Sunday, April 22, 2012

MAWAZIRI KUJIUZULU KESHO ? .. Wengine wanataka kugoma..yumo wa viwanda

WAKATI kishindo cha shinikizo la kutakiwa kujiuzulu mawaziri nane wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kikizidi kurindima, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali itatoa tamko lake rasmi kesho.

Awali Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenister Mhagama aliwaambia waandishi wa habari juzi usiku kuwa chama hicho kimefanya maamuzi magumu ambayo yangetangazwa na Pinda mjini hapa jana.


Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda alipoombwa na waandishi wa habari jana kuzungumzia sakata hilo, hakukanusha wala kukiri kuwapo kwa azimio hilo zaidi ya kusema wananchi wasubiri hadi kesho atakapotoa taarifa rasmi.

Alipoulizwa kama kuna mawaziri ambao wameshawasilisha barua zao za kujiuzulu hadi kufikia jana mchana, Pinda alijibu kwa kifupi kuwa ‘bado hatujapokea, lakini kama wapo watatuletea tu”.

Ingawa Waziri Mkuu hakukiri kupokea barua yoyote, taarifa zisizo rasmi, zilisema mawaziri watano waliokumbwa na msukosuko huo wamekabidhi barua zao huku Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami akikataa kufanya hivyo.

Mwingine ambaye anatajwa kuwa hajawasilisha barua yake, ni Waziri wa Fedha Mustapha Mkulo ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi.

Chami ajitetea

Dk. Cyril Chami amesema hataandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo na kusema anawaachia wananchi wapime kama kweli anastahili kujiuzulu ama la.

SOURCE : Mwananchi


No comments: