Friday, August 10, 2012

KAMA HUISIKIA IKIWASILISWA ISOME HII HAPA....


HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI MH. JOSEPH OSMUND MBILINYI (MB), WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI WA MASUALA YA KAZI NA AJIRA KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA KAZI NA AJIRA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kuniongoza vema katika kipindi chote cha utumishi wangu; Tangu aliponifanya kuwa Diwani wa Watu wa Karatu miaka saba iliyopita na hata sasa ninapopigania maslahi ya Watanzania wote kwa nafasi yangu ya ubunge, yeye- Muweza wa Yote- ndiye amekuwa dira na ngome yangu kuu katika uongozi.

Mheshimiwa Spika, nitumie wasaa huu kutoa pole na salamu zangu za rambi rambi kwa familia zote za Watanzania waliopoteza ndugu na jamaa zao katika ajali ya meli ya MV Skagit iliyotokea hivi karibuni; Aidha, nampa pole na kumtakia moyo wa uvumilivu Mhe. Joseph Selasini (Mbunge wa Rombo) katika kipindi hiki kigumu anapoomboleza kifo cha Baba yake Mzazi; aidha natoa pole kwa kifo cha aliyekuwa mtumishi wa Bunge Marehemu Peter Mazengo pamoja na kutoa pole kwa wabunge mbalimbali waliopatwa na misiba katika kipindi hiki. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote hao,  mahali pema peponi – Amina.

Mheshimiwa Spika, kwa nafasi ya kipekee kabisa naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni Mh. Freeman A. Mbowe (MB) kwa kipindi kifupi cha uwepo wangu hapa bungeni kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri kivuli wa Kazi na Ajira, Viongozi wote wa CHADEMA katika nafasi zao, Wananchi wote wa Jimbo la Karatu na mkoa wa Arusha kwa ujumla kwa kuniamini na kunifikisha hapa. Wote kwa ujumla nawaahidi kuwa nitakuwa Mtumishi wa watu kwa maslahi ya watu na Maendeleo ya watu. Aidha, nichukue fursa hii pia kutambua uwepo wa viongozi na wajumbe wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA - Wilaya ya Karatu, waliofunga safari kuja kuniunga mkono leo ndani ya Bunge hili, nawakaribisha sana.
 Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia Wazazi wangu, Mama na Baba yangu Mzee Paresso kwa Maelezi mema waliyonipatia hata kufikia hatua ya kuaminiwa kuwa kiongozi wa watu; Pia namshukuru Mume wangu, Bwana Steven Mmbogo, kwa kuwa na mimi bega kwa bega katika harakati zangu za kisiasa na kiuongozi – namshukuru sana!.
Mheshimiwa Spika, leo nawasilisha maoni ya Upinzani, huku nafsi na akili yangu vikiwa vimegubikwa na hisia na kumbukumbu za majonzi; Nikimkumbuka mbunge mwenzetu, mpendwa wetu Mheshimiwa - Marehemu Regia Estelatus Mtema - aliyekuwa Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira, na aliyetimiza wajibu kama huu mwaka jana kabla ya mauti kumfika; Mungu ampumzishe kwa amani dada Regia na aniwezeshe kuitekeleza vema azima yake ya kupigania haki na maslahi ya Watanzania kwa uadilifu, ujasiri na umakini mkubwa hadi hapo muda wangu utakapofika!
Mheshimiwa Spika, wa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la mwaka 2007) kifungu cha 99 (7), nachukua fursa hii kuwasilisha Maoni na Mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Mheshimiwa Spika,kwa taifa maskini kama Tanzania, kazi na ajira vinapaswa kuwa ndiyo kipaumbele cha msingi kuliko vyote katika kuchochea maendeleo ya nchi. Aliyekuwa Rais wa 26 wa Marekani, Theodore Roosevelt (1858-1919) aliwahi kusema, “It is only through labor and painful effort, by grim energy and resolute courage that we move on to better things” - “Ni kwa kupitia kazi na juhudi chungu, kwa nguvu yenye maumivu na ushujaa wa kijasiri, ndivyo vinavyopelekea sisi kupiga hatua kuelekea kwenye maendeleo“.
Mheshimiwa Spika,Serikali makini duniani huweka sera na mifumo thabiti ya kuhakikisha kuwa ajira za kutosha zinatengenezwa, mazingira ya kazi yanaboreshwa na wafanyakazi wanalipwa ujira na mishahara yenye staha, si tu kwaajili ya kuwawezesha kumudu gharama za maisha, bali pia kuwapa morali wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kwa maendeleo ya taifa.
Mheshimiwa Spika,vinginevyo Taifa lolote duniani ambalo vijana wake wengi hawana ajira, na wale walio vyuoni wanashindwa kusoma kwa sababu ya Serikali kushindwa au kupuuza kugharamia masomo yao; Taifa ambalo limejaliwa raslimali nyingi za utalii na madini ya thamani, lenye vyanzo vingi vya kodi na mapato, lakini limegubikwa na migogoro mingi, ya mara kwa mara na isiyokwisha, ya wafanyakazi wanaodai haki na mafao yao halali, huku wakiishia kunyamazishwa kwa kauli za kibabe na nguvu za dola; Kwa namna yoyote ile taifa hilo, ni kielelezo cha Nchi inayoongozwa na Serikali isiyo na vipaumbele, yenye viongozi wenye ubinafsi wasiojali na wanaotekeleza sera zilizoshindwa.

2.0 MADAI YA WAFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika, katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema;
“Uhalali wa Serikali yoyote ya kidemokrasia kuendelea kukaa madarakani na kuendelea kuongoza hautokani tu na Katiba na Sheria iliyoiweka Serikali hiyo madarakani, bali ridhaa ya wananchi kuendelea kutawaliwa au kuongozwa inatokana na matendo mema ya Serikali kwa raia wake.
Kwa kauli hii ya Baba wa Taifa, embu Bunge hili lijiulize, yako wapi matendo mema ya Serikali yetu kwa Wafanyakazi wa Kitanzania, ikiwa kwa miaka mingi, tangu mwaka 2007 na kabla ya hapo, Walimu wamekuwa wakigoma ili kudai stahili na mafao yao, lakini mpaka leo wengi wao hawajalipwa? Yako wapi matendo mema ya Serikali hii ikiwa Wazee wengi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa miaka 35, tangu mwaka 1977 hadi leo 2012 bado wanateseka wakidai mafao yao, ilhali wenzao wa nchi nyingine walishalipwa? Yako wapi matendo mema ya Serikali hii kwa wafanyakazi wa migodini ikiwa hadi leo hii wanalipwa malipo duni kwa kazi ngumu ya kuchimbia madini ya wawekezaji wa Kigeni, licha ya kuwa Nchi yao Tanzania iko katika nafasi za juu kwa uzalishaji wa dhahabu na Tanzanite duniani?
Mheshimiwa Spika, yako wapi matendo mema ya Serikali hii, ikiwa Wafanyakazi wanapunjwa huku sehemu kubwa ya mapato yatokanayo na kodi na nguvu za wafanyakazi yanatumika kuneemesha viongozi wa juu wa kiserikali na kisiasa, kwa kuwalipa mishahara mikubwa, posho na marupurupu mengi, huku wazalishaji wenyewe hususani wakulima na wafanyakazi wakizibwa midomo kwa kauli za kibabe na nguvu za dola? Iko wapi haki na huruma ya Serikali hii kwa Wananchi? Iko wapi ile CCM ya Wakulima na Wafanyakazi? Serikali hii inawezaje kujivunia uhalali wa kuwaongoza Watanzania hawa wanaoteseka hivi?


Mheshimiwa Spika,tunachukua fursa hii kwa mara nyingine tena kuliarifu Bunge lako tukufu na Watanzania wote kwa ujumla, kwamba sababu kuu, lakini isiyo ya msingi, inayosababisha Serikali isiwalipe Wafanyakazi mishahara na mafao yanayostahili kwa wakati, kama Madaktari, Walimu, wafanyakazi wa TAZARA, Polisi, Wanajeshi wa ngazi za chini, Wazee waliokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Wafanyakazi wa mashirika mengine, si kwamba madai yao hayalipiki au hakuna pesa, bali tatizo ni Nchi kuongozwa bila kufuata vipaumbele vya msingi.
Mheshimiwa Spika, wakati wakubwa wakisema madai ya walimu hayalipiki kwa sababu Serikali haina pesa; Kambi Rasmi ya Upinzani tuliionyesha Serikali vyanzo vingi mbadala vya mapato na kuitaka ipanue wigo wa ukusanyaji kodi, lakini hatukusikilizwa; Tuliishauri Serikali izibe mianya ya ufisadi, na ipunguze misamaha ya kodi ili kuokoa pesa nyingi zinazobaki kwa Wawekezaji wa Makampuni makubwa, lakini tulipuuzwa; Tulipendekeza Serikali ifute posho zote za vikao “sitting allowance” ili kuokoa matumizi makubwa ya fedha yasiyo ya lazima yanayofanywa kwenye taasisi nyingi za umma likiwemo Bunge, lakini tulibezwa; Tuliitaka Serikali kwa kutumia Madaraka ya Kikatiba aliyonayo Rais Kikwete, ipunguze Baraza kubwa la Mawaziri, ili kuokoa fedha za wananchi na kuwa na serikali ndogo inayofanya kazi kwa ufanisi, lakini hakuna kilichotekelezwa.
Mheshimiwa Spika, Matokeo yake nchi yetu imekuwa Kama vile imesimama, wafanyakazi hawalipwi inavyostahili na Taifa haliendelei.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaiasa Serikali kuwa jitihada zake za kuzima migomo na migogoro ya Wafanyakazi mahakamani athari yake itakuwa ni kubwa na mbaya sana kwa uhai wa Watanzania na maendeleo ya Taifa hili.  Hakuna Mtanzania atakayekuwa na uhakika wa kupona ikiwa tutaendelea kutibiwa na Madaktari hawa wanaolazimishwa kufanya kazi kwa mishahara duni, na wala raia wa nchi hii hawatakuwa na uhakika wa usalama wao na mali zao, ikiwa askari polisi wanalazimishwa kufanya kazi kwa malipo na maisha ya kudhalilisha.  Na Nchi hii huenda kabisa ikakosa viongozi na wataalam wa fani mbalimbali ikiwa Serikali itaendelea kujiona shujaa kwa kuzima madai ya Walimu Mahakamani.

3.0 MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Mheshimiwa Spika,
Aya ya 81 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2010 – 2015 iliahidi kwamba ili kuimarisha na kuendeleza hifadhi ya jamii CCM itazielekeza Serikali zake “… kufanya tathimini ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kurekebisha viwango vya mafao vinayotoa ili visipishane mno; kuanzisha na kuimarisha Mamlaka ya Uthibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii; na kuchukua hatua za makusudi za kupanua wigo wa kinga ya Hifadhi ya Jamii, ili Watanzania walio wengi waweze kufaidika na huduma za mifuko ya jamii.” Vile vile, kwa mujibu wa Ilani hiyo, Serikali za CCM zitapaswa “kuelimisha jamii ya wafanyakazi na waajiri juu ya umuhimu wa hifadhi ya jamii kwa maendeleo ya wafanyakazi na ya nchi kwa ujumla”; na “kuendelea kutumia uwezo wa kifedha uliopo katika kila Shirika la Hifadhi ya Jamii, kwa kuwekeza katika miradi mbali mbali ya maendeleo nchini.”

Mheshimiwa Spika,
Ahadi ya kwanza iliyotajwa katika Ilani ya CCM, yaani kurekebisha viwango vya mafao ili visipishane mno haijatekelezwa hadi sasa kwani viwango vya mafao vinavyotolewa na Mifuko mbali mbali ya Hifadhi ya Jamii ni vile vile vya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010. Aidha, hakukuwa na sababu yoyote ya msingi ya kuingiza ahadi ya pili katika Ilani hiyo kwani Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imekuwepo kisheria tangu mwaka 2008 wakati Bunge lako tukufu lilipotunga Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135 ya Sheria za Tanzania. Kuhusiana na utekelezaji wa ahadi ya tatu ya CCM kwa Watanzania, Taarifa ya Waziri wa Kazi na Ajira iliyotolewa kwa Kamati ya Huduma za Jamii mwezi Juni, 2012 inaeleza kuwa “asilimia 6 tu ya nguvu kazi ya Tanzania ndio wanaopata huduma za Hifadhi ya Jamii.” Kwa maana hiyo, ahadi ya kupanua wigo wa kinga ya hifadhi ya jamii ili Watanzania wengi zaidi wafaidike na huduma hiyo nayo haijatekelezwa!

Mheshimiwa Spika,
Ahadi ya nne kwenye Ilani ya CCM kuhusiana na hifadhi ya jamii nayo haijatekelezwa kwani, kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri kwa Kamati ya Huduma za Jamii, takwimu za Watanzania wanaopata huduma ya hifadhi ya jamii “… zinadhihirisha kuwa bado kuna uelewa mdogo wa masuala ya hifadhi ya jamii kwa watunga sera, waajiri, waajiriwa, wanachama na wananchi kwa ujumla.” Kama watunga sera, yaani Wizara na Serikali yenyewe, bado wana ‘uelewa mdogo wa masuala ya hifadhi ya jamii’ – kama anavyokiri Waziri katika Taarifa yake - maana yake ni kwamba Watanzania wasitegemee kwamba Serikali hii ya CCM ina uwezo wa kutekeleza ahadi zake za uchaguzi kuhusu kupanua wigo wa wapata huduma za hifadhi ya jamii!

Mheshimiwa Spika,
Ahadi pekee kuhusu hifadhi ya jamii iliyotekelezwa na Serikali ya CCM ni kuendelea kutumia fedha za wafanyakazi zilizomo katika Mifuko mbali mbali ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza katika miradi ambayo haina manufaa yoyote kwa wafanyakazi wenyewe. Hii ni kwa sababu, Serikali imechota mabilioni ya fedha za Mifuko hiyo na kuziingiza katika miradi ambayo haina manufaa yoyote kwa Mifuko yenyewe na hasa kwa wafanyakazi ambao ndio wenye fedha hizo. Ushahidi wa jambo hili, Mheshimiwa Spika, unapatikana katika Taarifa Kuu ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kuhusu Hesabu za Mashirika ya Umma na Taasisi Zingine kwa Mwaka 2010/2011 iliyowasilishwa kwa Rais Kikwete tarehe 28 Machi, 2012.

Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, kuna udhaifu mkubwa katika vitega uchumi vinavyosimamiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kwa mfano, ukaguzi wa vitega uchumi vya NSSF ulionyesha kwamba licha ya Mfuko huo kuwekeza shilingi bilioni 234.054 za wafanyakazi katika ujenzi wa Awamu ya Pili ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mfuko ulikuwa haujasaini mkataba na Serikali juu ya fedha za mradi huo. Vile vile, kwa mujibu wa Taarifa hiyo, licha ya NSSF kusaini mkataba na Serikali ili kuwekeza shilingi bilioni 35.218 kwa ajili ya ujenzi wa Awamu ya Kwanza wa Chuo hicho na licha ya majengo yaliyojengwa katika Awamu hiyo kuanza kutumika tangu Septemba 2008, “Mfuko haujapokea fedha ya pango, au malipo ya mkopo kutoka Serikalini ambao tayari umelimbikiza riba ya shilingi bilioni 14.157.”

Aidha, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu anaituhumu Serikali hii ya CCM kwa kukiuka masharti ya mkataba kwa kugeuza riba ya mkopo wa NSSF kuwa sehemu ya mtaji wakati NSSF ilitakiwa kupokea kodi ya pango ambayo ni gharama ya uwekezaji na riba ya asilimia 15 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka kumi.

Mheshimiwa Spika,
Sio fedha za NSSF tu ambazo zimetumiwa na Serikali hii ya CCM kwenye UDOM. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu inaonyesha kwamba Mifuko mingine nayo imepoteza mabilioni ya fedha za wafanyakazi kwenye ujenzi wa Chuo hicho. Hivyo, kwa mfano, PPF imekwishazamisha jumla ya shilingi bilioni 39.987; PSPF imechakachuliwa shilingi bilioni 105.921; LAPF imepoteza shilingi bilioni 22.030; wakati ambapo NHIF imekwishaunguza shilingi bilioni 13.403 za wanachama wake. Jumla ya fedha za wafanyakazi wanachama wa Mifuko hii mitano ambazo zimeunguzwa katika ujenzi wa UDOM ni shilingi bilioni 450.615. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali, vitega uchumi vyote hivi katika UDOM vilikuwa ‘non-perfoming’, ikimaanisha kwamba havirudishi fedha za mikopo ya Mifuko husika.

Mheshimiwa Spika,
UDOM sio White Elephant pekee anayeteketeza fedha za wafanyakazi. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, NSSF ‘ilikubali’ kutoa mkopo wa shilingi bilioni 5.33 kwa riba ya asilimia 15 kwa mwaka kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Idara ya Usalama wa Taifa. Mkopo huo na riba yake ulitakiwa kulipwa kwa njia ya kodi ya pango katika kipindi cha miaka kumi kuanzia 2007. Hata hivyo, “taasisi husika ya Serikali bado haijaanza kulipa mkopo huo na hakuna malipo yoyote yaliyofanywa hadi sasa. Vile vile, riba inayotokana na mkopo huo nayo bado haijalipwa. Taasisi husika ya Serikali ilitakiwa ianze kufanya malipo tangu tarehe 31 Desemba, 2010.” Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2011, Jengo hilo la Usalama wa Taifa pia lilikwishatafuna shilingi bilioni 6.5 za PSPF.

Mheshimiwa Spika,
Ujenzi wa Ukumbi huu wa Bunge lako tukufu pia umefanywa na mikopo inayotokana na fedha za makato ya wafanyakazi ambazo pia hazijalipwa hadi sasa. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2011, NSSF ilikuwa haijalipwa shilingi bilioni 8.96, na PPF ilikuwa inadai malipo ya shilingi bilioni 7.9 zilizotumika katika ujenzi wa Ukumbi huu wa Bunge. Aidha, hadi tarehe 30 Juni, 2011, LAPF ilikuwa imechangia shilingi bilioni 2.91 kwa ajili ya ujenzi huo.

Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu inaonyesha fedha nyingine nyingi za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zimetumika katika miradi ya ujenzi yenye manufaa yenye mashaka kwa wafanyakazi na kwa Mifuko yenyewe.  Hivyo, kwa mfano, mwaka 2007 NSSF ilitoa mkopo wa shilingi bilioni 20 wenye riba ya asilimia 15 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Jeshi la Polisi. Mkopo huo na riba yake ulitakiwa ulipwe katika kipindi cha miaka kumi baada ya mwaka mmoja wa ‘huruma.’ Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, “Mfuko haujaanza kukusanya kodi ya nyumba hizo kwani Mkataba wa Upangaji bado haujasainiwa licha ya kwamba nyumba zenyewe zimekuwa zinakaliwa.”

Mabilioni mengine ya wafanyakazi yameteketezwa katika ujenzi wa Machinga Complex ambayo ni mali ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, mwaka 2007 NSSF ilitoa mkopo wa shilingi bilioni 12.9 kwa riba ya asilimia 14.9 kwa mwaka kwa ajili ya ujenzi wa Machinga Complex jijini Dar es Salaam. “Mkopo haujaanza kulipwa bado na hakuna malipo yoyote yaliyofanywa. Hadi tarehe 30 Juni, 2011, mkopo huo ulikuwa umefikia shilingi bilioni 15.4.”

Mikopo mingine ambayo Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu inaitaja kama ‘not performing’ ni pamoja na Continental Venture Tanzania Ltd. inayodaiwa dola za Marekani milioni 3.5, Meditech Industrial Co. Ltd. (dola za Marekani milioni 1.45), General Tyre yenye kudaiwa dola za Marekani milioni 18.8 na Dar es Salaam Cement Co. Ltd. inayodaiwa dola za Marekani milioni 4.7. Wadaiwa wengine wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni pamoja na Kagera Sugar yenye kudaiwa shilingi bilioni 12, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) shilingi bilioni 78.6 na Kiwira Power Ltd. shilingi bilioni 13.5.

Mheshimiwa Spika,
Hukumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu juu ya uendeshaji, udhibiti na usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika nchi yetu inajieleza yenyewe: “Kushindwa kwa makampuni haya (baadhi yao yakiwa yamedhaminiwa na Serikali) kuheshimu majukumu yao ya mikopo kunatia shaka kama uchambuzi madhubuti ulifanywa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii juu ya uwezo wa wakopaji kulipa mikopo hiyo. Zaidi ya hayo, ukubwa wa biashara inayofanywa baina ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na taasisi za Serikali na malipo yasiyokuwa na uhakika ya mikopo hiyo yanatia shaka juu ya uendelevu wa Mifuko husika katika siku chache zijazo.”

Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya Waziri kwa Kamati ya Huduma za Jamii inaeleza kwamba NSSF imeanza kutekeleza mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 300 katika eneo la Mkuranga. Zaidi ya hayo, Taarifa ya Waziri inasema kwamba NSSF imeanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni “… ambapo mkandarasi amepatikana na kukabidhiwa eneo la kazi, na yuko katika hatua ya ukusanyaji vifaa kwa ajili ya kuanza ujenzi.” Aidha, katika mwaka wa fedha 2012/2013, NSSF itaendelea na ujenzi wa Daraja la Kigamboni na mradi wa uzalishaji umeme wa Mkuranga. Vile vile, NSSF itawekeza katika ujenzi wa nyumba za Jeshi la Wananchi (TPDF), kushiriki ujenzi wa Hospitali ya Apollo jijini Dar es Salaam, ujenzi wa ofisi za RITA, Chuo cha Sayansi na Hisabati katika UDOM na miradi mingine mingi ya ujenzi kwa kutumia fedha za akiba ya wafanyakazi.

Kwa kuzingatia yote ambayo yametokea kutokana na uwekezaji wa fedha za wafanyakazi katika miradi iliyokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kusitisha mara moja matumizi haya makubwa ya fedha za wafanyakazi katika miradi ambayo inaelekea kuifilisi Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na hivyo kuhatarisha maslahi ya moja kwa moja ya wafanyakazi wa Tanzania. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ieleze Bunge hili tukufu kwa nini inatumia mabilioni ya fedha za akiba ya wafanyakazi kwa majengo yasiyokuwa na umuhimu wowote kiuchumi kama ofisi za Idara ya Usalama wa Taifa. Vile vile, Serikali ilieleze Bunge hili tukufu kwa nini hadi sasa haijalipa mikopo na riba iliyotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa ujenzi wa miradi iliyotajwa na lini inatazamia kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika,
Kwa ushahidi wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, ni wazi kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Tanzania inaongozwa, kuendeshwa na kusimamiwa na watu ambao hawana uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ujuzi na uadilifu unaohitajika kwa maslahi ya wafanyakazi wanachama wa Mifuko hiyo. Ni wazi, kwa ushahidi huu, kwamba mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutendaji katika Mifuko hii yanahitajika na kwa haraka kabla mifuko hii haijafilisika kabisa. Kwa sababu hiyo, na ili kuinusuru Mifuko hiyo na kunusuru maslahi ya maelfu ya wafanyakazi wanachama wake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Rais Kikwete kuwawajibisha watendaji wakuu wote wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambao wameacha mabilioni ya fedha za wafanyakazi yazamishwe kwenye miradi mikubwa ya uwekezaji ambayo, kwa ushahidi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, imefanywa bila uchambuzi madhubuti wa uwezo wa wamiliki wa miradi hiyo kurudisha fedha za wafanyakazi.

4.0 MAREKEBISHO YA SHERIA YA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII

Mheshimiwa Spika,

Baada ya kutapanya fedha za wafanyakazi kwa kuwekeza katika grandiose projects isiyokuwa na manufaa ya kiuchumi kwa wafanyakazi wanachama na hata kwa Mifuko yenyewe, sasa Serikali hii ya CCM imeamua kuwadhulumu wafanyakazi fedha zinazotokana na makato ya mishahara yao. Vile vile, inaelekea Serikali hii ya CCM inataka kuficha uchafu ilioufanya katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kutunga Sheria inayowazuia wafanyakazi kupata fedha zao wakati wanapozihitaji zaidi, yaani wanapokuwa hawana ajira. Hii imefanyika kwa Serikali kupenyeza kinyemela, na kinyume cha Kanuni za Kudumu, masharti yanayowazuia wafanyakazi wote wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania kuchukua mafao ya kujitoa uanachama wa Mfuko husika kabla ya kufikisha umri wa miaka hamsini na tano au sitini. Kisheria, umri wa kustaafu kwa hiari ni miaka hamsini na tano wakati umri wa kustaafu kwa lazima ni miaka sitini. Kwa masharti haya, mfanyakazi hana haki au namna nyingine yoyote ya kupata fedha za makato yake ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii hata akiachishwa kazi na mwajiri wake bila kosa lolote, hadi atakapofikisha umri huo wa kustaafu kwa hiari au kwa lazima.

Mheshimiwa Spika,
Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, 2012 ulichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 12 Januari, 2012. Hakukuwa na masharti ya kuzuia mafao ya kujitoa uanachama wa Mfuko. Tarehe 1 Februari, 2012, Muswada huu uliletwa Bungeni kwa ajili ya Kusomwa kwa Mara ya Kwanza chini ya kanuni ya 83(1) ya Kanuni za Kudumu. Hapa pia hakukuwa na masharti ya kuzuia mafao ya kujitoa. Baada ya hapo, Muswada ulipelekwa kwenye Kamati ya Huduma za Jamii kwa ajili ya kuujadili kwa mujibu wa kanuni ya 84(1) ya Kanuni za Kudumu. Masharti hayo hayakujadiliwa wala kupendekezwa na Kamati ya Huduma za Jamii. Ingekuwa hivyo, kwa mujibu wa kanuni ya 84(3) na (4)ya Kanuni za Kudumu, masharti hayo yangeletwa Bungeni wakati wa Muswada kusomwa kwa Mara ya Pili. Hilo halikufanyika.

Kutoka kwenye Kamati, Muswada huu ulirudishwa Bungeni tarehe 13 Aprili, 2012 kwa ajili ya Kusomwa kwa Mara ya Pili na kujadiliwa na Bunge lako tukufu chini ya kanuni ya 86 ya Kanuni. Hotuba yote ya Waziri haina mstari hata mmoja unaoonyesha nia ya Serikali ya kufuta mafao ya kujitoa kwa wanachama ambao hawajafikisha umri wa kustaafu kwa hiari au kwa lazima. Aidha, hotuba za Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nazo ziko kimya juu ya kufutwa kwa mafao ya kujitoa uanachama. Ukimya huu unatokana na ukweli kwamba hadi kufikia hatua hiyo hakukuwa na jambo lolote la kuashiria nia ya Serikali kufuta mafao ya kujitoa.

Aidha, sio Mwenyekiti wa Kamati au Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani pekee waliokuwa kimya kuhusu masharti haya. Kwa mujibu wa Taarifa Rasmi ya Majadiliano ya Bunge ya Mkutano wa Saba, Kikao cha Nne cha tarehe 13 Aprili, 2012, hakuna hata mmoja wa Wabunge wote thelathini na nane waliochangia mjadala wa Muswada aliyezungumzia suala la kufuta mafao ya kujitoa uanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Suala hilo halikuzungumziwa katika michango ya Wabunge kwa sababu halikuwepo kwenye mjadala. Na wala halikuingizwa kwenye mjadala na Wabunge wengine watano waliowasilisha Majedwali ya Marekebisho ya vifungu mbali mbali vya Muswada.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kutumia udhaifu wa uongozi wa Bunge katika kusimamia Kanuni za Kudumu, na upungufu wa muda wa mjadala Bungeni ambao ni matokeo ya kuvurugwa kwa Kanuni za Kudumu zinazohusu muda wa Wabunge kujadili hoja za Serikali, Waziri aliwasilisha Jedwali la Marekebisho lililopendekeza marekebisho ya vifungu vipatavyo 45 na vifungu vidogo karibu 70 vya Muswada. Ni katika msitu huo wa Jedwali la Marekebisho ndiko Serikali ilikochomeka masharti ya kufuta mafao ya kujitoa kwa wafanyakazi wasiofikisha umri wa kustaafu kwa hiari au kwa lazima. Kwa sababu ya urefu wa Jedwali na uchache wa muda wa kulichunguza na kujadili, inaelekea hakuna Mbunge hata mmoja aliyeona mapendekezo hayo ya kufuta mafao ya kujitoa. Hansard inaonyesha kwamba ibara za 9, 10 na 11 “… zilipitishwa na Kamati ya Bungeni Zima pamoja na marekebisho yake.” Ibara ya 11 ndio iliyobadilishwa na Jedwali la Marekebisho la Waziri kwa kuweka masharti kwamba mfanyakazi atapata mafao ya kujitoa pale tu atakapofikisha umri wa miaka 55 au miaka 60.

Mheshimiwa Spika,
Mara nyingi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imelalamikia ukiukwaji wa kanuni zinazohusu muda wa mjadala Bungeni. Tumelalamika kwamba uongozi wa Bunge umeshiriki katika kupunguza muda wa mjadala kinyume cha Kanuni za Kudumu. Hatukusikilizwa. Tumepigia kelele kupunguzwa kwa muda wa mjadala wakati wa kupitisha vifungu vya Miswada ya Sheria na mafungu ya bajeti. Hakuna aliyetaka kuelewa kelele zetu. Tumepaza sauti zetu kwamba Bunge lako tukufu linageuzwa kuwa muhuri wa kuhalalisha maamuzi ya Serikali tunayotakiwa kuisimamia na kuishauri. Tumepuuzwa. Haya ndio matokeo ya kuruhusu kanuni za mjadala kukanyagwa jinsi zilivyokanyagwa. Sheria hii inayodhulumu wafanyakazi kwa kuzuia mafao yao ya kujitoa katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii sio tu ni matokeo ya hila za Serikali, bali pia ni uthibitisho wa ulegevu wa uongozi wa Bunge na udhaifu wa Bunge lenyewe katika kusimamia Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Kumbu Kumbu Rasmi, kifungu pekee kilichofanyiwa marekebisho ya kuzuia fao la kujitoa ni kifungu cha 21 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma. Hata hivyo, SSRA imedai kwamba Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yanahusu Mifuko yote na wafanyakazi wote. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako tukufu kama Sheria hii mpya imerekebisha vifungu vya Sheria nyingine by implication, kama inavyoelekea kuwa tafsiri ya SSRA. Kama Sheria mpya haijabadilisha vifungu vya Sheria za Mifuko mingine, ni kwa nini SSRA inang’ang’ania kwamba marekebisho ya Sheria ya PPF “… yanawahusu wafanyakazi wote nchini mwetu bila kubagua sekta yoyote ile.”

Mheshimiwa Spika,
Aidha tunaelewa kuwa Pensheni ni suala la msingi sana na hatuwezi kuwaacha wazee wetu waishi bila Pensheni. Vile vile tunatambua kuwa kuna mahitaji ya sasa ambayo hayasubiri mpaka mtu azeeke ndipo aweze kuyatatua ndio maana tunaunga mkono wafanyakazi katika kupata fao la kujitoa na tunapendekeza sheria irekebishwe na kuzingatia yafuatayo;

i.                    Uanzishwe utaratibu wa kuwa na mafao kwa wanachama ambao ama wamekosa kazi kutokana na sababu mbalimbali (Unemployment benefits) kama vile kumalizika kwa mkataba , kuachishwa kazi,kufukuzwa kazi nk kwa kipindi cha miezi sita mwanachama wa mfuko husika aweze kulipwa kiasi cha mshahara kamili na miezi sita mingine kama hajapata kazi alipwe nusu mshahara na mfuko na baada ya mwaka mmoja kama atakuwa hajapata kazi basi mfuko uache kuendelea kumlipa mwanachama huyo. Mifuko itenge fungu maalum kwa ajili ya kulipia mafao hayo.

ii.                  Mifuko itenge fedha kwa ajili ya masomo (Education fund) kwa ajili ya wanachama wake pindi watakapokuwa wanaenda masomoni wakiwa ni wanachama wa mfuko ,hii itawafanya wanachama kuweza kujiendeleza kielimu  na hivyo itapunguza idadi ya wanachama ambao wanajitoa kwa ajili ya kupata fedha za kusoma.
Mheshimiwa Spika,
Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kurejea pendekezo letu tuliloishauri katika bajeti ya Wizara hii ya mwaka 2011/2012 katika kuona umuhimu wa kuiunganisha mifuko yote ya hifadhi za jamii na kubaki katika wizara moja ambayo ni ya Kazi na Ajira. Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa lengo kuu la kuunganisha mifuko hii ya hifadhi za jamii ni katika kuirahisishia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii (SSRA) katika kutekeleza Sheria moja na kuunda vifungu sawa vya kisheria vitakavyosimamia utekelezaji na uendeshaji wa mifuko hii ambapo kwa sasa mifuko hii imekuwa chini ya wizara tofauti na hivyo hata utekelezaji wake unakua mgumu na kuleta ukinzani kwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii. Tunasisitiza kuwa pendekezo letu ni kuifanya PPF na NSSF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwaajili ya Sekta Binafsi vilevile LAPF, PSPF na GEPF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwaajili ya Sekta ya Umma. Pia, kambi ya Upinzani inapendekeza mifuko yote isimamiwe chini ya Wizara ya Kazi na Ajira.

4.0 KODI YA PATO LA MSHAHARA Pay As You Earn- PAYE).
Mheshimiwa spika,
Tarehe mosi Julai mwaka huu, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipokea taarifa kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imebadilisha viwango vya kodi ya mapato kwa watu ambao ni wafanyakazi wakaazi. TRA imesamehe kodi kwa wafanyakazi wanaopata mshahara mpaka Shilingi 170,000, lakini imeendelea kutoza kiwango kikubwa cha kodi kwa wafanyakazi wanaopata shilingi 360,000 kwa mwezi, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 14 ya mshahara huo.

Mheshimiwa Spika,
Mapato ambayo yanazidi shilingi 360,000 lakini hayazidi shilingi 540,000, hutozwa aslimia 20 ya kiasi kinachozidi, mapato yanayozidishilingi 540,000 lakini hayazidi shilingi 720,000 hutozwaaslimia 25 ya kiasi kinachozidi. Kiasi kinachozidi 720,000, lakini hakizidi 1,076,000 hutozwa asilimia 30 ya kiasi kinachozidi.

Mheshimiwa Spika,
Viwango hivi vya tozo mpya za kodi ya mapato ni vikubwa sana.Tunalitaka Bunge lako tukufu kupitia viwango hivi upya na kwa umakini ili kutafuta kila namna ya kumuondolea Mfanyakazi mzigo huu mzito wa kodi. Badala ya Serikali kulimbikiza kodi nyingi kwa Wafanyakazi pekee, Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri kuongeza wigo wa wananchi wanaotozwa kodi kwa kuzingatia vipato vyao, kama ilivyobainishwa na ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) iliyoonyesha kuwepo kwa idadi kubwa ya wananchi wanaopaswa kulipa kodi, lakini hawatozwi.
Mheshimiwa Spika,
Ili kupunguza mzigo mkubwa wa kodi wanayokatwa Wafanyakazi, Kambi Rasmi ya Upinzani inarejea pendekezo lake la kuitaka Serikali ipunguze viwango vya sasa vya kodi mpaka asilimia 9 kwa kiwango cha chini na asilimia 27 kwa kiwango cha juu. Uamuzi huu utawezesha wafanyakazi kubakia na fedha kutoka kwenye mishahara yao na hivyo kuishi vizuri kumudu maisha yao ya kila siku.

5.0 SHERIA ZA KAZI NA HAKI ZA WAFANYAKAZI
Mheshimiwa spika, pamoja na kuwepo na sheria za kazi ambazo zinajaribu kulinda haki za wafanyakazi, kama vile Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na 6 ya Mwaka 2004 na Sheria ya Taasisi za Kazi Na 7 ya 2004, bado kuna pengo la sheria katika kulinda haki za wafanyakazi pindi kunapotokea uhamisho wa shughuli yaani (Transfer of Undertakings) kwa upande wa muajiri hususani kwenye sekta binafsi ambapo kumekuwa na migogoro mingi baina ya pande mbili hizi inayotakana na kukosekana na sheria hii.
Mheshimiwa Spika,mkataba wa miaka 25 ambao serikali iliingia na kampuni ya Rites ya India mwaka 2009, katika kusimamia shughuli na uendeshaji wa Shirika la Reli Tanzania(Tanzania Railway Limited- TRL) ni mfano mzuri wa uhamisho wa shughuli. Mkataba huu ulileta mgogoro wa kazi baina ya menejementi na wafanyakazi baada ya mwajiri mpya kusitisha mikataba ya kazi na ajira na kufanya wafanyakazi wapatao 3,204 kuwa hatarini kupunguzwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulipa uzito mkubwa suala hili kwa kuleta muswada wa sheria bungeni utakaosimamia maslahi wafanyakazi katika suala hili.  Afrika Kusini ni nchi inayokua kwa kasi kiuchumi na yenye fursa mbalimbali za uwekezaji, lakini kwa kugundua hili na kwa lengo la kulinda haki za wafanyakazi, wenzetu wameweza kutunga sheria inayoitwa Transfer of undertakings Act (Protection of Employment) ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Spika, ni matumaini yetu kwamba Serikali, ambayo ina sera mbalimbali zenye nia ya kuikuza sekta ya uwekezaji, bila shaka itaona umuhimu wa dhati wa kutunga sheria ambazo zitalinda haki za kazi pale panapotokea uhamisho wa shughuli ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea kama kuvunjwa kwa mikataba, kupunguzwa kwa wafanyakazi kazini bila kufuata sheria za kazi, ushurutishwaji wa wafanyakazi kufanya kazi kwa muajiri mpya, kupoteza haki za msingi za wafanyakazi na mengineyo.

6.0 MKATABA WA TANZANIA NA ZAMBIA (TAZARA)
Mheshimiwa spika, Kamati ya Bunge ya Miundombinu, ilifanya mazungumzo na uongozi pamoja na wafanyakazi wa TAZARA na kukiri kuwa mkataba ambao serikali za Tanzania na Zambia uliingia miaka 36 iliyopita, umeisababishia Serikali hasara kubwa na umechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa migogoro isiyokwisha baina ya uongozi na wafanyakazi wa TAZARA.
Mheshimiwa Spika, moja ya athari za makubaliano ya mkataba huu, ni Wazambia kunufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na mapungufu ya kimkataba huo kuliko Watanzania; Kwa mfano wafanyakazi 52 kutoka Zambia wanaofanya kazi katika tawi la TAZARA Tanzania wamekuwa wakipata marupurupu ya kufanya kazi kama wafanyakazi wa kigeni wakati kuna wafanyakazi 4 tu wa Tanzania wanaofanya kazi katika tawi la TAZARA nchini Zambia, lakini hawapewi marupurupu hayo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imebaini kuwa hali hii imesababishwa pia na kuhodhiwa madaraka na Mkurugenzi wa TAZARA ambaye ni raia wa Zambia. Kama ambavyo imeshauri Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Kambi Rasmi ya Upinzani tunaitaka Serikali na Bunge hili kupitia mkataba huu ili kuweza kuleta usawa na haki katika sheria za kazi utakaolinda maslahi ya wafanyakazi wa nchi zote mbili bila kuleta mpasuko.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka wizara kutoa maelezo ya kutosha juu ya hatua gani zimechukuliwa katika kutatua madai haya ya msingi ya wafanyakazi wa TAZARA; Na je wizara ina mikakati gani katika kuhakikisha kuwa mkataba huu unaangaliwa na kupitiwa upya ili kuleta muswada wa sheria utakaolinda haki za wafanyakazi wa TAZARA pindi kunapotokea mabadiliko yoyote ya mkataba?
7.0 KAZI ZA MIGODINI
Mheshimiwa Spika, kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilikua cha kwanza kutoa taarifa kwa umma juu ya ukiukwaji mkubwa uliokithiri wa haki za wafanyakazi wa Geita Gold Mine (GGM), Resolute ‘Resources’ Golden Pride -Nzega, Tabora baada ya uchunguzi wa kipelelezi kwenye migodi hiyo miwili mwezi Mei, 2011. Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ilipeleka ripoti kwa Waziri wa Kazi na Ajira Mh. Gaudensia Kabaka, ambaye aliahidi kuchukua hatua.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani, inamtaka waziri kulieleza Bunge hili ni hatua zipi zilichukuliwa dhidi ya muajiri kwa kukiuka Sheria na Kanuni za Kazi na kutoa majibu yasiyoridhisha juu ya fidia ambazo wafanyakazi walilipwa baada ya kuonekana kwa ukiukwaji wa haki zao.
8.0 VYAMA VYA WAFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika, lengo kuu la Vyama vya Wafanyakazi toka vianzishwe mwaka 1929 lilikuwa ni kutetea maslahi ya wafanyakazi, lakini hadi leo ambapo tumefikisha zaidi ya miaka 50 ya uhuru bado wafanyakazi wanakabiliwa na matatizo yaleyale yaliyopelekea kuanzishwa kwa vyama hii. Sheria zetu zinazoratibu masuala ya kazi ikiwemo Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 na Sheria ya Taasisi za Kazi Na 7 ya mwaka 2004, zinaruhusu wafanyakazi kuunda umoja wao ili kuwa na sauti moja katika kutetea maslahi katika sehemu za kazi.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kwa mujibu wa tafiti (rasmi na zisio rasmi) wafanyakazi wa Tanzania wanakabiliwa na hali mbaya ya maisha kutokana na kushindwa kwa uongozi wa kisiasa katika kutawala uchumi na matumizi ya rasilimali katika kufikia malengo ya kuboresha maslahi pamoja na mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa sekta zote. Katika kuthibitisha hili Shirikisho la kimataifa la Vyama vya Wafanyakazi (International Trade Union Confederation- ITUC) katika taarifa ya ripoti yake ya Annual Survey of Violations around the World in 2011, ripoti imeonesha kuwa haki za muungano wa wafanyakazinchini mara nyingihupuuzwa kwa kiwango kikubwa, Wafanyakazi huwa na hatua ya migomo mikubwa kinyume cha sheria na hii inasababishwa na mahitaji ya muda mrefu na upindishwaji wa sheria katika kuruhusu vyama vya wafanyakazi kutoa wito wa mgomo wa kisheria. Katika sekta binafsi, ripoti inaonesha kuwa baadhi ya waajiri mara nyingi wanawanyima wafanyakazi wao haki ya kuandaa na kushiriki katika majadiliano ya pamoja.
Mheshimiwa Spika, licha ya Wafanyakazi kufuata taratibu zote za kisheria pindi wanapotaka kuandamana au kugoma ili kushinikiza utelekezaji wa madai yao, bado Serikali imekuwa ikitumia mabavu kuwakandamiza wafanyakazi na vyama vyao. Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuacha mara moja kutumia mabavu katika kushughulikia madai ya wafanyakazi, kwani kufanya hivyo ni kukiuka haki za binadamu na sheria halali za nchi.

9.0 TUME YA USULUHISHI NA UAMUZI (CMA)
Mheshimiwa Spika, tume hii ni muhimu sana kutokana na majukumu yake katika kutatua migogoro sehemu za kazi kwa ufanisi, usawa na kwa haraka tofauti na ilivyo kwa mahakama za kawaida. Pamoja na tume kuwa na jukumu hilo kuu, bado yapo malalamiko mengi sana juu ya utendaji wake hasa katika kutoa haki sawa baina ya mwajiri na mfanyakazi au baina ya wafanyakazi na vyama vyao.
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa ya maelezo ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ya Juni 2012, katika maeneo yanaongoza kwa migogoro kazini, migogoro katika sekta ya Afya kwa kipindi cha Oktoba-Disemba 2011 ilikuwa 33 na kutoka Januari- Machi 2012 migogoro ilikuwa ni 53 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 23 kwa kipindi cha miezi mitatu tu, hii ni ishara kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za wafanyakazi na hii pia imeonesha ongezeko la usajili wa migogoro kwenye viwanda, migodi, mashirika ya umma, vyakula na vinywaji na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, malalamiko mengi yanayotolewa na wananchi ni kukosekana kwa haki katika maamuzi ya tume kutokana na waajiri wengi kuwa na nguvu ya fedha. Pia waajiri wengi wanatumia mwanya wa baadhi ya wafanyakazi ambao hawana uelewa wa masuala ya kisheria ambapo maamuzi ya tume hawazingatii, na badala yake baadhi ya wafanyakazi hufukuzwa kazi mara tu maamuzi yakishatoka.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa wito kwa watendaji wa tume hii kuzingatia weledi katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua waamuzi ambao hawazingatii taratibu za kazi pamoja na kutoa haki pale inapostahili. Aidha vyombo vingine vya kiserikali ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) vifuatilie kwa karibu tume hiyo na mamlaka nyingine za wafanyakazi ili kudhibiti mianya ya ufisadi katika utetezi wa haki na maslahi ya wafanyakazi. Hata hivyo bado kuna changamoto nyingi ikiwa ni pamoja tume kuwa na mashauri mengi ambayo hayajafanyiwa maamuzi/usuluhishi.

10.0 WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI (OSHA)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuanzishwa kwa Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA), bado Wafanyakazi wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu yasiyozingatia usalama wa afya zao.Taasisi hii haijafanya kazi vya kutosha ili kulinda usalama wa afya za wafanyakazi kazini. Ni muhimu kuweka utaratibu wa kuhakikisha mashirika, taasisi na makampuni yote nchini yanatekeleza matakwa ya OSHA na kuongeza adhabu kwa taasisi ambazo hazizingatii taratibu hizo. Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, inaitaka serikali kuhakikisha kuwa uongozi wa viwanda na makampuni unaweka taratibu wa kupima afya za wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yetu ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 Kambi ya upinzani tuliendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa serikali kuhakikisha kuwa waajiri wanatengeza mazingira salama. Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi wa sekta ya madini ambao wamekuwa wakiathiriwa na mazingira magumu na hatarishi mahali pa kazi, Kwa mujibu wa matokeo ya tafiti hizo, idadi kubwa zaidi ya wafanyakazi wa sekta ya madini ambao walitibiwa katika hospitali mbalimbali, uchunguzi wa madaktari umeonesha kwamba wengi wao maradhi yametokana au kuhusiana na shughuli za madini. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2011.

11.0 BARAZA LA KAZI, UCHUMI NA JAMII (LESCO)
Mheshimiwa Spika, Baraza la kazi na Uchumi na Jamii, ambalo linaundwa na idadi ya wateule 17 ambao wanateuliwa na waziri wa ajira na kazi, ni sawa na kuibebesha serikali mzigo mkubwa hasa ukizingatiwa kuwa kazi na majukumu makuu ya baraza hili ni masuala ya ushauri hasa katika kuishauri serikali na waziri kwenye masuala yanayohusiana na kazi, uchumi na jamii kwa kiasi kikubwa kama zilivyoainishwa kwenye sheria. Kambi rasmi ya upinzani bungeni inasisitiza umuhimu wa serikali katika kuhakikisha kuwa inapunguza matumizi yake kutokana na utegemezi wa bajeti yake ili kutoa unafuu na kuelekeza fedha hizi katika sekta nyengine ambazo zinaweza kutumia fungu hili.
Mheshimiwa Spika, mwaka wa kifedha wa 2011/2012 baraza hili (LESCO) lilitengewa kiasi cha shilingi 30,000,000 ili kuwezesha vikao vya baraza na kiasi cha shillingi 12,508,500.00 kuwezesha vikao viwili tu vya baraza. Katika bajeti ya mwaka huu, baraza hili limetengewa kiasi cha shilingi 37,325,000.00 Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, inaitaka serikali kupunguza matumizi yake kwa kurekebisha sheria hii na kulifuta baraza la kazi kutokana na kuwa na taasisi nyingine zinazofanya kazi za kulingana nazo vikiwemo vyama vya kazi, vyama vya waajiri pamoja na wataalamu wa masuala ya kazi katika wizara.
12.0 Kamati ya Huduma Muhimu (Essential Services Committee)
Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa Kamati ya Huduma Muhimu (Essential Services Committee) inaanza kazi mara moja ili kutatua kisheria migogoro inayojitokeza katika sekta zitoazo huduma muhimu kama vile afya, usafiri n.k.  kama ilivyohainishwa katika Vifungu Namba 29-33 cha Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya mwaka 2007.

13.0 WAKALA WA HUDUMA ZA AJIRA TANZANIA (TaESA)
Mhesimiwa Spika, wakala wa huduma za ajira Tanzania ilianzishwa mwaka 2008 chini ya sheria ya wakala wa serikali na. 30 ya mwaka 1997, ili kuleta ufanisi katika kuboresha utoaji wa huduma za ajira kwa watafuta kazi, waajiri na serikali kwa ujumla. Katika hotuba ya ajira na kazi ya kambi rasmi ya upinzani bungeni, tulitoa pendekezo la TAESA kujitangaza vya kutosha na kuhakikisha kuwa inaweka taarifa za shughuli zake ili kutoa fursa kwa nguvu kazi kuweza kufuatilia nafasi za kazi zinazotangazwa na vigezo rasmi kwa ajili ya nafasi hizo.

Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inaendelea kutoa ushauri kwa TAESA tukiitaka iandae “database” ambayo itakua na taarifa muhimu kama namba ya wahitimu wa elimu ya juu nchini, taaluma zao na uzoefu wao ili kuweza kupata takwimu rasmi zitakazoweza kumuunganisha mtafuta kazi na mwajiri. Kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaishauri TAESA kuhakikisha kuwa nafasi za kazi hazitolewi kwa upendeleo na kuwa sheria na kanuni zinazingatiwa kwa kutoa nafasi hizo za kazi, kwakuwa kumekuwepo malalamiko mbalimbali kuhusu uunganishwaji wa watafuta ajira na waajiri. Kwa mamlaka waliyopewa Taesa, yanaweza pia kufungua mianya ya rushwa na kupeana kazi kwa vimemo na hii itasababisha kupoteza watu walio na sifa kamili na uwezo ambao wangeweza kufanya kazi ka ufanisi.

Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inahoji; je ni mikakati gani ambayo TAESA inatumia katika kuhakikisha kuwa nafasi za kazi zinatolewa bila upendeleo wowote? Je ni kwa kiwango gani TAESA imefanikiwa katika kuhakikisha kuwa wadau pamoja na umma unapata taarifa sahihi kuhusu soko la ajira kwa kuzingatia viwango na taratibu zilizowekwa?
 
14.0 TAFITI ZA NGUVU KAZI NA AJIRA NCHINI
Mheshimiwa Spika, utafiti wa nguvukazi na Ajira uliofanyika mwaka 2006 ndio utafiti wa mwisho katika kutoa takwimu za hali ya sekta ya ajira nchini na kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2011, huo ndio utafiti pekee uliofanyika miaka ya hivi karibuni ilhali tafiti za ajira hupaswa kufanyika kila baada ya miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali kuhakikisha kuwa inaweka utaratibu rasmi na kuhakikisha kuwa inatenga fungu la kutosha kuwezesha tafiti za nguvukazi na ajira kufanyika katika muda uliowekwa (yaani kipindi cha kila baada ya miaka 5).
Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya hali ya uchumi, takwimu zilizoendelea kutumika mpaka sasa ni za Sensa ya mwaka 2002 na pia imekuwa ikifanyiwa makadirio kutokana na taarifa za shirika la takwimu za taifa. Kambi rasmi ya Upinzani, inapenda kujua ni lini taarifa rasmi za soko la ajira nchini zitatolewa kwa umma pamoja  na hayo tunataka kujua idadi ya watu waliopata ajira 1,000,000 kama ilivyoahidiwa  na Serikali ya CCM. Kambi ya Upinzani, inajua kuwa ukusanyaji wa taarifa za soko la kazi ni muhimu ili kutoa taswira ya ajira kwa taifa letu lakini kama Serikali itaendelea kutegemea fedha za wafadhili kwa ajili ya ukusanyaji wa taarifa za soko la ajira ni wazi kuwa hata mianya ya wafanyakazi wa kigeni wanaofanya kazi nchini kinyume na sheria itazuia uwezekano wa watanzania wenye uwezo kuweza kupata nafasi na kuonesha ujuzi na utaalamu wao katika sekta mbalimbali.

15.0 ONGEZEKO LA RAIA WA KIGENI NA MUSTAKABALI WAKE KATIKA SOKO LA AJIRA NCHINI
Mheshimiwa Spika, kuna wimbi la kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi wa nchi nyingine wanaoingia kwa mgongo wa wawekezaji kinyume cha taratibu na ambao hufanya kazi za kawaida ambazo Watanzania wana uwezo nazo. Wafanyakazi wetu wengi wanaonekana kuwekwa pembeni si kwa sababu hawana uwezo bali kwa sababu waajiri wanaleta watu wao toka nje.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Uwekezaji Na. 26 ya mwaka 2007, Sura 38 Kifungu cha 24, inaruhusu Mwekezaji kuleta wataalam wasiozidi watano kutoka nje ya nchi. Aidha, iwapo Mwekezaji ataona haja ya kuongeza wataalam zaidi kutoka nje ya nchi, atapaswa kuwasilisha maombi maalum Kituo cha Taifa cha Uwekezaji ambacho kitawaruhusu ikiwa tu itathibitika hakuna Mtanzania hata mmoja mwenye utaalam husika. Kumekuwa na malalamiko kutoka katika kampuni ya SBC- Pepsi kuzidisha idadi ya wafanyakazi ambao ni raia wa India ambao pia wamekuwa wakifanya kazi ambazo Mtanzania anaweza kufanya, kwa mfano kuna raia wa India ambao wamepewa hadi kazi za Ulinzi.
Kambi Rasmi ya Upinzani imegundua malalamiko kama haya yapo kwenye kiwanda cha Jambo Plastic cha dar es salaam na pia kiwanda cha mable stones cha Marmo kilichopo Mbeya ambako kuna ushahidi wa wageni kutoka india kufanya kazi zisizohitaji utaalamu maalumu wa kitaaluma kama ulinzi na kazi zingine za mikono kwenye viwanda hivi.
Mheshimiwa Spika, kinyume kabisa na Sheria hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani imebaini kuwa migodi na kampuni nyingi nchini, wamekuwa wakiajiri raia wengi wa kigeni.
Mheshimiwa Spika, hali hii imekuwa ikiwanyima Watanzania wengi fursa ya kuajiriwa wakati kumbe nafasi zipo, lakini wanapewa wageni kinyume kabisa cha sheria. Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kupitia Wizara hii, kufanya ukaguzi maalum katika migodi, viwanda na mashirika yote yanayolalamikiwa kuajiri wageni kinyume cha sheria (yakiwemo tuliyoyataja), ili kuhakikisha sheria husika inaheshimiwa na Watanzania wazawa wananufaika nayo kikamilifu.

16.0 SEKTA ISIYO RASMI
Mheshimiwa Spika, Sekta isiyo rasmi ni mhimili mkubwa sana katika uchumi wa Tanzania, lakini bado haipewi kipaumbele kinachostahili. Zaidi ya asilimia 80% ya Watanzania wapo sekta hiyo, sekta rasmi ni asilimia isiyozidi 10% ambapo kitakwimu Watanzania walioajiriwa rasmi hawazidi laki nne. Kwa hiyo utaona kuwa wavuja jasho ndio wengi hapa nchini, na ndio wanaoendesha maisha yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, mara ngapi tunashuhudia au kusikia wafanya biashara wadogowadogo/wajasiriamali wakinyanyasika zaidi ya wakimbizi kwa kufukuzwa maeneo wanayojitafutia riziki bila ya kuoneshwa maeneo mbadala? Mara ngapi tunashudia mama lishe wakifukuzwa kama mbwa na kukatazwa kufanya biashara bila ya sababu za msingi wala kuwekewa mazingira ya kujiendeleza.Vijana waliowengi hawana ajira rasmi, na wanajituma ili waweze kupata kianzio cha mtaji wafanye biashara/shughuli halali ili wajipatie kipato lakini hakuna taasisi yoyote inayoweza kuwapa mikopo kama mtaji.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 22, 23 na ya 24, ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano zinazungumzia haki ya kufanya kazi. Ibara hizi zimeweka bayana misingi ya kisheria na msimamo thabiti unaowalinda Watanzania wanaojishughulisha katika sekta zisizo rasmi. Kwa mfanoIbara ya 22 kifungu kidogo cha kwanza kinasomeka hivi, “kila mtu anayohaki ya kufanya kazi’ na cha pili kinasomeka ‘kila raia anastahili fursa na haki sawa, kwa masharti ya usawa ya kushika nafasi yoyote na shughuli yoyote iliyo chini ya mamlaka ya nchi”.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 23 kifungu kidogo cha kwanza kinasomeka hivi; “kila mtu bila ya kuwepo ubaguzi wa aina yoyote anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanayoifanya”.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali kuhakikisha kuwa nguvukazi iliyo katika sekta isiyo rasmi inalindwa kwa kuzingatia misingi bora iliyowekwa na kuainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

16.0 AJIRA KWA WALEMAVU
Mheshimiwa Spika, Upatikanaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu ni changamoto kubwa inayolikabili taifa. Kwa mujibu wa taarifa za watumishi wenye ulemavu zilizokusanywa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Desemba 2007, inaonesha kuwa ni asilimia 0.2 tu ya watumishi wote wa umma walioajiriwa.
Mheshimiwa Spika, kama hali ni hiyo kwenye utumishi wa umma basi hali ni mbaya zaidi kwenye sekta ya binafsi kwani waajiri wengi binafsi wamekuwa wakikwepa kuajiri watu wenye ulemavu kutokana na visingizio mbalimbali


Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe ili kuongeza ajira kwa wenye ulemavu;
·        Serikali ifanye utafiti na kupata takwimu za watu wenye ulemavu walioko katika soko la ajira na walioajiriwa kwenye sekta binafsi.

·        Serikali iimarishe na kuboresha miundombinu kwenye ofisi na maeneo ya kazi kote kwa sekta ya umma na binafsi.


·        Serikali iharakishe utungwaji wa Kanuni za Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya 2010.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kupitia taasisi zake mbalimbali, kuhakikisha kuwa makundi mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa hukabiliwa na ubaguzi wa kazi kama, walemavu, wanawake na watu wenye maambukizi ya ugonjwa Ukimwi, yanapewa fursa sawa katika masuala ya kazi na ajira. Kambi rasmi ya upinzani inaitaka wizara kuhakikisha kuwa, inawapatia mafunzo waajiri na waajiriwa yanayohamasisha masuala ya fursa sawa kwa wote, kufuatilia kwa usahihi na ukaribu mgawanyo wa kazi katika ngazi zote.
Mheshimiwa Spika, aidha tunaitaka Serikali ipitie kwa umakini vigezo vinavyoonesha stahili za mafao kwa waajiriwa, kuweka viwango vya wazi vya malengo ya fursa sawa kwa wote katika ngazi zote na kupitia taratibu za kuajiri na kupandisha vyeo pamoja na kuhakikisha kuwa ‘majina yote yalipotishwa’ kwa ajili ya usaili wa ajira na kupandisha vyeo yamejumuisha waombaji wa makundi yote wenye sifa stahili na kuweka mawasiliano ya moja kwa moja na taratibu za kutoa malalamiko ya ubaguzi katika maeneo na mazingira ya kazi.

17.0 AJIRA HATARISHI KWA WATOTO
Mheshimiwa Spika, kauli mbiu ya mwaka huu katikakuadhimisha siku ya kupinga ajira kwa watoto iliyoadhimishwa tarehe 12 June 2012 ilisema “Haki za binadamu na haki za kijamii, tutokomeze ajira kwa watoto” ukiwa ni ujumbe wa kuikumbusha jamii kwa ujumla wake kuwa ajira kwa watoto siyo kitu kinachoungwa mkono, utumikishaji wa watoto ni ukiukaji wa haki za msingi za watoto. Nchini Tanzania asilimia 18.7 ya watoto wote wanatumikishwa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwenye mashamba makubwa, migodini hasa ya wachimbaji wadogowadogo, majumbani, na kwenye shughuli za uvuvi.

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka wizara kueleza mikakati endelevu ambayo itatatua tatizo la kutokulindwa kwa haki za watoto, hali inayochangiwa kwa serikali yenyewe kuruhusu hali hii kutokea au kuchelea kukemea ajira kwa watoto.
18.0 SHIRIKA LA TIJA LA TAIFA (NIP)
Mheshimiwa Spika, Shirika la Tija la Taifa (NIP) ni chombo muhimu kinachoweza kulisaidia Taifa katika kuhakisha shughuli zinafanyika kwa Tija ikizingatiwa uchache wa rasilimali tulizonazo.
Mheshimiwa Spika, shirika hili likitumiwa vizuri litapunguza upotevu wa fedha za umma unaofanyika katika nyanja za mafunzo toka kwa taasisi ambazo baadhi hazina nyenzo na uwezo wa kutoa mafunzo yenye ubora unaotakiwa. Kambi ya upinzani inapenda kutoa pendekezo la kuendesha shughuli za mafunzo ambazo NIP imekuwa ikiyafanya kwa kupitia chuo chake cha mafunzo nchini Swaziland zifanyike hapa Tanzania. Kuna baadhi ya taasisi hapa nchini ambazo zinatoa mafunzo kwa gharama nafuu na pia baadhi ya vyuo vikuu vyenye wataalamu na wakufunzi wenye ujuzi wa kutosha, ambao wanaweza kutumika kama njia mojawapo ya kupunguza gharama ambazo Shirika hili linatumia katika mafunzo yanayofanyika nje ya nchi. Mafunzo haya yakifanyika nchini si tu yatachangia kupunguza gharama  na matumizi bali itachangia pia katika kuhakikisha uwezeshaji wa walengwa wa mafunzo haya katika kutumia yale waliyofundishwa katika mazingira halisi ya kazi kwa kuwa mafunzo yanafanyika kwenye maeneo sahihi **kuhamisha kujifunza*** (transfer of learning).

UCHAMBUZI WA BAJETI KWA MWAKA 2012/2013
Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi kwa Wizara kwa mwaka wa fedha 2012/2013 imeomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi 15,945,298,000 ambacho ni sawa na punguzo la asilimia 12 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2011/2012.
Mheshimiwa Spika katika maagizo na ushauri ulioletwa hapa mwaka wa fedha wa 2011/2012 serikali ilipewa ushauri wa kutoa pensheni ya wazee kwani waziri mkuu alishaahidi serikali kuanza kutoa pensheni kwa wazee lakini katika bajeti ya mwaka huu hakuna mahali ambapo bajeti inaonesha kuhusu utekelezaji wa shauri hilo zaidi ya maelezo ya wizara ya kuandaa tafiti kwa kupitia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii. Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa ni lini tafiti hizi zitakamilika na kutelekezwa kama ilivyoelezwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015. Ni dhahiri kuwa Serikali imeendelea kupiga danadana suala la posho la wazee kwa kuwa imeshindwa kusimamia ahadi zake walizotumia kwa ajili ya kupata kura za wazee masikini wasio na msaada, wenye maisha duni na ya kusikitisha, ikizingatiwa kuwa wazee wanakabiliwa na matatizo mengi.

Bajeti Ya Maendeleo
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya maendeleo ya Wizara hii , imetengewa kiasi cha shilingi 2,835,800,000 fedha za nje ambazo ni kwa ajili ya uboreshaji wa ofisi za kazi na ajira, kuimarisha mfumo wa utawala na utunzaji kumbukumbu, masuala ya utokomezaji wa ajira ya watoto, utekelezaji wa sera na sheria, mapambano dhidi ya UKIMWI na uboreshaji wa mazingira wezeshi ya Biashara.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizi, inamaanisha kuwa bajeti ya nchi yetu kwa Wizara ya Kazi na Ajira ni tegemezi kwa asilimia 100. Hii ni hatari sana kwa maendeleo ya ajira na kazi hapa nchini kwani ni mara nyingi tumeona jinsi ambavyo fedha za ufadhili zisivyo na uhakika kwa kuwa mara nyingi hazifiki kwa muda uliopangwa na mara nyingine zinakuja lakini si kwa kiwango kile kilichotegemewa.
Mheshimiwa Spika, utegemezi huu wa wafadhili katika kutelekeleza maendeleo katika sekta ya ajira na kazi ni ishara tosha kuwa Serikali imeamua nguvu kazi ya taifa katika hatari kubwa ya kuporomoka kiuchumi na katika kuwapa maisha bora watanzania. Kambi rasmi ya Upinzani inauliza, je ni vipi suala la ajira hatarishi kwa watoto litafanikiwa ikiwa bajeti ya maendeleo ni tegemezi kwa asilimia 100 kutoka kwa wafadhili?  Je Serikali imeamua kuweka rehani maisha ya watoto ambao wanafanya kazi zilizo hatarishi kwa kuwategemea wafadhili na wahisani? Je Serikali imeamua kuweka pembeni mapambano dhidi ya UKIMWI na kuamua kutegemea wafadhili katika kutoa elimu ya hamasa ya masuala ya UKIMWI ambapo tunajua athari zake ni kubwa kwa nguvukazi ya taifa letu? Ni vipi bajeti tegemezi itaweza kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025?
Mheshimiwa Spika, ninapohitimisha hotuba hii, ujumbe wangu kwa Walimu wa Tanzania, Madaktari na Askari Polisi, Wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Wafanyakazi wote wanaonyanyasika kwa kudai haki na mafao yao, ni kwamba wasihofu, kwani kama alivyosema Mahatma Gandhi, Dunia imekuwa na watu katili, lakini mwisho wa yote nao pia walianguka”.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.

……………………………………
Cecilia Paresso (Mb)
K.n.y  Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Wizara ya Kazi,Habari  Utamaduni na Michezo
07.08.2012

No comments: