Sunday, March 25, 2012

ZITTO KABWE : URAIS NAUTAKA...


MZEE NIMESHAKUA ...NIKUPOKEE 2015 ....

Kwanza niseme wazi kabisa kabisa kuwa Urais ninautaka.

Ninaamini ninao uwezo wa kuwa Rais. Ninaamini nina uzalendo wa kutosha na utashi wa kuleta mabadiliko stahili wa namna nchi yetu inavyoongozwa. Ninajua kuwa nchi yetu imesahau maendeleo ya watu na kujikita katika maendeleo ya vitu. Ninajua kuwa hivi sasa viongozi wetu wengi wanaangalia zaidi mitindo (styles) badala ya mambo ya msingi (content). Ninajua kuwa maendeleo vijijini yamesahaulika. Ninajua nchi yetu inahitaji Uongozi wa kufanya mabadiliko makubwa (transformation) badala ya mabadiliko ya juu juu (cosmetic change).

Ninajua ‘transformation’ inahitaji maamuzi magumu yatakayoudhi wengi na hasa mabwana wakubwa wa nchi za magharibi mfano kuzuia nchi yetu kuuza malighafi tu. Ninajua rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa Mali ya Umma ni kikwazo kikubwa cha maendeleo yetu na kwamba lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuzuia na kutokomeza ufisadi. Ninajua rasilimali kama Madini, Mafuta na Gesi, Ardhi n.k. ni lazima zifaidishe wananchi wa nchi yetu.

Hivyo, nchi inahitaji Kiongozi wa juu atakayekabili changamoto hizi. Ninaamini ninaweza kuwaongoza Watanzania wenzangu kukabili changamoto hizi. Sio kazi rahisi lakini ni kazi ambayo lazima Mtanzania mmoja aifanye. Mimi nataka kuifanya. Nina uwezo wa kuifanya.


Hata hivyo kazi hii hata kama naitaka ni lazima wenye nchi waamue kunipa kazi hii. Ni lazima kwanza Chama changu kiseme wewe ndio mwanachama unaestahili kuifanya kazi hii. Ni lazima Watanzania wengi waseme wewe ndio mwananchi mwenzetu unayeweza kuchukua jukumu hili. Kuitaka tu haitoshi. Ni lazima wananchi wakuamini na kukupa jukumu hili.

Sasa kama wananchi watasema huyu Zitto anapaswa kubeba jukumu hili mwaka 2015 tuache iwe. Kama watasema hapana wewe bado mpaka mwaka 2020 au hata 2025 tuache iwe hivyo. Pia Kama hawataki kabisa tuache iwe hivyo.

Mjadala wa umri wa kugombea Urais imekuwa mjadala mkali sasa. Mjadala huu baadhi ya watu kwa sababu wanazojua wao wameamua kuita ni mjadala wa Zitto na January. Kwamba ni mjadala unaobagua Wazee. Mjadala unaopandikiza chuki na sumu za kibaguzi. Kwamba ni mjadala wa Kitabaka na kuwa Zitto na January sio tabaka stahili la vijana walio wengi. Sitamsemea January, nitajibu baadhi ya hoja za mwandishi wa makala mojawapo kama Zitto. January akitaka atamjibu naye kivyake.

Mwandishi anasema yeye hapingi hoja ya umri, bali anapinga aina ya watu wanaoshadidia hoja hiyo. Anaipenda hoja ila hapendi watoa hoja. Hoja nzuri lakini Zitto na January wabaya. Amelisema hilo mwanzo kabisa wa makala yake. Kwa hiyo kwake yeye hoja ingeletwa na vijana wengine asingekuwa na shida wala isingekuwa hoja hatari. Kwa kuwa hoja imeletwa na Zitto na January (ingawa sisi sio waanzilishi wa hoja hii) ni hoja ya kibaguzi. Nawashangaa sana wasomi wa siku hizi. Wasomi wanaojadili watu badala ya masuala.

Mwandishi anasema kwamba vyama vya siasa haviandai vijana kuwa viongozi. Nitamweleza.

Chama changu kinalea na kukuza vijana kuwa viongozi. Mimi binafsi nimejiunga na chama changu nikiwa na umri wa miaka 16, mtoto. Nimekulia ndani ya chama. Nimepewa majukumu ya kawaida kabisa ya chama kama kusimika miti ya bendera, kupokea viongozi na kuandaa mikutano. Nikiwa Chuo Kikuu Mwenyekiti wa sasa wa Chadema ndugu Mbowe alikuja kuniomba sasa nishiriki kikamilifu kukijenga upya chama. Yeye alikuwa Mbunge wa Hai akitaka chama kiwe imara zaidi, akaambiwa kuna mwanachama wenu kule Mlimani. Wakati huo CHADEMA kilikuwa chama ambacho watu wanakikimbia isipokuwa watu wa Kigoma na Kilimanjaro, Shinyanga, Karatu na Ukerewe. Vijana walikuwa wanajipambanua na CCM zaidi ama CUF au TLP kuliko hiki chama cha mabwanyenye. Huu ni mwaka 2001, muongo mmoja tu uliopita. Mimi na Freeman Mbowe ndio tumefanya mabadiliko yote yanayoonekana CHADEMA. Tumeingiza watu wapya, tumeandika Katiba upya. Ilipofika mwaka 2005 tukasema Freeman Mbowe nenda kwenye Urais, tulijuwa tunashindwa lakini tulitaka kujenga chama chetu. Tukapata Wabunge. Wabunge Wakafanya kazi. Tukaingia mwaka 2010 katika uchaguzi kama chama imara tunachokwenda kuchukua dola.

Katika mchakato huu tukaingiza vijana kwenye chama na kuwalea. John Mnyika hakuwa CHADEMA, tena alikuwa mgumu sana kuingia kwenye chama chetu. Tukampa moyo. Tukampa majukumu. Leo ni mmoja wa rasilimali watu kubwa sana katika siasa za nchi yetu. Halima Mdee hakuwa mwanasiasa kabisa. Tukampa moyo. Tukampa majukumu. Leo ni Mbunge mahiri kabisa.

Baadhi ya watu wazima waliingia CHADEMA kufuata vijana. Vijana tulifyeka pori kwanza. Nani anasema hatulei vijana kuwa viongozi wazuri? Nani haoni hazina ya viongozi vijana hivi sasa ndani ya Bunge kutoka vyama vyote? Kuna namna bora ya kulea viongozi zaidi ya kuwapa majukumu?

Mbowe alikuwa ananifuata pale Hall 1, tunakwenda kufanya kazi za chama usiku kucha, kusoma na kuchambua makabrasha ya kisera na mikakati. Ninarudi chuo usiku wa manane wakati wanafunzi wengine ama wapo wanajisomea au wamelala. Kazi ya kujenga taasisi inayoitwa chama cha siasa.

Lakini kujengwa kuwa kiongozi sio kazi ya chama pekee. Ni kazi ya jamii kwa ujumla. Wakati wanafunzi wenzangu walikuwa wanaomba kufanya kazi za mafunzo kwenye taasisi kubwa Kama Benki Kuu, nikiwa mwaka wa pili Chuo Kikuu nilikwenda kufanya internship TGNP. Kujifunza Bajeti ya kijinsia na kuipa hoja za kiuchumi. Kina mama wa TGNP wakanijenga na kunipika kiuongozi.
Chuo Kikuu sikuwa nasoma Sosholojia, lakini rafiki yangu mkubwa alikuwa Chachage. Sikuwa nasoma lugha, lakini mshauri wangu alikuwa Lwaitama. Sikuwa nasoma sheria lakini nilikuwa namwakilisha Shivji na kusoma mada zake alizopasa kuwakilisha kwenye semina kadhaa kuhusu haki za binadamu. Nimefunzwa na makundi ya watu mbalimbali na sio chama changu pekee. Jamii ndio yenye jukumu la kufunda vijana kuwa viongozi. Jamii inafanya kazi hiyo?

Inasemwa mjadala huu ni hatari kwa namna ulivyopenyezwa. Kupenyezwa? Huu mjadala wa umri umeanza kuzungumzwa mimi nikiwa nipo Chuo Kikuu. Vijana kupitia National Youth Forum Kama Taasisi ya vijana wamekuwa wakisema jambo hili toka miaka ya katikati ya tisini. Jukwaa hili la Vijana chini ya viongozi wake kina Hebron Mwakagenda wamekuwa wakitoa Maazimio na Maazimio kwamba umri wa kugombea Urais upo juu sana toka miaka ya tisini. Taasisi ya TYVA imekuwa ikijenga hoja hii toka miaka ya 2000. Hii sio hoja mpya hata kidogo. Hoja hii haijapenyezwa. Hii ni hoja ya vijana ya miaka mingi sana. Lakini sishangai kuona inaonekana ni hoja mpya kwani watanzania uwezo wetu wa kutunza kumbukumbu ni mdogo sana. Pia tunapenda kujadili mtoa hoja na sio hoja yenyewe. Mfuatiliaji yeyote makini wa siasa za vijana wa Tanzania kupitia makongamano ya vijana anajua hii sio hoja iliyopenyezwa na Zitto au January. Kuijadili kwa kumwangalia Zitto na January ni kuchoka kufikiri.

Hoja hii haina hatari yeyote inayosemwa na mwandishi. Hoja hii ni hoja kama hoja nyingine yeyote na inaweza kupita au kukataliwa. Hii sio hoja ya watu fulani. Ni hoja ya vijana ya siku nyingi sana. Vijana hawa wanajiona kupitia vijana wengine walio kwenye nafasi mbalimbali kisiasa au hata katika sekta binafsi. Mfano vijana wa Kigoma ninakotoka wakiniangalia wanajiona. Ndio wanaona tuko sawa. Wanaona mimi ni mwenzao. Nimekua miongoni mwao. Nimesoma nao. Nimecheza nao. Nimehangaika nao. Wanaona Ubunge nilionao ni Dhamana tu na hawanizungumzishi kama mtu kutoka tabaka fulani, bali kama mwenzao.

Ninaishi maisha ninayoishi. Siishi Manzese kwa Mfuga Mbwa. Siishi Masaki pia. Naishi Tabata, kwenye nyumba ya kupanga. Tabata wanaishi vijana wote wale wa tabaka la chini kama asemalo mwandishi na pia tabaka la kati na labda tabaka la juu. Najua na kusikia machungu ya vijana wasio na ajira na ndio maana nahangaika kwa kutumia nafasi ya Ubunge kujaribu kuisukuma Serikali iweke sera zinazotekelezeka za kutatua tatizo la ajira kwa vijana. Ndio maana nahangaika kila siku kujenga hoja kwamba Serikali iingilie kati ukuaji wa uchumi ili pia wanyonge wafaidike. Ninasikia machungu ya vijana wasio na ajira maana ndio walionipigia kura kuwa Mbunge. Zaidi ya hayo nakutana nao sana kuzungumza namna ya kusaidiana.

Nakutana nao mitaani kwa mijini na vijijini ninakokwenda kila wakati. Nakutana nao kwenye mitandao ya kijamii, wananiandikia na mimi ninawajibu. Nagawana nao kidogo nilichonacho ili nao waweze kijikwamua. Nawasaidia vijana wenye vipaji kukuza vipawa vyao na kupata kipato. Mwandishi anapata wapi haki ya kusema sentensi rahisi rahisi kwamba mimi sisikii machungu ya vijana wenzangu?

Ninashinda na vijana wa aina zote, ndio kazi kubwa ya Mwakilishi anayefanya kazi yake. Nina marafiki wavuvi, mafundi seremala, waimbaji wa Bongo Flava, machinga na hata wasio na ajira. Nina marafiki wenye makampuni yao, wafanyakazi wa mashirika ya Umma, wasomi wa Vyuo Vikuu na wafanyabiashara wakubwa. Mwakilishi yeyote wa wananchi lazima asikie machungu ya jamii nzima vinginevyo hatoshi.

Kijana mwenye umri wangu ana mambo mengi anayofanana nami. Ana mambo mengi ya kujifunza kutoka kwangu. Hapa katikati ilikuwa ni kama jambo lisilowezekana kijana wa aina yangu kutoka familia masikini kabisa kuwa Mbunge. Baada ya Zitto kuwa Mbunge na kutokana na kazi niliyofanya Bungeni katika Bunge la Tisa, vijana wengi walihamasika na kusema wanaweza. Leo tuna vijana wadogo kabisa kutoka familia za kawaida kabisa ni Wabunge na wanafanya vizuri. Kina Kafulila, kina Mkosamali, kina Silinde hawa ni watoto wa kimasikinj kabisa ambao ni wa kwanza kupata shahada kwenye familia zao. Hii ni nguvu ya ‘inspiration’ kutoka kwa rika linalofanana. Sugu ni mkubwa kwangu kiumri, lakini kuingia kwake siasa kumechangiwa sana na kazi zangu pamoja na wenzangu kwenye Bunge.

Kuna vijana wengi zaidi nchini kwetu wanasema ninataka niwe kama Zitto, kama January, kama Halima Mdee. Tunazungumza nao. Tunaishi nao. Ni ndugu zetu. Ni rafiki zetu. Tunaishi nao mtaani. Tunakwenda nao kwa kinyozi mmoja. Tunakwenda muziki pamoja. Ninajua machungu ya vijana. Ninafanyia kazi machungu ya vijana. Ndio kazi yangu ya kila siku kama Mbunge, kama Mwakilishi wao.

Mwandishi anasema mjadala unalenga kuleta ubaguzi. Sioni hoja yake. Wanaosema umri wa kugombea Urais ushushwe chini ya miaka 40 hawasemi wazee wasigombee. Wanasema tupanue wigo wa haki hii ya kugombea. Wanaozungumza ubaguzi ndio wenye kupenyeza mbegu za kibaguzi. Kwa kuwa wanawaza kibaguzibaguzi basi kila jambo huliangalia kibaguzi. Kama Katiba inasema yeyote mwenye haki ya kupiga kura ana haki ya kugombea nafasi yeyote ya uongozi, ubaguzi unatoka wapi? Hoja zote zinazotolewa na mtoa hoja kuhusu ubaguzi zinasambaza mbegu ya ubaguzi.

Mwandishi sasa anawaambia Watanzania waanze kufikiri sasa zamu ya nani. Mimi binafsi sijawahi kusema hii ni zamu ya vijana. Ila nimesema changamoto za sasa za nchi zinahitaji mtu mwenye uwezo wa kuzikabili, ninaamini mtu huyo ni kijana. Ninaamini kuwa kila kizazi kina ajenda zake. Kizazi chetu kina kazi ya kuhakikisha uhuru wa kiuchumi wa nchi yetu. Kizazi cha kina Mwalimu kilikuwa cha ukombozi na kujenga Taifa moja. Mwandishi hamwamini Frantz Fanon?
Hoja ya kwamba mjadala huu unataka kununua hisia za wanyonge ni hoja isiyo na [mashiko] kabisa. Mimi nimechaguliwa na wanyonge mara mbili kuwa Mbunge wao. Wanyonge wamenipa Ubunge bila kutoa rushwa. Wamenipa Ubunge kwa kuniamini. Sasa kwa nini sasa ninunue hisia zao? Hii hoja ina misingi gani? Hii ni hoja ya kubandika. Hii ni hoja ya kubumba maneno ili mwandishi aonekane kwamba anafanya uchunguzi wa kitabaka. Hakuna dhana ya tabaka katika hoja hii kama ilivyo kuwa hakuna dhana ya tabaka kwa wazee au hata wanawake. Hoja hii haizuii kwa namna yeyote ile wananchi kuhoji chanzo cha ufukara wao. Kwanza wanaosemwa kwenye hoja hii ndio wapo mstari wa mbele kuhakikisha Mali ya Nchi inatumika wa maendeleo ya wananchi. Mimi binafsi nimeanzisha mjadala wa rasilimali Madini nchini mpaka kutungwa kwa sheria mpya inayoweka misingi ya nchi kufaidika na Madini. Mimi binafsi na wenzangu tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha serikali inatekeleza sheria mpya.

Mwandishi amesahau Buzwagi? Mwandishi amesahau hoja ya Mkonge inayotaka wanyonge wapewe mashamba ya Mkonge na wawezeshwe na Serikali kulima Katani? Mwandishi amesahau hoja ya kusimamia sekta ya nyumba ili wanyonge wasinyonywe na wenye nyumba ambayo imetolewa na mmoja wa wanaotetea hoja ya umri kushushwa? Ama mwandishi ana wanyonge wake anaowasemea? Sio hawa manamba kwenye Mkonge. Sio hawa vijana wachimbaji wadogo. Sio hawa vijana wanaoshindwa kulipa kodi ya nyumba mwaka mzima? Wanyonge wa mwandishi ni wanazuoni wanaoishi kwa fedha za walipa kodi ambao hawana shida ya kujiuliza kama watakula au watalala maana Serikali au wafadhili wa masomo yao wanawalipia malazi na chakula. Kama wanyonge wake ni hawa waliotupigia kura sisi ili kuwawakilisha Bungeni, basi mwandishi hajui asemalo.

Hoja ya umri wa kugombea Urais, kwa kuweka pa kuanzia ama kuweka kikomo inapaswa kujadiliwa bila kuangalia majina ya wanaotetea hoja hii. Ijadiliwe kwa faida na hasara zake. Kujenga hoja kwa misingi ya kitabaka ni kuchochea ubaguzi na kunyweshea mbegu za kibaguzi. Nani ana uhakika kuwa Zitto atakuwa anaishi ifikapo mwaka 2015? Kwamba tusiandike Katiba yenye kupanua wigo wa kutoa haki ya kugombea Urais kwa sababu ya Zitto?

Huu woga dhidi ya Zitto unatoka wapi?

CHANZO  : zittokabwe.wordpress.com

No comments: