Tuesday, June 4, 2013

TUTAKUWEKEA RASIMU YOTE YA KATIBA MPYA >>> HII HAPA NI SEHEMU YA KWANZA


UTANGULIZI
KWA KUWA, Sisi, Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamuarasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayoheshimu na kuzingatia misingi yautu, uhuru, haki, usawa, udugu, amani, umoja na mshikamano katika nyanja zote za maisha yetu;
NA KWA KUWA, tunaamini kuwa misingi hiyo inaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye mfumo wa demokrasia na utawala bora ambayo Serikali yake inasimamiwana Bunge lenye Wabunge waliochaguliwa na wanaowawakilisha wananchi na Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, nakuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa na kudumishwa na kwamba wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu;
NA KWA KUWA, umuhimu wa kutunza mali ya Mamlaka za Nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu, ubadhilifu, na kuhimiza matumizi bora na endelevu ya rasilimali na maliasili zetu pamoja na kulinda na kuhifadhi mazingira yetu kwa mustakabali wa maisha ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo;
NA KWA KUWA, umuhimu na faida za kujenga, kukuza na kuendeleza, amani, umoja, urafiki na ushirikiano miongoni mwa Watanzania, Mataifa mbalimbali ya Afrika na Dunia kwa ujumla;
KWA KUWA, azma ya kujenga Umoja wa Bara la Afrika katika misingi ya Umajimui wa Afrika ambao inadhihirishwa na Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar;
NA KWA KUENDELEZA, dhamira yetu hiyo ni muhimu:
(a) kulinda, kuimarisha na kuudumisha Muungano wa nchi za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar;
(b) kujenga Taifa huru na linalojitegemea;
(c) kuimarisha na kuendeleza utawala wa sheria;
(d) kukuza na kuendeleza maadili, uwajibikaji na uwazi;
(e) kujenga umoja na mshikamano utakaowezesha kutimiza malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kimazingira na kulinda urithi kwa ujumla;
(f) kujenga na kuendeleza ukuu wa mamlaka ya watu;
(g) kujenga na kuendeleza utii wa mamlaka ya Katiba; na
(h) kuimarisha na kudumisha uzalendo kwa Taifa miongoni mwa Watanzania;
NA KWA KUZINGATIA, urithi tulioachiwa na Waasisi wa Taifa letu wa kujenga
nchi yenye Umoja wa Watu wake ambao hawabaguani kwa misingi ya ukabila, udini,
rangi, jinsi au ubaguzi wa aina nyingine yoyote;
NA KWA KUZINGATIA, uzoefu wa zaidi ya Miaka Hamsini ya Uhuru na Miaka Hamsini ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na umuhimu wa ushiriki mpana na bayana wa wananchi katika utungaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; 2
HIVYO BASI, KATIBA HII YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ILIYOPENDEKEZWA NA BUNGE MAALUM LA KATIBA imetungwa na SISI WANANCHI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA  upitia KURA YA MAONI kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na utawala wa sheria, kujitegemea na isiyokuwa na dini. ‐ 3 ‐
SURA YA KWANZA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
SEHEMU YA KWANZA
MIPAKA, ALAMA, LUGHA, UTAMADUNI NA TUNU ZA TAIFA

Jamhuri ya Muungano
1.-(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho lenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.
(2) Jamhuri ya Muungano ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.
(3) Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa katika Ibara ndogo ya (1), ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii, kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano hayo.
Eneo la Jamhuri ya Muungano
2. Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na  eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari.
Alama na Siku Kuu za Taifa
3.-(1) Alama za Taifa ni:
(a) Bendera ya Taifa;
(b) Wimbo wa Taifa; na
(c) Nembo ya Taifa,
kama zitakavyoainishwa katika sheria itakayotungwa na Bunge.
(2) Siku Kuu za Kitaifa zitakuwa ni:
(a) Siku ya Uhuru wa Tanganyika, itakayoadhimishwa tarehe 9 Disemba;
(b) Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar, itakayoadhimishwa tarehe 12 Januari;
(c) Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, itakayoadhimishwa tarehe 26 Aprili; na
(d) Siku Kuu nyingine zitakazoainishwa na sheria za nchi.
(3) Kila Siku Kuu ya Kitaifa itakuwa ni siku ya mapumziko.
Lugha ya Taifa na lugha za alama
4.-(1) Lugha ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano ni Kiswahili na itatumika katika mawasiliano rasmi ya kitaifa na kiserikali.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), lugha ya Kiingereza inaweza kutumika kuwa lugha rasmi ya mawasiliano ya kiserikali pale itakapohitajika.
(3) Serikali itaweka mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa mawasiliano ya lugha mbadala zikiwemo lugha za alama na nukta nundu kwenye sehemu muhimu za umma na katika vyombo vya habari vinavyotangaza habari zake kitaifa kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.
‐ 4 ‐ Tunu za Taifa
5. Jamhuri ya Muungano itaenzi na kuzingatia Tunu za Taifa
zifuatazo:
(a) utu; (b) uzalendo; (c) uadilifu; (d) umoja; (e) uwazi; (f) uwajibikaji; na (g) lugha ya Taifa.
SEHEMU YA PILI
MAMLAKA YA WANANCHI, UTII NA HIFADHI YA KATIBA
Mamlaka ya wananchi
6. Jamhuri ya Muungano ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia inayozingatia haki ya kijamii, na kwa hiyo:
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka za nchi, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi ambao kwa umoja na ujumla wao wanaimiliki na kuipatia Katiba hii uhalali;
(b) lengo kuu la Serikali litakuwa ni maendeleo na ustawi wa wananchi;
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi; na
(d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
Watu na Serikali
7.-(1) Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake, katika uendeshaji na utekelezaji wa shughuli zake utazingatia azma ya kukuza umoja wa kitaifa na kudumisha heshima ya Taifa.
(2) Kwa madhumuni ya masharti ya Ibara ndogo (1), mamlaka ya nchi na vyombo vyake vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote kwa lengo la kuhakikisha kwamba:
(a) utu na haki nyingine zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa;
(b) sheria za nchi zinasimamiwa na kutekelezwa;
(c) Serikali itahakikisha kuwa shughuli zinazofanywa zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine;
(d) ardhi ikiwa rasilimali kuu na msingi wa Taifa, inalindwa, inatunzwa na kutumiwa na wananchi wa Tanzania kwa manufaa, maslahi na ustawi wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo;
(e) maendeleo ya uchumi wa Taifa yanapangwa na kukuzwa kwa ulinganifu na kwa pamoja na kwa namna ambayo inawanufaisha wananchi wote;
(f) kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu kipato chake; ‐ 5 ‐
(g) utu, heshima na haki nyingine zote za binadamu zinahifadhiwa na kudumishwa kwa kuzingatia mila na desturi za kitanzania na kwa kufuata mikataba mbalimbali iliyoridhiwa na Jamhuri ya Muungano;
(h) mamlaka za nchi zinatoa fursa na haki zilizo sawa kwa wananchi wote, wanawake na waume, bila ya kujali rangi, kabila, nasaba, dini au hali ya mtu;
(i) aina zote za dhulma, vitisho, ubaguzi, unyanyasaji, rushwa, uonevu au upendeleozinaondolewa nchini;
(j) utajiri wa rasilimali na maliasili za Taifa unaelekezwa katika kuleta maendeleo, kuondoa umaskini, ujinga na maradhi; na
(k) nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia na kujitegemea.
Mamlaka na utii wa Katiba
8.-(1) Bila ya kuathiri masharti ya Katiba za Washirika wa Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, Katiba hii itakuwa sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano.
(2) Mtu yeyote, chombo, taasisi, jumuiya na wakala wowote wa mamlaka ya nchi na mamlaka binafsi zinao wajibu wa kuzingatia masharti ya Katiba hii na kuyatii.
(3) Sheria yoyote, mila, desturi au uamuzi wowote wa chombo cha dola, ofisa wa Serikali au mtu binafsi ni sharti ufuate na kuendana na masharti yaliyomo kwenye Katiba hii na kwamba, sheria, mila, desturi
au uamuzi wowote ambao hautawiana au kwenda sambamba na masharti ya Katiba hii utakuwa batili.
Hifadhi ya Katiba
9.-(1) Mtu au kikundi cha watu hakitachukua au kushikilia mamlaka ya nchi isipokuwa kwa mujibu wa Katiba hii.
(2) Kitendo chochote kinachokiuka masharti ya Ibara ndogo ya
(1) ni batili na ni kitendo cha uhaini kama itakavyoelezwa katika sheria za nchi.
(3) Kwa madhumuni ya kuhifadhi masharti ya Ibara ndogo ya (1) na (2), Serikali itaweka utaratibu wa kuisambaza Katiba hii kwa wananchi na kuiweka katika mitaala ya elimu ili kuwezesha wananchi kuifahamu, kuilinda na kuitii.
SURA YA PILI
MALENGO MUHIMU, MISINGI YA MWELEKEO WA
SHUGHULI ZA SERIKALI NA SERA ZA KITAIFA
Utekelezaji wa malengo ya Taifa
10.-(1) Malengo ya Taifa yaliyoainishwa ndani ya Katiba hii yatakuwa ni mwongozo kwa Serikali, Bunge, Mahakama, vyama vya siasa, taasisi, asasi na mamlaka nyingine na kwa kila mwananchi katika matumizi au kutafsiri masharti ya Katiba hii au sheria nyingine yoyote na katika utekelezaji wa uamuzi wa kisera kwa madhumuni ya kujenga jamii huru, makini na iliyo bora.
(2) Serikali itatoa taarifa Bungeni si chini ya mara moja katika ‐ 6 ‐ kila mwaka, kuhusu hatua zilizochukuliwa na mamlaka ya nchi ili kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Taifa yaliyoainishwa katika Katiba hii.
Malengo Makuu
11.-(1) Lengo Kuu la Katiba hii ni kulinda, kuimarisha na kudumisha udugu, amani, umoja na utengamanowa wananchi wa Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia ustawi wa wananchi na kujenga Taifa huru lenye demokrasia, utawala bora na kujitegemea.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), lengo hilo kuu litaendelezwa na kuimarishwa katika nyanja zote kuu, ikijumuisha nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kimazingira.
(3) Katika kutekeleza malengo ya Taifa ya:
(a) kisiasa, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili –
(i) kuhakikisha kuwa inazuia, inapinga na kuondoa dhulma, vitisho, ubaguzi, unyanyasaji, rushwa, uonevu na upendeleo miongoni mwa wananchi kwa misingi ya asili ya mtu, sehemu anayotoka, nasaba,kabila, jinsi, dini au imani yake;
(ii) kuhakikisha uwepo wa amani na kujenga utamaduni wa kuenzi, kuheshimu na kudumisha amani, umoja na utengamano, ushirikiano na uvumilivu wa kisiasa kwa madhumuni ya kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi;
(iii) kuhakikisha uwepo wa ulinzi, usalama na ustawi wa watu na mali zao, na kuepuka kufanya jambo lolote litakalohatarisha au kwenda kinyume na lengo hilo;
(b) kijamii, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili:
(i) kuhakikisha kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata mila, desturi na Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu na mikataba mingine ya kimataifa iliyoridhiwa na Tanzania;
(ii) kuhakikisha kwamba Serikali na vyombo vyake vyote vya umma vinatoa nafasi na fursa zilizo sawa kwa raia wote, bila ya kujali rangi, kabila, dini, nasaba, hali ya mtu au mahali alipo;
(iii) kujenga utamaduni wa kuwepo ushirikiano, maelewano na maridhiano, uvumilivu na kuheshimu mila, desturi na imani ya dini ya kila mtu;
(iv) kuhakikisha kuwa msaada na hifadhi ya jamii inatolewa kwa watu wasiojiweza, wazee, wagonjwa,  watoto na watu wenye ulemavu;
(c) kiuchumi, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili:
(i) kuwaletea wananchi maisha bora kwa kuondoa umaskini;
(ii) kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kuwa utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine;
(iii) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi;
(iv) kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na kukuza fursa za uwekezaji;
(v) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao;
(vi) kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa mazao kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, utafutaji na uendelezaji wa masoko ya mazao yao;
(vii) kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji wa mizania ya bei za mazao na pembejeo;
(viii) kuimarisha na kuendeleza uwekezaji wa ndani, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, maeneo ya ufugaji na vifaa vya uvuvi;
(ix) kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa fursa na nafasi za wazi kwa watu wote na kuanzisha shughuli za kiuchumi na kukuza mazingira yaliyo bora kwa ajili ya kuhamasisha sekta binafsi katika uchumi;
(x) kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anapata fursa ya kufanya kazi, kwa maana ya kufanya shughuli yoyote halali inayompatia kipato;
(xi) kuweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kujipatia elimu na kuwa huru kupata fursa sawa ya kutafuta elimu katika fani anayoipenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake;
(d) kiutamaduni, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili:
(i) kulinda na kuhifadhi urithi wa asili, malikale na sehemu zenye umuhimu wa kihistoria au kidini ili
kuepuka uharibifu, udhalilishaji na wizi au utoroshwaji nje ya nchi;
(ii) kulinda, kuhifadhi na kuendeleza tamaduni za watu wa jamii mbalimbali ambazo zinaendeleza
na kukuza utu na hadhi yao kwa namna ambayo haikinzani na Misingi ya Kitaifa, na Malengo Muhimu na Sera za Taifa;
(iii) kutambua, kulinda na kuendeleza lugha ya Kiswahili; na
(e) kimazingira, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha kuwa ni haki na jukumu la kila kizazi kulinda na kudumisha mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Sera kuhusu Mambo ya Nje
12. Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano inalenga nainazingatia maslahi ya Taifa na mamlaka kamili ya nchi na kwamba sera hiyo inatekelezwa kwa uwazi ili:
(a) kukuza ushirikiano wa kikanda na ushirikiano wa kimataifa;
(b) kukuza ushirikiano wa kiuchumi wenye tija kwa Taifa;
(c) kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa mataifa ya Afrika kwa kushiriki katika hatua mbalimbali za mtangamano wa kiuchumi wa kikanda;
(d) kuheshimu sheria za kimataifa;
(e) kuzingatia mikataba ya kimataifa, mikataba ya kikanda yenye maslahi kwa Jamhuri ya Muungano na kutatua migogoro ya kimataifa kwa njia ya majadiliano, usuluhishi, maridhiano na mahakama;
(f) kukuza uzingatiaji wa haki za binadamu na uhuru wa watu;
(g) kupambana na makosa ya kimataifa ya kijinai; na
(h) kuheshimu uhuru wa mataifa mengine.
SURA YA TATU
MAADILI NA MIIKO YA UONGOZI NA UTUMISHI WA UMMA
SEHEMU YA KWANZA
MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
Dhamana ya Uongozi wa Umma
13.-(1) Madaraka anayopewa kiongozi wa umma:
(a) ni dhamana na atatumia madaraka hayo na kutekeleza wajibu wake kwa:
(i) kuzingatia masharti ya Katiba hii; (ii) kuheshimu wananchi; (iii) namna inayokuza hadhi ya taifa na kulinda heshima ya ofisi anayoitumikia; na (iv) kukuza imani na heshima ya ofisi kwa wananchi;
(b) yanatoa wajibu kwa kiongozi kuwatumikia wananchi.
(2) Dhamana ya uongozi na heshima kwa kiongozi wa umma itazingatia mambo yafuatayo:
(a) uteuzi kwa misingi ya mwenendo wa mtu, uwezo, sifa au uchaguzi uliyo huru na haki;
(b) uwezo pasipo upendeleo katika kufanya uamuzi na kuhakikisha kwamba uamuzi haufuati udugu, ukabila, udini, upendeleo, rushwa au vigezo vingine visivyo sahihi;
(c) utoaji wa huduma pasipo upendeleo na kwa kufuata maslahi ya umma kwa kuonyesha-
(i) uaminifu katika utekelezaji wa kazi za umma; (ii) wajibu wa kutangaza maslahi binafsi ili kuepuka
mgongano wa maslahi; (d) uwajibikaji kwa umma katika kufanya uamuzi na vitendo; na
(e) nidhamu na kujituma katika kutoa huduma kwa umma.
Kanuni za Uongozi wa Umma
14.-(1) Kiongozi wa umma, akiwa ama katika kazi za ofisi au kazi binafsi au wakati amejumuika na watu wengine, atahakikisha kwamba mwenendo wake:
(a) hauruhusu kutokea mgongano wa maslahi kati ya maslahi binafsi na maslahi ya utumishi wa umma;
(b) hauhatarishi maslahi ya umma kwa ajili ya maslahi binafsi; au
(c) haushushi hadhi ya ofisi anayofanyia kazi.
(2) Kwa madhumuni ya Ibara ndogo ya (1), mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji kusimamia utekelezaji wa masharti yanayohusu kanuni za  uongozi wa umma.
(3) Wadhifa “Kiongozi wa Umma” kama ulivyotumika katika Sehemu hii utajumuisha viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa kama watakavyoainishwa kwenye sheria itakayotungwa na Bunge.
Zawadi katika Utumishi wa Umma
15.-(1) Zawadi au kitu chochote kitakachotolewa kwa mtumishi wa umma katika shughuli za kiserikali ni zawadi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na itawasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara au taasisi ya Serikali inayohusika, akiainisha:
(a) aina ya zawadi; (b) thamani ya zawadi; (c) sababu ya kupewa zawadi; na (d) mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo.
(2) Mtumishi wa Umma -
(a) hatafungua au kuendesha akaunti ya benki nje ya Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu; na
(b) hataomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya mtumishi wa umma. ‐ 10 ‐
(3) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi inayohusika na masharti ya Sehemu hii na masharti mengine yanayohusu utekelezaji wa masharti ya Ibara hii.
Wajibu wa kutangaza mali na madeni
16.-(1) Kiongozi wa Umma atalazimika kutangaza, ndani ya siku thelathini baada ya kupata uongozi na baada ya kuacha uongozi, mali na thamani zake na madeni yake katika Tume ya Maadili na Uwajibikaji.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), Kiongozi wa Umma atalazimika kutangaza mali zake  na madeni:
(a) yake binafsi; (b) ya mwenza wake wa ndoa; na (c) watoto wake walio chini ya umri wa miaka kumi na nane, mara moja kila mwaka, au kadri itakavyoamuliwa na sheria.
Mgongano wa kimaslahi
17.-(1) Kiongozi wa Umma hatashiriki katika jambo au shughuli yoyote ambayo ana maslahi nayo yeye  binafsi, mwenza wake, mtoto wake, jamaa yake, rafiki au mtu yeyote wake wa karibu.
(2) Kiongozi wa umma hatozungumzia kitu chochote katika Baraza la Mawaziri, Bunge, kamati au chombo kingine chochote rasmi ambacho ana maslahi nacho ya moja kwa moja au vinginevyo, isipokuwa tu kama atatoa taarifa ya mgongano huo wa maslahi katika vyombo hivyo.
(3) Itakuwa ni marufuku kwa Kiongozi yeyote wa Umma, kushiriki kuongeza au kwa namna yoyote ile, kuboresha maslahi yanayohusu wadhifa alionao, na endapo atashiriki, basi masharti hayo mapya yataanza kutumika kwa Kiongozi atakayekuja baada ya yeye kuondoka au kumaliza muda wa kukaa  madarakani.
(4) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, masuala ya:
(a) ngazi au orodha ya Viongozi wa Umma, wanaopaswa kutangaza mali zao;
(b) utaratibu wa utwaaji wa mali za Viongozi wa Umma zilizopatikana kwa njia za ukiukaji wa sheria;
(c) utaratibu wa kumwajibisha Kiongozi wa Umma aliyeenda kinyume na maadili na Miiko ya Uongozi;
(d) uanzishaji wa mitaala inayohusu maadili na uraia, mashuleni na vyuoni; na
(e) uanzishaji wa mitaala inayohusu Katiba mashuleni na vyuoni.
(5) Kiongozi wa Umma hataruhusiwa kushika nyadhifa mbili au zaidi au kutumikia Mihimili ya Dola zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.
Matumizi ya mali ya umma
18. Haitaruhusiwa kwa Kiongozi yeyote wa Umma kutumia au kuruhusu kutumika kwa mali yoyote ya umma, zikiwemo zilizokodishwa kwa Serikali, kwa madhumuni ya kumpatia yeye binafsi au mtu mwingine yeyote manufaa ya kiuchumi.
Matumizi ya masharti ya maadili kwa Watumishi wa Umma
19. Masharti yaliyoainishwa katika Ibara za 13 mpaka 18 yatatumika pia kwa watumishi wa umma baada ya kufanyiwa marekebisho stahiki.
SEHEMU YA PILI
MIIKO YA UONGOZI WA UMMA
Utii wa Miiko ya Uongozi wa Umma
20.-(1) Bila ya kuathiri masharti yoyote ya Katiba hii, kiongozi yeyote wa Umma atapaswa kuheshimu na  kutii maadili ya viongozi wa umma, ikiwemo Miiko ya Uongozi.
(2) Miiko ya Uongozi inayorejewa katika Ibara ndogo (1), itakuwa kama ifuatavyo:
(a) Kiongozi wa umma hatopaswa:
(i) kuvunja au kukiuka masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano;
(ii) kutoa au kupokea rushwa;
(iii) kujilimbikizia mali kinyume cha sheria;
(iv) kusema uongo au kutoa taarifa zisizo za ukweli;
(v) kutoa siri za Serikali kinyume na sheria;
(vi) kutumia wadhifa, nafasi au cheo chake kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa au marafiki zake au mtu yeyote aliye na uhusiano naye wa karibu;
(vii) kufanya vitendo vya uzembe, uvivu, ubaguzi, kiburi, dharau au unyanyasaji wa kijinsia.
(b) Kiongozi wa umma atapaswa:
(i) kuheshimu na kuendeleza dhana ya uwajibikaji wa pamoja, kwa viongozi wanaohusika; na
(ii) kuheshimu na kuendeleza maadili ya viongozi wa umma, ikijumuisha:
(aa) kuwa na tabia na mienendo inayokubalika katika jamii;
(bb) kuheshimu, kutunza na kulinda mali za umma; na
(cc) kutambua, kuheshimu na kuzingatia Kanuni za Maadili na Mienendo ya Watumishi wa Umma, Kanuni za Kudumu za Watumishi wa Umma, nyaraka za umma na miongozo mbalimbali ya Serikali kuhusu viongozi na watumishi wa umma.
(iii) kutenganisha shughuli za biashara na masuala yanayohusiana na uongozi.
(3) Kiongozi yeyote wa umma ambaye anatuhumiwa na kuthibitika kwa makosa ya:
(a) kimaadili;
(b) udhalilishaji wa mtu au wa kijinsia; na
(c) wizi au ubadhirifu wa mali za umma,  atasimamishwa kazi mpaka suala lake litakapoamuliwa kwa mujibu wa sheria au taratibu nyingine zinazowahusu viongozi wa umma.
Marufuku baadhi ya vitendo
21.-(1) Mtumishi wa umma aliye katika ajira ya kudumu hataruhusiwa kuingia katika ajira nyingine yoyote yenye malipo ya mshahara.
(2) Mtumishi wa umma haruhusiwi kuchaguliwa au kuteuliwa kushika madaraka katika chama cha siasa.
(3) Mtumishi wa umma aliyestaafu na anayepokea malipo ya pensheni kutokana na fedha za umma haruhusiwi kuwa mwenyekiti, mkurugenzi au mtumishi zaidi ya vipindi viwili katika:
(a) shirika au kampuni inayomilikiwa au kuendeshwa kwa fedha za umma; au
(b) chombo chochote cha umma.
SURA YA NNE
HAKI ZA BINADAMU, WAJIBU WA RAIA NA MAMLAKA ZA NCHI
SEHEMU YA KWANZA
HAKI ZA BINADAMU
Uhuru, utu na usawa wa binadamu
22.-(1) Binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa.
(2) Kila mtu anayo haki ya kuheshimiwa, kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Haki ya kuishi
23. Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kutoka katika Serikali na jamii kwa mujibu wa sheria.
Marufuku kuhusu ubaguzi
24.-(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki ya kulindwa na kupata haki sawa mbele ya  sheria.
(2) Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu, mamlaka ya nchi au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika kutekeleza kazi au shughuli yoyote ya mamlaka ya nchi.
(3) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.
(4) Haki ya raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya mamlaka ya nchi vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.
(5) Kwa madhumuni ya masharti ya Ibara hii na kwa kuzingatia masharti ya Ibara ndogo ya (4), neno “kubagua” maana yake ni kutimiza utashi, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, kabila, mahala walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsi au hali yao ya maisha kwa namna ambayo watu wa aina fulani wanafanywa au kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya vipingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima.
(6) Neno “kubagua” lilivyotumiwa katika Ibara ndogo ya (2), halitafafanuliwa kwa namna ambayo itaizuia mamlaka ya nchi kuchukua hatua za makusudi zenye lengo la kurekebisha matatizo mahsusi katika jamii.
(7) Kwa madhumuni ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria, mamlaka ya nchi itaweka utaratibu unaofaa na unaozingatia misingi kwamba -
(a) wakati haki na wajibu kwa mtu yeyote vinapohitajika kufanyiwa uamuzi na mahakama au mamlaka nyingine inayohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia atakuwa na haki ya kukata rufani au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na uamuzi wa mahakama au mamlaka nyingine inayohusika;
(b) ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu aliyehukumiwa kwa kutenda kosa hilo hadi itakapothibitika mahakamani kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo;
(c) ni marufuku kwa mtu kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chochote ambacho wakati alipotenda kitendo hicho hakikuwa ni kosa chini ya sheria;
(d) ni marufuku kwa mtu kupewa adhabu ambayo ni kubwa kuliko adhabu iliyokuwapo wakati kosa linalohusika lilipotendeka;
(e) kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu na faragha itahifadhiwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi wa tuhuma na uendeshaji wa masharti ya jinai na katika shughuli  nyingine ambazo mtu anakuwa katika kizuizi cha mamlaka ya nchi au katika kuhakikisha utekelezaji wa adhabu; na
(f) ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazotweza au kudhalilisha.
Haki ya kutokuwa mtumwa
25.-(1) Kila mtu ana haki ya kutotendewa au kutotumikishwa kama mtumwa, kutofanyishwa kazi za kulazimishwa au kutweza, na kwa msingi huo, ni marufuku kwa mtu:
(a) kufanywa au kutendewa kama mtumwa;
(b) kulazimishwa kufanya kazi bila hiyari yake; au
(c) kusafirishwa kwa nia ya kufanyiwa biashara au faida ya mtu mwingine.
(2) Biashara ya kusafirisha binadamu ni marufuku katika Jamhuri ya Muungano.
Uhuru wa mtu binafsi
26.-(1) Kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi akiwa mtu huru.
(2) Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake vinginevyo, isipokuwa tu katika-
(a) hali na kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria; au
(b) kutekeleza hukumu, amri au adhabu iliyotolewa na mahakama kutokana na shauri au kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.
Haki ya faragha na usalama wa mtu
27.-(1) Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na nyumbani kwake, kutoteswa au kudhalilishwa, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi.
(2) Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu, mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria kuhusu hali, namna na kiasi ambacho haki ya mtu ya faragha na ya usalama wa nafsi yake, mali na maskani yake, yanaweza kuingiliwa bila ya kuathiri masharti ya Ibara hii.
Uhuru wa mtu kwenda anakotaka
28.-(1) Kila raia anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa, kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(2) Kitendo chochote halali au sheria yoyote yenye madhumuni ya -
(a) kupunguza uhuru wa mtu kwenda anakotaka na kumweka chini ya ulinzi au kifungoni; au
(b) kuweka mipaka kwa matumizi ya uhuru wa mtu kwenda anakotaka ili-
(i) kutekeleza hukumu au amri ya mahakama;
(ii) kumlazimisha kutimiza kwanza wajibu wowote anaotakiwa na sheria nyingine kuutimiza; au
(iii) kulinda manufaa ya umma kwa jumla au kuhifadhi maslahi fulani mahsusi au maslahi ya sehemu fulani ya umma, hakitahesabiwa au sheria hiyo haitahesabiwa kuwa ni kinyume cha masharti ya Ibara hii.
Uhuru wa maoni
29.-(1) Kila mtu:
(a) anao uhuru wa-
(i) kuwa na maoni na kueleza fikra zake; (ii) kufanya mawasiliano na vile vile anayo haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake; (iii) ubunifu na sanaa; (iv) kitaaluma na tafiti za kisayansi; na
(b) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu:
(i) matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi; na
(ii) utekelezaji wa mamlaka ya nchi kuhusu sera za kitaifa na shughuli ya maendeleo ya jamii; na
(iii) masuala mengine muhimu kwa jamii.
(2) Utekelezaji wa haki zilizoainishwa katika Ibara ndogo ya (1), utajumuisha wajibu muhimu kwa mwananchi na wajibu huo unaweza kupunguza haki hizo kutokana na:
(a) vita au machafuko ya kisiasa; au
(b) propaganda kuhusu vita, ushawishi wa chuki kwa misingi ya rangi, ukabila, ubaguzi wa kijinsia, dini au masuala yoyote yanayoweza kuleta madhara kwa Taifa.
Uhuru wa habari na vyombo vya habari
30.-(1) Kila mtu anao uhuru wa-
(a) kutafuta, kupata na kutumia habari na taarifa na kusambaza taarifa hizo; na
(b) kuanzisha vyombo vya habari na njia nyingine za upashanaji wa habari bila kujali mipaka ya nchi.
(2) Vyombo vya habari vitakuwa huru na vile vile vitakuwa na:
(a) haki ya kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa wanazopata;
(b) wajibu wa:
(i) kusambaza habari na taarifa kwa wananchi; na
(ii) kuheshimu na kulinda utu, heshima, uhuru na staha ya wananchi dhidi ya habari na taarifa wanazozitumia, wanazozitayarisha na kuzisambaza.
(3) Serikali na taasisi zake, asasi za kiraia na watu binafsi watakuwa na wajibu wa kutoa habari kwa umma juu ya shughuli na utekelezaji wa shughuli zao.
(4) Masharti ya Ibara hii yatalazimika kuzingatia masharti ya sheria ya nchi itakayotungwa kwa ajili hiyo na kwa madhumuni ya kulinda usalama wa Taifa, amani, maadili ya umma, haki, staha na uhuru wa watu wengine.
Uhuru wa imani ya dini
31.-(1) Kila mtu anao uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya imani ya dini na anao huru pia wa kubadilisha dini, imani yake au kutokuwa na imani na dini.
(2) Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari kwa mtu binafsi ili mradi asivunje sheria za nchi.
(3) Shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini itakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya Serikali.
(4) Hifadhi ya haki zilizotajwa katika Ibara hii itakuwa chini ya taratibu zilizowekwa na sheria ambazo ni muhimu katika jamii ya kidemokrasia kwa ajili ya usalama, amani, maadili na umoja wa jamii na wa kitaifa na vitasimamiwa kwa utaratibu ulioainishwa kwenye sheria za nchi.
(5) Ni marufuku kwa mtu, kikundi au taasisi ya dini kutumia uhuru wa kutangaza dini kwa kukashifu imani na dini nyingine, kujenga chuki au kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya kutetea imani au dini.
(6) Dini na imani ya dini haitatumika kwa namna yoyote itakayowagawa wananchi, kuleta uhasama au kuharibu amani miongoni mwa wananchi.
(7) Neno “dini” kama lilivyotumika katika Ibara hii litatafsiriwa kwamba maana yake ni pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengine yanayofanana au kuambatana na neno hilo nayo yatatafsiriwa kwa maana hiyo.
Uhuru wa mtu kujumuika na kushirikiana na wengine
32.Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kujumuika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.
Uhuru wa kushiriki shughuli za umma
33.-(1) Kila raia wa Jamhuri ya Muungano ana haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
(2) Kila raia ana haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa.
Haki ya kufanya kazi
34.-(1) Kila mtu ana haki ya kufanya kazi ya kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe.
(2) Kila mtu ana haki na fursa sawa kushika nafasi yoyote ya kazi, uongozi au shughuli yoyote iliyo chini ya mamlaka ya nchi.
Haki za wafanyakazi na waajiri
35.-(1) Kila mfanyakazi ana haki zifuatazo:
(a) kufanya kazi bila ubaguzi wa aina yoyote;
(b) kupata ujira na malipo halali kulingana na kiasi na sifa za kazi anayofanya;
(c) kuunda au kujiunga na chama cha wafanyakazi mahala pa kazi; na
(d) kushiriki katika shughuli za chama cha wafanyakazi;
(2) Kila chama cha waajiri na wafanyakazikitakuwa na haki ya:
(a) kuamua kuhusu uongozi, programu na shughuli zake; na
(b) kuanzisha, kujiunga na kusimamia shirikisho lao.
(3) Kila chama cha wafanyakazikitakuwa na haki ya kufanya majadiliano ya pamoja na mwajiri na kuingia mikataba ya hali bora ya kazi.
(4) Bunge litatunga sheria itakayoweka masharti kuhusu haki za wafanyakazi na utaratibu utakaowezesha wafanyakazi kutumia haki zao.
Haki ya kumiliki mali
36.-(1) Kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na hifadhi ya mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengine bila malipo yanayolingana na thamani halisi ya mali hiyo na yatakayotolewa mapema.
(3) Kwa madhumuni ya masharti ya Ibara hii, haki ya umiliki na hifadhi ya mali haitahusu mali iliyothibitishwa kwamba haikupatikana kwa njia halali.
Haki ya uraia
37. Kila raia ana haki ya kutambuliwa uraia wake na kwa madhumuni haya, mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha wananchi kupata hati ya kuzaliwa, kitambulisho cha uraia wake bila ya upendeleo na ubaguzi wa aina yoyote, na pale inapohitajika, nyaraka za kumwezesha kusafiri.
Haki ya mtuhumiwa na mfungwa
38.-(1) Mtu aliyekamatwa au aliyewekwa kizuizini anayo haki ya:
(a) kuelezwa kwa lugha anayoifahamu -
(i) sababu ya kukamatwa;
(ii) haki ya kutokutoa maelezo yoyote; na
(iii) matokeo ya kutoa maelezo;
(b)kutoa maelezo;
(c) kuwasiliana na wakili na mtu mwingine ambaye msaada wake ni muhimu kwa mtuhumiwa;
(d) kutolazimishwa kutoa maelezo ya kukiri kosa ambayo yatatumika kama ushahidi dhidi yake; na
(e) kupelekwa mahakamani mapema iwezekanavyo.
(2) Mamlaka za nchi zitaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha:
(a) mtuhumiwa kupata nakala ya mashtaka yanayomkabili na kumbukumbu ya mwenendo wa mashtaka;
(b) mtuhumiwa au mfungwa kupata nakala ya mwenendo wa mashtaka baada ya shauri kukamilika mahakamani;
(c) mtuhumiwa au mfungwa kufikishwa mahakamani ili kuthibitisha uwepo wake.
Haki ya watu waliyo chini ya ulinzi
39.-(1) Mtu aliye katika kizuizi au ulinzi ataendelea kuwa na haki zote za msingi zilizoainishwa katika Katiba hii kwa kiwango anachostahiki katika mazingira ya kuwekwa kizuizini au katika ulinzi.
(2) Mtu aliye katika kizuizi au ulinzi ana haki ya kuiomba mahakama ili mamlaka ya nchi inayomuhifadhi kueleza sababu za yeye kuwekwa au kuendelea kuwa katika kizuizi au ulinzi.
(3) Raia wa Jamhuri ya Muungano hatapelekwa katikanchi ya nje yoyote kujibu mashtaka au kufanyiwa mahojiano ya aina yoyote kinyume cha ridhaa yake.
Uhuru na haki ya mazingira safi na salama
40.-(1) Kila mtu anayeishi katika Jamhuri ya Muungano ana haki ya kuishi katika mazingira safi, salama na ya kiafya.
(2) Haki ya kuishi katika mazingira safi, salama na ya kiafya inahusisha haki kwa kila raia kutumia maeneo ya umma au sehemu mbalimbali za mazingira yaliyotengwa kwa madhumuni ya burudani, elimu, afya, ibada, utamaduni na shughuli za kiuchumi.
(3) Mtu yeyote anayeishi Tanzania anao wajibu wa kutunza na kuendeleza mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka za nchi kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo ni hatarishi au linauwezekano mkubwa wa kuharibu au kuathiri mazingira.
Haki ya elimu na kujifunza
41.-(1) Kila mtu ana haki ya:
(a) kupata fursa ya kupata elimu bila ya vikwazo;
(b) kupata elimu bora ya msingibila ya malipo na inayomtayarisha kikamilifu mwanafunzi ama kuendelea na elimu ya ngazi inayofuatia au kuweka msingi wa kuanza kujitegemea;
(c) kwa elimu inayotolewa nje ya utaratibu wa umma, kupata elimu kwa gharama nafuu; na
(d) kupata fursa sawa ya kupata elimu ya juu ili mradi ana sifa stahiki kupata elimu hiyo, bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
(2) Kwa madhumuni ya Ibara ndogo ya (1), kila mtu ana haki ya kuchagua taaluma na ajira anayoitaka kwa mujibu wa elimu yake na ujuzi aliyonao.
Haki ya mtoto
42.-(1) Kila mtoto ana haki ya-
(a) kupewa jina na uraia;
(b) kutoa mawazo, kusikilizwa na kulindwa dhidi ya uonevu, ukatili na udhalilishaji;
(c) kucheza na kupata elimu;
(d) kuhifadhiwa katika mazingira mazuri, kwa walio katika ukinzani na sheria;
(e) kupata lishe bora, makazi na huduma ya afya; na
(f) kushiriki katika shughuli zinazolingana na umri alionao; na
(g) kupata malezi na ulinzi wa wazazi, walezi au mamlaka ya nchi, bila ya ubaguzi wa rangi, utaifa, lugha, mtazamo wa kisiasa, jamii anayotokea, mali, uzazi, kabila, dini, jinsi au aina nyingine za hadhi.
(2) Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha utekelezaji na usimamizi wa haki za mtoto kwa kufuata msingi wa kutoa kipaumbele kwa maslahi na manufaa ya mtoto.
Haki na wajibu wa vijana
43. Kila kijana ana haki na wajibu wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Jamhuri ya Muungano pamoja na jamii kwa ujumla, na kwa mantiki hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali za Washirika wa Muungano na jamii zitahakikisha kuwa vijana wanawekewa mazingira mazuri ya kuwa raia wema na kupatiwa fursa za kushiriki kikamilifu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi,kijamii na kiutamaduni.
Haki za watu wenye ulemavu
44.-(1) Mtu mwenye ulemavu anastahiki:
(a) kuheshimiwa, kutambuliwa na kutendewa kwa namna ambayo haishushi utu wake;
(b) kupata elimu kwa kutumia vifaa maalum na kushiriki katika shughuli za kijamii;
(c) kuwekewa miundombinu na mazingira yatakayowezesha kwenda anapotaka, kutumia vyombo vya usafiri na kupata habari;
(d) kutumia lugha za alama, maandishi ya nukta nundu au njia nyingine zinazofaa;
(e) haki ya kusoma na kuchanganyika na watu wengine; na
(f) haki ya kupata ajira na kugombea nafasi za uongozi katika nyadhifa mbalimbali kwa usawa.
(2) Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha watu wenye ulemavu kushiriki katika nafasi za uwakilishi.
Haki za makundi madogo katika jamii
45.-(1) Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha makundi madogo katika jamii:
(a) kushiriki katika uongozi wa mamlaka za nchi;
(b) yanapewa fursa maalum za elimu na fursa za kujiendeleza kiuchumi na fursa za ajira;na
(c) kutengewa maeneo ya ardhi ambayo kwa desturi makundi hayo kuitumuia kama eneo la kuishi na kupata riziki ya chakula.
(2) Serikali na mamlaka za nchi zitachukua hatua za makusudi za kukuza na kuendeleza shughuli za kiuchumi na kuweka miundombinu ya makazi, elimu na afya kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo vya jamii ya watu walio katika makundi madogo.
Haki za wanawake
46.-(1) Kila mwanamke ana haki ya:
(a) kuheshimiwa utu wake;
(b) kuwa salama dhidi ya unyonyaji na ukatili;
(c) kushiriki bila ya ubaguzi katika chaguzi na ngazi zote za maamuzi;
(d) kupata ujira sawa na mwanaume katika kazi;
(e) kulindwa dhidi ya ubaguzi, uonevu na mila zenye madhara;
(f) kulindwa kwa ajira yake wakati wa ujauzito na pale anapojifungua; na
(g) kupata huduma ya juu ya afya inayopatikana.
(2) Mamlaka husika za nchi zitaweka utaratibu wa kisheria utakaosimamia masuala yanayohusu utekelezaji wa masharti ya Ibara hii ikiwa ni pamoja na kukuza utu, usalama na fursa za wanawake wakiwemo wajane.
Haki za wazee
47. Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu utakaowezesha wazee kupata fursa ya:
(a) kushiriki katika shughuli za kijamii;
(b) kuendeleza maisha yao;
(c) kutambuliwa utu wao na kuheshimiwa pasipo kudharauliwa;
(d) kulelewa na kupata misaada kutoka katika familia zao jamii na mamlaka ya nchi; na
(e) kupewa fursa ya kuendelea kutumia utaalamu na ujuzi wao kwa faida na manufaa ya jamii. 

No comments: