Friday, June 1, 2012

KIONGOZI WA UAMSHO ZANZIBAR - AONGEA



Sheikh Farid Hadi Ahmed

ZANZIBAR IJUMAA JUNI 1, 2012. SIKU moja tu baada ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein, kuzungumza na Waandishi wa Habari Ikulu mjini Zanzibar kuhusiana na Vurugu zilizotokea wiki iliyopita, leo Kiongozi wa kundi la Uamsho Sheikh Farid Hadi Ahmed, amezungumza na Waandishi wa Habari na kusema kuwa wataendelea na harakati zao ya kupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mpaka kieleweke.

Sheikhe Farid ambaye amelaani vikali vitendo vya uharibifu wa mali ukiwemo wa uchomwaji moto magari na baadhi ya makanisa mjini Zanzibar, amesema pamoja na wao kulisaidia Jeshi la Polisi katika kukusanya taarifa za kuwabaini wale wote waliohusika na uharibifu huo, lakini pia wataendeleza harakati za kudai kura ya maoni ya kupinga Muungano wa Jamhuri ya Tanzania.

Ingawa alikataa wafuasi wake kushiriki katika vurugu, lakini amesema leo wanakesha msikitini kuwaombea heri vija wote waliokamatwa kufuatia vurugu hizo ili waachiliwe bila ya masharti.

Sheikhe Farid pia amewalaumu baadhi ya vijana wakiwemo wa chama kimoja cha siasa kuwa wao ni miongoni mwa wanzilishi wa vurugu hizo.

Amesema kwa hatua hiyo anajenga imani kuwa miongoni mwa watu waliochoma makanisa siku ya tukio hilo, walikuwa ni mmoja miongoni mwa vijana hao na wanakamilisha taarifa zao ili kuwapatia Polisi kwa hatua zao.

Amesema mbali ya kuwa Serikali imepiga marufuku mikutano na maandamano, lakini Jumuiya yao ya Uamsho itafanya Mhadhara mkubwa Jumapili Juni 3, mwaka huu kwenye Viwanja vya Lumbumba mjini Zanzibar mhadhara ambao utafuatiwa na maandamamo yatakayofanyika Juni 26, mwaka huu.

Wakati wa mkutano huo, Sheikhe Farid pia amevilaumu baadhi ya Vyombo vya Habari hapa nchini na kusema wameandika habari zenye chumvi nyingi na kuupotosha umma kwa kuongeza hofu miongoni mwa wananchi wa ndani na nje ya Zanzibar.

Hata hivyo Shehe huyo ameshindwa kufafanua baadhi ya hoja alizoulizwa na waandishi wa habari kwa mfano kuzibwa kwa barabara kwa mawe na magogo ya minazi ama kuchomwa matairi na makanisa kuwa inauhusiano gani na madai ya kuwepo kwa muungano.

CHANZO : Michuzi blog

No comments: