Kwa muda mrefu kumekuwa na shinikizo kutoka kwa watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wanaharakati na wanasheria wanaotaka kuwepo kwa mgombea binafsi jambo ambalo pia kiliwahi kupigiwa debe na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mnamo mwaka 1995.
Mwalimu aliwahi kusema: “Mimi nadhani sheria imekosea kuzuia wagombea binafsi. Hili jambo limekosewa ni la msingi. Ndiyo maana napenda kulisema ni la msingi, linahusu haki yangu na yako ya kupiga kura na kupigiwa kura. Hii ni haki ya uraia.”
Jana, katika kikao cha semina ya viongozi ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM, Kamati iliyoundwa na chama hicho kuangalia jinsi kinavyoweza kuwasilisha maoni yake katika Tume ya Katiba, ilitaka wanachama kujiandaa kwa suala hilo.
Suala la mgombea binafsi limekuwa likipingwa na chama hicho kwa muda mrefu kwa hofu kuwa lingeweza kukiumiza pindi wanachama wake wanaposhindwa kura za maoni, kwani wangeweza kusimama binafsi na kushinda.
Lakini, kamati hiyo ambayo iliongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Abdulrahman Kinana, jana ilitoa mapendekezo mbalimbali ikiwamo muundo wa Muungano huku ikiwataka wanaCCM kujiandaa kukabiliana na mgombea huyo binafsi. (Source Mwananchi)
No comments:
Post a Comment