Saturday, June 30, 2012

KAMA UNATARAJIA KUINGIA KWENYE NDOA CHUKUA HII ...CHANGAMOTO KWA VIJANA KABLA YA NDOA


Na, Daudi Charles Mponda

NAANDIKA mada hii nikiwa na uhakika kwamba, vijana wengi wa sasa wanatamani kuingia kwenye ndoa wakiwa na mitazamo mbalimbali. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, wengi wana matarajio ya kupata vitu vizuri zaidi kwenye ndoa hizo.Nasema hivyo nikimaanisha kuwa, wanaamini wakiwa kwenye ndoa watatimiza ndoto zao za muda mrefu. Hupiga picha kuhusu idadi ya watoto watakaozaa, namna watakavyowasomesha na jinsi ambavyo familia yao itakuwa yenye furaha.

Kifupi wanafikiria zaidi kuhusu mambo ambayo yatawafurahisha. Kamwe hawapati muda wa kufikiria namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha watakazokutana nazo. Hawaelewi kwamba kuna siku wanaweza kukaa wiki nzima ndani bila kuzungumza! 
Je, ni kweli kwamba ndoa ni furaha tu? Hakuna huzuni? Hakuna ugomvi? Rafiki zangu, hata viongozi wa dini wanapofungisha ndoa husisitiza kuhusu kuvumiliana, kutunzana na kupendana kwa dhati hata katika kipindi cha shida na raha.
Kwa bahati mbaya, baadhi ya rafiki zetu wanapokea tofauti maneno haya, wanaamini kwa kuambiwa hivyo humaanisha kwamba kupendana labda hata kama fedha ya kula itakosekana nyumbani, mwenzake akiumwa n.k. Huo ni mtazamo tasa. Katika mada hii nitakufumbua ujue nini zaidi utakutana nacho ukiwa ndani ya ndoa. 
Hizi ni changamoto muhimu kwa vijana kuzijua na kujiandaa kukabiliana nazo tangu mapema.KWA NINI CHANGAMOTO?Rafiki zangu ipo haja ya kujadiliana juu ya jambo hili tena kirafiki kabisa. Haya ni mambo ambayo sisi vijana tunakutana nayo sasa. Ni wazi kwamba, kila kijana anawaza kuhusu ndoa.
Anawaza kuoa au kuolewa. Anatamani kuwa na familia yake ili aitwe mama au baba, au siyo jamani? Sasa kabla ya kuingia kwenye hizo ndoa ni lazima tuzijue kwanza, hii ndiyo sababu hasa iliyonisukuma kuandika mada hii.
Kama nilivyoeleza hapo juu, fikra za wengi ni tofauti. Asilimia kubwa wanafikiria zaidi kuhusu maisha mazuri yasiyo na mikwaruzano. Wanawaza kufurahia ndoa na kudhani hakuna changamoto nyingine.
Wapo wanaofikiria hata suala la tendo la ndoa. Kwamba watakuwa huru kukutana kila siku kadiri watakavyoweza kwa kuwa wapo pamoja ndani. Hii ni mitazamo mibaya katika ndoa.
Ni kweli unaweza kufanya tendo la ndoa na mwenzako mara nyingi uwezavyo, lakini nani amekudanganya kwamba kila siku utaendelea kumuona kama umuonavyo leo? Amini usiamini, zipo ndoa nyingi zinazolalamikia suala la tendo la ndoa.
Kuna ambao wanadai hawatoshelezwi huku wengine wakilalama kuwa wenzi wao hawataki kabisa kutoa unyumba. Unajua kwa nini? Ama ana mtu mwingine pembeni au amechoshwa na mapenzi ya aina moja kila siku.Mitazamo ya wanaumeHawa fikra zao huwa kwenye suala la usafi, wanaamini wakiwa kwenye ndoa nyumba itakuwa safi, nguo zitafuliwa, kupikiwa na mambo mengine ya kifamilia.
Akili zao zinakomea hapo tu, hawawazi kuhusu migogoro na namna ya kutatua. Wanaota kuwa na maisha mazuri, kuwa na watoto na kujijengea heshima kwa jamii. Hilo tu, basi!Wanawake vipi?Baadhi ya hawa ninaowazungumzia hufikiria kuhusu kuvaa vizuri, kutolewa out, kupata watoto na mengineyo. Kamwe hawana muda wa kufikiria juu ya matatizo ambayo yanaweza kutokea katika maisha ya ndoa.
Hili ni tatizo. Rafiki zangu, maisha ya ndoa hayana furaha siku zote. Kuna wakati dhoruba hutokea na kusababisha mifarakano hivyo kuhitajika umakini wa hali ya juu katika kumaliza tatizo. Si kila siku kuna amani.NINI TATIZO?Kwa wale ambao wana mitazamo ambayo nimeeleza hapo juu, huwa hawana muda kwanza wa kuwachunguza wapenzi wao, lakini pia wao wenyewe kuonesha tabia zao halisi ili wenzi wao waweze kusoma kama wataweza kuendana nao.
Rafiki zangu, kwa ujumla hatutakiwi kufikiria mazuri pekee kwenye ndoa, kuna mengi ya kuvumiliana. Lakini pia kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa na mwenzako kuna vitu muhimu sana vya kuzingatia.

Mdau amaeyaandika haya katika ururasa wake wa facebook

No comments: