiyo kwa kile walichodai ni kutoingizwa kipengele cha dini  kwenye dodoso la Sensa.

Hii ni mara ya pili kwa Mufti Simba kuzungumzia suala hilo, mara ya kwanza ikiwa ni Juni 6, mwaka huu alipozungumza na waandishi wa habari mkoani Tanga na kuitaka Serikali kuingiza kipengele cha dini katika dodoso la Sensa.

Alisema kalenda iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa takwimu zinazoonyesha idadi ya Watanzania ni 43 milioni, kati yao wakristo ni asilimia 52, waislamu asilimia 32 na dini nyingine wako asilimia 16.

Mufti Simba alipinga na kulaani takwimu hizo kwamba si sahihi na zinapotosha wananchi, kwa sababu Sensa iliyofanyika mwaka 2002 haikuhusisha  kipengele kinachobainisha dini za Watanzania.
“Kwa kuwa taarifa hizi zinaonekana kwenye kalenda ya waziri mkuu, tunaitaka Serikali kurudisha kipengele kinachobainisha dini za Watanzania mwaka huu ili ukweli ubainike kwa lengo la kuondoa kabisa sintofahamu hiyo,” alisema Mufti Simba.

Lakini, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mufti Simba alisema walichokuwa wakipinga Waislamu ni baadhi ya watu kuanza kutoa takwimu za idadi ya Wakristo na Waislam wakati hawana dhamana na mamlaka ya kufanya hivyo.

Akisisitiza umuhimu wa Waislam kujitokeza kuhesabiwa, Mufti Simba alisema, “Mimi kama kiongozi wa Waislamu natoa wito kwa Waislamu wote hapa nchini, kushiriki kwa ukamilifu katika zoezi la Sensa litakalofanyika nchini mwetu.”

Aliongeza: "Katika nchi yetu Sensa zimefanyika nyingi miaka ya nyuma na hazikuhusishwa na dini wala ukabila, ni jambo lililo zoeleka na kukubalika."

Mufti Simba alisema kilichojitokeza hivi karibuni ni takwimu za Sensa kutolewa na watu ambao hawana dhamana hiyo, na Serikali inatakiwa kutunga sheria itakayomuainisha atakaye kuwa na dhamana ya kutoa taarifa hizo.

“Waislamu wasisite kuiomba Serikali iwafafanulie takwimu za Sensa ambazo zilikuwa zikitolewa kuwa Waislamu wako kadhaa, na Wakristo wako kadhaa, kama serikali inazitambua takwimu hizo,” alisema Mufti Simba na kuongeza:

"Katika tovuti mbalimbali na hata za Serikali kuna taarifa kuwa Waislamu wako takriban asilimia 35. Sasa hizi hatujui zimepatikana wapi na nani amezitoa."

Source: http://www.wavuti.com/ Gazeti la Mwananchi

1 comment:

Mzee Salehe said...

Jamai Huyu mufti anatakiwa awe makini anapofanya maamuzi kwani kauli yake ya mwanzo ni waislamu kugomea sensa na sasa anahairisha mgomo huo kama muislamu anatakiwa awe na msimamo ajue kuwa anayumbisha waumini.