JK akifafanua jambo wakati alipozindua mkutano wa REPOA |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa moja ya magonjwa makuu yanayowakumba Watanzania kwa sasa ni ugonjwa wa Kitanzania wa kulalamika, kunung’unika wakimlaumu kila mtu isipokuwa wao wenyewe.
Aidha, Rais Kikwete amesisitiza kuwa Serikali yake itahakikisha kuwa utajiri na manufaa yanayopatikana na yatakayopatikana kutokana na raslimali za madini na gesi asilia nchini yanamnufaisha kila Mtanzania.
Rais Kikwete pia ameahidi, kwa mara nyingine tena, kuwa Serikali yake itaendelea kuwekeza katika huduma za jamii kwa kuboresha huduma za elimu na afya, kuendeleza kilimo na kuinua hali ya uchumi wa vijijini kama njia ya kuwainua Watanzania wengi zaidi, na hasa wale masikini zaidi, kutoka kwenye umasikini.
Rais Kikwete ameyasema hayo, leo, Jumatano, Machi 28, 2012, wakati alipofungua Warsha ya 17 ya Utafiti ya Mwaka ya shirika lisilokuwa la kiserikali la Research on Poverty Alleviation (REPOA) inayofanyika kwa siku mbili kwenye Hoteli ya White Sands mjini Dar es Salaam.
Rais Kikwete amewaambia washiriki wa Warsha hiyo wanaotoka nchini na nje ya nchi, na hasa wale kutoka nje ya nchi kujitahidi sana kuepukana kuambukizwa ugonjwa wa Kitanzania wa kulalamika, kunung’unika na kulaumu wakati wanapojadili changamoto na njia bora zaidi na za haraka zaidi kupunguza ama kumaliza umasikini nchini.
“Nawaombeni nyote mlioko hapa leo kutumia nafasi ya Warsha ya Utafiti hii kwa kutathmini kwa kina kabisa changamoto zinazohujumu dhamira yetu ya kupata mageuzi ya haraka zaidi ya kiuchumi na kijamii“, amesema Rais Kikwete na kuongeza: “Mnaweza kufanya hivyo kwa kutumia
ujuzi wenu wa nyuma ama kwa kutumia uzoefu wa nchi nyingine. Tafadhalini sana epukeni na jizuieni sana kutokuambukizwa ugonjwa wa Kitanzania wa kulalamika na kulaumu wengine wote isipokuwa sisi wenyewe. Ni ugonjwa usiokuwa na tija.”
Kuhusu nafasi ya raslimali za madini na gesi asilia nyingi iliyogunduliwa nchini, Rais Kikwete amerudia tena ahadi yake ambayo ameitoa huko nyuma kuwa Serikali yake itahakikisha kuwa raslimali hizo zinawanufaisha Watanzania wote bila kubagua kwa sababu kila Mtanzania anayo haki ya kunufaika na raslimali za nchi yake.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete ambaye amesisitiza mageuzi makubwa ya sera ambako sasa wajibu wa Serikali ni kufungua njia za uwezeshaji na sekta binafsi kufanya biashara tofauti na sera za zamani ambako Serikali ilikuwa inafanya hata biashara ya bucha za nyama na maduka ya sindano na viberiti amewaambia
washiriki wa Warsha hiyo:
“Serikali kwa upande wake itaendelea kutekeleza mipango na sera ambazo zinamnufaisha kila
mtu na zenye kuhudumia maslahi ya jamii zilizo masikini zaidi na zisizojiweza.
Tutaendelea pia, kuwekeza zaidi katika huduma za jamii kwa kuinua kiwango na ubora wa elimu, huduma za afya, kuboresha kilimo na uchumi wa maeneo ya vijijini.”
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
28 Machi, 2012
No comments:
Post a Comment