Saturday, June 30, 2012

MCHAKATO WA MAHAKAMA YA KADHI TANZANIA WAKAMILIKA

Serikali imesema uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi itakayoshughulikia migogoro na masuala mbalimbali ya usatawi wa Waislamu nchini umefikia katika hatua nzuri.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema jana wakati akijibu hoja za wabunge zilizojadili kwenye hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na  Wizara na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Alisema itaanzishwa wakati wowote baada ya maandalizi kukamilika na kwamba utekelezaji wake uko katika hatua nzuri baada ya kamati ndogo iliyoteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria yenye wawakilishi wa Waislamu na Serikali imetoa taarifa yake ya mwanzo ya  namna ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.

Waziri Mkuu alisema mambo yatakayoshughulikiwa na mahakama  hiyo ni pamoja na ndoa na talaka, mirathi, wosia, hiba/zawadi na wakifu vilevile itahusika na mashauri ya jinai.

Alisema, “upo umuhimu na dhamira ya kweli ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara aidha, mahakama hiyo itagharamiwa na kuendeshwa na Waumini wa Dini ya Kiislamu wenyewe.”

Alisema wataalamu wa kuanzisha mahakama hiyo watakwenda  nchini Kenya, India, Uingereza  na Zanzibar kujifunza jinsi ya kuanzisha chombo hicho na kwamba ziara hiyo itagharamiwa na serikali.

Source: http://www.wavuti.com na Nipashe 

No comments: