Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) unafuraha kuwatangazia kuwa huduma za safari za abiria kwenda Kigoma zitaanzia tena Dar es Salaam hapo Jumanne Mei 22, 2012 badala ya Dodoma. Itakumbukwa kuanzia Januari 24, 2012 huduma za usafiri wa abiria ilibidi zihamishiwe Dodoma baada ya eneo kati ya Stesheni za Godegode na Gulwe za reli ya kati ( mkoani Dodoma) kukumbwa na mafuriko makubwa.
Hata hivyo mamlaka iliyokuwa inafanya ukarabati sehemu hiyo imeithibitishia TRL kuwa eneo hilo sasa liko imara kwa safari za treni za abiria.
Kwa mujibu taarifa rasmi za TRL kuanzia Jumanne ijayo usafiri wa abiria utakuwa mara mbili kwa wiki na utakuwa katika siku za Jumanne na Ijumaa kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma ambapo treni zitaondoka saa 11 jioni. Aidha kutoka Kigoma kuja Dar safari zitakuwa kwa siku za Alhamis na Jumapili treni itaondoka Stesheni ya Kigoma saa 12 jioni.
Taarifa imefafanua kuwa hakuna mabadiliko kwa safari ya treni ya abiria iliyopangwa kuondoka siku ya Jumapili Mei 20, 2012 kutoka Dodoma kwenda Kigoma saa 1 usiku, isipokuwa wakati wa kurejea itasafiri moja kwa moja hadi Dar es Salaam ili kukidhi matakwa ya ratiba mpya inayoanza Jumanne Mei 22 na Ijumaa Mei 25, 2012.
Halikadhalika Uongozi unawahimiza wananchi wanaotaka kusafiri kuanzia Dar es Salaam kwenda Kigoma wafike katika Stesheni zilizo karibu nao kwa kupata maelezo ya safari husika na kukata tiketi wanazohitaji.
Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi K.A.M Kisamfu
Imesainiwa na:
MIDLADJY MAEZ
MENEJA UHUSIANO- TRL
MEI 16, 2012
No comments:
Post a Comment