Wednesday, January 9, 2013

DAKIKA 45, ZA VIONGOZI WA VYAMA VYA UPINZANI MBELE YA JESHI LA POLISI


Story ya Idrisa Bandali
VIONGOZI wa Umoja wa Vyama vya Siasa mkoani Mtwara leo wamehojiwa na polisi kwa dakika 45 kabla ya kuachiwa huru, huku habari za ndani ya mahojiano hayo zikidai kuwa ziara ya Rais Jakaya Kikwete inayotarajia kufanyika mkoani hapa hivi karibuni ndiyo iliyosababisha kuhojiwa kwao.
Habari zilizoifikia Migongo Blog zinadai kuwa Rais Kikwete anatarajia kufanya ziara mkoani Mtwara hivi karibuni, hata hivyo kumekuwapo na hofu ya usalama wa kiongozi huyo kutokana na wananchi kupinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Msimbati hadi Dare s Salaam unaotekelezwa na serikali yake.
Habari za kuhojiwa kwa viongozi hao Tisa na jeshi la Polisi wilaya ya Mtwara zilisambaa haraka ndani na nje ya mji wa Mtwara hali iliyozua hofu kwa wananchi hata hivyo mda mfupi baadaye taarifa za kuachiwa zilienea.
“Ni kweli tuliitwa polisi majira ya saa 5 asubuhi…tulikuwa tunabadilishana mawazo… tulikutana na OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) wanasema kauli tulizotoa katika mikutano yetu ya mwisho zinatishia amani, kauli ambazo zinachochea, wanasema ile mikutano ya mwanzo ilikuwa na kauli zuri ila sasa kauli zimekuwa kali” alisema Mustafa Nchia mwenyekiti wa Chadema ambaye ni mmoja wa viongozi aliyekuwapo katika kikao hicho.
Alibainisha kuwa “Tuliulizwa je akifika Rais anaweza kuongea na wananchi na hali ikawa shwari? … tulimthibitishia kuwa hali itakuwa ya amani…hata akitaka kuzungumza wananchi wa mkoa wa Mtwara watakuja kwa kujitegemea na hali itakuwa shwari..aje rais tumweleze sisi tunataka mitambo ya kufua umeme ijengwe Mtwara”
Alisema viongozi hao katika mazungumzo yao walimweleza mkuu huyo wa polisi wilaya kuwa hasira za wananchi zinachagizwa na kauli za kejeli zinazotolewa na viongozi wandamizi wa serikali akiwemo waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhngo.
“Ni kweli tuliwaita tukazungumza nao
saa 6 mchana, ilikuwa ni sehemu ya kazi zetu za kawaida…hatukuwakamata…tulizungumza nao baada ya mazungumzo waliondoka, hakuna kesi iliyofunguliwa…wananchi waondoe hofu” alisema Tuntufye Mwakagamba mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mtwara hata hivyo hakueleza mazungumzo yalihusu nini

No comments: