Saturday, July 16, 2011

TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE NISHATI NA MADINI


Bw, Januari Makamba, Mwenyekiti wa kamati yakudumu ya bunge nishati na madiniJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


BUNGE LA TANZANIA


TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2010/2011 PAMOJA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012Ofisi ya Bunge

S.L.P 941

DODOMA

15 Julai, 2011


TAARIFA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2010/2011 PAMOJA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012.


1.0 UTANGULIZI


Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 99 (7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Mwaka 2007, napenda kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuwasilisha maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011, pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012.


Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 30 Mei hadi 1 Juni, 2011, Kamati ilifanya vikao na Wizara ya Nishati na Madini katika Ofisi Ndogo ya Bunge Dar es Salaam kwa lengo la kupokea na kujadili utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. Aidha, pamoja na mambo mengine, Wizara ilielezea kuhusu Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kamati kwa Mwaka wa Fedha 2010/2011.


2.0 UTEKELEZAJI WA MAONI NA USHAURI WA KAMATI KWA MWAKA WA FEDHA 2010/2011

Mheshimiwa Spika, kwa kiasi fulani, Wizara imeyafanyia kazi mapendekezo hayo ya Kamati. Hata hivyo, utekelezaji wa baadhi ya maoni na ushauri wa Kamati bado unaendelea. Yapo mapendekezo ambayo bado hayatekelezwa kwasababu moja au nyingine. Kamati inahimiza Wizara iharakishe kutekeleza mapendekezo hayo.


3.0 MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2010/2011

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2010/2011, Wizara ilitengewa bajeti ya shilingi bilioni 281.7. Hadi kufikia mwisho wa Mwaka wa Fedha, yaani tarehe 30 Juni 2011, ni shilingi 226.9 zilizokuwa zimepokelewa. Maana yake ni kwamba, Wizara ya Nishati na Madini, pamoja na umuhimu wake kwa maendeleo na ustawi wa nchi, ilipokea asilimia 80.5 tu ya fedha ilizokuwa imetengewa mwaka jana.

Waziri alieleza kuwa, upatikanaji wa fedha hizo uliwezesha Wizara kutekeleza baadhi ya kazi ilizojipangia na kupata mafanikio ambayo Waziri ameyaelezea.

4.0 MAOMBI YA FEDHA KWA MATUMIZI YA WIZARA NA KAZI ZILIZOPANGWA KUTEKELEZWA KATIKA MWAKA WA 2011/2012

Mheshimiwa Spika, Wizara, kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012, inaomba jumla ya shilingi 402,402,071,100/=. Kati ya fedha hizo, shilingi 76,953,934,100/= kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo kati ya fedha hizo, shilingi 10,053,413,100/=kwa ajili ya mishahara ya Wizara na Mashirika yaliyo chini yake na shilingi 66,900,521,000/=kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC). Aidha, Miradi ya Maendeleo inaombewa jumla ya Shilingi 325,448,137,000/=, kati ya fedha hizo shilingi 236,311,391,000/= ni fedha za ndani na shilingi 89,136,746,000/= ni fedha za nje.

Mheshimiwa Spika, Kiasi kinachoombwa ni nyongeza ya asilimia 42 ya kiasi cha shilingi 281,741,179,253/= kilichotengwa katika Mwaka wa Fedha 2010/2011. Kamati inaipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuongeza Bajeti ya Wizara hii hususan katika Miradi ya Maendeleo ambayo bajeti yake imeongezeka kutoka shilingi 184,001,395,000/= Mwaka 2010/2011 hadi kufikia shilingi 325,448,137,000/= Mwaka 2011/2012 sawa na ongezeko la asilimia 78.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ongezeko hili, Kamati inaamini kwamba kiasi cha fedha kilichotengwa, hasa kwa miradi ya maendeleo ni kidogo mno na bado kingeweza kuongezwa zaidi kwa kuzingatia umuhimu na udharura wa shughuli za Wizara, hasa uzalishaji wa umeme.


7.0 MAONI NA USHAURI WA KAMATI

Mheshimiwa Spika, katika kupitia Bajeti ya Wizara, yapo mambo kadhaa ambayo Kamati iliyabaini na ambayo tungependa kuyatolea maoni na mapendekezo.


A. Suala la Uzalishaji Umeme Nchini

Bila kutumia maneno mengi, Kamati inapenda kutamka jambo lililo dhahiri kwa Watanzania wote kwamba hali ya uzalishaji umeme nchini ni mbaya. Tatizo hili sasa limedumu kwa muda mrefu na sasa limekuwa janga. Janga hili limeleta adha kwa wananchi, limeleta athari kubwa kwa uchumi, na fedheha kwa nchi na kwa Serikali.

Uzalishaji viwandani unazorota, gharama za uzalishaji bidhaa zinaongezeka na hivyo bei za bidhaa kupanda, wajasiriamali wadogo wanaathirika, mikopo kwenye mabenki inashindwa kurudishwa, huduma mahospitalini zinaathirika, Mapato ya Serikali yanashuka, na iko hatari kwamba Pato la Taifa na ukuaji wa uchumi utaathirika.

Mheshimiwa Spika, Kamati inatambua juhudi mbalimbali zilizofanywa na zinazofanywa na Serikali kukabiliana na tatizo hili. Hata hivyo, juhudi hizi, kwa miaka kadhaa sasa, hazijazaa matunda kwani tatizo limeendelea kuwepo.

Kamati inakubali kwamba upungufu wa mvua umeendelea kuathiri uzalishaji wa umeme kwasababu kwa kiwango kikubwa nchi yetu inategemea umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji yanayotokana na mvua. Hata hivyo, Kamati inaamini kwamba sababu hii ya upungufu wa mvua haiwezi kuendelea kuwa sababu ya kudumu kwasababu mbili:


i) Mwenendo wa mvua na majira ya mvua yanajulikana kwa miaka mingi sasa. Na, Serikali, katika kuhimiza kilimo cha kisasa, imekuwa inasema kwamba kilimo cha umwagiliaji ndio mkombozi kwasababu mvua hazitabiriki. Kwa msingi huo huo, kama mvua haziwezi kuaminika katika kuendeleza kilimo, basi pia haziwezi kuaminika katika kuzalisha umeme.


ii) Nchi yetu imejaliwa kuwa na vyanzo karibu vyote vya kuzalisha umeme: gesi, jua, upepo, makaa ya mawe, na joto-ardhi na vyanzo vingine mbadala. Ni nchi chache duniani zenye neema kama hii. Kwa msingi huo, badala ya kuendelea kutaja uhaba wa mvua kama sababu ya mgawo, juhudi ziongezwe kwenye kuwekeza katika kuzalisha umeme kwa vyanzo hivi.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaamini kwamba, katika karne ya sasa, na kwa kuzingatia uwepo wa vyanzo vingi vya kuzalisha umeme, Serikali isiendelee kutegemea majaaliwa ya mvua kumaliza tatizo la mgao wa umeme. Kamati inaishauri Serikali iongeze kasi ya uwekezaji katika vyanzo vingine vya umeme. Kamati imeshangazwa kwamba, katika miaka saba iliyopita, ni Megawati 145 tu za umeme wa kudumu ndizo zilizowekezwa wakati mahitaji ya umeme yanaongezeka kwa wastani wa Megawati 100 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la umeme, Kamati inapendekeza yafuatayo:

i) Serikali ilichukulie tatizo la umeme katika udharura kama ilivyolichukulia tatizo la mdororo wa uchumi duniani mwaka 2008, kiasi cha kuamua kutenga shilingi trilioni 1.7 kukabiliana nalo. Kamati inaamini kwa dhati kabisa kwamba, athari za tatizo la umeme kwa uchumi wa nchi zinalingana au hata zinazidi athari za mdororo wa uchumi duniani. Kwa kuwa Serikali kupitia Waziri wa Nishati imekwishatangaza tatizo la umeme kuwa ni janga la taifa, basi hatua zinazoendana na kauli hiyo zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kutenga fedha ambazo zitawezesha kupatikana kwa Megawati 500 na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa gesi. Aidha, Kamati inapendekeza Serikali itengeneze Mpango wa Dharura wakulinusuru Taifa na Janga la Umeme. Kamati inapendekeza Mpango huu ujumuishe uharakishaji wa miradi iliyopo kwenye Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano uliopitishwa hapa Bungeni katika mkutano huu.

ii) Katika Bajeti ya Wizara kwa mwaka huu, Serikali imetenga shilingi bilioni 111.3 kwa miradi miwili ya dharura ya kuzalisha umeme, ambayo hata hivyo ilikuwa ikamilike mwaka 2010: mradi wa mtambo wa gesi wa Megawati 100 Ubungo, na Mradi wa mtambo wa mafuta mazito (HFO) wa Megawati 60 Mwanza. Hata hivyo, Kamati imebaini na ina maoni yafutayo kuhusu miradi hiyo:

a) Kuhusu mradi wa Megawati 100 za umeme wa gesi Ubungo utakaokamilika Disemba 2011, Kamati imebaini kwamba utekelezaji kamili wa mradi huo unategemea kuongezwa kwa kiasi cha gesi inayosafirishwa kutoka Songosongo hadi Ubungo Dar es Salaam. Kamati imejulishwa kwamba mitambo ya kusafisha gesi na bomba la kusafirisha gesi imefikia ukomo wa juu, na hata mtambo wa Symbion uliopo sasa hauzalishi umeme kwa uwezo wake wa Megawati 112 kutokana na kutokuwepo kwa gesi ya kutosha Ubungo. Hata juhudi za sasa za kuongeza uwezo wa kusafisha gesi (re-rating) haziwezi kukidhi mahitaji haya mapya hadi upanuzi wa miundombinu ya gesi utakapokamilika miezi 18 baadaye. Kwa maana hiyo, Kamati inapendekeza Serikali iuhakikishie umma kwamba mtambo huu utapata gesi mara utakapofungwa mwezi Disemba na hautakuwa Tembo Mweupe (White Elephant). Kamati pia inapendekeza Serikali itoe maelezo kwamba ilikuwaje TANESCO inunue mtambo mkubwa na wa gharama kama huu bila kupanga kuwepo kwa gesi ya kuundesha ikizingatiwa kwamba mtambo huu umeagizwa zaidi ya miezi 18 iliyopita.

b) Kuhusu mradi wa Megawati 60 za umeme wa kuzalishwa na mafuta mazito (HFO) Mwanza, mradi ambao uliopaswa kukamilika mwaka jana, na ambao sasa utakamilika mwezi Juni 2012, licha ya taarifa ya Serikali hapa Bungeni mwezi Februari kwamba ungekamilika mwezi Januari 2012, Kamati haikupata maelezo ya kuridhisha juu ya upatikanaji wa mafuta mazito ya kutosha na utaratibu na gharama za kuyasafirisha hadi Mwanza ukizingatia umbali kutoka bandari ya Dar es Salaam, ukizingatia ugumu wa kusafirisha mafuta mazito kwa barabara, na ukizingatia historia ya mradi kama huu wa kuzalisha umeme kwa mafuta Mwanza wa Alstom Power Rentals mwaka 2006/2007 ambao haukuzalisha umeme hata Megawati moja licha ya Serikali kulipa dola za Kimarekani milioni 21. Pamoja na ushauri wa Kamati ambao haukuzingatiwa hapo awali, Kamati inaendelea kuishauri Serikali ijiridhishe na iuridhishe umma kuhusu upatikanaji wa mafuta katika eneo la uzalishaji (Mwanza). Aidha, Kamati inaishauri Serikali iangalie uwezekano wa Mtambo huo wa kutumia mafuta mazito uende sehemu ambayo upatikanaji wa mafuta hayo ni rahisi kama Dar es Salaam na badala yake mtambo wa kutumia dizeli ndiyo uende Mwanza.

iii) Katika bajeti hii, Wizara pia imetenga shilingi bilioni 12 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo za matumizi ya mtambo huo, fedha hizi zilizotengwa zitawezesha kununua mafuta si zaidi ya mwezi mmoja kutokana na matumizi ya mafuta kwa mwezi kuwa ni shilingi bilioni 15. Kamati inaamini kwamba fedha hizi ni kidogo, ukizingatia hoja ya Serikali kwamba kuendelea kutumika kwa mtambo huu ni sehemu ya mkakati wa dharura wa kumaliza tatizo hili. Kamati inapendekeza fedha hizi ziongezwe ili mtambo huu uzalishe umeme kwa uwezo wake wa juu wa MW 100 na kwa muda mrefu zaidi ya sasa.

iv) Aidha, Kamati inaipongeza Serikali kwa kufanya mgawanyo mpya wa fedha (reallocation) katika mwaka wa fedha uliopita na kuipa Wizara kiasi cha shilingi bilioni 28.5 kwa ajili ya kununua mafuta ya kuendesha mtambo huu. Hata hivyo, Kamati inapendekeza uwepo utaratibu mzuri na wa wazi wa manunuzi ya mafuta haya, na mchanganuo utolewe kuonyesha mapokeo ya fedha kutoka Hazina kwenda Wizarani, na kutoka Wizarani kwenda Mfilisi wa IPTL, na hatimaye kwa wauzaji wa mafuta, na hatimaye mchanganuo wa kiasi cha matumizi ya mafuta yenyewe kulingana na mauzo ya umeme kwa TANESCO. Kamati inaamini uwazi huu utasaidia kuondoa shaka kwamba fedha hizi nyingi za umma zinazotengwa kwa manunuzi ya mafuta zimekuwa hazitoi matokeo yanayotarajiwa kuhusiana na uzalishaji wa umeme kutoka kwenye mtambo huu.

v) Kwa kuwa Serikali iliahidi hapa Bungeni mwezi Februari mwaka huu kwamba, itakapofika mwezi huu wa Julai, zitakuwa zimepatikana Megawati 260 za umeme wa dharura, na kwa kuwa hadi sasa hakuna dalili za ahadi hiyo kutimia, Kamati inashauri, ili kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali juu ya uwezo wake wa kumaliza tatizo hili, basi Serikali itoe maelezo kuhusu sababu za kutotimia kwa ahadi hiyo na ni lini umeme huo utapatikana.

vi) Kamati imebaini kasi ndogo ya uwekezaji wa sekta binafsi katika miradi ya muda mrefu ya uzalishaji umeme. Zaidi ya miradi ya IPTL (1997) na Songas (2004), hakuna uwekezaji wowote wa sekta binafasi katika uzalishaji umeme uliofanyika nchini, zaidi ya miradi ya dharura ya muda mfupi. Kamati inaishauri Serikali kuangalia upya na kuboresha mazingira ya uwekezaji wa sekta binafsi katika uzalishaji umeme nchini.

vii) Sera ya Nishati inayotumika ni ya Mwaka 2003 na haijaongelea suala la matumizi ya Urani, na kwa kuwa nchi yetu imegundua kuwepo madini hayo muhimu, Kamati inashauri Serikali itengeneze mwongozo wa matumizi na udhibiti wa madini ya urani nchini ikiwemo matumizi katika uzalishaji wa nishati ya umeme

viii) Ili kukabiliana na kasi ndogo ya uwekezaji na uhaba wa fedha za kuwekeza katika sekta ya nishati, Kamati inapendekeza Serikali ianzishe mfuko wa kuendeleza nishati ya umeme nchini. Mfuko huo utatumika kama mtaji katika kuwekeza katika mitambo ya ufuaji umeme na miundombinu ya usafirishaji, usambazaji na uuzaji wa umeme. Kamati inapendekeza mfuko huo utunishwe kwa vyanzo vifuatavyo:

a) Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) itokanayo na mauzo ya umeme iwe inalipwa moja kwa moja kwenye mfuko badala ya kwenda Hazina.
b) Kodi ya kuagiza vipuri na mafuta ya kuendesha mitambo ya kufua umeme iwe inalipwa moja kwa moja kwenye mfuko huo badala ya kwenda Hazina.

c) Kuanzisha ushuru wa huduma ya nishati ya umeme (surcharge) kwa makampuni yanayotumia umeme mwingi.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi zitasaidia TANESCO kupata fedha za kutosha na hivyo kuweza kujiendesha tofauti na ilivyo sasa.

B. Suala la Gesi

Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini kwamba gesi asili, kama ikitumika vizuri kama inavyopaswa, inayo fursa ya kubadilisha kabisa sura ya uzalishaji wa umeme, maendeleo ya viwanda na uchumi wa nchi. Hata hivyo, Kamati imepata mashaka kwamba nchi hainufaiki ipasavyo kutokana na kuwepo kwa gesi nchini, kwa maana ya unafuu wa bei, uharaka wa upatikanaji wa gesi na kujenga uwezo kwa watanzania katika uwekezaji na utaalamu katika masuala ya gesi. Licha ya kwamba gesi ni maliasili muhimu kwa uchumi na usalama wa nchi, Kamati imebaini kwamba biashara na utaratibu mzima wa uchimbaji, usafishaji, usambazaji na uuzaji nchini vimegubikwa na utata mkubwa wa kimkataba usio na maslahi kwa taifa pamoja na ukiritimba. Kamati haijaridhishwa na ushiriki, ufanisi na uadilifu wa Kampuni ya Pan African Energy Tanzania katika mchakato wa uendelezaji gesi nchini. Hivyo basi, Kufuatia utata huu uliopo, Kamati ya Nishati na Madini inaunda Kamati yake ndogo ili kufuatilia utata huu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Kamati pia inashauri:-

i) Serikali, kupitia TPDC, sasa ichukue uongozi madhubuti katika suala zima la gesi na sio tu kukaa pembeni na kusubiri tu mapato.

ii) Serikali ichukue hatua za haraka za kuondoa ukiritimba uliopo katika biashara ya usafirishaji na usambazaji wa gesi nchini kwa kushinikiza makampuni ya Songas na Pan-African Energy yaruhusu wachimbaji na watumiaji wengine wa gesi watumie miundombinu ya kusafisha na kusafirisha gesi. Aidha, fedha zote zitokanazo na mapato ya uzalishaji wa Petroli (Production Sharing Agreement) ambazo Pan African Energy wameipunja TPDC zikabidhiwe kwa TPDC.

iii) Ili kuvutia wawekezaji, Serikali ihakikishe inaondoa vikwazo vya urasimu visivyo vya lazima hususan katika upatikanaji wa leseni.

iv) Kwa kuwa Taifa sasa linaelekea kutegemea umeme utokanao na gesi kwa kiasi kikubwa, Kamati inapendekeza Serikali ihakikishe inaweka ulinzi wa kutosha katika maeneo yanayochimbwa gesi ili kuweza kukabiliana na maharamia.

v) Kutokana na unyeti wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na kutoka Songosongo hadi Somanga Fungu Serikali ichukue jitihada za makusudi za kuhakikisha bomba hili linajengwa na kumilikiwa na Serikali yenyewe au Shirika ambalo linamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Kamati inatoa angalizo kuwa bila ya ujenzi wa Bomba hili miradi iliyopangwa kutekelezwa yenye zaidi ya MW 570 haitawezekana.

i) Kwa kuwa Rasimu ya Sheria ya Gesi imeshaandaliwa na kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali tangu mwaka 2009, ni vyema basi mchakato wake uharakishwe ili iweze kujadiliwa na bunge na hatimaye kuwa sheria rasmi.

C. Umeme Vijijini: WAKALA WA NISHATI VIJIJINI (REA)

Mheshimiwa Spika, Kamati inaamini kwamba sio sahihi na wala sio haki kwa Watanzania wachache wa maeneo ya mijini kunufaika na umeme, wakati asilimia 86 za kaya zote hapa nchini hazina umeme. Kamati inapendekeza kwamba mipango ya usambazaji umeme vijijini iharakishwe ili nchi yetu ipate maendeleo ya uwiano sawa katika maeneo yote.

Serikali ilianzisha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kuhamasisha, kuwezesha na kuratibu uendelezaji wa miradi ya nishati bora vijijini. Pamoja na nia nzuri ya REA ya kuhakikisha inaendeleza miradi ya nishati bora vijijini, bado imekuwa ikipata changamoto hasa za kutotengewa fedha za kutosha na pia kutopata fedha zote na kwa wakati. Kwa mfano katika Mwaka wa Fedha 2010/2011 jumla ya shilingi bilioni 58.9 zilipitishwa lakini hadi kufikia Mei, 2011 ni shilingi bilioni 13.6 tu sawa na asilimia 23 tu ndiyo zilikuwa zimetolewa. Hali hii haiendani na dhamira ya Serikali ya kupeleka umeme kwa kasi vijijini.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Mwaka huu, kiasi kilichotengwa kwa ajili ya REA ni shilingi bilioni 56.7. Kiasi hiki ni kidogo kuliko kilichotengwa mwaka jana na ni kidogo pia ukilinganisha na mahitaji. Kamati inapongeza jitihada zinazofanywa na Serikali kutunisha Mfuko wa REA, na inapendekeza fedha hizi, tofauti na mwaka jana, zitolewe zote na kwa wakati. Kamati pia inapendekeza maamuzi ya maeneo ya kupeleka umeme yasizingatie nguvu au ushawishi wa viongozi na watendaji waandamizi wa Serikali wa maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mipango ya kusambaza umeme nchini, bado gharama za kuunganisha umeme majumbani kwa wananchi wengi wa vijijini ni kubwa mno. Kamati inaishauri Serikali iangalie upya utaratibu wa manunuzi ya vifaa (kwa maana ya nguzo, nyaya, vipoza umeme na meter) vya kusambaza umeme ili kupata vifaa hivyo kwa gharama nafuu. Kwa kuwa mpango wa usambazaji umeme vijijini ni mkubwa na wa muda mrefu, Kamati inaamini kabisa kwamba Serikali inaweza kuingia mkataba wa kutengenezewa na kununua kwa mkupuo vifaa vya usambazaji wa umeme na hivyo kupunguza gharama za vifaa hivyo.

Vilevile, Kamati inashauri Serikali iangalie uwezekano wa kubadilisha utaratibu ambapo sasa wananchi watalipa asilimia 25 ya gharama za kufungiwa umeme na kumalizia asilimia 75 kidogo kidogo wakati wakiwa na umeme ndani ya nyumba.

D. SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI (TPDC)

Mheshimiwa Spika, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) linajihusisha na kazi za msingi za utafiti, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili nchini. Pia Shirika hili linalo jukumu la kusimamia shughuli za utafutaji na uchimbaji unaofanywa na makampuni ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa shughuli za utafutaji mafuta na gesi zimepiga kasi kubwa katika miaka ya karibuni, na kwa kuwa dalili zote zinaonyesha kwamba nchi yetu inayo gesi nyingi baharini. Kamati inapendekeza kwa Serikali kuchukua hatua madhubuti na za haraka za kuliimarisha Shirika hili. Kwa hali ya sasa, kuwa upande wa fedha, kwa maana ya mtaji, na rasilimali watu, Shirika hili haliko katika hali nzuri.

Kwa mantiki hiyo basi Kamati inashauri:

i) Serikali itekeleze dhamira yake ya kuidhamini TPDC ili iweze kupata mikopo itakayowezesha utekelezaji wa miradi yake, hasa mradi wa kusambaza gesi majumbani, kwenye magari na viwandani ambao utaleta ahueni kwa Watanzania kiuchumi na kimazingira. Katika mahitaji ya fedha za kutekeleza miradi kiasi cha shilingi bilioni 164, TPDC wameruhusiwa kutumia shilingi bilioni 8 tu zinazotokana na asilimia 50 ya mapato yake. Kamati inapendekeza TPDC waruhusiwe kuchukua mapato yake yote kwa asilimia 100 ili kutekeza miradi yake muhimu.

ii) Serikali itoe kibali ili TPDC waweze kuajiri watumishi wengine kutokana na watumishi wengi kuanza kustaafu.

iii) Kutokana na fursa tuliyonayo ya kuwa na gesi, Serikali ichukue hatua za makusudi za kusomesha vijana kila mwaka wakachukue elimu ya juu katika nchi na vyuo duniani vilivyobobea kwenye masuala ya utafutaji na uchimbaji gesi na mafuta pamoja na ukaguzi wa rasilimali hizi.

iv) TPDC wahusishwe kikamilifu katika shughuli zote za uagizaji, uhifadhi na usambazaji wa mafuta jamii ya Petroli na ili kupata ufanisi na manufaa wakati umefika sasa TPDC isimamie uanzishwa ji wa kampuni ya Taifa ya Mafuta (National oil Company)

E. MAFUTA

i) Bei ya Mafuta

Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua katika kupunguza bei ya mafuta. Hata hivyo, hadi sasa bei ya mafuta bado haijashuka kwa kiwango kilichotarajiwa, na bei ya mafuta ya taa imepanda kwa kiwango ambacho hakikutarajiwa. Kamati imebaini hadi sasa maelekezo ya Serikali ya kuondoa tozo mbalimbali za mafuta hayajatekelezwa. Kamati inaishauri Serikali itoe maelezo ya kina na fasaha kuhusu sababu za bei kuendelea kubaki juu na jitihada zinazofanyika kudhibiti bei.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na hali hii, Kamati inapendekeza yafuatayo:

a) EWURA ipewe uwezo na mamlaka zaidi ya kudhibiti bei ya mafuta, na hatua kali zichukuliwe kwa wale wataokuwa wanauza mafuta kwa bei ya juu ya bei elekezi.

b) Destination Inspection ambayo ni asilimia 1.2 ya gharama halisi ya manunuzi ya mafuta (FOB) iondolewe. Aidha, gharama ya kudhibiti ubora kwa kutumia vinasaba ya dola 3.9 kwa kila lita 1000 na yenyewe ipunguzwe.

c) Serikali inashauriwa kuwa makini katika kudhibiti usambazaji wa mafuta ya ndege na yale yanayosafirishwa kwenda nchi jirani (Transit Cargo) ili yasije yakaingia sokoni na kuharibu dhamira nzuri ya Serikali. Aidha, mafuta yote ya ndege yalipiwe ushuru yanapotoka kwenye hifadhi na kampuni husika zidai kurudushiwa fedha zake baadae ili kuweza kudhibiti mafuta haya kutumika tofauti na ilivyolengwa.

ii) Miundombinu ya Kuingiza na Kushusha Mafuta

Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini athari kubwa za kasi ndogo ya ushushaji wa mafuta bandarini kutokana na ufinyu wa miundombinu. Ili kuongeza ufanisi wa ushushaji wa mafuta kwa mahitaji ya sasa na baadaye kupitia bandari ya Dar es Salaam, Kamati imeona kuna haja kubwa ya kujenga Boya kubwa la kupakuwa mafuta baharini (SPM) na kujenga KOJ mpya, ambapo:-

a) Kwa hali ya uharaka, mipango ya TPA ya ujenzi wa SPM iwekwe wazi kwa wadau wote. Aidha, Kamati inapendekeza mipango ya ujenzi wa SPM izingatie usalama katika upokeaji wa mafuta, mahitaji ya baadae, ubora kulingana na thamani ya fedha (value for money) kwa mlaji.

b) Kama uwezo mdogo wa fedha wa TPA ni kikwazo katika utekelezaji wa haraka wa mradi wa SPM, Serikali ialike wawekezaji wengine mara moja chini ya mpango wa Build Operate Transfer (BOT) na Public Private Partnership (PPP).

c) Makampuni ya mafuta pamoja na TPA chini ya uongozi wa EWURA waanze mipango ya urekebishaji wa mfumo wa mabomba (Expansion of Pipelines) ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia ucheleweshaji wa ushushaji wa mafuta.

d) Ili kuleta ufanisi katika upakuaji wa mafuta na kumpunguzia gharama mlaji, flow meter zenye uwezo wa kupakua mafuta mengi kwa wakati mmoja na kutoa takwimu sahihi zitafutwe na zitumike. Kamati inayo barua ya tarehe 2 Februari, 2011 kutoka kwa Wakala wa Mizani na Vipimo akipiga marufuku, kwa mujibu wa Sheria, matumuzi ya flow meter kutokana na kuchakachuliwa. Lakini, hadi leo flow meter hiyo inatumika na hivyo kutia shaka juu ya usahihi wa takwimu na hivyo kuathiri ukusanyaji wa mapato.

e) Serikali kwa kushirikisha wadau husika, isimamie uboreshaji na hatimaye ufanisi ya hifadhi ya mafuta ya TIPER.
iii) Ubora wa Mafuta

Mheshimiwa Spika, uchakachuaji ni tatizo kubwa sana hapa nchini. Serikali inapoteza kodi kati ya shilingi bilioni 25 hadi 33 kwa mwezi kutokana na tatizo hili. Kamati inaipongeza Serikali kwa kuweka uwiano wa ushuru wa dizeli na petroli ili iendane na mafuta taa, Kamati inaamini kwa kuwepo uwiano wa bei hizo kutapunguza uchakachuaji wa mafuta. Pamoja na hayo Kamati inaendelea kushauri yafuatayo:-

a) EWURA iongeze jitihada kwa kutafuta njia zinazoweza kuzuia tatizo hili. EWURA itumie teknolojia tofauti ya kudhibilti ubora na kodi kwani teknolojia ya kuweka vinasaba inayotumika sasa imebainika kushindwa kudhibiti tatizo hili kwa kiwango kinachotakiwa.

b) Kutokana na gharama kubwa za kupima sampuli za mafuta nje ya nchi , na kwa kuzingatia kwamba zipo maabara ndani ya nchi zinazoweza kufanya kazi hiyo, kwa mfano maabara ya TBS, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Serikali izijengee uwezo maabara hizi ili ziweze kutoa huduma hii kwa gharama nafuu.

c) Kwa kuwa EWURA na TBS wanafanya shughuli inayofanana ya kupima ubora wa mafuta na wote wanatoza kwa huduma hiyo hiyo, Serikali ifanye uamuzi wa kuiachia taasisi moja ifanye shughuli ya kudhibiti ubora wa mafuta.

d) Adhabu kali zitolewe kwa wale wanajihusisha na uchakachuaji wa mafuta ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni, kutozwa faini kubwa kwa mfano shilingi bilioni 2 kwenye hifadhi (Depot), shilingi milioni 500 kwenye kituo cha mafuta na shilingi milioni 100 kwenye magari na pia iwepo adhabu ya kifungo.

iv) Bulk Procurement System

Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Serikali kwa kufikiria kuanzisha Mfumo wa ununuaji mafuta kwa wingi (Bulk Procurement). Kamati inatambua faida za mfumo huu hasa katika kudhibiti bei ya mafuta. Hata hivyo, Kamati imebaini kuwa utayarishaji wa kanuni zitakazoongoza utaratibu huu haukushirikisha wadau wote. Hali hiyo imeleta mashaka kwa baadhi ya wadau ambao wanatarajiwa watoe ushirikiano. Kutokana na hali hiyo, Kamati inashauri:-

a) Wadau wote wakuu katika ununuzi wa mafuta kwa wingi (TPA, TIPER, EWURA, TPDC na Makampuni ya Mafuta) wakae pamoja na Serikali kwa uhuru na kuondoa mashaka miongoni mwao. Kamati imegundua kutokuwepo mawasiliano ya msingi katika jambo ambalo wanalolenga kulitekeleza kwa pamoja.

b) Utekelezaji wa utaratibu wa Bulk Procurement uende sambamba na matumizi ya miundombinu itakayoleta manufaa yanayokusudiwa kama matumizi ya SPM (upakuaji wa tani 3000 kwa saa) na KOJ iliyoboreshwa (upakuaji wa tani 1200 kwa saa)

c) Kwakuwa mpaka sasa hamna mfumo ulio rasmi na madhubuti kwa ajili ya kupokea mafuta, na kwa kuwa utekelezaji wa mfumo huu utaanza karibuni kama Waziri alivyoeleza, ni vyema basi mabomba na matenki ya TIPER yakarabatiwe ili kuweza kupokea mafuta hayo.

d) Utaratibu wa ununuzi kwa wingi ufanyike kwa mfumo ambao utakuwa wazi, utaondoa mianya ya rushwa na upendeleo, hautaiweka biashara ya kuagiza mafuta kwenye ukiritimba na hautawaingiza watu wa kati (Middle men) na kuongeza gharama kwa mlaji.

e) Wakati Serikali inapanga kutekeleza mfumo huu wa Bulk procurement, ni vyema iwaeleza Watanzania namna itakavyoweza kuweka usalama kutokana na vitendo vya uharamia vinavyoendelea ili nchi isije kukosa mafuta kabisa endapo meli itatekwa.

F. SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA (STAMICO)

Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Serikali kwa kuamua kulibakisha Shirika la Madini la Taifa STAMICO katika mikono yake ili liweze kusimamia uwekezaji wa Serikali katika sekta ya Madini. Hata hivyo, mafanikio ya Shirika hili yatategemea Shirika hili kuwezeshwa hasa ikizingatiwa lilisimama kwa takribani miaka13. Kwa mantiki hiyo, Kamati inatoa ushauri ufuatao: -
i) STAMICO ikabidhiwe fedha zilizopatikana kutokana na kuuzwa kwa nyumba zake nne na mali zake nyingine ili zitumike katika kutekeleza kazi zake za maendeleo.

ii) Uwekezaji au hisa katika sekta ya madini kunahitaji fedha nyingi. Fedha zaidi zitengwe kwa STAMICO ili kuhakikisha Shirika linawekeza na kusimamia vyema sekta ya madini kwa manufaa ya taifa.

iii) Serikali ihakikishe kuwa mgodi wa Buhemba iliyoikabidhi STAMICO unasimamiwa kwa umakini ili kuondoa hujuma na malalamiko yaliyopo kutoka kwa wananchi.

G. WAKALA WA UKAGUZI WA MADINI TANZANIA (TMAA)

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania ulianzishwa kwa lengo la kuhakikisha kiasi na ubora wa madini yanayozalishwa na kuuzwa nje ya nchi; kukagua gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi mikubwa na ya kati kwa lengo la kukusanya taarifa sahihi za kodi na kuziwasilisha TRA na vyombo vingine vya Serikali; Kufuatilia na kukagua shughuli za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya migodi, bajeti iliyotengwa na matumizi ya fedha kwa ajili ya ukarabati endelevu wa mazingira; kufuatilia na kuzuia utoroshaji wa madini na ukwepaji wa kulipa mrabaha; na kutathmini thamani ya madini yaliyozalishwa ili kupata mrabaha stahiki.

Mheshimiwa Spika, Kamati imeridhishwa na utendaji kazi wa Wakala kwani wakala umesaidia nchi kwa kiasi fulani kunufaika na madini kutokana na makampuni yenye migodi kuanza kulipa mrabaha stahiki pamoja na kodi nyinginezo. Kamati inatambua mchango na kazi hii nzuri ya TMAA na inashauri yafuatayo:-

i) Serikali itenge fedha ili kuwezesha Wakala kujenga ofisi yake tofauti na ilivyo sasa inatumia fedha nyingi kulipa kodi ya pango.

ii) Serikali iiwezeshe Wakala huu ili iwe Mamlaka badala ya Wakala kwani itasaidia kuipa nguvu ya udhibiti, ufanisi na utendaji kazi wake.

iii) Kutokana na fursa ya madini tuliyonayo, Serikali ichukue vijana kila mwaka na kuwadhamini kwa mafunzo ya elimu ya juu ya uchumi wa madini na ukaguzi na udhibiti wa mapato ya madini.

H. TASNIA YA UZIDUAJI (EITI)

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 18 Novemba, 2008, Serikali ya Tanzania ilitoa tamko juu ya nia yake ya kujiunga na Asasi ya EITI kwa dhamira ya kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, gesi asili na mafuta na ilipatiwa usajili wa awali tarehe 14 Februari, 2009. Tangu ilipoanzishwa TEITI imetoa taarifa yake ya kwanza juu ya kodi zilizolipwa Serikalini na makampuni makubwa ya uchimbaji wa madini na gesi asilia katika kipindi cha Julai, 2008 hadi Juni, 2009. Taarifa hiyo inaonyesha makampuni yamelipa jumla ya shilingi bilioni 174.9 wakati Serikali imeonesha kupokea jumla ya shilingi bilioni 128.4 hivyo kufanya tofauti ya malipo na mapato kuwa ni shilingi bilioni 46.5 kwa Mwaka wa Fedha 2008/2009.

Mheshimiwa Spika, Kamati inapongeza juhudi zilizofanywa za kuanzishwa kwa chombo hiki ambacho kinahusisha wadau kutoka makundi ya vyama vya kijamii, Serikali na Kampuni za madini. Aidha, Kamati inashauri yafuatayo:-

i) Serikali kukitumia chombo hiki ipasavyo ili kuleta uhuru na uwazi katika mapato ya rasilimali za madini.

ii) Serikali sasa ilete Muswada wa Sheria Bungeni ili chombo hiki muhimu kiwepo rasmi kisheria.

iii) Tofauti iliyojitokeza ya shilingi bilioni 46.5 za malipo yaliyofanywa na makampuni ya madini kwa Serikali zitolewe ufafanuzi ili kuleta dhana ya uwazi na uwajibikaji.

I. WACHIMBAJI WADOGO WADOGO

Mheshimiwa Spika, wachimbaji wengi wadogo wadogo ni wazawa wa nchi na wengi wao wanakaa na kufanya kazi karibu na maeneo ya migodi ya wachimbaji wakubwa. Wachimbaji hawa wamekuwa wakitegema kazi hii kama njia ya kujikimu kimaisha na wamekuwepo katika maeneo hayo hata kabla wachimbaji wakubwa hawajafika. Hata hivyo, yamekuwepo malalamiko mengi kutoka miongoni mwao kuwa wamekuwa wakikosa haki ya kutumia rasilimali zao wakati wageni wakinufaika. Malalamiko ya namna hiyo yamesababisha kudhoofisha mahusiano kati ya pande hizo mbili na hivyo kuhatarisha hali ya usalama na amani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri kwamba jitihada kubwa zaidi zifanyike kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo waweze kuendesha shughuli zao kwa tija, katika mazingira ya usalama zaidi na waweze kunufaika na jasho lao.

Katika bajeti ya mwaka huu, Mfuko wa Wachimbaji Wadogo umetengewa shilingi 1,189,630,000/= kwa ajili ya kuwasaidia. Kamati haijaridhishwa na fedha hizi kwani ni ndogo mno ikilinganishwa na mahitaji makubwa ya Wachimbaji, hivyo Kamati inashauri yafuatayo:-

i) Kwa kuwa shughuli za uchimbaji wa madini zinahusisha kuwaondoa wakazi wa maeneo husika ili kupisha shughuli za uchimbaji, Kamati inashauri kuwa wakazi hao wapewe fidia stahiki kabla shughuli za uchimbaji madini hazijaanza. Aidha, kwa nia ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo wanaokutwa katika maeneo hayo, Serikali iweke utaratibu utakaowezesha wachimbaji hao kunufaika.

ii) Wachimbaji wadogo wadogo watengewe fedha za kutosha ambazo zitawawezesha kununua vifaa ambavyo ndiyo nyenzo muhimu katika biashara yao .

iii) Kwa kuwa Wizara ilieleza ina mpango wa kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo kwa kuwaunganisha kwenye vikundi, ni vyema wachimbaji hawa wakahamasishwa na kushawishiwa na wakaungana katika vikundi ili kurahisisha azma ya Serikali ya kuwasaidia.

v) Ili kuleta mahusiano mazuri kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo wadogo, Kamati inashauri wachimbaji wakubwa wachangie katika mfuko wa wachimbaji wadogo wadogo.

v) Serikali iweke program maalum ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo wa Nyamongo na maeneo mengine ili waweze kunufaika na teknolojia na miundombinu ya uwekezaji mkubwa katika Mgodi wa North Mara na maeneo yanayofanana na hayo.

vi) Kutokana na uchimbaji wa madini ya Tanzanite kuwa unatofautiana na uchimbaji wa madini mengine, kwa maana ya jiolojia ya kipekee ya madini ya Tanzanite, Serikali ihakikishe inatunga kanuni mahsusi kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya hayo yatakayowahusisha wachimbaji wote.

vii) Baada ya sheria ya madini kupitishwa ambayo inayomilikisha madini kwa asilimia 100 kwa wazawa na kufuatia maelekezo ya Waziri ya kuzuia usafirishaji wa madini ghafi nje ili kuleta thamani ya madini, ipo haja ya Serikali kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo kwa kuanzisha vituo vya kuongeza thamani ya madini kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

viii) Serikali ihakikishe inadhibiti ajira ya watoto katika migodi ambao hujulikana kama nyoka.

Mheshimiwa Spika, tangu kuundwa kwa Kamati hii, muda mwingi imeutumia katika kushughulikia masuala ya Nishati kwa maana ya Umeme na Mafuta. Hatahivyo, Kamati imejipanga kwa siku zijazo kujikita zaidi katika Sekta ya Madini ili kuweza kuifahamu vizuri. Pamoja na hayo, Kamati inatoa maoni yafuatayo:-

i) Kutokana na Makampuni yenye mikataba ya madini ambayo yamekuwa yakinufaika msamaha wa kodi ya mafuta kutumia vibaya fursa hiyo na kuiibia Serikali kodi yake, Kamati inashauri Serikali ifuatilie suala hili ili kuhakikisha fursa hiyo inatumiwa vizuri.

ii) Kwa kuwa Watanzania wengi hawashiriki katika kutoa huduma za ugavi kwenye migodi, na kwa kuwa huduma hii inafaida sana hasa katika kukua kwa pato la taifa, Kamati inashauri Serikali isaidie ili watanzania wengi zaidi waweze kujikita katika huduma na kunufaika na hatimaye kuinua pato la taifa.

J. CHUO CHA MADINI – DODOMA

Mheshimiwa Spika Chuo cha Madini Dodoma ni muhimu sana katika kuendeleza taaluma ya masuala ya madini nchini hivyo kinahitaji kuangaliwa kwa maana ya kuwezeshwa ili kiweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Chuo hiki kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa Jengo la Utawala, ukumbi wa Mikutano, ufinyu wa bajeti, ukosefu wa vitendea kazi vya kutosha na miundombinu isiyoridhisha.

Mheshimiwa Spika, Kamati inatambua mchango mkubwa unaotolewa na chuo hiki na ina amini kuwa endapo kitaboreshwa basi kitasaidia ukuaji wa Sekta ya Madini na Nishati. Kutokana na umuhimu huo, Kamati inashauri yafuatayo:-

i) Fedha za kutosha zitengwe ili miundombinu muhimu iweze kujengwa.

ii) Badala ya Chuo hiki kuwa kitengo cha mafunzo cha Wizara, basi kijitegemee na kuwa kama kilivyo chuo cha DIT (Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam) au Chuo cha Maji cha Rwegalulira.

iii) Wanafunzi wanaomaliza katika Chuo cha Madini wathaminiwe na makampuni ya madini na kuwezeshwa kufanya mazoezi ya vitendo kwenye migodi na kupewa kazi ambazo uwezo wao na elimu yao inastahili.

iv) Kwa kuwa mitaala ya mafuta na gesi inaanzishwa katika chuo hiko, na kwa kuwa sasa nchi yetu inapiga kasi katika utafutaji wa gesi na mafuta, Kamati inashauri mtazamo wa sasa uwe ni kukiwezesha Chuo hiki kuwa Chuo cha Nishati na Madini badala ya kuwa Chuo cha Madini peke yake kama ilivyo sasa.

8.0 MAMBO MENGINE YALIYOJITOKEZA

Mheshimiwa Spika, yapo mambo kadhaa kuhusiana na mgawanyo wa fedha za Bajeti ya Wizara ambayo Kamati inaona ni muhimu kuyazungumzia.

A. Mradi wa Uendelezaji wa Gesi ya SongoSongo na Mnazi Bay.

Mradi huu umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 8,373,000,000. Hata hivyo, kati ya fedha hizi, shilingi bilioni 1,820,000,000 ni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi SongoSongo, na shilingi 5,173,000,000 ni kwa ajili ya ruzuku kwa kampuni binafsi ya Wentworth Resources ya kuuza umeme Mtwara na Lindi ili iuze umeme sawa na bei ya TANESCO.

Kamati inaamini kabisa kwamba miradi hii miwili haihusiani kabisa na Uendelezaji wa Gesi ya SongoSongo na Mnazi Bay . Pia, Kamati inaamini kwamba sio kazi ya Wizara ya Nishati na Madini kujenga kituo cha Polisi. Kamati inapendekeza fedha hizi zipelekwe TPDC ili kuwaongezea uwezo wa kutekeleza miradi yao ya kusambaza gesi katika Jiji la Dar es Salaam; na Serikali, kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania, ipeleke ulinzi katika eneo la SongoSongo ukizingatia tishio la maharamia kuvamia eneo hili. Aidha, kutokana na umuhimu wa kuwa na kituo cha Polisi katika eneo la kijiji cha Songosongo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ianze mchakato wa kujenga kituo hicho.

B. UJENZI WA JENGO LA OFISI YA KANDA YA MASHARIKI

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti ya Wizara, zimetengwa shilingi 3,889,000,000 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Kanda ya Mashariki. Kamati imebaini kwamba gharama za mradi mzima hazijajulikana, na inashauri kwamba, si vyema kwa Serikali kuanza mradi wa ujenzi bila kujua gharama halisi za ujenzi wenyewe na uwezo wa Serikali kwa siku zijazo kumalizia mradi huo.

9.0 HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napenda kuchukua nafasi hii kutambua mchango wa Wajumbe wa Kamati kwani wamekuwa makini katika kuchambua Bajeti hii na walifanya kazi hadi usiku kwa moyo wote na hatimaye kukamilisha taarifa hii. Napenda kuwatambua kwa majina kama ifuatavyo:-


1. Mhe. Januari Y. Makamba (Mb) Mwenyekiti

2. Mhe.Diana M. Chilolo (Mb) M/ Mwenyekiti.

3. Mhe. Yussuf Haji Khamis (Mb) Mjumbe

4. Mhe. Mariam Nassoro Kisangi, (Mb) Mjumbe

5. Mhe. Catherine Valentine Magige (Mb) Mjumbe

6. Mhe.Amos Gabriel Makalla (Mb) Mjumbe

7. Mhe.Khalfan Hilaly Aesh (Mb) Mjumbe

8. Mhe. Abia Muhama Nyabakari (Mb) Mjumbe

9. Mhe. Charles Poul Mwijage (Mb) Mjumbe

10. Mhe. Yusuph Abdallah Nassir (Mb) Mjumbe

11. Mhe. Christopher Olonyokie. Ole Sendeka (Mb) Mjumbe

12. Mhe. Mussa Khamis Silima (Mb) Mjumbe

13. Mhe. Dr. Festus Bulugu Limbu (Mb) Mjumbe

14. Mhe. Shafin Amedal Sumar (Mb) Mjumbe

15. Mhe. Selemani Jumanne Zedi (Mb) Mjumbe

16. Mhe. Lucy Thomas Mayenga (Mb) Mjumbe

17. Mhe. Josephine Tabitha Chagulla (Mb) Mjumbe

18. Mhe. Mwanamrisho Taratibu Abama (Mb) Mjumbe

19. Mhe. David Ernest Silinde (Mb) Mjumbe

20. Mhe. Suleiman Nchambis Suleiman (Mb) Mjumbe

21. Mhe. Kisyeri Werema Chambiri (Mb) Mjumbe

22. Mhe. Ali Mbarouk Salim (Mb) Mjumbe

23. Mhe. Sarah Ali Msafiri (Mb) Mjumbe

24. Mhe. Munde Abdallah Tambwe (Mb) Mjumbe

25. Mhe. Vicky Kamata (Mb) Mjumbe

26. Mhe. John Mnyika (Mb) MjumbeMheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kuliongoza Bunge letu vizuri.

Mheshimiwa Spika, Napenda kumshukuru Waziri wa Nishati na Madini Mhe. William M. Ngeleja (Mb), Naibu Waziri Mhe. Adam K. Malima, (Mb) kwa kuwasilisha hoja vyema mbele ya Kamati na ushirikiano ambao wamekuwa wakiipa Kamati. Napenda pia kumshukuru Katibu Mkuu Ndg. David Jairo pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri waliyofanya ya kushiriki kikamilifu katika vikao vya uchambuzi wa bajeti na kutoa ufafanuzi pale ilipohitajika.

Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kuishukuru Ofisi ya Bunge hasa Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah na Katibu wa Kamati hii Ndugu Pamela Pallangyo kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuratibu shughuli zote za Kamati. Pia nawashukuru wafanyakazi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kuihudumia Kamati katika hatua zote za Maandalizi ya taarifa hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naliomba Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, Fungu 58 kwa Mwaka wa Fedha wa 2011/2012, jumla ya shilingi 402, 402, 071,100/=

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha, na naunga mkono hoja hii.

January Y. Makamba , Mb

MWENYEKITI

KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI

1 5 Julai, 2011

No comments: