Wednesday, April 4, 2012

CUF na HADITHI YA MBILIKIMO (Sehemu ya kwanza)


Rashid Mtagaluka-Mwandishi wa makala hii.

Kwanini wanakataa maumbile yao?

MBILIKIMO ni mtu mfupi sana, kibilikizi kwa jina jingine. Kwa kiasi kikubwa watu wa jamii hii ambao ukiachia kimo chao hawana kasoro yoyote, mbilikimo wanapatikana kwa wingi Congo Brazavill, na jijini Kinshasa pale DRC.

Mbilikimo ni jamii ya watu wenye uwezo mkubwa kiakili, wabunifu na wenye nguvu. Ukwa na Aki wasanii wa filamu nchini Nigeria ni ushahidi mmoja wapo.

Hata hivyo Mbilikimo wana tatizo moja la ajabu, kwamba hawapendi kutambulika kuwa ni wafupi sana. Haijafahamika sababu zinazowafanya wachukie kuonekana ni wafupi wakati ndivyo walivyo!

Inafikia wakati mbilikimo anaweza kumshughulikia mtu yeyote akibaini kuwa kimo chake kinageuzwa utambulisho mbele ya kadamnasi.

Haijalishi mtu huyo atamtambulisha mbilikimo kwa bayana ama kitaathira, vyovyote vile iwavyo, ikibainika kuwa ililengwa kumuonesha jinsi alivyo mfupi sana, cha mtemakuni atakiona!

Mbilikimo au Emoroh jina la mcheza shoo wa mwanamuziki maarufu nchini DRC Kabasele yampanya (Pepe Kale) wanafurahi sana ukiwatambua kama watu warefu.

Ndo maana akifika mahala inasemekana anakuuliza kwanza kwa kukutega, umemuonea wapi? Ukisema ndo unamuona pale pale alipo, ndugu yangu utaambulia kichapo. Kwani anaamini kuwa hukumuona akiwa mbali kutokana na ufupi wake!

Bali inabidi umjibu umemuona tokea akiwa mbali, kwa maana kumbe yeye ni mrefu. Na hapo mtakuwa marafiki sana na kama ana uwezo Mbilikimo atakupa hata gari ya kutembelea.‘Tall’ ni jina ambalo linawafurahisha kwelikweli Mbilikimo duniani kote!, japokuwa ndani ya nafsi zao wanajua kuwa wao sio warefu ki hivyo, lakini inashangaza kuona wanachukia kupita kiasi kuitwa wafupi ingawa kwa upande mwingine ndio uhalisia wenyewe.

Kwa ufupi Mbilikimo yuko tayari kufukuza hadi rafiki zake wa karibu ambao walianza maisha ya ugumu pamoja hapo zamani za kale, mara anapobainikiwa wenziwe hao wanamtambulisha katika jamii kuwa ni mtu mfupi!

Hali kadhalika ndani ya vyama vyetu vya siasa nako hakujawa salama. Mitazamo, fikra na mihemko ya baadhi ya wanasiasa haina tofauti yoyote na Mbilikimo.

Vyama vingi vya siasa Barani Afrika kama sio vyote, hususan hapa nyumbani, havipendi kuonekana dhahifu, vimekosa mwelekeo (dira), vinaongozwa kwa utashi wa mtu mmoja na kadhalika.

Na mtu yeyote atakayethubutu kusema hivyo hadharani au hata mafichoni, akibainika na wenye vyama vyao, cha moto atakiona!

Ama kwa vyombo vya habari vikidiriki kuueleza umma kupitia vyombo vyao juu ya hali halisi ya vyama hivyo, ‘Mbilikimo’ wa siasa hukurupuka na kuanza kuwasakama huku wakidai vyombo hivyo vinatumika kuwahujumu.

Badala yake baadhi ya vyama hivyo na viongozi wake wanafurahi sana vyombo vya habari vikiandika habari za kuwasifia hata kama ‘Mbilikimo wetu’ hao wanayakini kuwa sifa hizo hawastahikinazo!

Mathalani CUF-Chama cha Wananchi, baada ya kupoteza muelekeo wake wa kisiasa kutokana na maamuzi ya pupa yaliyosukumwa na utashi wa kisultan uliopelekea kuwafuta uanachama wanachama wake wane mapema mwaka huu, bado kinahitaji kipewe sifa ya kuwa kinaimarika!

CUF inaimarikaje huku takriban wilaya 54 kati ya 90 za Tanzania Bara zikiwa hazina viongozi wa kuchaguliwa?

CUF tuisifieje kuwa iko ngangari kinoma wakati ambapo wilaya moja tu ya Mtwara mjini viongozi na wanachama zaidi ya 400 wamehama na baadhi kujiunga na NCCR-Mageuzi?

Tutasemaje CUF bado hai ilihali Dodoma pekee wanachama wake wasomi wa Vyuo Vikuu wapatao 800 wamejiengua hivi karibuni kutokana na viongozi wa chama hicho kujifanya Mitume wasioshaurika?

‘Mbilikimo’ wetu wa siasa wanataka wanahabari tusiseme kwamba CUF inachungulia kaburi hata pale Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar Ismael Jussa Ladhu alipobainisha kuwa CUF haishindi mahala walipo Watanganyika na Wakristo?

Hivi ikisemwa kuwa CUF Bara inakufa kuna makosa gani ikiwa Jussa kiongozi mwandamizi wa chama amesikika akisema katika viwanja vya Gombani kule Pemba kuwa lengo la CUF ni kuistawisha Zanzibar (sio Bara) na watu wake?

Au ‘Mbilikimo’ wetu wa siasa wanataka tusiandike kwamba CUF iko mahututi kwa kuwa imefanikiwa kumfungia ngulai mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kwa mapokezi yale ya kihistoria?

Itakuwa ni upumbavu unaomzidi hata Mbilikimo mwenyewe wa kule Congo kujidanganya kuwa CUF iko imara kwa kigezo cha mapokezi wakati ukweli hauko hivyo.

Ni jambo lililo wazi kabisa kwamba, uimara wa chama cha siasa abadan haupimwi kwa uwingi wa mapokezi au mahudhurio katika mikutano yake ya hadhara.

Tujiulize umati ule tulioushuhudia pale uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Machi 11, 2012, ni wakaazi wa jijini Dar es Salaam ama ni nchi nzima?

Vyovyote itakavyokuwa, bado kuna maswali mengine ya kujiuliza.

Kwamba, kama wote ni wa Dar es Salaaam maana yake CUF bado iko ngangari sana Dar- es- Salaam, iwapo ni hivyo kwanini imeshindwa kupata Halmashauri ama walau Jimbo moja kati ya saba yaliyopo Dar katika uchaguzi mkuu wa 2010 na kuambulia madiwani wasiozidi watano kati ya madiwani wote wa Dar na kura 103,487 tu kwa mgombea wa urais kati ya kura 1,987,908?

Na iwapo umati ule umetoka maeneo mbalimbali ya nchi kuja kuongeza hamasa ya kumpokea Profesa Lipumba, hatuwezi kujisifu sana kwamba CUF bado iko hai!

Kwa kuwa hata TLP, TADEA, UPDP, NCCR-Mageuzi na Chadema wakiamua kuhamasishana waje kwa wingi ‘air port’ kumpokea kiongozi wao, naamini patakuwa hapatoshi pale ni suala la utashi tuu!

Na hili ni miongoni mwa makosa makubwa yanayoendelea kufanywa kwa makusudi na viongozi wa chini ili kuwapotosha viongozi wao wa juu kuhusiana na uhai na maendeleo ya jumla ya chama chao.

Ndio maana tokea siku ile tumekuwa tukisikia kauli za viongozi hao pamoja na baadhi ya wafuasi wanaozidekeza akili zao na kusubiri mtu mwingine afikiri kwa niaba yao, wakiponda kauli za watu wanaodai kuwa CUF inakufa pasi na kutafakari.

Binafsi nawaheshimu sana viongozi wa CUF, na hivyo siamini kama wataendeleza kuwa na muono wa ki-Mbilikimo, usiotaka kuambiwa ukweli hata baada ya kusoma makala haya na kuangalia alama za nyakati.

Kwamba kama ilivyo kwa Mbilikimo wetu wa kule Brazavill, haijajulikana ni kwanini viongozi wa chama hicho nao wanaona kinyaa kukubali yalivyo ‘maumbile’ yao kwa sasa.

Wanalazimisha jamii ikubaliane na ummati uliokwenda kumpokea Lipumba Machi 11 kwamba ni kigezo cha uhai wa CUF!

Haiwezekani kutuaminisha hivyo bila ya ushahidi wa kisayansi, labda hilo litakubalika tu katika jamii ya watu wavivu wa kufikiri!

Tusiende mbali, CUF sio mara ya kwanza kufanya mapokezi makubwa ya namna hile kila Mwenyekiti wao anaporejea kutoka Ulaya na Marekani.

Tunachojiuliza ni vipi mapokezi hayo yanakisaidia chama hicho katika kushinda chaguzi zinazoshirikisha vyama vingi vya siasa?

Tokea mwaka 1993 vyama vilipopata usajili wa kudumu ni CUF pekee kinachoongoza kufanya mapokezi ya jinsi ile pamoja na maandamano ya nguvu jijini Dar es Salaam ikilinganishwa na vyama vingine vya upinzani. Hakuna atakayediriki kupinga ukweli huo!

Lakini ukiondoa jimbo la Kigamboni mwaka 2000-2005, chama hicho hakijawahi kupata kiti kingine jijini humo, na kwa hali ilivyo sasa kama hawajajipanga, sidhani kama wanayo matumaini ya kupata jimbo tena!

Ikiwa kutetea tu kiti cha diwani wao aliyefariki kule Vijibweni jimbo la Kigamboni imekuwa mtihani, itakuwaje kupata jimbo 2015? Achilia mbali kukamata dola!

Sasa watu wakisema hali ya chama hicho ni tete, sio nzuri wanakuja juu kama moto wa kifuu mithili ya Mbilikimo anavyohamaki akiambiwa “nimekuonea hapa hapa”! Anataka aambiwe nimekuonea tokea ukiwa kuleeeeee.

Kwa muktadha kwamba Chadema ina majimbo mawili ya Ubungo na Kawe bila ya kuwahi kufanya mapokezi au maandamano jijini Dar, ni ushahidi kuwa, mapokezi, maandamano na watu kujaa mikutanoni sio vigezo vya kisayansi kuwafanya viongozi wajiridhishe na uimara wa chama chao!

Na hilo la kuporomoka kwa CUF nimekusudia kulibainisha hapa kwa kutumia takwimu za matokeo ya chaguzi Kuu mbili zilizopita, 2005 na 2010.

Nimedhamiria kufanya hivyo kwa kutumia takwimu kwa sababu ndio ushahihidi pekee unaoaminika duniani kote na kada tofautitofauti wakiwemo na wataalamu.

Takwimu kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu ni nambari zinazoeleza na kulinganisha ukweli juu ya matukio ya mambo kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawa.

Kutokana na umuhimu wake, takwimu (statistics) imekuwa ni miongoni mwa fani mahususi zinazofundishwa katika vyuo mbalimbali vya elimu hapa ulimwenguni.

Katika uchaguzi Mkuu wa 2005 CUF ilikuwa moto wa kuotea mbali, hakuna atakayebisha ukweli huo.

Japokuwa matokeo ya urais katika uchaguzi huo yalimtangaza Dk Jakaya Kikwete kuwa ni mshindi, lakini Profesa Lipumba alishika nafasi ya pili baada ya kupata kura 1,327,125 sawa na 11.68% ikilinganishwa na mwaka 2010 alipoambulia kura 695, 667 sawa na 8.06%.

Bado tu ‘Mbilikimo’ wetu wanakataa wakiambiwa wao ni wafupi? Kwamba mgombea urais wao ameshuka kwa asilimia 50 ni dalili ya chama kupoteza dira?

Matokeo haya ni kabla chama hakijapasuka vipande viwili, bado kulikuwa na mshikamano ingawa ulikuwa ni wa kiujanja-ujanja ambao ndio uliozaa matokeo hayo ya kusikitisha.

Nikija kwa upande wa viti vya ubunge na hasa nijikite jijini Dar es Salaam ambako mwaka 2005 kulikuwa na majimbo sita ya uchaguzi na mwaka 2010 kuliongezeka jimbo moja la Segerea.

Ni muhimu kuanzia hapa kwa sababu hata mapokezi yaliyofanywa na CUF hivi karibuni yalifanyika Dar ambapo kwa utashi wa viongozi wake wanadhani ni mahala panapotosha kuwashawishi Watanzania waamini kuwa chama hicho bado ni hai! Kitu ninachokifananisha na mtu anayejaribu kujitekenya halafu akacheka mwenyewe!

Ungana nami wiki ijayo katika mfululizo wa makala haya ili ufahamu takwimu katika chaguzi zilizopita zinavyobashiri waziwazi kifo cha CUF, na jinsi ‘Mbilikimo’ wa siasa wanavyofanya juhudi za kumshughulikia kila anayebainika kuonesha kimo halisi alichonacho (udhaifu).

Na Rashidi Mtagaruka
O784438546

No comments: