Monday, July 9, 2012

MADAKTARI WALIOGOMA POSHO ZAO ZASITISHWA...

Wizara imepokea malalamiko kuwa kati ya tarehe 23 juni, 2012 hadi  tarehe  29 juni, 2012, Madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo  372 kati ya 763 katika hospitali mbalimbali nchini, waligoma kutoa huduma kwa wagonjwa ikiwa ni wajibu wao  kama madaktari.

Kitendo hicho sio tu kilihatarisha usalama wa wagonjwa waliohitaji huduma za matibabu katika hospitali hizo, bali kilikuwa ni ukiukwaji wa maadili ya taaluma.

Madaktari hao waliogoma walirejeshwa Wizarani kwa barua kutoka kwenye mamlaka za hospitali walikokuwa wakifanyia mafunzo kwa vitendo.

Kwa kuwa Wizara ndio yenye dhamana ya usimamizi wa huduma za afya nchini, na kwa kuwa madaktari hao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika, hivyo Wizara imewasilisha malalamiko haya huko ili Baraza liwachunguze na kuamua hatma yao kitaaluma.

Kwa hivi sasa madaktari hao hawako maeneo yao ya kazi, na suala hili limepelekwa Baraza la Madaktari kwa uchunguzi kuhusu kitendo walichokifanya, hivyo Wizara inasitisha posho zao kuanzia Tarehe 1 Julai, 2012 hadi hapo itakapopata taarifa ya uchunguzi wa Baraza la Madaktari.

Madaktari wengine waliogoma, taratibu za kiutumishi zitachukuliwa na mamlaka ya ajira zao kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

Regina L. Kikuli
KAIMU KATIBU MKUU


Source: http://www.wavuti.com

No comments: