Wednesday, April 25, 2012

SMZ yakanusha kuzuia Jumuiya za kidini kuliombea taifa katika mkesha wa maadhimisho ya miaka 48 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Idara ya Habari - MAELEZO,Zanzibar.


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema haijazuia Jumuiya za kidini kuomba dua kuombea nchi katika mkesha wa maadhimisho ya miaka 48 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini hapa jana,Waziri wa Katiba na sheria, Abubakar Khamis Bakar amesema kimsingi Serikali imekubaliana na suala zima la dua kwani ni jambo zuri.

Matamshi ya Serikali yamekuja baada ya kuwepo uvumi kwamba huenda kisomo cha Jumuiya za kidini kilichopangwa kufanyika jana kisingefanyika au kingeambatana na maandamano.

“Serikali haijazuia dua,isipokuwa tulipata wasi wasi baada ya kupata ujumbe mfupi wa simu kwamba watu wanahamasishwa kushiriki maandamano…mimi nimepata meseji hiyo” Alisema Waziri Abubakar.

Waziri Abubakar alisema suala la umoja na amani ni jambo muhimu sana hivyo ni wajibu wa wananchi wote kuhakikisha wanadumisha kwa vitendo mambo hayo.

Katika mkutano huo, Waziri huyo aliwakumbusha wananchi kujiandaa kutoa maoni yao wakati Tume ya Katiba itakapoanza kazi,lakini akasisitiza ulazima wa kufuata sheria na taratibu.

“Tunawakumbusha kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yenu, kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake namna anavyotaka iwe katiba mpya na hii ni fursa pekee kwa wananchi” Alisisitiza Waziri huyo.

Katika hatua nyengine, Serikali imeviomba vyombo vya habari kufuata na kuzingatia maadili ya Tasnia hiyo hasa wakati huu ambao Tanzania inatarajia kuingia katika mchakato wa katiba mpya.

Mkutano huo awali, ulitanguliwa na kikao baina ya Serikali,viongozi wa dini uliokuwa chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Katiba na Sheria. Mawaziri wengine waliohudhuria ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Mohammed Aboud Mohammed na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Mwinyihaji Makame Mwadini.

No comments: