Wednesday, April 4, 2012

BEI MPYA ZA MAFUTA KUANZIA APRIL 7


Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini.

Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Tarehe 7 Aprili 2012. Pamoja na kutambua bei kikomo za bidhaa mbalimbali za petroli nchi nzima, ni muhimu kuzingatia yafuatayo.


(a) Bei za jumla na rejareja kwa aina zote za mafuta zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe 07 Machi 2012.

Katika toleo hili, bei ya rejareja kwa mafuta aina zote zimepanda kama ifuatavyo: Petroli imeongezeka kwa Sh 87/lita sawa na asilimia 4.06; Dizeli imeongezeka kwa Sh 3/lita sawa na asilimia 0.14; na Mafuta ya taa yameongezeka kwa Sh 12/lita sawa na asilimia 0.59.

Mabadiliko haya ya bei za mafuta hapa nchini yametokana na mabadiliko ya bei katika soko la dunia ambapo bei ya mafuta ya petroli imeongezeka kwa wastani wa dola za marekani 95.7 kwa tani sawa na asilimia 9.09, mafuta ya dizeli yameongezeka kwa wastani wa dola za marekani 27.1 kwa tani sawa na asilimia 2.76, na mafuta ya taa kwa dola za marekani 34.04 kwa tani sawa na asilimia 3.28. Bei za jumla kwa kulinganisha matoleo haya mawili zimebadilika kama ifuatavyo:

Petroli imeongezeka kwa Sh 87.18/lita sawa na asilimia 4.21; Dizeli imeongezeka kwa Sh 2.61/lita sawa na asilimia 0.13; na Mafuta ya taa yameongezeka kwa Sh 12.32/lita, sawa na asilimia 0.62.

(b) Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.

Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.

(c) Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na fomula mpya iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 454 la tarehe 23 Desemba 2011.

(d) Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika.

(e) Wanunuzi wanashauriwa kuhakikisha kuwa wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita. Stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo; ama endapo utakuwa umeuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.


Haruna Masebu
MKURUGENZI MTENDAJI
EWURA

No comments: