VIONGOZI wa kijiji cha Nyangoto wilayani Tarime mkoani Mara,wamewatuhumu viongozi waandamizi wa Serikali wakiwemo Mawaziri kuwa chanzo cha migogoro inayojitokeza kati ya wananchi na wa wawekezaji wa mgodi wa North Mara.
Wamedai viongozi hao wamekuwa wakishindwa kukutana na wananchi pindi wanapofika mgodini hapo ili kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili badala yake wamekuwa wakitumia ziara zao kukutana na uongozi wa mgodi pekee.
Viongozi hao wa Serikali ya kijiji hicho cha Nyangoto wakiongozwa na mwenyekiti wao Bw Elisha Nyamhanga wametoa tuhuma hizo mbele ya wajumbe wa kikosi kazi maalum ambacho kimeundwa na serikali kwaajili ya kushughulikia malalamiko mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na mgodi huo pamoja na wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo unaomilikiwa na Afrika Barrick Gold.
Wamesema pamoja na wananchi kuwa na malalamiko mengi kuhusu kunyang’anywa ardhi yao bila fidia,uharibifu wa mazingira kutotekelezwa kwa mikataba lakini viongozi hao wamekuwa wakitumia ziara zao kukutana na uongozi wa mgodi jambo ambalo limesababisha wananchi kuwa na chuki dhidi ya serikali yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikosi kazi hicho Bw Adam Yusuf,akizungumza na wajumbe hao wa serikali ya kijiji,amesema serikali imeunda kikosi kazi hicho baada ya uongozi wa mgodi kutoa malalamiko dhidi ya wananchi wa vijiji saba vinavyozunguka mgodi huo huku wananchi pia wakilalamikia matatizo makubwa wanayoyapata kutokana na uwekezaji huo likiwemo tatizo kubwa la ulipwaji wa fidia na uharibifu wa mazingira katika vijiji hivyo.
No comments:
Post a Comment