Wednesday, April 3, 2013

BARUA KWA MWALIMU..

WARAKA WA WAZI KWA MWALIMU JK NYERERE
UMEANDIKWA NA RASHIDI MTGALUKA....(kwenye facebook)
Kama kuna mtu humu kundini ana anuani ya Mwl Nyerere naomba amtumie barua hii:
Dear Mwl Julius K Nyerere, Shikamoo; salaam nyingi sana ama baada ya salaam mimi ni mzima, hofu na mashaka juu yako.
Madhumuni ya barua hii BABA yetu wa Taifa ni kutaka kukufahamisha kuwa, tangu uondoke Oktoba 14, 1999, hali hapa Tanzania imebadilika.Siku hizi mlima Kilimanjaro uko Kenya ziwa Nyasa liko Malawi,Tanzanite iko Afrika kusini, TANESCO ni ya Mafisadi.
Ni kwamba vitu hivi haviwasaidii kabisa Watanzania wanyonge uliotuacha, ndio maana nakwambia kwasasa ni kama vile maliasili hizo hazipo hapa nchini!
Pia Mheshimiwa Rais wetu siku hizi anaishi Airport na zaidi amegeuka Vasco da Gama, hatulii nyumbani!
Mwl huku historia imebadilika, kwamba eti Tanzania imetokana na Muungano wa visiwa vya Pemba, Unguja na Zimbabwe, ajabu Mwalimu ni kwamba aliyebadili historia hiyo ni Naibu Waziri aliyefeli mtihani wa kidato cha sita na kupata Digree yake kwa miaka 6 badala ya mi 3 ya kawaida.
Mwalimu hali huku si shwari tena, mwanafunzi anaanza kidato cha kwanza sekondari akiwa hajui kusoma wala kuandika! Haijulikani amefauluje!!
Mwalimu huku siku hizi rushwa imebadilika na kuitwa takrima! Tena siku hizi rushwa sio tena ADUI wa haki, bali ni RAFIKI wa haki.
Ukiweza kutoa rushwa siku hizi, basi unaweza hata ukampiga mtu risasi akafa na wewe ukapewa dhamana!
Mwalimu nisije nikasahau, kale kachama kako ulikokaasisi ambako kabla hujasafiri, uliwahi kutuambia wanao kwamba Si mama yako, sasa hivi sio tena ka wakulima na wafanyakazi! Ni kachama ka wenye fedha na wafanyabiashara.
Kachama kanaonekana kupoteza mvuto wake ule wa asili kutokana na viongozi uliowaachia kijiti kulegeza miiko ya uongozi na hatimaye kusahau hata zile ahadi za mwana TANU.
Mwalimu mpendwa, kibaya zaidi hata wale uliowahi kuwanyooshea kidole na kuwaambia hawafai kuongoza Taifa kutokana na kutofahamika walikopata utajiri mkubwa, leo hii ndio vinara wa kupiga jalamba kuomba ridhaa ya kwenda Magogoni.
Mwalimu hali ni mbaya sana kwa kweli, wale mabepari, makabaila na wakoloni wote kwa ujumla wake uliowatangazia vita kipindi kile, siku hizi wanaitwa WAWEKEZAJI!
Mzee Nyerere, siku hizi hatuko tena kwenye ulimwengu wa Analogia, tupo kwenye Digital, kwa hiyo Watanzania wote nasi tunaota, sio kama ulivyokuwa ukiota wewe peke yako!
Mpendwa Mwalimu Nyerere, nina mengi sana ya kukueleza kuhusiana na nchi yako uliyoiasisi ila nahofia kukuchosha.
Hata hivyo Mwalimu siku hizi rasilimali za Taifa zinatafunwa na wale uliowaachia nchi. Tembo, Ndovu, Nyati mpaka Simba wanapakiwa kwenye chopa baada ya kudungwa sindano za usingizi safari ya Ulaya!
Mwalimu Nyerere, sasa hivi unga wa mahindi (sembe) unaotoka hapahapa Tanzania unauzwa sh; 1500/- kwa kilo moja, wakati unga wa ngano kutoka nje ya nchi unauzwa sh; 1200/- tu kwa kilo!
Hali hii ni tofauti kabisa na wakati wa enzi zako. Japo ulikuwa na mapungufu mengi, lakini hili la upandaji holela wa bidhaa uliweza kuli udhibiti.
Mwalimu, jambo jingine unalopaswa kulijua na lililokuwa gumzo kwa miaka hii ya karibuni ni ile mbegu ya UDINI uliyoipanda siku zileeeee, sasa imeshaanza kualika maua, hivyo karibu matunda yake yataonekana.
Mwalimu nadhani unakikumbuka kile kitabu kiitwacho Development and Religion in Tanzania cha Bwana Pvan Bergen ambapo alikunukuu katika ukurasa wa 335 ukisema hivi; “I will not come against my own church” (Bergen uk 335).
Tafsiri isiyo rasmi ni kwamba wewe eti ulimaanisha kuwa; “Kamwe huwezi kuwa kinyume na Kanisa lako”
Pia ukumbuke Mheshimiwa Mwalimu pale Agosti 3, 1970 ulipomwita Ikulu Padri Rweyemamu katika mazungumzo maalum ambapo ulimuahidi Rweyemamu kuwa, kipindi kile Kanisa ndilo lililoshika hatamu za kuongoza dola nawe utahakikisha hali inaendelea kuwa hivyo.
“Tanzania is not Catholic country, but Catholics is strong, I want to give the church a better chance here”. Kwa tafsiri yangu ni kwamba;
“Tanzania si nchi ya Kikatoliki, lakini Ukatoliki una nguvu, hivyo nataka kulipa Kanisa nafasi ya pekee hapa nchini” (soma Bergen uk 335).
Kwa hiyo mbegu hii imeshaota na wakati wowote wanao tutakufuata uliko baada ya matunda haya kutamali katika kila kona ya nchi yetu.
Mwisho kabisa Mwalimu, wale makabwela waliokupokea wakati ukitokea Butiahama ukiwa na kaptura na kuja Pugu kuanza kazi ya Ualimu na baadaye wakakushauri uungane nao katika chama cha TAA ili kuendeleza harakati za kumng’oa mkoloni na hatimaye mkafanikiwa, siku hizi wanaitwa magaidi, Al-Shabaab, Wachochezi na majina yote mabaya unayoyajua wewe.
Pia kama utaonananaye Samora Machel wa msumbiji mwambie kuwa Mandela amesha mchukua mkewake, lakini Mzee Mugabe naye mpaka leo bado anaendelea kuwatawala Wazimbabwe, hataki kabisa kung’atuka kufuata nyayo zako.
Na vilevile nikitaka kusahau, waambie kina Mzee Abeid Aman Karume kwamba mwanawe Amani alifanikiwa kuwa Rais kwa miaka 10 nchini Zanzibar, na Mzee Jomo Kenyetta mpe habari kwamba na yeye kijana wake ameshakalia kiti cha Ikulu ya Nairobi licha kwamba anakabiliwa na kesi ya mauaji katika mahakama ya Kimataifa ya makosa ya jinai ICC huko The Hage.
Sasa hivi tufanyeje Mwl ili kuinusuru nchi yetu?
Ni mimi Rashid Abdallah Mtagaluka
BONYEZA HAPA KUPATA CHANZO CHA BARUA HII

No comments: