Sunday, April 22, 2012

CUF na HADITHI YA MBILIKIMO (Sehemu ya Pili)

                                                               ·     Kwanini wanakataa maumbile yao?
Na Rashid Mtagaluka
BAADA ya kuangalia matokeo ya kura za uras za jumla katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na 2010, na kugundua jinsi CUF inavyoporomoka, juma hili niliahidi kugeukia majimboni na hasa Dar es Salaam.

Hata hivyo niwashukuru wasomaji wangu walionipigia simu na baadhi kunitumia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yangu ya kiganjani (Sms).


Pamoja na lugha chafu kutamalaki katika sms hizo, lakini pia nikiri kwamba wapo waliojaribu kutoa kauli za kuunga mkono makala haya, na hasa kwa kitendo cha baadhi ya vyama kutokubali kujitazama na hatimaye kujihakiki.

Yote kwa yote, nimeahaidi kuijbu ama niseme kutoa ufafanuzi kuhusiana na madai mbalimbali ya wasomaji hao katika sehemu ya tatu na ya mwisho ya muendelezo wa uchambuzi huu juma lijalo Mwenyezimungu akitujaalia.

Katika makala yangu yaliyopita nilieleza namna Mbilikimo alivyo mkali anapoambiwa ‘live’ kuwa yeye ni mfupi, hapendi na lazima mtakunjana mashati.

Bali pamoja na ufupi wake, anajisikia raha kwelikweli Mbilikimo akiitwa ‘tall’ yaani mrefu, ingawa si kweli!.

Yote kwa yote pamoja na propaganda za kukusanya watu kutoka maeneo mbalimbali ya jiji na mikoa ya jirani katika mapokezi ya Profesa Lipumba kwa lengo la kuwaonesha wanaodai CUF imekufa, kwamba haijafa, bado huwezi kupingana na ushahidi wa kitakwimu. Labda mtu ajifanye mwendawazimu ama Mbilikimo anayekana maumbile yake!

Wapembuzi wa mambo ya siasa watakosaje kuiona CUF imepoteza muelekeo wakati matokeo ya urais mwaka 2005 jimbo la Temeke mgombea wake Profesa Lipumba alijizolea kura 51,599 sawa na asilimia 29.05 wakati ambapo mwaka 2010 aliambulia kura 22,632 tu sawa na asilimia 18.88?

Wakati ambapo Chadema iliyowakilishwa na mgombea wake Freeman Aikael Mbowe 2005 Temeke ilipata kura 6,205 sawa na asilimia 3.3 tu, mwaka 2010 ilipanda na kupata kura 32,836 ikiwa ni sawa na asilimia 27.04 chini ya mgombea wake Dk Willbroad Petro Slaa.

Kana kwamba haitoshi, CUF kupitia aliyekuwa mgombea wake wa ubunge mwaka 2005 Richard Hiza Tambwe kupata kura 47,448 sawa na asilimia 27.5, mwaka 2010 japo ndiyo jimbo pekee mkoa wa Dar es Salaam kushika nafasi ya pili, bado ilishuka kwa kuambulia kura 28,877 sawa na asilimia 23.86.

Ukenda jimbo la Kigamboni mwaka 2005 ambapo CUF ilimsimamisha Athuman Mbwana Bawji utakuta ilishika nafasi ya pili nyuma ya mgombea wa CCM Mwinchumu Msomi kwa kuwa na kura 45,671 sawa na asilimia 35, ikiiacha Chadema mbaali kwa kura 3,497 chini ya mgombea wake Dayness Samwel Mosha.

CUF iliyokamata nafasi ya pili kwenye matokeo ya mwaka huo, ilijkuta inashika nafasi ya tatu mwaka 2010 bila kupenda pale ilipoambulia kura 24,419 sawa na asilimia 22.09, nyuma ya Chadema iliyoshika nafasi ya pili kwa kuwa na kura 25,166 sawa na asilimia 23.6.

CUF kama kawaida mgombea anayepata kura nyingi jimboni hawamtaki tena, na kwa namna moja ama nyingine mwenyewe anamwaga manyanga.

Mwaka 2010 haikumsimamisha Mbwana kwa kuwa alishatimkia CCM, badala yake alisimama Mustafa Ismail, kama ilivyokuwa jimbo la Temeke ambapo Tambwe alihamia CCM na Kadawi Lucas Limbu aliyerithi mikoba yake Temeke mwaka 2010 kesha hama na kuanzisha chama cha siasa cha Alliance for Democratic Change (ADC).

Takriban wagombea wengi wa CUF wakimaliza uchaguzi mmoja sirahisi kurudia kugombea tena kabla ya kuhama chama hicho au kutupwa na chama chenyewe nahii zaidi ni kwa Tanzania bara ! majina na takuwimu zao tunazo

Katika sura hiyo nadhani ni Mbilikimo tu ndiye atakayeendelea kunga’anga’nia madai kwamba CUF bado ingali ngangari! Vinginevyo ni kutaka kuwaadaa Wanachama wao.

Ubungo kule CUF bado inahitaji kufanya jitihada za makusudi katika kujiimarisha, kwani matokeo ya chaguzi zote yanaonesha inakamata nafasi ya tatu.

Ispokuwa jambo moja hapa liko wazi, kwamba kama CUF haifi basi wagombea inaowaweka katika baadhi ya majimbo hawauziki kwa wapiga kura.

Mfano mwaka 2005 CUF ilimsimamisha marehemu Justina Melchior Minja kuwa mgombea wake na kupata kura 28,412 sawa na asilimia 15.7 nyuma ya John John Mnyika wa Chadema.

Ambapo mwaka 2010 CUF ilimsimamisha Sanday Charles Julius Mtatiro aliyeambulia kura 12,964 sawa na asilimia 9.63 ya kura zote zilizopigwa na kujikuta ikishika nafasi ya tatu.

Baada ya hapo twende Kawe, ambako mwaka 2005 Salim Omar Mandari (CUF) alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 16,449 sawa na asilimia 16.2 akiwa nyuma ya Deogratias Francis Mushi (Chadema) aliyepata kura 17,073 sawa na asilimia 16.8.

Badala ya kuweka mikakati ya kupanda kama ambavyo vyama vingine vinavyofanya, CUF wanawekeza katika mapokezi makubwa ya viongozi wao ili kuonesha kuwa mziki wao ni mnene!

Na kweli mwaka 2010 ikiwa imemsimamisha Shaaban Salim Mapeyo, CUF ikajikuta ikiangukia pua kwa kutupwa nafasi ya nne nyuma ya NCCR-Mageuzi ikiwa imepata kura 9,121 sawa na asilimia 9.08.

Katika anguko kama hili la kutoka kura 16,449 mpaka kura 9,121 bado wanataka wasionekane wanakufa, bali waitwe wako hai, kuna tofauti gani na Mbilikimo wa Brazavill anayelazimisha aonekane mrefu?

Jimbo jingine lenye vichekesho ni la Kinodoni kwa Idd Mohamed Azzan ambako mwaka 2005 Chadema kupitia kwa mgombea wake Hassan Yahaya Hussein ilishika nafasi ya tatu nyuma ya CUF kwa kuambulia kura 7,267 tu sawa na asilimia 5.2.

Wanangangari kinoma wao kupitia mgombea wao Hamis Hassan Makapa (sasa ni mkurugenzi wa Blue Gurd Afisi Kuu) walijinyakulia kitita cha kura 34,508 sawa na asilimia 24.7.

Lakini kutokana na viongozi wa chama hicho kubweteka na kutotilia mkazo ukuaji wa chama chao Tanzania Bara kama inavyodaiwa, CUF ikajikuta ikiporomoka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Ambapo kwa mujibu wa tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) CUF ambayo ilimsimamisha Al-haji Shaaban Alli Nassor ilipata kura 22,660 sawa kabisa na asilimia 21.65 nyuma ya Chadema iliyojinyakulia jumla ya kura 27,355 sawa na asilimia 26.19, Makapa 2010 aligombea jimbo la Kahama lilioko mkoa wa Shinyanga na kusulubiwa vibaya na James Lembeli wa CCM .

Pale Ilala ambako CUF mwaka 2005 ilikuwa ya pili kwa kupata kura 9,637 sawa na asilimia 19.6, huku Chadema ikiambulia nafasi ya tatu kwa kuwa na kura 2,229 sawa na asilimia 4.5,

Mwaka 2010 ilianguka vibaya kwa kuambulia kura 3,988 ya kura zote wakati wenzao Chadema bila ya mapokezi ya kihistoria walipata kura 8,053.

CUF mwaka 2005 jimbo la Ilala ilimsimamisha Omar Ahamad Mnyanga ambaye mpaka sasa haijulikani kama yupo ndani ya chama au vipi!

Bali inawezekana naye keshaondoka kwani CUF haina utamaduni wa kuthamini wagombea wake, ndio maana hata Hussein Peter Syovelwa aliyegombea jimbo hilo mwaka 2010 amekwishahamia CCM!

Siyo huyo tu, bali hata Mchungaji Bethuel Heko Pori aliyegombea jimbo la Ukonga katika chaguzi zote za 2005 na 2010 hivi sasa ameshahama CUF amehamia CCM kama alivyohamia Ayubu Musa Kimangale ADC Kimangale alijkuwa mgombea wa jimbo la Segerea.

Mpaka juzijuzi Leopold Leonard Mahona aliyepepetana na Rostam Abdul Rasul Aziz kule Igunga mwaka 2010 na kupata zaidi ya kura 11,000 na kushikilia nafasi ya pili, mwaka jana 2011 alipambana tena katika uchaguzi mdogo ulioitishwa kufuatia kujiuzulu kwake (Rostam), akapata kura 2000 tuu nyuma ya Chademe iliyopata kura ……. Ikiongazwa na CCM kwa kuwa na kura …… naye keshahamia NCCR Mageuzi!

Kwanini kila anayegombea Ubunge kwa tikiti ya CUF badala ya kubaki ndani ya chama kwa lengo la kugombea tena kipindi kijacho, anaamua kuhama?

Majibu yake yakiambatana na orodha ndefu ya wanaCUF waliopata kugombea katika majimbo na baadae kung’oka ndani ya chama hicho nitakuletea wiki ijayo katika sehemu ya tatu ya mfululizo wa makala haya.

O784438546

No comments: