Thursday, October 9, 2014

MBARONI KWA KUTWA WAKILIMA WAKIWA UCHI

POLISI mkoani Simiyu inawashikilia watu wanne wa familia moja kwa tuhuma za kukutwa wakilima katika shamba la familia yao, huku wakiwa watupu kama walivyozaliwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Venance Kimario alisema ofisini kwake jana kuwa wanafamilia hao wamekamatwa wakihusishwa kushiriki katika imani za kishirikina.
Alisema polisi walipata taarifa za siri kutoka kwa raia wema kuhusu wanafamilia hao, kulima shamba huku wakiwa watupu na kuamua kufuatilia, na walipofika eneo la tukio saa 12 za asubuhi, walikuta wanafamilia hao wakilima huku wakiwa uchi wa mnyama.

Alitaja waliokamatwa kuwa ni baba wa familia hiyo, Makoye Gamoge (42) na mke wake Neema Kigela (31), watoto wao wawili (majina yamehifadhiwa).

Kamanda Kimario alidai familia hiyo inatuhumiwa kwamba wamekuwa wakilima huku wakiwa uchi, kutokana na imani za kishirikina kuwa kwa kufanya hivyo, wataongeza tija na mazao yataongezeka maradufu na hivyo kuwakwamua kiuchumi.

“Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na baba wa familia hiyo kwenye kituo cha Polisi, kulima kwa mtindo huo kunalenga kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo cha jembe la mkono,” alisema Kamanda Kimario.

Makoye anadaiwa kusema mbinu hiyo mpya na ya aina yake ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya ndugu yao ambaye ni mganga wa jadi, aliyefariki mwaka jana kwa maradhi ambayo hata hivyo hawayafahamu.

Kwa sasa watuhumiwa hao wanashikiliwa Polisi na baada ya uchunguzi kukamilika, watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

No comments: